Tafuta

Muhtasari wa Sinodi -Siku ya 6:Euro 62,000 zimekusanywa kwa ajili ya Parokia ya Gaza

Katika taarifa iliyotolewa kwa wanahabari ya siku ya 6 kuhusu Sinodi inayoendelea ilishuhudiwa ushiriki wa makardinali 3 kati ya 21 waliochaguliwa hivi karibuni na Papa na kueleza kwamba washiriki wa Mkutano walichanga kiasi cha euro 62,000 kwa ajili ya Parokia katoliki ya Familia Takatifu huko Gaza.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Jumla ya euro 62,000 zilikusanywa katika Sinodi tarehe 7 Oktoba 2024  kwa ajili ya wahanga wa vita huko Gaza. Hayo yalitangazwa Jumanne tarehe 8 Oktoba 2024 na Dk. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa  Baraza la Kipapa la Mawasiliano na Rais wa Tume ya Habari ya Sinodi, wakati wa mkutano wa kila siku na waandishi wa habari kuhusu shughuli za Sinodi kwenye Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Vatican. Pia waliohudhuria mkutano wa waandishi wa habari, ulioratibiwa na Naibu Msemaji Mkuu wa Vyombo vya habari Bi Cristiane Murray, miongoni mwao walikuwa ni Makardinali 3  kati ya Makardinali 21 waliochaguliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko aliowatangaza Dominika tarehe 6 Oktoba 2024: Askofu Mkuu Ignace Bessi Dogbo wa Jimbo Kuu la Abidjan, Ivory Coast, Askofu Mkuu Tarcisio Isao Kikuchi wa Jimbo Kuu la Tokyo Japan, na Askofu Mkuu Jaime Spengler wa  Jimbo Kuu la Porto Alegre nchini Brazil.

Fedha tayari zimetumwa Gaza

Dk Ruffini aliripoti kwamba kiasi kilichokusanywa kilitangazwa na Kardinali Konrad Krajewski, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Upendo, kwamba Euro 32, 000 zilichangwa na washiriki katika Sinodi, na euro zingine 30,000 zilitolewa na Baraza la Kipapa la Upendo. Kwa njia hiyo Jumla ya euro 62,000, Kardinali alisema, zilipelekwa kupitia Ofisi ya Ubalozi wa Vatican huko  Yerusalemu na tayari ziko mikononi mwa Paroko Padre Gabriel Romanelli wa Parokia ya Kanisa la Familia Takatifu huko Gaza. Kulingana na Dk. Ruffini, washiriki katika Mkutano huo  walijibu kwa shangwe kwa  njia ya video ya shukrani (iliyooneshwa kwenye Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Vatican) iliyotumwa na Padre  wa Argentina.

Umuhimu wa kuanzishwa kwa Kikristo

Dk Ruffini pia aliripoti kwamba siku ya Jumatatu tarehe 7 Oktoba 2024, Kardinali Grech alitangaza katika mkutano huo kwamba Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha limewateua wanachama wapya ishirini wa Baraza la Kimataifa la Ushauri la Vijana (IYAB), ambalo lilianzishwa baada ya Sinodi ya mnamo 2018. Kwa niaba ya washiriki wote wa Sinodi, Katibu Mkuu aliwatakia kila la heri “vijana waliojitolea kulitumikia Kanisa. Sehemu ya kati ya Jumanne asubuhi tarehe 8 Oktoba 2024  ilikuwa na  watu 350 katika Ukumbi wa Paulo VI  ambapo ilijitolea kuwachagua wanachama 7 kati ya 14 wa Tume ya kuandaa Hati ya Mwisho. Kabla ya upigaji kura, Katibu wake, Monsinyo Riccardo Battocchio, aliwakumbusha kila mtu kwamba Tume haitayarishi Hati ya Mwisho bali inasimamia mpango wa kazi. Baada ya kura, Dk. Ruffini aliendelea, kueleza kuwa kulikuwa na ripoti kutoka katika  meza za vikundi kulingana na  lugha, ambao ni upya wa mkutano huo. Hasa, waliabarishwa “umuhimu wa kuanzishwa kwa Kikristo, na uhusiano katika kuunda Kanisa la kisinodi zaidi, na ubadilishaji muhimu wa sinodi na uhusiano. Uhusiano kati ya karama na huduma pia ulisisitizwa na washiriki walitafakari juu ya jinsi ya kuepuka ubaridi wa kikasisi, jukumu muhimu la maisha ya kuwekwa wakfu, huduma ya kusikiliza, utambuzi tofauti kuhusu huduma zinazohusiana na utume na mazingira ya kiutamaduni na ya mahalia.”

