Muhtasari wa Sinodi-Siku ya 15:Uwasilishaji wa hati ya mwisho

Katika mkutano na waandishi wa habari wa sinodi Jumatatu tarehe 21 Oktoba 2024,wasemaji wanaripoti kwamba rasimu ya Hati ya Mwisho imewasilishwa kwenye mkutano wa sinodi.

Na  Tiziana Campisi,Roberto Paglialonga na Angella Rwezaula – Vatican.

Rasimu ya Hati ya Mwisho imesambazwa Jumatatu tarehe 21 Oktoba 2024 kwa washiriki wote wa Sinodi. Akizungumza wakati wa mkutano wa kila siku katika Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Vatican, Dk. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa  Baraza la Kipapa la Mawasiliano na Rais wa Tume ya Sinodi ya Habari, alisema: "Tumefikia wakati muhimu."

Nyakati za maombi na mipango ya sinodi

Dk. Ruffini alieleza furaha waliyonayo washiriki wa Sinodi kufuatia na Misa ya Papa katika Uwanja wa Mtakatifu Petro siku ya Dominika Oktoba 20  ambapo watakatifu wapya 14 walitangazwa kuwa watakatifu. Tukio hili muhimu lilifanyika wakati wa Dominika ya Kisimisionari Ulimwenguni, kitovu cha safari ya Sinodi. Dk. Ruffini pia alitaja kipindi cha maombi kilichofanyika  alasiri Dominika 20 Oktoba, kilichowaleta pamoja wamisionari wa kidijitali mtandaoni, kama sehemu ya mpango wa Kanisa wa “Kusikiliza”, ulioakisiwa katika Instrumentum laboris yaani Kitendea Kazi. Siku ya Ijumaa Oktoba 25 alisema, saa 11:00 jioni katika Jumba la Mtakatifu  Calisto, tukio la "Sinodi ya Michezo", lililoandaliwa na Timu ya Mchezo ya wanariadha wa Vatican na Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu litafanyika.  Washiriki wengi wa Sinodi wamejiandikisha kwa ajili ya tukio hilo, ambalo litajumuisha majadiliano na wanariadha—wakimbizi, Wacheza Olimpiki Walemavu, na Washiriki wa Olimpiki—kuhusu mada za amani na kuhudumiana.

Uwasilishaji wa rasimu ya hati ya mwisho

Bi Sheila Pires, Katibu wa Tume ya Habari, alitoa muhtasari wa shughuli za Jumatatu 21 Oktoba akibainisha kwamba "sasa tuko katika Juma la mwisho wa Sinodi ya kisinodi." Siku ilianza kwa Ibada ya Misa Takatifu katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, ambapo Kardinali Mario Grech alisisitiza katika mahubiri yake kwamba Sinodi ionekane kuwa ni mwanzo mpya unaolenga kutangaza Neno la Mungu kwa watu wote. Baadaye, Ushiriki Mkuu uliunganika katika Ukumbi wa Paulo VI ambapo waliohudhuria ni  washiriki 35, kwa kulifunguliwa kwa tafakari ya Padre Timothy Radcliffe kuhusu mada za uhuru na wajibu. Kisha, rasimu ya Hati ya Mwisho iliwasilishwa na Kardinali Jean-Claude Hollerich. Ikifafanuliwa kuwa “maandishi ya muda,” yanahitaji usiri—si kwa sababu ya ukosefu wa uwazi bali kudumisha hali nzuri ya majadiliano. Kila mshiriki alipokea nakala ya rasimu, ambayo ni matokeo ya kazi ya ushirikiano. Rasimu hiyo, ilisisitizwa tena, "sio tu zao la majadiliano katika mkutano lakini inatokana na mchakato mzuri na inajumuisha kazi zote zilizofanywa kwa miaka mingi wakati wa awamu mbalimbali za safari ya sinodi." Bi Pires pia alibainisha kuwa "Wanahabari maalum na wataalam walifanya kazi kwa bidii ili kusikiliza kwa makini kile kilichosemwa na kuchunguza ripoti kutoka katika makundi madogo." Michango ya wataalimungu  ilikuwa "muhimu kwa waraka na kwa vikao."

