Mtakatifu Yosefu Allamano, Padre Na Mwanzilishi wa Shirika: Utakatifu na Umisionari
Na Padre Dietrich Pendawazima, IMC. – Morogoro, Tanzania.
Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wa Kitume “Gaudete et exsultate” yaani “Furahini na kushangilia, wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo” (Mt. 5:12) anasema Kristo Yesu anawaalika wote wanaoteseka au kudhulumiwa kwa ajili yake, kufurahi na kushangilia, kwani yeye ni chemchemi ya maisha na furaha ya kweli. Anataka waja wake kuwa kweli ni watakatifu, mwaliko na changamoto inayojionesha katika sehemu mbalimbali za Maandiko Matakatifu. Baba Mtakatifu anasema, lengo la wosia huu ni mwaliko wa kuwa watakatifu katika ulimwengu mamboleo; kwa kutambua vizingiti, changamoto na fursa ambazo zinaweza kutumiwa na waamini kufikia utakatifu wa maisha. Kristo Yesu anawaalika waja wake ili wawe watakatifu, watu wasiokuwa na hatia mbele zake katika upendo. (Rej. Ef. 1:4).
Baba Mtakatifu Francisko anasema, watakatifu ni watu wanaotia shime pamoja na kuwasindikiza waamini wenzao kama vyombo na mashuhuda wa imani na matumaini kama ilivyokuwa katika Agano la Kale; hata leo hii hawa ni watu wanaoweza kuwa ni ndugu, jamaa na marafiki; watu wanaosadaka maisha yao, mashuhuda wa upendo wa Kristo na wale wanaoendelea kujitosa kwa ajili ya umoja wa Kanisa. Hawa ni majirani wanaotangaza na kushuhudia utakatifu wa maisha katika uhalisia wa maisha ya kila siku pasi na makuu. Ni watu wanaoshuhudia unyenyekevu katika maisha, kiasi hata cha kuacha alama za mvuto na mashiko katika uekumene wa damu kama unavyofafanuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II. Wakristo wote wanahamasishwa kuwa watakatifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo Mtakatifu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata wewe unaitwa kuwa mtakatifu katika maisha yako kama mtu wa ndoa, maisha ya kuwekwa wakfu, mfanyakazi na mhudumu wa upendo kwa jirani zako!
Neema ya utakaso inaweza kuwasaidia waamini kuambata njia ya utakatifu, kwa kukumbatia Matunda ya Roho Mtakatifu. Waamini kwa njia ya maisha na ushuhuda wao, wasaidie kuyatakatifuza malimwengu kama vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu: kiroho na kimwili. Wakristo watambue kwamba, wanashiriki katika maisha na utume wa Kristo Yesu hapa duniani, kumbe, wanatumwa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao kadiri ya historia na changamoto za Kiinjili; daima kwa kuungana na Kristo Yesu katika Fumbo la maisha na utume wake, kielelezo makini cha ufunuo wa huruma ya Baba kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu! Utakatifu ni mchakato unaowawezesha waamini kuishi upendo katika utimilifu wake kadiri ya nguvu na mwanga wa Roho Mtakatifu.
Maisha ya kila mwamini yawe ni kielelezo cha utume kutoka kwa Kristo Yesu anayetaka kuwaletea waja wake mabadiliko katika maisha, licha ya udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu, daima wakijitahidi kuambata upendo wa Kristo katika maisha yao! Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna vitendo ambavyo vinatakatifuza watu, hasa pale waamini wanapojizatiti katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika misingi ya: haki, amani na upendo; maisha ya sala yanayomwilishwa katika huduma kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee anawataka waamini kujifungamanisha na tasaufi ya utume kama inavyodadavuliwa kwenye Waraka wake wa kitume, “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili”; tasaufi ya Ikolojia inayofumbatwa katika Waraka wake wa kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Tasaufi ya maisha ya familia imefafanuliwa kwenye Waraka wake wa kitume “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia.”
