Bambino Gesù,Kenya:Utume kwa ajili ya mafunzo ya mbinu za uchunguzi wa picha za watoto!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Hivi karibuni Timu ya fani mbalimbali iliandaa mafunzo ya kinadharia na vitendo ya upigaji picha wa watoto katika chuo kikuu cha Hospitali ya Ruaraka Neema. Mpango huo ulihamasishwa pamoja na World Friends Kenya, Timu ya wataalam mbalimbali kutoka Hospitali ya Kipapa ya Bambino Gesù walioshiriki utume katika Hospitali ya Ruaraka Neema jijini Nairobi ambao walirejea siku za hivi karibuni. Mpango huo uliotekelezwa kwa ushirikiano na World Friends Kenya na kufadhiliwa na Mfuko wa Maria Enrica (Maria Enrica Foundation,)ukiwa na lengo la kuimarisha ujuzi wa wahudumu wa afya nchini Kenya katika njia za uchunguzi wa kimatibabu kupitia mafunzo ya mbinu za hali ya juu kama vile uchunguzi wa ultrasound na matumizi ya CT katika mazingira ya watoto. Timu hiyo iliundwa na daktari wa watoto na mtaalam wa(X-ray) radiolojia ambao pamoja na wafanyakazi wa afya wa eneo hilo, walipanga vikao vya mafunzo ya kinadharia na vitendo juu ya picha za watoto, usimamizi wa kesi ngumu za kliniki na ukuzaji wa itifaki za uchunguzi.
Umakini kwa Ultrasound na mionzi kwa watoto
Uangalifu hasa ulipewa kwa uchunguzi wa ultrasound() wa uhakika, mbinu ambayo inaruhusu uchunguzi kufanywa moja kwa moja kando ya kitanda cha mgonjwa, ikithibitisha kuwa muhimu sana kwa uchunguzi wa dharura wa haraka. “Tumewafunza wafanyakazi wa hospitali ya Nairobi jinsi ya kutumia kipimo cha uangalizi wa uhakika, hata kwa wagonjwa wa watoto walio katika hali ya dharura kwenye chumba cha dharura”, alisema Dk. Anna Maria Musolino, mkuu wa Hospitali ya Dharura ya Watoto katika Hospitali ya Kipapa la Bambino Gesù. “Kupitia uigaji wa kesi za kliniki na tathmini ya ujuzi, tumepata uboreshaji mkubwa katika ujuzi uliopatikana, ambao utaruhusu usimamizi bora zaidi wa wagonjwa wa watoto.”
Kwa upande wa Daktari Marco Cirillo, mkuu wa Radiology (X-ray)katika makao makuu ya Mtakatifu Paolo ya Bambino Gesù, alisisitiza umuhimu wa mafunzo juu ya matumizi ya CT katika magonjwa ya watoto kwamba: “Moja ya malengo muhimu ya utume ilikuwa kuboresha matumizi ya CT na kupunguza mfiduo wa mionzi hasa kwa idadi ya watoto. Tulifanya kazi juu ya upekee katika utumiaji wa mashine katika uwanja wa watoto, juu ya kanuni za ulinzi wa mionzi na uboreshaji wa kipimo kilichotolewa kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya marejeo, shukrani kwa vikao maalum vya kinadharia na vitendo kwenye vifaa vilivyotolewa hivi karibuni ba hospitali.”
Mpango wa Hospitali ya kipapa ni mpana kwa sasa unafanya kazi na nchi 12
Utume huo nchini Kenya ni sehemu ya mpango mpana wa Hospitali ya Kipapa ya Bambino Gesù unaolenga kutoa usaidizi na mafunzo katika nchi mbalimbali, kupitia mipango ya mshikamano. Mpango huo kwa sasa unafanya kazi katika nchi 12: Ukraine, Jordan, Cambodia, Japan, Kenya, Tanzania, Ivory Coast, Ethiopia, Peru, Panama, Ecuador na Colombia. Zaidi ya hayo, kuna mikataba iliyotiwa saini na nchi nyingine 4 ambazo ni: Misri, Bolivia, Albania na Kazakhstan. Mikutano zaidi ya kujifunza umbali imepangwa katika miezi ijayo ili kufuatilia maendeleo katika matumizi ya mbinu zilizofunzwa na kutoa usaidizi katika usimamizi wa kesi za watoto.