Majadiliano ya alasiri katika vikundi vidogo

"Mchana wa Jumatatu Oktoba 21," Bi  Pires alisema, "washiriki watakusanyika katika vikundi vyao vidogo kwa ajili ya kubadilishana zawadi kiukweli, kama Kardinali Grech alivyosema, 'kushiriki changamoto, ndoto, mienendo ya ndani, na motisha mpya zilizojitokeza kutokana na kusoma maandishi.' Ni njia mpya ya kupata mafungo, labda isiyojulikana." Kwa hivyo, Jumatatu ilitolewa kwa maombi, kutafakari, na kushiriki rasimu ya hati ya mwisho. Bi Pires aliongeza kuwa kikao cha asubuhi kilifungwa kwa maombi kwa ajili ya Padre Mjesuit Marcelo Pérez, aliyeuawa Dominika 20 Oktoba 2024 huko Chiapas, Mexico, muda mfupi baada ya kuadhimisha Misa katika parokia yake huko Cuxtitali, kitongoji cha Mtakatifu Cristóbal de Las Casas.

Kardinali Zuppi:Mazungumzo"msingi kwa Kanisa lenyewe"

Katika mkutano huo, wazungumzaji walikuwa ni Kardinali Matteo Zuppi, rais wa Baraza la Maaskofu wa Italia(CEI), Padre Timothy Peter Joseph Radcliffe, mshauri wa mambo ya kiroho wa Sinodi (ambaye atawekwa wadhifa wa  kuwa Kardinali tarehe 7 Desemba). Sista Nathalie Becquart, Katibu Msaidizi wa Sekretarieti Kuu ya Sinodi, na Monsinyo Manuel Nin Güell, mjumbe wa  kitume kwa Wakatoliki wa Byzantine huko Ugiriki. Kwa upande wa Kardinali Zuppi alitafakari juu ya uzoefu wa mazungumzo katika sinodi yote, akielezea kama "sio muhimu, lakini msingi wa Kanisa lenyewe." Alionesha meza ambazo washiriki huketi kuzungumza, kusikiliza, na kukutana katika mchakato ambao, alisisitiza, daima ni wa kiroho.

Padre Radcliffe:Hati ya mwisho itakuwa na "picha za Ufalme"

Padre Radcliffe alitafakari juu ya safari ya upyaisho wa Kanisa inayoendelea hivi sasa, safari ambayo itajitokeza katika hati ya mwisho.Alisisitiza kuwa waraka huo haupaswi kuonekana kuwa ni mahali pa maamuzi au kauli za kunyakua vichwa vya habari. Mbele ya mgawanyiko wa jamii, vita, na nyakati ngumu ambazo ulimwengu unastahimili, Kanisa lina wito maalum: kuwa ishara ya Kristo, ishara ya amani, na kubaki katika ushirika na Kristo. Kupitia Sinodi hii, Padre Radcliffe alisema, njia mpya ya kuliwazia Kanisa inajitokeza, na hati ya mwisho itaonesha picha hizo, kama vile Yesu alitumia mifano kutangaza Ufalme.

Sr Becquart: Sinodi na uekumene

Sr Nathalie Becquart, Katibu Msaidizi wa Sekretarieti Kuu ya Sinodi, alishirikisha ufahamu kuhusu hali ya kidugu miongoni mwa wajumbe wa kiekumene. Yeye anashiriki katika Tume ya Sinodi ya Uekumene. Kwa njia hiyo “Sinodi inatupatia sura mpya ya kuwa Kanisa, alisema, akimaanisha sura ya Papa ameketi kati ya washiriki, akisikiliza, na pia picha kutoka katika ibada ya maombi ya kiekumene, ambapo washiriki walisali pamoja, kukumbuka kifo cha imani cha Mtakatifu Petro. Sr alisema, hii ilifungua awamu mpya ya mahusiano ya kiekumene na umoja wa Kikristo, kwani Sinodi hii inatanguliza njia mpya ya kuelewa utekelezaji wa ukuu wa upapa na umoja wa maaskofu na watu wote wa Mungu.

