Tafuta

2024.09.12 Viaggio Apostolico a Singapore - Santa Messa nello Stadio Nazionale

Sikukuu ya Kutukuka Kwa Msalaba: Ufunuo wa Huruma na Upendo wa Mungu

Fumbo la Msalaba ni alama ya upendo wa Mungu kwa binadamu; kielelezo cha sadaka ya hali ya juu kabisa ya Kristo Yesu dhidi ya ukosefu wa haki msingi za binadamu; uchoyo na ubinafsi; dhuluma na nyanyaso. Msalaba ni alama ya ushindi dhidi ya dhambi na kifo. Msalaba ni kielelezo cha kiti cha enzi, madhahabu ya Agano Jipya na la Milele. Mwaka 1908 Priori ya Masista wa Benediktini wa Tutzing Ndanda, Jimbo Katoliki Mtwara, ilianzishwa rasmi nchini Tanzania.

Na Sr. Bonifasia Ngonyani, OSB. - Roma

Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba iwasaidie waamini kutambua na kuthamini ukuu wa Msalaba, madhara ya dhambi na thamani ya mateso ya Kristo Yesu Msalabani kwa ajili ya ukombozi wa watu wote. Fumbo la Msalaba ni alama ya upendo wa Mungu kwa binadamu; kielelezo cha sadaka ya hali ya juu kabisa ya Kristo Yesu dhidi ya ukosefu wa haki msingi za binadamu; uchoyo na ubinafsi; dhuluma na nyanyaso. Msalaba ni alama ya ushindi dhidi ya dhambi na kifo. Msalaba ni kielelezo cha kiti cha enzi, madhahabu ya Agano Jipya na la Milele. Msalaba ni kielelezo cha mateso, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo wanaouwawa kikatili kwa kuchomwa moto wangali hai; na wakati mwingine nyanyaso na dhuluma hizi zinatendwa katika hali ya kimya kikuu! Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 14 Septemba, anaadhimisha Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba “Exaltatio Sanctae Crucis” kwa lugha ya Kilatini. Hii ni Sikukuu ambayo inapata chimbuko lake kunako mwaka 335 Mfalme Costantino alipojenga Makanisa makuu mawili na kwa mara ya kwanza akawaonesha watu Masalia ya Msalaba Mtakatifu. Hata hivyo, hii ni Sikukuu yenye ukuu na maana yake kwani inadhihirisha kuwa Msalaba wa Kristo Yesu ni chombo cha wokovu na utukufu wa Mungu; ni siku ambayo Msalaba wa Kristo unang’ara duniani! Badala ya kashfa na utupu, Msalaba unakua ni chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu unaweza kuonekana kana kwamba ni upuuzi mtupu! Kila mara mwamini anapoutazama Msalaba, anagundua upendo na huruma ya Mungu iliyotundikwa Msalabani. Msalaba ni Kitabu kikuu kinachosimulia huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu wa nyakati zote.

Sikukuu ya Kutukuka kwa Fumbo la Msalaba: Huruma ya Mungu
Sikukuu ya Kutukuka kwa Fumbo la Msalaba: Huruma ya Mungu

Msalaba ni chombo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu! Ni ishara ya neema, sala, msamaha, upatanisho na matumaini. Ni kutokana na maana hii mpya, Mama Kanisa anaona fahari kuu kuimba sifa kuu za Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Msalaba unaendelea kumfunza mwamini kwamba, hakuna mapendo kamili yasiyokuwa na mateso na matumaini ya uzima wa milele. Msalaba pia ni alama ya ushindi ya vita iliyopiganwa ili kumkomboa mwanadamu na ni ngazi iliyotuunganisha na Mwenyezi Mungu. Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 14 Septemba, anaadhimisha Sikukuu ya Kutukuka kwa Fumbo la Msalaba “Exaltatio Sanctae Crucis” kwa lugha ya Kilatini. Fumbo la Msalaba linayagusa maisha ya mwamini kwa namna ya pekee. Msalaba katika mapokeo ya kale, ilikuwa ni alama ya uovu wa kutisha na hali ya kukatisha tamaa, lakini, kwa njia ya Kristo Yesu Mkombozi wa dunia, Msalaba sasa ni kielelezo cha ushujaa wa Kristo Yesu na mashuhuda wa imani, wanaoendelea kuteseka pamoja na kuyamimina maisha yao kwa ajili ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake sehemu mbalimbali za dunia. Nimesema kuwa mwezi Septemba ni mwezi wa pekee katika shirika letu la Wamisionari wa Benediktini wa Tutzing na nyumba yetu ya Ndanda, kwa sababu shirika letu lilianzishwa Mwezi Septemba mwaka 1885, huku Ujerumani mahali panapoitwa Reichenbach na mwazilishi wetu ni Padre Andreas Amrhein. mpaka sasa tuko masista wapatao 1300 ulimwenguni kote tunamshukuru Mungu kwa kulitunza shirika letu hadi sasa. Pia katika mwezi huu wa Septemba katika Sikukuu ya kutukuka kwa Msalaba tunakumbuka siku ya kuanzishwa kwa “Priori yetu ya Ndanda” iliyoko Jimbo Katoliki la Mtwara, nchini Tanzania yaani tarehe 14 Septemba mwaka 1908 na katika shirika, “Priori yetu ya Ndanda” ni kati ya nyumba kongwe ndani ya Shirika.