Ushemasi, upendo na utume

Sheila Pires, Katibu wa Tume ya Habari, kisha aliripoti kwamba wakati wa majadiliano ya wazi wasemaji 18 walitoa michango yao juu ya mada ya uanzishaji wa Kikristo. Wengi wao walionesha hitaji la kuweka uhusiano na ubadilishaji wa uhusiano katika kituo hicho, kama ambavyo tayari kimefanywa na watoa habari za vikundi vya meza za mduara. Baadhi, alisema, walionesha hitaji la kuponya uhusiano uliojeruhiwa na kashfa katika Kanisa, kuanzia na dhuluma, wakisisitiza umuhimu wa uaminifu ili kuimarisha njia ya sinodi. Wengine walipendekeza uchunguzi wa kina wa ushemasi ili kufanya upya Kanisa, au walielekeza kwenye Kanisa la Watu wa Mungu na umuhimu wa mapendo na utume. Walisisitiza kwamba upendo kwa maskini huzaliwa kutokana na Ekaristi na kwamba tunapaswa kuwajali kama Injili inavyofundisha, hasa kwa wale waliotengwa, kukataliwa, na ambao wakati mwingine wanahisi kutengwa hata na Kanisa,” alieleza Bi. Pires

Kusindikiza waliobatizwa hivi karibuni

Wazungumzaji pia waliona kwamba katika ulimwengu usio na malimwengu, mchakato wa kuanzishwa ukristo unazidi kuwa muhimu zaidi na zaidi. Ili kuwa mashuhuda wa Injili, walisema, ni lazima tuwe manabii, na mchakato wa malezi ya imani unahitajika tangu umri mdogo; ukihusisha jumuiya nzima. Aidha walibainisha kuwa mkutano huo lazima ujadili ushiriki wa wanawake katika uongozi wa Kanisa. Zaidi ya hayo, mada ya msamaha iliyohusishwa na upendo wa Kristo ilishughulikiwa, na wazungumzaji waliobainisha kwamba hapawezi kuwaanzisha ukristo bila jumuiya. Kwa sababu hiyo, wengine waliomba kujitolea zaidi kusindikiza wale waliobatizwa hivi karibuni.” Hatimaye, Bi. Pires alieleza, baadhi ya wazungumzaji walisema kwamba Instrumentum laboris, hati ya kitendea kazi ya Sinodi, haitoi umakini wa kutosha kwa baadhi ya ukweli na harakati za kikanisa, ambazo umuhimu wake unapaswa kutambuliwa.”  Waliomba tena kwamba nyaraka za Kanisa zikiwemo za Sinodi, ziandikwe kwa lugha inayoeleweka na  inayoweza kueleweka kwa  kila mtu.

Kubadilisha namna ya kuliona Kanisa

Akirejea moja ya mada kuu za kazi ya Sinodi, Kardinali Mteule Ignace Bessi Dogbo alijikita katika Sakramenti ya Ubatizo. "Shukrani kwa hilo, tunafananishwa na Kristo, na sote tunaweza kujitambua kuwa watoto wa Mungu na ndugu katika Kristo. Hii inaruhusu kila mmoja wetu, kwa upande wake, kuona na kupata ndani ya wengine utu na uso wa Yesu.” Alifafanua ulinganifu kati ya kile kinachotokea katika Kanisa la Ulimwengu na kile kinachotokea majuma haya  katika mkutano wa  sinodi, ambapo Askofu Mkuu wa Abidjan alisisitiza umuhimu wa kusikilizana na mahusiano yanayopatikana katika Ukumbi wa Paulo VI, katika mazingira ya ajabu ya ushirika na kushirikiana. "Tunafahamu kwamba hatubadilishi Kanisa kimwili, lakini tuko katika mchakato ambao utasababisha kurekebisha njia ya kuishi Kanisa katika siku za usoni, kwamba uwezo wa kusikiliza  unatokana na kutambuana, ambayo inaruhusu kila mtu kuwa na nafasi yake katika maisha ya jumuiya ya kikanisa.”