Wakatoliki wa Mashariki huko Ugiriki

Sinodi inatoa fursa ya uelewa wa kina zaidi, alifafanua Askofu Manuel Nin Güell, wa Kanisa la Kitume la Wakatoliki wa Ibada ya  Byzantine nchini Ugiriki, ambaye anaongoza jumuiya ndogo iliyoanzishwa takriban karne moja iliyopita. Jumuiya hii ilianzishwa wakati wakimbizi wengi wa Kigiriki waliofika Athene kufuatia na Vita vya Kigiriki na Kituruki. Upatriaki huo unajumuisha parokia mbili: moja ni Kanisa kuu huko Athene, na nyingine iko karibu kilomita 500 kaskazini, karibu na Thessaloniki, huko Yannitsa. Kuna makuhani saba—Wagiriki wawili, Mslovaki mmoja, na Mkaldayo mmoja. Jumuiya tatu zza sehemu ya Upatriaki ni pamoja na Wakatoliki wa Ugiriki, Wakatoliki wa Kiukreni ambao walifika yapata miaka 28 iliyopita baada ya kuanguka kwa Ukomunisti huko Ukraine (na hivi karibuni zaidi, kutokana na vita), na Wakatoliki wa Wakaldayo, ambao ni Wakristo wa Iraqi wa mapokeo ya Mashariki ya Siria. Kanisa hili  pia inaendesha shirika la Caritas linalofanya kazi na Wakristo wa Kiorthodox na Waislamu, na ina msingi kwa watu binafsi wenye tawahudi. Askofu Nin alisema kwamba Eneo la Upatriaki  huko Ugiriki ni Kanisa la Kisheria ( sui iuris) ndani ya mapokeo ya Kikatoliki. Sio kila mtu anafahamu hilo, na Sinodi imetoa fursa ya kufahamiana na nafasi ya Makanisa Katoliki ya Mashariki, ambayo yanashiriki liturujia, taalimungu, kiroho, na taaluma za kisheria kama Makanisa dada yao ya Kiorthodox.

Ufafanuzi wa Kardinali Fernandez kuhusu ushemasi wa kike

Tarehe 21 Oktoba 2024, Kardinali Fernández, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, alisisitiza wakati wa mkutano mkuu wa Sinodi kwamba Papa anahisi suala la mashemasi wanawake bado haliko tayari kushughulikiwa. Hata hivyo, mjadala juu ya majukumu ya wanawake katika Kanisa ulikuwa lengo kuu la kikao cha kuhitimisha cha muhtasari huo. Padre Radcliffe aliwataka watu wasizingatie kuwekwa wakfu katika hilo  pekee bali wazingatie pia nyadhifa za juu yake ambazo wanawake wameshikilia katika historia kama Waimu wa Kanisa. Iwapo tutapunguza kila kitu kuwekwa wakfu, alisema, tuna hatari ya kutumbukia katika mawazo ya ukleri sana.

Sr. Becquart alisisitiza hoja hizi, akisisitiza kwamba wanawake tayari wana vyeo vya juu katika Kanisa, kama vile marais wa vyuo vikuu vya Kikatoliki, viongozi wa mashirika kama Caritas, au wakuu wa sehemu ndani ya Mabaraza ya kipapa ya Maaskofu. Alieleza kuwa kuna njia nyingi za kukuza uongozi wa wanawake, na maaskofu wengi sasa wanawateua wanawake kuwa wajumbe wa majimbo makuu, majimbo, na  kuwapa nafasi katika utawala. Sr Becquart aliongeza kuwa vikwazo vya kijamii na kiutamaduni bado vipo kwa sababu Kanisa ni sehemu ya jamii. Kwa mfano, alisema, wakati akizungumza na maaskofu wa Kianglikani, mara nyingi ni wazi kwamba michango ya mwanamume katika mazingira ya Kanisa inapewa uzito zaidi kuliko mwanamke, hata wakati wanawake wamewekwa wakfu. Kwa hivyo, ubadilishaji wa kweli wa mawazo unahitajika, na itachukua muda. Tunarithi mawazo sio tu kutoka katika Kanisa bali kutoka katika jamii tunamoishi, alibainisha Becquart.

21 October 2024, 16:44