Waamini wanaalikwa kumwomba Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa Uinjilishaji, kuwaongoza Mababa wa Sinodi katika kipindi hiki wanapokaribia mwisho wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu ili awaongoze. Waamini wanaalikwa kumwomba Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa Uinjilishaji, kuwaongoza Mababa wa Sinodi katika kipindi hiki wanapokaribia mwisho wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu ili awaongoze.  (Vatican Media)

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu: Roho Mtakatifu Mhimili Mkuu wa Uinjilishaji

Huu ni muda wa kutathmini mambo msingi ambayo Yesu amependa kulijalia Kanisa lake katika kipindi hiki cha wa ujenzi wa umoja, ushirika na utume wa Kanisa. Kanisa limejifunza utamaduni wa kujadiliana na kusikilizana; madonda na udhaifu wa watu wa Mungu unaodhihirisha neema ya Mungu inayotimilika katika udhaifu. Rej. 2 Kor 12:9. Huu ni mwaliko wa kuendelea kufanya kazi ili kutafuta suluhu ya matatizo, changamoto na fursa mpya zinazojitokeza katika maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mwanzoni kabisa mwa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu 2021-2024, Jumamosi tarehe 9 Oktoba 2021, alitoa hotuba elekezi, ambayo ni msingi wa maadhimisho ya Sinodi katika hatua mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Watu wa Mungu wakajitambua kuwa wao ni sehemu ya Kanisa la Kisinodi, tayari kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Mungu, kwa kushirikiana na binadamu wote, kwa kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini kile ambacho Roho Mtakatifu anataka kuyaambia Makanisa. Huu ni mwendelezo wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu iliyozinduliwa kunako mwaka 2021 na itafikia kilele chake tarehe 27 Oktoba 2024. Tajiri mpumbavu ni mtu aliyejitafuta, kiasi cha kumezwa na ubinafsi na uchoyo, huku akijikweza kupita kiasi. Mambo muhimu ya kuangalia ni haya yafuatayo: wingi wa mazao yaliyopatikana shambani mwake; mafanikio haya yalimhakikishia usalama wa maisha kiasi kwamba, angeweza kupumzika, akala, akanywa na kufurahi, kielelezo cha amani na utulivu wa maisha. Lakini kwa bahati mbaya, maneno ya Mungu “yanafyekelea mbali ndoto ya tajiri mpumbavu.” Mwenyezi Mungu anamwambia “Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako” badala ya kufurahia maisha kwa “kula kuku kwa mrija” akashindwa kujitajirisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Matokeo yake tajiri mpumbavu anaulizwa swali kwa kejeri: “Na vitu alivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?” 

Safari ya Sinodi Ilianza mwaka 2021 hadi 27 Oktoba 2024
Safari ya Sinodi Ilianza mwaka 2021 hadi 27 Oktoba 2024

Tajiri huyu ni mpumbavu kwa sababu katika sera, mikakati na mipango yake yote, alimweka Mwenyezi Mungu pembezoni mwa vipaumbele vyake, “akaonekana kama tai inayoning’nia mtini.” Mwinjili Luka anahitimisha mfano huu wa tajiri mpumbavu kwa kutoa angalisho kwamba, “ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.” Utajiri, mali ya dunia na karama ni mambo muhimu sana katika maisha ya mwanadamu. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, utajiri, mali na karama hizi ambazo ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu zinamwilishwa katika uaminifu pamoja na kuwashirikisha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Utajiri, mali na karama mbalimbali zisiwe ni kizingiti cha kwenda mbinguni. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kuishi mintarafu mtindo wa tunu msingi za Kiinjili, ili kamwe wasimezwe na malimwengu. Kwa muhtasari huu ni upendo kwa Mungu na kwa jirani; na kuwahudumia maskini na wahitaji kwa moyo wa upendo na ukarimu; pamoja na kujisadaka bila ya kujibakiza hata kidogo. Upendo wa kweli ni chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani. Rej. Lk 12:16-21. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Mario Grech, Katibu Mkuu wa Sinodi za Maaskofu, Jumatatu tarehe 21 Oktoba 2024 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kwa kumwomba Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa Uinjilishaji, kuwaongoza Mababa wa Sinodi katika kipindi hiki wanapokaribia mwisho wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu.

