Papa amekutana na Rais wa Liberia Bwana Nyuma Boakai
Vatican News
Ijumaa tarehe 18 Oktoba 2024, Baba Mtakatifu Francisko amekutana katika Jumba la Kitume na Rais wa Jamhuri ya Liberia, Mheshimiwa Joseph Nyuma Boakai Sr. Na baadaye Rais huyo alikutana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican akiambatana na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu wa Mahusiano na Mataifa na Mashirika ya Kimataifa.
Wakati wa mazungumzo ya dhati katika Sekretarieti yaVatican, uhusiano mzuri wa Vatican na Liberia uliibuliwa, pamoja na ushirikiano na Kanisa Katoliki katika nyanja za elimu na afya, na baadhi ya masuala ya hali ya kijamii na kiuchumi ya nchi ilijadiliwa.
Hayo yote yameelezwa Msemaji Mkuu wa Vyombo vya Habari Vatican akibainisha kuwa Mazungumzo yaliendelea kwa kubadilishana maoni juu ya mambo ya sasa ya kimataifa, kwa kuzingatia hasa hali ya kikanda na matukio ya uhamaji.
Zawadi
Wakati wa kubadilishana zawadi, Papa Fransisko alimpa rais kazi ya shaba inayoonesha njiwa aliyebeba tawi la mzeituni, yenye maandishi “Kuweni wajumbe wa amani, pamoja na nakala ya Ujumbe wa Amani wa mwaka huu 2024 na wingi wa nyaraka za kipapa.