Kujenga msingi wa pamoja katika njia ya sinodi

Kardinali mteule Kikuchi pia alizungumza kuhusu kusikiliza, akizingatia uzoefu wa Kanisa nchini Japani. "Kati ya Vikao viwili vya Sinodi, katika nchi yangu, tuliweka misingi ya sinodi ya kweli," Askofu Mkuu wa Tokyo alisema. Majimbo  15 yalifanya mkutano wa kitaifa wa mapadre, waamini, wahudumu wa kujitolea na wahudumu walioshiriki katika shughuli mbalimbali, “ambapo mazungumzo yetu katika Roho, tunayoyafanya pia hapa Vatican katika siku hizi za kazi za Sinodi yalitiwa nguvu.” Lengo la pamoja, ni kutafuta na kujenga msingi wa pamoja katika njia ya sinodi,” Kardinali mteule Kikuchi, ambaye amekuwa rais wa Caritas Internationalis tangu Mei 2023, alihitimisha

Mshangao kwa kuchaguliwa kuwa Kardinali

Askofu Mkuu Jaime Spengler wa Brazil alizungumza juu ya mshangao wake wa kuchaguliwa kuwa kardinali, akichochewa na swali kutoka kwa mshirika wake Christiane Murray. "Nilikuwa namalizia kusoma kitabu kizuri cha Carlo Maria Martini, kilichoitwa Sequela Christi, simu yangu ilipoanza kuita na kutetemeka. Nilikuwa nikipokea jumbe nyingi za pongezi, lakini sikujua kwa nini. Kisha, marafiki wengi walioniandikia walinishauri nitazama sala ya  Malaika wa  Bwana ya Papa, kwa sababu alikuwa akinitaja, na hapo ndipo nilipoelewa,” alisema. “Kwa kawaida ilikuwa ni furaha kubwa, katika kufahamu kwamba kuwa Kardinali maana yake ni kutumikia Papa na Kanisa. Ninamshukuru Baba Mtakatifu kwa nafasi ya kushirikiana katika wakati mgumu kama huu katika historia ya ulimwengu, ubinadamu, na jumuiya ya kikanisa yenyewe."

Utawala wa Sinodi

Makardinali hao wapya watatu walijibu maswali kutoka kwa wanahabari. Alipoulizwa kuhusu mtindo wa utawala ambao Sinodi inapaswa kufuata, Askofu Mkuu Spengler alionesha utata wa swali katika ulimwengu ulioathiriwa na mgogoro wa demokrasia, ambapo, kwa hiyo, swali la mamlaka linakuwa muhimu. Askofu Mkuu wa Porto Alegre alikumbuka maneno ya Papa Paulo VI, ambaye alieleza jinsi wanadamu huwasikiliza mashuhuda kwa uangalifu zaidi kuliko waalimu, na ikiwa wanawasikiliza walimu, ni kwa sababu wao ni mashuhuda pia.”Kwa hiyo, alisema, nguvu hazitokani na sababu ya kisosholojia bali kutokana na ushuhuda wa kimaadili, kiadili, na kidini.” Dhana hii iliungwa mkono na Kardinali mteule Kikuchi, ambaye alisisitiza haja ya kuondokana na mtindo wa "piramidi" kuelekea "sinodi".

Kardinali Mteule Kikuchi wa Jimbo Kuu la Tokyo
Kardinali Mteule Kikuchi wa Jimbo Kuu la Tokyo

Hata hivyo, hii lazima isitokeze katika kufanya maamuzi kwa kuzingatia tu makubaliano. Lazima tuwe na uhakika tunaelewa sinodi kwa njia sawa,"alieleza Askofu Mkuu wa Tokyo. Hata kupitia utambuzi wa kawaida, bado kuna mtu ambaye lazima afanye maamuzi ya mwisho. Makardinali 3 wateule kutoka sehemu tatu tofauti za dunia, waliulizwa jinsi gani ya kutambua sifa bainifu ya jumuiya zao. Wote walikubaliana kusindikiza na kanuni bora ya sinodi ya kubadilishana zawadi. Kardinali mteule Kikuchi alibainisha kwamba hapo awali ilitokea Magharibi hadi Mashariki, kutoka nchi zilizoendelea hadi zile zinazoendelea, lakini sasa kumekuwa na mabadiliko ya dhana ambapo pembezoni zilizotajwa na Papa Francisko mara kadhaa  zimekuwa sehemu muhimu za kitovu hivyo kuliko hapo awali  kwa bara la Ulaya.