Roho Mtakatifu ndiye mhimili mkuu wa Uinjilishaji
Roho Mtakatifu ndiye mhimili mkuu wa Uinjilishaji

Anasema, huu ni muda muafaka wa kutathmini mambo msingi ambayo Kristo Yesu amependa kulijalia Kanisa lake katika kipindi chote hiki, katika mchakato wa ujenzi wa umoja, ushirika na utume wa Kanisa. Kanisa limejifunza utamaduni wa kujadiliana na kusikilizana; madonda na udhaifu wa watu wa Mungu unaodhihirisha neema ya Mungu inayotimilika katika udhaifu. Rej. 2 Kor 12:9. Huu ni mwaliko wa kuendelea kufanya kazi ili kutafuta suluhu ya matatizo, changamoto na fursa mpya zinazojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa. Zawadi na karama ya Mungu iliyogunduliwa wakati wa maadhimisho ya Sinodi hii inapaswa kuwekezwa katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kupanua hema na kutandaza mapazia ya maskani ya Kanisa kwa kuongeza urefu wa kamba na kukaza vizingiti vya hema la Kanisa. Rej. Isa 54:2. Kanisa linapaswa kuwa makini katika maisha na utume wake, kwa kutambua kwamba, Maadhimisho ya Sinodi si mkutano wa Bunge, si mahali pa kufanya upembuzi yakinifu kuhusu mawazo ya waamini. Sinodi ni tukio muhimu la maisha na utume wa Kanisa chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Sinodi ni kielelezo cha Pentekoste mpya, Kanisa linalojadili, kusikiliza na kutenda kwa umoja na mshikamano. Tamko la Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo linanogeshwa na kauli mbiu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5 na kwamba, kiini cha maadhimisho haya ni matumaini yatakayowawezesha watu waaminifu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia kufanya hija ya maisha ya kiroho mjini Roma sanjari na maadhimisho haya kufanyika kwenye Makanisa mahalia, ili kukutana na Kristo Yesu aliye hai na ambaye pia ni Mlango wa uzima. Rej, Yn 10:7.9. Mama Kanisa anaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini dhidi ya hofu na mashaka; ukosefu wa imani na furaha ya kweli; kwa kumsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu, ili Neno la Mungu liendelee na kutukuzwa. Rej. 2 The 3:1. Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa awasaidie Mababa wa Sinodi kuisikiliza sauti ya Roho Mtakatifu, ili hatimaye, kumwimbia Mungu sifa na utukufu, kwani Yeye ndiye chemchemi ya matumaini na wokovu wa waja wake.

Kardinali mteule Timothy Radcliffe, O.P., Uhuru wa ndani
Kardinali mteule Timothy Radcliffe, O.P., Uhuru wa ndani

Kwa upande wake, Kardinali mteule Timothy Radcliffe, O.P., katika tafakari yake amekazia kuhusu uhuru wa ndani, kama sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa, kwa sababu Mwenyezi Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema; yaani wale walioitwa kwa kusudi lake. Rej. Rum 8:28 na kwamba, neema ya Mungu hukamilisha asili ya binadamu, kwa sababu kama watoto wa Mungu; katika kufikiri na kutamani kwao; kwa uchafu na unyofu wa moyo, Roho Mtakatifu anatenda kazi ndani mwao; changamoto na mwaliko wa kufuata maongozi ya Roho Mtakatifu; kwa kufikiri, kuzungumza na kusikiliza bila woga, tayari kupokea matunda ya Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu kwani neema ya Mungu inatenda kazi ndani ya Kanisa. Mababa wa Sinodi wawe na uhuru wa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu; wawajibike kikamilifu katika maamuzi yao, huku wakiendelea kujenga na kudumisha umoja na ushirika wa watu wa Mungu katika ujumla wao!

Sinodi Misa
21 October 2024, 14:19