Wamisionari Wabenediktini wa Tutzing kutoka Ndanda, Tanzania
Wamisionari Wabenediktini wa Tutzing kutoka Ndanda, Tanzania

Mwezi Septemba mwaka 2024 tunapoadhimisha Sikukuu hii ya kutukuka kwa Msalaba, katika nyumba yetu ya Ndanda tuna matukio makuu mawili: Mosi; Masista watatu wanasherekea Jubilei ya miaka 25 ya kujitoa sadaka bila ya kujibakiza katika Kanisa kwa maisha ya kitawa. Nao ni: Sr. Tumaini Ajali OSB, Sr. Fides Msanga OSB., pamoja na Sr. Clare Nyoni OSB.  Hawa wamejitoa kwa moyo wote katika kumtumikia Mungu katika nafasi mbalimbali katika Shirika na Ndanda. Tunamshukuru Mungu kwa wito, sadaka na majitoleo yao ya kila siku.Tena katika Sikukuu hii ya kutukuka kwa Msalaba. Mungu anatupatia tena zawadi ya pekee ya masista wanne ambao wanajitoa kwa nadhiri ya daima kupitia Shirika letu la Wamisionari Wabenediktini wa Tutzing Ndanda kuendelea   kufanya utume katika Kanisa.  Hao ni Sr. Neema Mkolokoti OSB, Sr. Hildegard Shayo OSB, Sr. Victoria Danga OSB na Sr. Faustina Kadinde OSB. Wao kwa zaidi ya miaka sita baada ya kufunga nadhiri ya kwanza wamejitafiti na kujihoji na leo tarehe hii ya pekee ya kutukuka Msalaba wameamua kwa hiari yao kumtumikia Mungu. Kutoka Zaburi ya (45: 11-12), inasema ‘sikia ewe binti utege sikio lako mfalme anatamani uzuri wako.’ Hayo ni maneno ambayo wameyachagua kuwa ni kiooo cha maisha yao, maana ni matamanio yao katika maisha yao yote, kumsikiliza yeye aliyewachagua na kuwaita katika Kanisa lake.

Wanaitwa kumsikiliza Mungu, matamanio ya maisha yao siku zote
Wanaitwa kumsikiliza Mungu, matamanio ya maisha yao siku zote

Pia kwenye Kanuni ya Mtakatifu Benedikto utangulizi mstali wa kwanza kabisa Baba Benedikto Abate anasema sikiliza mwanangu, tega sikio la moyo wako. Huo ni mkazo wa pekee katika maisha ya kitawa. mtawa lazima awe na uwezo mkubwa wa kusikiliza, mtawa akifaulu kusikiliza vyema ataelewa ujumbe anaoambiwa, atakapo tumwa atafanya vyema. Basi tuna waombea dada zetu hawa wanne ambao leo wanajitoa kabisa katika maisha yao yote kumtumikia Yeye ambaye amewaita nao wakasema mimi hapa. Kama mtoto Samweli alivyo msikiliza Mungu kupitia msaada Eli Mtumishi wa Mungu (1 Samuel 3:1-14) Nasi basi tunawaombea usikivu wa ndani ya mioyo yao, kamwe wasikatishwe tamaa wala kukengeuka na kufuata malimwengu. Bali wakaze mwendo na kusonga mbele katika utumishi wao mpaka siku ile ambayo Yeye ambae wana mwamini, kumtumikia na kumtumainia atakapo sema njoo mtumishi wangu niliye pendezwa nawe, kama Mtume Paulo kwa Wafilipi anasema (Fil.3:12-21) Sisemi kwamba nimekwisha kupokea haya yote, au kwamba nimekwisha kuwa mkamilifu, la hasha; bali nazidi kukaza mwendo ili nipate kile ambacho, kwa ajili yake, Kristo amenifanya niwe wake.  Tunapo mshukuru Mungu kwa zawadi ya miito katika Kanisa kupitia Shirika letu la Wamisionari Wabediktini wa Tutzing, hasa katika nyumba yetu ya ndanda, tunazidi kumwomba Mungu atujalie miito ya kutosha, atuletee watumishi wengi na wenye moyo wa kujitolea katika Kanisa; wema na watakatifu. Sisi kama shirika tunaendeleza kazi ya ukombozi hapa duniani kwa kufanya kazi mbalimbali za kumkomboa mwanadamu katika nyanja mbalimbali kama vile katika sekta ya: Elimu, Afya, Katekesi na Maarifa ya nyumbani na kwa kufanya hivi tunaendeleza kazi ya ukombozi wa mwanadamu.

Kutukuka kwa Msalaba
13 September 2024, 16:28