2024.06.04 Wakati wa maadhimishi ya Siku Kuu ya Mashahidi wa Uganda 2024 2024.06.04 Wakati wa maadhimishi ya Siku Kuu ya Mashahidi wa Uganda 2024 

Salamu za Papa Francisko katika miaka 60 ya kutangazwa mashahidi wa Uganda

Ni miaka 60 tangu kutangazwa kwa Mashahidi wa Uganda waliotangazwa na Mtakatifu Papa Paulo VI tarehe 18 Oktoba 1964 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.Katika kumbukizi,Ibada ya misa Takatifu ilifanyika tarehe 19 Oktoba 2024 kwa kuongozwa na Kardinali Turkson kwa niaba ya Papa.Dominika 20 Oktoba Papa alikumbusha tukio hilo baada ya misa ya kutangaza Watakatifu 14.

Na Angella Rwezaula na– Vatican

Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 20 Oktoba 2024 katika fursa ya maadhimisho ya kuwatangaza Watakatifu, wapya 14 wa Kanisa, sambamba na Mama Kanisa kuadhimisha Siku ya 98 ya Kimisionari Ulimwenguni, mara baada ya misa Takatifu pamoja na salamu nyingine alisema: "Ninasalimia kundi kubwa la mahujaji wa Uganda, pamoja na Makamu Rais wa nchi hiyo, ambao wamekuja kwa ajili ya kuadhimisha miaka 60 tangu kutangazwa kuwa watakatifu Mashahidi wa Uganda."

Namugongo Uganda
Namugongo Uganda

Kundi hili lilionekana katika Uwanja wa Mtakatifu Petro lakini pia hata katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican Jumamosi asubuhi, majaira ya saa 4.00 za ulaya,  tarehe 19 Oktoba 2024 katika maadhimisho ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Kansela wa Taasisi ya Kipapa ya Elimu ya Sayansi na Taasisi ya Elimu ya Sayansi ya Kijamii, Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Kikristo, na Mjumbe Maalum wa Papa Francisko katika siku hiyo, wakiwemo maaskofu, mapadre, watawa na kwa ujumla Jumuiya nzima nchini Italia na wale waliotoka nchini Uganda, ambapo misa hiyo ilikuwa ni ya kiutamaduni kweli!

Kardinali Turkson:kuweni na msukumo wa mashihidi wa Uganda

Katika mahubiri ya Kardinali Turkson, aliwataka Waafrika wote kupata msukumo kutoka kwa Mashahidi wa Uganda waliotangazwa kuwa watakatifu miaka 60 iliyopita, ili kujenga mustakabali mwema unaosimikwa katika imani, uadilifu na uwazi. Kardinali Turkson aliwasifu pia wafiadini kama "Waafrika wa kweli waliobadilishwa na Injili kuwa wanafunzi wa Yesu  wanaostahili." Ka upande wake alisisitiza umuhimu wao katika kuunda utambulisho wa Kikristo wa Afrika. "Mashahidi wa Uganda wanatufundisha masomo muhimu: imani, uadilifu, uwazi, na utawala na ushahidi wao unatutia moyo kujenga mustakabali bora wa ardhi na watu wetu.” Kardinali Turkson aidha alaakisi juu ya ujana wa mashahidi, huku akibainisha kwamba Karoli Lwanga na wenzake walikuwa vijana wazima ambao walijumuisha maadili ya Injili. Alisema "jambo hili linawapatia changamoto vijana wa kisasa kujihusisha tena na imani. Tuwe mafundi wa matumaini, tukikumbatia maadili ya injili na kukuza Afrika isiyo na ufisadi,” alisema.

Balozi wa Vatican nchini Uganda,Askofu Mtaafu Wamala& Askofu Mkuu Ssemwongerere

Miongoni mwa makardinali, maaskofu wakuu na maaskofu, kulikuwa na Balozi wa Vatican nchini Uganda, Askofu Mkuu Luigi Bianco ambaye aliwafafanua  Mashahidi wa Uganda kama “mfano wa ajabu wa kujitolea na uaminifu kwa Bwana, mifano ya imani na matumaini, na mashahidi wa kweli  na ushirika. Ushahidi wao, ni wito kwa wote kuwa vinara wa matumaini na vyombo vya amani, pamoja na wakuzaji na watetezi wa utu uliopewa na Mungu kwa kila binadamu.” Kwa Upande wa Askofu Mkuu Mstaafu wa Kampala, Kardinali Emmanuel  Wamala, aliwasifu Wafiadini kama "mashujaa wa Uganda, mifano na washauri wa imani ya Kikatoliki." Na alitoa "shukrani nyingi kwa wale waliochangia kutangazwa kwao kuwa watakatifu." kwa upande wa Askofu Mkuu, Paul Ssemwogerere wa Jimbo Kuu la Kampala Uganda, alisisitiza "ushujaa na kujitolea kwa Mashahidi."