Kardinali Mteule Dogbo,Askofu Mkuu wa Abdjan
Kardinali Mteule Dogbo,Askofu Mkuu wa Abdjan

Kardinali mteule Bessi Dogbo, kwa upande wake, alisisitiza utajiri wa kiroho wa majimbo ya Afrika, ambapo imani inaishi kwa furaha. Alishiriki sha jinsi gani  baada ya kusikia kuchaguliwa kwake kama Kardinali, Jumuiya ya kijiji chake waliingia mitaani na bendi ya ndani ilicheza na kusherehekea. "Afrika lazima ishiriki furaha hii rahisi ya watu maskini, wanyenyekevu ambao wanafurahi na vitu vidogo," Askofu Mkuu wa Ivory Coast alisema. Askofu Mkuu Spengler aliakisi  mchango wa wahamiaji wa "Wajerumani, Kiitaliano, Kipolandi, Kiukreni na Kijapani", miongoni mwa wengine, katika uinjilishaji wa Amerika ya Kusini. Mara nyingi "walidanganywa, waliteseka, lakini walikuwa na ubora mzuri sana wa kufanya uamuzi," alieleza

Dhana ya ibada maalum kwa Amazonia

Askofu Mkuu wa Porto Alegre pia alijibu baadhi ya maswali kuhusu Amazonia na uwezekano wa kuunda ibada maalum kwa Jumuiya za kiasili ambapo miezi, hata miaka hupita bila maadhimisho ya  Ekaristi. Ndani ya Baraza la Maaskofu la Amerika Kusini (CELAM), ambalo yeye ni rais, makundi yanafanyia kazi uwezekano wa muungano huo. Kando ya dhana hii ni wazo la kueneza"kwa ibada ya kiutamaduni ya Kirumi kati ya wakazi wa eneo hilo. Kardinali mteule Spengler alikumbuka hadhi ya waamini wa kiasili katika kutekeleza kazi zao za kijadi. "Thamani ambayo wakati mwingine hatuioni tena katika Misa zetu wenyewe, haijalishi ni za dhati kiasi gani."

Kardinali Mteule Spengler
Kardinali Mteule Spengler

Kulikuwa pia na swali kuhusu mabadiliko ya hali ya tabianchi na uharibifu wa hivi majuzi, mkubwa uliosababishwa na mafuriko huko Rio Grande do Sul, janga la asili mbaya zaidi katika historia yake. Mnamo 2024, moto katika nchi ya Amerika Kusini uliongezeka kwa 76%, ukiashiria idadi kubwa zaidi katika miaka 14, huku biashara ya kilimo ikichunguzwa. Kulingana na Askofu Mkuu Spengler, kati ya “mahusiano” mbalimbali yaliyochambuliwa na Sinodi, ni lazima umakini mkubwa utolewe kwa uhusiano na “nyumba yetu ya pamoja.” Mawazo haya, yanapita zaidi ya tishio kwa maisha ya mwanadamu na ynachukua mwelekeo muhimu zaidi wakati wa kuzingatia sayari kama uumbaji wa Mungu.

Suala la useja wa kipadre

Hatimaye, Askofu Mkuu wa Brazil aliulizwa kuhusu suala nyeti  la useja wa kipadre. Kwa kutumia uzoefu wa ushemasi wa kudumu, Kardinali mteule, alisema kwamba "pengine, katika siku zijazo, wanaume hawa wanaweza kuwekwa wakfu  wa kikuhani  kwa ajili ya Jumuiya maalum." Njia ya mbele?  "Sijui, lakini tunaweza kuishughulikia kwa kuzingatia mambo ya kitaalimungu pamoja na alama za nyakati," alihitimisha.

Mhutasari wa kikao cha 6 cha Sinodi inayoendelea

 

09 October 2024, 11:26