Balozi Acerbi,kuwa Kardinali akiwa na umri wa miaka 99!
Na Salvatore Cernuzio na Angella Rwezaula – Vatican.
Zaidi ya miaka hamsini katika Ubalozi wa Vatican, duniani kote kutoka Pasifiki hadi Ulaya ya Kati, ikiwa ni pamoja na utekwaji nyara uliofanywa na waasi nchini Colombia, huduma ya uaminifu kwa Papa na Kanisa na jukumu la Askofu wa Shirika Kuu la Kijeshi la Malta na miaka ya mwisho amekuwa akiishi katika Nyumba ya Kitume ya Mtakatifu Marta, akiwa na Papa Francisko. Akiwa na umri wa miaka 99, Askofu Mkuu Angelo Acerbi atakuwa Kardinali kuanzia tarehe 8 Desemba 2024, tarehe ambayo Baba Mtakatifu Francisko ataadhimisha Consistory(Baraza la Maakardinali) la kumi, aliyotangaza mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana Dominika tarehe 6 Oktoba 2024. Kwa njia hiyo Kardinali Angelo Acerbi atakuwa mjumbe mzee zaidi wa Baraza la Makardinali. Kwa sasa anashikilia rekodi ya kuwa Kardinali mwenye umri mkubwa zaidi kuundwa. Sherehe kumbukumbu ya miaka hamsini ya kuwekwa wakfu wa kiaskofu ulifanyika huko Mtakatifu Marta mjini Vatican.
Jina lake lilikuwa la kwanza katika orodha iliyosomwa na Papa Francisko kwenye dirisha la Jumba la Mitume na mara moja lilimfanya mtu kufikiria ishara ya umakini na heshima kwa upande wa Papa kwa mtawa na miaka yake karibu sabini ya huduma kwa Kanisa na Vatican. Jorge Mario Bergoglio (Papa Francisko) alikuwa tayari alitaka kutoa heshima kwa Askofu Mkuu Acerbi tarehe 27 Juni iliyopita, akisherehekea katika Kanisa dogo la Mtakatifu Marta ambako Mzee huyo anaishi, katika Misa ya kumbukumbu ya miaka 50 ya kuwekwa wakfu wa kiaskofu kunako tarehe 22 Juni 1974. Wakati wa familia pamoja na mapadre, watawa wa Shirika la Mabinti wa upendo wa Mtakatifu Vincent wa Paulo na wafanyakazi wa Nyumba hiyo ya Vatican.
Katika mabara matano
Kardinali Acerbi aliyezaliwa tarehe 23 Septemba 1925 huko Sesta Godano, katika jimbo la La Spezia, Italia, alipewa daraja la Upadre mnamo tarehe 27 Machi 1948. Aliingia kufanya huduma ya kidiplomasia ya Vatican mnamo mwaka 1956, akifanya kazi katika Uwakilishi wa Ubalozi wa Upapa Papa huko Colombia, Brazil, Ufaransa, Japan na Ureno na pia katika Baraza la Masuala ya Umma ya Sekretarieti ya Vatican. Mtakatifu Papa Paulo VI, mnamo mwaka 1974, alimteua kuwa mwakilishi wa kitume huko New Zealand na mjumbe wa kitume katika Bahari ya Pasifiki, akimkabidhi kanisa la Zella na kupandishwa wadhifa wa Askofu mkuu. Na kutoka kwa Papa Montini, tarehe 30 Juni iliyofuata, alipokea daraja la uaskofu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro. "In fide et lenitate" ndiyo kauli mbiu yake.
Papa Yohane Paulo wa II alimtuma mnamo mwaka 1979 kama balozi wa Vatican huko nchini Colombia. Katika nchi ya Amerika Kusini moja ya nyakati ngumu zaidi za huduma yake: pamoja na wanadiplomasia wengine, Askofu Mkuu Acerbi alishikiliwa mateka kwa majuma sita na waasi wa Harakati 19 de Abril. Katika kipindi chake cha kifungo, Askofu Mkuu Acerbi mwenyewe baadaye alisema, aliruhusiwa kusherehekea Misa kila siku kwa waliohudhuria.
