2024.09.06 Makaribisho ya hivi karibuni  ya Balozi Mpya  wa Vatican nchini Sudan Kusini. 2024.09.06 Makaribisho ya hivi karibuni ya Balozi Mpya wa Vatican nchini Sudan Kusini. 

Sudan Kusini,Balozi Horgan na changamoto ya utume katika nchi maskini zaidi

Askofu mkuu wa Ireland alianza jukumu lake siku za hivi karibuni baada ya kuteuliwa kuwa mwakilishi mkazi wa kwanza wa Vatican katika nchi ya Sudan Kusini. “Nitajitahidi niwezavyo kuwa uwepo wa Papa katika nchi hii ambayo ni muhimu sana moyoni mwake.”

Na Francesca Sabatinelli na Angella Rwezaula -Vatican.

Kanisa la Sudan Kusini liko hai na licha ya changamoto kubwa zinazoikabili nchi hiyo changa zaidi duniani, iliyozaliwa mwaka 2011 na pia miongoni mwa maskini zaidi, linashuhudia kwa uthabiti imani yake thabiti na ukarimu wake wamisionari ambao, kwa kuhatarisha usalama wao wenyewe, hawawaachi waamini wao. Katika siku hizi, ambapo Umoja wa Mataifa unaongeza kutoa miito  kwa hali mbaya ambayo nchi ya Kiafrika inapitia kwenye mpaka na Ethiopia, iliyokumbwa na mafuriko yaliyoathiri zaidi ya watu elfu 700, Balozi mpya wa Vatican  alianza huduma yake huko Juba, Askofu Mkuu Séamus Patrick Horgan, aliyeteuliwa na Papa Francisko mnamo tarehe 14 Mei 2024. Akiwa na  Mwandishi wa Vatican News- Radio Vatican, alizungumzia changamoto zinazoingoja nchi na Kanisa mahalia.

Mwashamu  Séamus Patrick Horgan, ulianza huduma yako siku chache zilizopita kama balozi katika mojawapo ya nchi ngumu zaidi duniani, nchi changa zaidi, lakini pia miongoni mwa nchi maskini zaidi. Kufika Juba, Sudan Kusini kulimaanisha nini kwako?

Nimekuwa hapa kwa Juma moja tu na ufahamu wangu wa nchi ni wazi  kwamba bado ni mdogo. Imekuwa Juma lililo jaa matukio mbalimbali, kuanzia na makaribisho mazuri  na juma  moja lililopita katika uwanja wa ndege wa Juba. Kanisa la mahali hapo lilikuwepo, kama baadhi ya maaskofu na waamini na wa dini nyingi, lazima niseme kwa sababu katika nchi kuna uwepo wa taasisi za kidini, na kisha waamini waliofika kutoka parokia mahalia ambao walinikaribisha kwa furaha, na kwa hivyo tuseme kwa uchangamfu kwamba ulikuwa mwanzo mzuri, mara moja nilihisi kuwa nyumbani lazima niseme.

Mwashamu, Kanisa la Sudan Kusini limedhihirisha siku za hivi karibuni, kwa ziara ya Kardinali Parolin mwaka 2022, kwa ziara ya Papa Francisko mwaka 2023, kwamba kweli ni hai sana nchini humo, hili ndilo wazo linaloanza pia kuibuka kwako katika siku hizi za mapema?

Kiukweli, pia kwa sababu Dominika  nilipata fursa ya kusherehekea katika Kanisa Kuu la Jimbo kuu hili, na Kardinali Stephen Ameyu Martin Mulla alikuwepo, pamoja na idadi kubwa ya mapadre na waamini, hivyo niliweza kukutana na jumuiya ya jimbo la Juba na kupata sherehe ya furaha. Ndiyo, mtu ana hisia ya Kanisa lililo hai, la Kanisa lenye furaha, tuseme hili ndilo jambo kuu. Ingawa ni mazingira ambayo yanakabiliwa na changamoto kubwa, lakini furaha inaonekana. Changamoto zinazoikabili Sudan Kusini, na kwa hakika si hivi karibuni bali kwa muda mrefu sasa, kwa hakika ni hali ngumu sana ya kibinadamu, mafuriko makubwa ambayo yameharibu sehemu muhimu ya nchi hiyo, na kisha pia athari za mzozo wa Sudan ambayo ilisababisha msafara mkubwa wa watu kuhama.