Pongezi kutoka kwa Rais Museveni, Uganda

Katika hotuba iliyotolewa kwa niaba ya rais Yoweri Museveni, wa Jamhuri ya Uganda, Naibu Spika wa Bunge,  Thomas Tayebwa, alipongeza matokeo ya Ukristo kwa Uganda wakati wa kuadhimisha miaka 60 tangu kutangazwa kwa Mashahidi wa Uganda. Rais Museveni aliakisi "Ukristo wa kuongeza thamani ulioletwa Uganda, ukianzisha maarifa ya kisayansi, elimu, na maadili ya kijamii. Rais alibainisha kuwa watu wa asili wa Uganda tayari wanaamini katika Mungu mmoja lakini Ukristo uliboresha uelewa huu. Kadhalika aliwasifu wahubiri wa Kikristo kwa kuanzisha ujuzi wa kisayansi kutoka Ulaya, kupunguza mizigo ya magonjwa." Katika ujumbe huo kutoka Uganda, Naibu Spika aliambatana na Bi Justine Kasule Lumumba, Waziri wa Fedha wa Nchi, Bwana Henry Musasizi, na wabunge Sarah Opendi, Joseph Ssewungu, na Herbert Ariko aliyekuwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Mhe. Mathias Mpuuga pia alijiunga na ukumbusho uliowakumbuka mashahidi wa Uganda waliotangazwa watakatifu na Mtakatifu Papa Paulo VI mwaka 1964.

Mashahidi wa Uganda ni wasimamizi wa Bara la Afrika

Leo, Mashahidi wa Uganda wanaheshimiwa kama watakatifu walinzi wa Afrika, wakichochea vizazi kwa ujasiri na imani yao. Urithi wao unaenea zaidi ya Uganda, ikiashiria matumaini na uthabiti kwa Wakristo wanaoteswa  ulimwenguni kote. Madhabahu ya Namugongo huko  Uganda, yamekuwa mahali pa kuhiji, na kuvutia mamilioni ya watu kila mwaka.

Ziara ya Kitume ya Papa Francisko 2015

Kipawa cha Roho Mtakatifu ni zawadi inayotolewa kushirikishwa", hata katika kifo cha kishahidi. Kwa maneno haya, tarehe 28 Novemba 2015, akiwa katika ziara yake ya XI ya kitume, Baba Mtakatifu Francisko nchini Uganda alikumbusha kujitoa mhanga kwa Mtakatifu Karoli Lwanga na wenzake katika mahubiri ya Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Madhabahu ya  Mashahidi wa Uganda wa Namugongo kilomita chache kutoka Kampala, Uganda,  Papa Francisko aliomba, katika hafla hiyo, pia kuwakumbuka mashahidi wa Kianglikani, "ambao kifo chao kwa ajili ya Kristo kinatoa ushuhuda wa uekumene wa damu. Kisha mwaliko ulikuwa kwa waamini wote kupokea na kuthamini urithi wa mashahidi wa Uganda kwa utimilifu wake, bila kuifanya "kito cha makumbusho."

Wakati wa misa Papa huko Uganda 2015
Wakati wa misa Papa huko Uganda 2015

Baba Mtakatifu alisema: ” Wapendwa kaka na dada, huu ndio urithi mliopokea kutoka kwa Mashahidi wa Uganda: maisha yaliyo na alama ya uwezo wa Roho Mtakatifu, maisha ambayo hata sasa yanashuhudia nguvu inayobadilisha ya Injili ya Yesu Kristo. Urithi huu hauwezi kupitishwa kwa kumbukumbu ya muda au kwa kuuhifadhi kwenye jumba la makumbusho kana kwamba ni kito cha thamani. Kiukweli tunamheshimu, na tunawaheshimu Watakatifu wote, tunapotoa ushuhuda wao kwa Kristo katika nyumba zetu na kwa majirani zetu, katika sehemu zetu za kazi na katika mashirika ya kiraia, iwe tunasalia katika nyumba zetu au tukienda kwenye kona ya mbali zaidi ya ulimwengu.”

21 October 2024, 13:36