Huko Hungaria baada ya Ukomunisti
Mnamo 1990, baada ya Colombia, Askofu mkuu Acerbi alihamishiwa Hungaria, akiwa Balozi wa kwanza baada ya kuanzishwa kwa Ukomunisti (Ubalozi ulikuwa umefungwa mnamo 1920). Katika Nchi hiyo alitoa msukumo kwa ujenzi wa Kanisa na mapadre baada ya kuanguka kwa utawala na wakati wa shughuli zake kutiwa saini kwa makubaliano mbalimbali kati ya nchi na Vatican kunakumbukwa. Pia alikuwa Balozi wa kwanza huko Moldovia tangu 1994 hadi 1997, mwaka ambao alihamishiwa Uholanzi. Mnamo tarehe 27 Februari 2001, Papa Yohane Paulo II alikubali kujiuzulu kwa sababu ya kufikia kikomo cha umri wake. Lakini kuanzia mwaka huo hadi kumi na nne mwaka uliofuata (2015), alishikilia wadhifa wa kiaskofu katika Shirika la Kijeshi la Malta. Na kuanza sasa akiwa katika kizingiti cha miaka mia moja na utume mpya.
Orodha ya Makardinali wapya
1. Askofu Mkuu Angelo Acerbi, Balozi wa Kitume wa Vatican
2. Askofu Mkuu Carlos Gustavo CASTILLO MATTASOGLIO, Jimbo Kuu la Lima (Peru)
3. Askofu Mkuu Vicente BOKALIC IGLIC C.M., wa Santiago ya Estero (Argentina).
4. Askofu Mkuu Luis Gerardo CABRERA HERRERA, O.F.M., Jimbo Kuu la Guayaquil (Ecuador).
5. Askofu Mkuu Fernando Natalio CHOMALÍ GARIB, Jimbo Kuu la Santiago ya Chile (Chile).
6. Askofu Mkuu Tarcisio Isao KIKUCHI, S.V.D., jimbo Kuu la Tokyo (Japan).
7. Askofu wa Pablo Virgilio SIONGCO DAVID, Jimbo la Kalookan (Philippines).
8. Askofu Mkuu Ladislav NEMET, S.V.D., Jimbo Kuu la Beograd -Smederevo, (Serbia).
9. Askofu Mkuu Jaime SPENGLER, O.F.M., Askofu Mkuu wa Jibo la Porto Alegre (Brazil).
10. Askofu Mkuu Ignace BESSI DOGBO, Jimbo Kuu la Abidjan (Ivory Coast).
11. Askofu Mkuu Jean-Paul VESCO, O.P., Jimbo Kuu la Alger (Algeria).
12. Askofu Paskalis Bruno SYUKUR, O.F.M., wa Jimbo la Bogor (Indonesia).
13. Askofu Mkuu Dominique Joseph MATHIEU, O.F.M. Conv., Jimbo Kuu la Tehran Ispahan (Iran).
14. Askofu Mkuu Roberto REPOLE, Jimbo Kuu la Torino (Italia).
15. Askofu Baldassare REINA, Askofu Msaidizi wa Jimbo la Roma, na Vica Mkuu wa Jimbo la Roma.
16. Askofu Mkuu Francis LEO, Jimbo Kuu la Toronto (Canada).
17. Askofu Mkuu Rolandas MAKRICKAS,Msimamizi wa Basilika ya Kipapa la Mtakatifu Maria Mkuu.
18. Askofu Mykola BYCHOK, C.S.R., wa Upatriaki wa Watakatifu Petro na Pauli huko Melbourne ya Ukraine
19. Padre Timothy Peter Joseph RADCLIFFE, OP, (Mdominikani)Mtaalimungu.
20. Padre Fabio BAGGIO, C.S., alikuwa Ofisi ya Katibu wa Baraza la Kipapa ma Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu.
21. Monsinyo George Jacob KOOVAKAD, Afisa wa Katibu wa Vatican, katika masuala ya Ziara za Kipapa.