2024.10.17 Askofu Giuseppe Yang Yongqiang wa Jimbo la Hangzhou,na  Papa Francisko. 2024.10.17 Askofu Giuseppe Yang Yongqiang wa Jimbo la Hangzhou,na Papa Francisko. 

Maneno ya Maaskofu wa China katika Sinodi:tuko katika ushirika

Askofu Giuseppe Yang Yongqiang na Vincenzo Zhan Silu wamezungumza katika ukumbi wa Sinodi kwa kutoa salamu zao.

Andrea Tornielli

"Kanisa la China ni sawa na Kanisa Katoliki katika nchi zingine ulimwenguni: sisi ni wa imani moja, tunashiriki ubatizo sawa na sisi sote ni waaminifu kwa Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume." Kwa maneno haya, katika siku za hivi karibuni, Akofu Giuseppe Yang Yongqiang, wa Hangzhou, mji mkuu wa Zhejiang Nchini  China, alitoa salamu zake katika Sinodi. Ni mmoja wa wachungaji wawili kutoka China bara waliopo kwenye kazi inayoendelea mjini Vatican. Askofu Vincenzo Zhan Silu, wa Funing/Mindong katika jimbo la pwani la Fujian, anashiriki pamoja naye.  Hii ni kwa mara ya tatu kwa maaskofu wawili wa Jamhuri ya Watu wa China kushiriki katika Sinodi: ya awali ilifanyika mnamo mwaka 2018 na 2023 (Sinodi ya Vijana na kikao cha kwanza cha Sinodi ya Kisinodi).

Kabla ya kutiwa saini kwa mkataba wa muda kati ya Vatican na serikali ya China, uliotiwa saini mnamo Septemba 2018, hakukuwa na mchungaji kutoka China Bara aliyeweza kushiriki katika Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na Sinodi za Maaskofu zilizofuata. Askofu Yang Yongqiang, baada ya kukumbuka ushiriki huu katika ushirika na Kanisa la ulimwengu, alieleza: "Tunafuata roho ya kiinjili ya "Kuwa vitu vyote kwa watu wote", tunabadilika kikamilifu kwa jamii, tunaitumikia, tunashikamana ili kuondoka mwelekeo wa kudhalilisha Ukatoliki, na tunahubiri Habari Njema. Kanisa Katoliki nchini China limeanza mazungumzo ya dhati ya kutembeleana na jumuiya za kikatoliki duniani kote kwa kuzingatia misingi ya usawa, urafiki na kuheshimiana.

Tunafanya mabadilishano juu ya mada kama vile uinjilishaji na huduma ya kichungaji katika Kanisa, huduma za kijamii na masomo ya theolojia; tunashiriki kikamilifu katika mikutano ya kimataifa na shughuli za maombi ya dini kwa ajili ya amani; tuwe kama “nuru na chumvi” kwa ajili ya amani ya ulimwengu na uendelezaji wa jumuiya ambamo wanadamu wanaweza kufurahia hatima ya pamoja; hatimaye, tunakuza maendeleo na aina tofauti za mipango." Askofu alihitimisha kwa "kukaribisha jumuiya za Kikatoliki na makundi ya kidini kutoka nchi zote zinazotaka kutembelea Kanisa nchini China". Salamu za Askofu Zhan Silu zilijikita zaidi katika historia ya Ukristo nchini China, akikumbuka sura ya Mjesuit Matteo Ricci na "jaribio" lake la "kurekebisha Injili ya Kikristo juu ya mazoea tofauti ya maisha ya mwanadamu." Hata hivyo, baadaye, aliongeza, “kutambua kati ya tofauti za kiutamaduni na uhitaji wa kuhifadhi uhalisi wa imani ya Kikristo kumekuwa chanzo cha mkanganyiko kwa wamisionari nchini China. Mkanganyiko huu ulisababisha mabishano maarufu ya (Rites,) ambayo yalitokea katika Jimbo  langu mwenyewe, huko Mindong.

Kwa mtazamo wa kihistoria, moja ya sababu za kushindwa huku ni kwamba Kanisa lilipuuza tofauti na ukamilishano wa tamaduni za wanadamu."Kuwa Kanisa la Kisinodi lenye nia ya utume wa uinjilishaji - alisema Zhan Silu - inamaanisha kuheshimu na kusikiliza sauti za historia, tamaduni na mila tofauti katika safari ya kutafuta lengo kuu la mwanadamu, ambalo ni Mungu." Miongoni mwa mambo ambayo Kanisa la China linapaswa kushughulikia kwa mtazamo mpya, ni “jinsi ya kushughulikia changamoto ambazo ndoa za mseto zinapatikana katika elimu ya familia; au jinsi ya kukabiliana na sheria na kanuni za mitaa; au jinsi ya kutatua mkanganyiko uliopo kati ya watu wa kawaida wa imani maarufu na baadhi ya vipengele vya utamaduni wa jadi.” Kanisa katika wakati huu mpya limekabidhiwa kazi mpya ya utambuzi, hata kama sauti ya Roho Mtakatifu daima ni laini na ngumu kutofautisha. Kwa sababu hii, kujifunza kwa unyenyekevu kutokana na uzoefu wa kihistoria na wa sasa ni njia muhimu ya kuinjilisha, yaani, kutambua njia mpya ambayo Bwana anaonesha kwa Kanisa,"alihitimisha Askofu huyo.

Papa na maaskofu wa China
18 October 2024, 10:50