Tafuta

Kardinali Matteo Zuppi askofu Mkuu Bologna. Kardinali Matteo Zuppi askofu Mkuu Bologna.  (Francesco Pierantoni)

Kard.Zuppi arudi Moscow,kwa utume wa watoto wa Kiukraine na kufikia amani

Rais wa CEI ameanza ziara mpya nchini Urusi Oktoba 14,ikiwa ni sehemu ya utume aliokabidhiwa na Papa tangu 2023.Mkutano na mamlaka umepangwa Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Vatican:"safari ya kutathmini juhudi zaidi za kuhimiza kuunganishwa kwa familia na watoto Ukraine na kubadilishana wafungwa kwa nia ya kufikia amani inayotarajiwa kwa muda mrefu."

Na Salvatore Cernuzio na Angella Rwezaula – Vatican.

Baada ya miezi 16, Kardinali Matteo Zuppi, Rais wa Baraza la Maaskofu Italia (CEI) anarudi kwa mara nyingine tena katika utume mpya katika muktadha wa mpango wa kibinadamu wa Vatican ili kupata njia ya amani  kwa ajili ya Ukraine iliyopigwa. Haya yalitangazwa na Msemaji Mkuu wa Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Vatican, Dk. Matteo Bruni: “Ninathibitisha kwamba Kardinali Matteo Zuppi alianza ziara mpya huko Moscow leo, (Oktoba 14,2024)ndani ya mfumo wa utume aliokabidhiwa na Papa Francisko mwishoni mwa mwaka ulipita, kukutana na mamlaka na kutathmini juhudi zaidi za kuhimiza kuunganishwa kwa familia na watoto wa Kiukraine na kubadilishana wafungwa, kwa nia ya kufikia amani inayotarajiwa.”

Ujumbe wa Juni 2023

Kardinali Zuppi alikuwa tayari amefika huko Moscow mnamo tarehe 28 na 29 Juni 2023, ambapo ilikuwa hatua ya pili ya utume wake baada wa Kyiv nchini Ukraine, ambapo pia alikuwa na mkutano na Rais Volodymyr Zelensky, na kabla ya safari katika miezi iliyofuata kwenda Washington na Beijing. Katika masaa 48 katika ardhi ya Urusi, Kardinali alikuwa na mkutano na Kirill, msimamizi wa Moscow na Urusi yote.  Mkutano “wenye matunda,” Vatican ulifafanua katika taarifa, ambayo ilisisitiza kwamba Kardinali alikuwa amewasilisha salamu za Baba Mtakatifu kwa Kirill; mjumbe wa Papa alikuwa amejadili mipango ya kibinadamu ambayo inaweza kuwezesha suluhisho la amani na Patriaki.

Mazungumzo na kamishna wa haki za watoto

Kisha Kardinali huyo alikuwa na mikutano miwili tofauti ya kitaasisi, kwanza na Yuri Ushakov, msaidizi wa Rais Vladimir Putin kwa masuala ya sera za kigeni, na kisha na Maria Lvova-Belova, kamishna wa haki za watoto. Katika mazungumzo hayo, kipengele cha kibinadamu cha mpango huo kilisisitizwa kwa nguvu, pamoja na haja ya kuweza kufikia amani inayotarajiwa sana. Hasa na Lvova-Belova,  tovuti ya kamishna iliripoti siku hiyo, akichapisha picha ya ziara ya Kardinali Zuppi alikuwa amejadili kile kinachoitwa masuala ya kibinadamu yanayohusiana na operesheni za kijeshi na ulinzi wa haki za watoto.  Hiyo ni, lengo lilikuwa juu ya suala la zaidi ya watoto 19,000 wa Kiukraine walioletwa kwa lazima nchini Urusi, suala ambalo Rais Zelensky aliomba msaada kutoka Vatican katika Mkutano wa Mei 2023 na Papa Francisko. Ombi pia lilitolewa mbele ya Mkutano na Papa mjini Vatican Ijumaa iliyopita, tarehe 11 Oktoba 2024, ambapo kiongozi huyo wa Ukraine alilenga wafungwa wote wa Ukraine. Sio watoto tu, bali pia waandishi wa habari.

Matokeo ya juhudi za kidiplomasia

Shukrani kwa chaneli iliyofunguliwa na Kardinali Zuppi, idadi fulani ya watoto wa Kiukraine waliohamishiwa Urusi na vikosi vya kukalia waliweza kurudi nyumbani. Katika miezi ya hivi karibuni, makamu rais wa Bunge la Ukraine Olena Kondratiuk – akifanya  mkutano  wa umma huko Roma na rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia (CEI)  alimshukuru Kardinali, akisisitiza kwamba“diplomasia ya kibinadamu ya Vatican  imetoa matokeo muhimu.  Miongoni mwa haya, pia kuachiliwa kwa mapadre wawili wa Shirika la Redemptorist waliokamatwa mnamo Novemba 2022 na kuachiliwa na Urusi kwa kubadilishana wafungwa wa Ukraine mnamo 29 Juni. Matokeo ambayo Zelensky mwenyewe alitoa shukrani kwa Vatican kwa juhudi zake.

Kuheshimu haki za binadamu

Kwa ufupi, safari hii imeanza utaratibu, “polepole” kama Kardinali, Pietro Parolin, Katibu wa Vatican, alivyosema kwa nyakati tofauti, lakini ambayo inasonga mbele. Kardinali Parolin mwenyewe alikuwa na mkutano kwa njia ya video mnamo Septemba iliyopita na Tatiana Moskalkova, Kamishna wa haki za binadamu wa Shirikisho la Urusi. Katika mazungumzo hayo, Ofisi ya Wanahabari wa Vatican ilifahamisha siku hiyo, kwamba "Kardinali alisisitiza haja ya kulinda, katika muktadha wa mzozo huo, haki za kimsingi za binadamu zilizoainishwa katika Mikataba ya Kimataifa."

 

14 October 2024, 16:08