Hivyo Sudan Kusini, pamoja na umaskini wake wote, inajikuta ikikabiliwa na ujio wa wakimbizi wa kiume na wa kike, wakiwemo wanaume na wanawake watawa…

Kiukweli, changamoto hizi zote zinaunganishwa kwa wazi. Kanisa mahalia pia linasonga mbele kusaidia kuwakaribisha wakimbizi ambao sasa wanatoka Sudan, kama ulivyotaja, na pia kuleta Injili kwenye kambi za wakimbizi, kwa sababu, kutokana na kile nimeona hadi sasa, kila mahali nchini kuna kambi mbalimbali pamoja na wakimbizi wa ndani na wakimbizi wanaotoka nje. Kwa hiyo, hii ni changamoto kubwa kwa nchi ambayo tayari ina matatizo yake ya ndani. Kuhusu wale waliowasili kutoka Sudan, nilikuwa katika Juma langu la  kwanza hapa, na mkutano wa kusisimua sana na kikundi cha watawa wa Kisalesian ambao waliendesha kituo cha akina mama na watoto wachanga huko Khartoum kabla ya vita, ambayo ilianza zaidi ya mwaka mmoja uliopita. Kwa mwaka wa kwanza wa vita walibaki Khartoum, hawakuweza kuondoka, lakini wakabaki karibu na wale waliokabidhiwa uangalizi wao. Kisha, baada ya mwaka wa mzozo, walifanikiwa kwa njia ya ajabu kuondoka Khartoum, kando ya Mto Nile, kufika Bandari ya Sudan na kufika Juba siku ile ile nilipokuwa nikitembelea nyumba ya Wasalesian, kwa hiyo niliweza kukutana nao, kusikiliza historia yao na kuwahakikishia uwepo na ukaribu wa Baba Mtakatifu. I

likuwa ni wakati mzuri na wanawake hawa, licha ya janga waloteseka, walitoa ushuhuda wa furaha na uaminifu kwa utume wao. Ulikuwa mkutano wenye kugusa moyo kwangu, pamoja na wanawake wenye imani kubwa, wanaojaribu kurudi walikotoka ili kuanza kazi yao tena, wakati wowote wawezapo. Kwa hivyo huu, kwa maoni yangu, ni uso wa Kanisa la kimisionari. Huu ndio uso wa wamisionari wetu wa ajabu, wanaume na wanawake, ulikuwa wakati wa kugusa moyo na, wakati huo huo, onyesho la kile Kanisa linaweza kufanya katika hali kama hii. Hizi ni historia za ushujaa wa wamisionari wetu ambazo hatupaswi kuzisahau. Kwa hivyo, hii ni sehemu ya Juma la  kwanza hapa, ilikuwa wakati mzuri sana ambao pia ulionesha ukweli wa hali ya kushangaza iliyopatikana nchini Sudan na matokeo  waliyonayo kwa Sudan Kusini. Zaidi ya hayo, siku zilizopita tulikuwa na mkutano ambapo uzito wa suala la mafuriko ulisisitizwa tena. Nchi inakabiliwa na mvua kubwa kwa sasa na hii inaweza kusababisha mafuriko, ambayo mara nyingi hutokea wakati wa Septemba na Oktoba.

Wewe ni Balozi wa kwanza mkazi, utakuwa Juba kabisa na ni mara ya kwanza kwa hili kutokea...

Ni wazi kwamba sikutarajia uteuzi huo, lakini nimefurahishwa sana na jambo hilo kwa sababu sasa tumetoka kwa Balozi mmoja aliyekuwa akiishi Nairobi na tukafuata kutoka huko hadi kwa Balozi mkazi wa hapa, ambapo ni wazi natumaini itasaidia Kanisa hili la karibu. Nitajitahidi niwezavyo kuwa uwepo wa Papa katika nchi hii ambayo ni muhimu sana kwa moyo wa Papa, kama tujuavyo. Kanisa katika nchi zote, katika hali zote, linapaswa daima kuhubiri Injili ambayo ni kazi ya Kanisa katika hali ya umaskini wa mali, pia katika hali ya umaskini wa kiroho. Nitafanya kila niwezalo hapa kuunga mkono kazi muhimu ya Kanisa na pia kusaidia, kwa njia zote zinazowezekana, mali, lakini utume wetu ni wazi, kama Papa alisema na katiba ya kitume Praedicate evangelium, ndio changamoto kuu katika mashirika yote.

Balozi wa Vatican Nchini Sudan Kusini atoa ushuhuda wa utume wake mpya
09 September 2024, 14:59