Waamini wajenge utamaduni na sanaa ya kukaa kimya mbele ya Mungu, ili waweze kusikia kile ambacho Mwenyezi Mungu anataka kuzungumza nao kutoka katika undani wa dhamiri zao nyofu! Moyo wa utakatifu upambe upweke wa maisha! Hakuna sababu ya kuogopa kuambata utakatifu wa maisha! Kama iliwezekana kwa Bakhita aliyetekwa nyara na hatimaye kuuzwa utumwani, lakini kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake, amekuwa mtakatifu, hii inaonesha kwamba, utakatifu ni jambo linalowezekana kabisa! Uinjilishaji mpya unafumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa kuwa chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa! Maafa makubwa yanayoweza kumkumba mwanadamu ni kushindwa kuwa mtakatifu!
Mwenyeheri Yosefu Allamano aliishi miaka 75 ya neema na ari kubwa ya kimisionari, bila mipaka, akiamini kwa dhati “kwanza utakatifu kisha umisionari” tunayemkumbuka kama Baba, mwalimu, mlezi wa Wakristo wasio na idadi duniani. Tarehe 21/01/1851 alizaliwa huko Castelnuovo d’Asti nchini Italia, tunaweza kusema wakati ule walitoka kijiji kimoja na Mtakatifu Don Yohane Bosco ambaye aliwahi kuwa mwalimu wake.Ni mtoto wa nne kati ya watano toka familia ya kikristo: wazazi wake baba Yosefu Allamano na mama Marianna Cafasso dada yake Mt. Yosefu Cafasso. Hatimaye alijiunga na seminari ya jimbo la Torino hadi tarehe 20/09/1873 alipadrishwa, na kutumwa seminarini kama mlezi msaidizi 1873-1876 na pia 1876-1880 akateuliwa kama mlezi wa kiroho na baadaye Oktoba 1880 akapewa jukumu la kuwa mkurugenzi wa Kanisa la Consolata (Torino – Italia) hadi alipofariki. Ikumbukwe akiwa katika majukumu hayo aliendelea na masomo hadi tarehe 30/07/1876 na hapo alitunukiwa shahada ya udaktari katika masomo ya Taalimungu na 12/06/1877 alipata cheti cha kuruhusiwa kufundisha.
Kwa muda mrefu zaidi ya miaka 40 alikuwa mchungaji mkuu wa Kanisa la Consolata, akiwa hapo aliweza kufanya mambo mengi, ukarabati wa Kanisa, utume uliotukuka na utayari wa hali ya juu katika kuwahudumia na kuwasikiliza watu mbalimbali. Alisukuma kushamili kwa Ibada ya Bikira Maria wa Consolata, Bikira Maria Mfariji. Mang’amuzi hayo hadi yalipelekea tarehe 29/01/1901 alianzisha shirika la wamisionari wa Consolata yaani mapadri na mabruda. Miaka kumi baadaye alianzisha Shirika la Masista Wamisionari wa Consolata. Tarehe 16/02/1926 alifariki dunia akiwa Torino kwenye Kanisa la Consolata wakiwepo wamisionari wake wapendwa mapadre, mabruda na masista akiwaachia wosia wa upendo na utume mwema. Na tarehe 07/10/1990 alitangazwa kuwa Mwenyeheri na Mtakatifu Yohane Paulo II na maadhimisho hayo kufanyika katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican Na sasa tunafurahi na kushangilia kwani Mwenyeheri Yosefu Allamano ataingizwa katika orodha ya watakatifu tarehe 20/10/2024, Dominika ya Kimisionari, siku aliyoidhamiria sana katika maisha yake.
Baba Mtakatifu Francisko aliidhinisha agizo hilo ambalo linahusisha mwanzilishi wa Wamisionari wa Consolata kwa muujiza wa kumponya mtu wa asili mzawa katika msitu wa Amazonia Brazil ambaye alishambuliwa na mnyama anayeitwa “Jaguar” aina ya chui. Huyu mtu alisaidiwa, miongoni mwa wengine na watawa sita na mmisionari wa Consolata, ambao kwa maombezi ya Mwenyeheri Yosefu Allamano waliweka nia moja na masalio yake wakaweka kando ya kitanda cha mtu aliyejeruhiwa. Mungu akajalia uponyaji kwa maombezi ya Mwenyeheri Allamano.
Katika kesha la kutangazwa watakatifu hao Dominika 20 Oktoba 2024 sambamba na Siku Kuu ya Kimisionari dunia, Radio Vatica imezungumza na Padre Erasto Mgalama, wa Shirika la Wamisionari wa Consolata (IMC):