Askofu Jovitus Francis Mwijage, Rais mpya wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari Nchini Tanzania. Askofu Jovitus Francis Mwijage, Rais mpya wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari Nchini Tanzania. 

Ujumbe Mahususi Kutoka Kwa Rais Mpya wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari Tanzania

Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari nchini Tanzania katika ujumbe wake mahususi kwa watu wa Mungu anazungumzia kuhusu umuhimu wa kuyafahamu vema Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari, Nafasi ya Sala katika Mashirika ya Kipapa; Kukuza na kustawisha moyo wa Ukarimu; Ushiriki hai wa Maadhimisho ya Siku maalum zihususo utume wa Mashirika ya Kipapa; Dominika ya Kimisionari, Dominika ya Miito, Sikukuu ya Watoto Mashuhuda na Ushirikiano!

Na Askofu Jovitus Francis Mwijage, - Dar es Salaam, Tanzania.

Kama inavyokaririwa katika Mwongozo (Statutes), Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari, yanaakisi/yanabeba sura mbili, yaani, yako chini ya Baba Mtakatifu Mwenyewe kwa namna ya pekee kabisa, na wakati huo huo yako chini ya dhamana ya Maaskofu (Na.16-17). Ndio maana, kadiri ya muundo wa Uongozi kwa ngazi ya Taifa, huwepo Askofu ambaye anapewa dhamana na Maaskofu wenzake ili kuyasimamia katika ngazi ya Taifa, na katika ngazi ya kijimbo yako chini ya usimamizi/uangalizi wa Askofu Jimbo. Ni katika msingi huu, kumekuwapo na desturi njema ya ‘kupokezana vijiti’ katika uongozi baina ya Maaskofu katika Baraza, kama ilivyo pia kwa nafasi nyingine. Kwa awamu hii, iliwapendeza Mababa Askofu kunipa dhamana ya Kusimamia Mashirika haya kwa hapa Tanzania kwa nafasi ya Rais wa Tume ya Uinjilishaji, nikipokea kutoka mikononi mwa Mhashamu Askofu Mkuu Damian Denis Dallu, Askofu Mkuu wa Songea ambaye amehudumu katika nafasi hii kwa takriban miaka 15 sasa. Tunapomshukuru Mungu kwa zawadi ya utumishi uliotukuka wa Baba Askofu Mkuu Damian Denis Dallu kwa nafasi ya Rais wa Tume ya Uinjilishaji kwa kipindi chote hicho, ninapenda pia kutumia nafasi hii kutoa mwaliko wangu kwa kila mwamini katika kuiendeleza kazi nzuri tuliyoipokea kutoka kwa watangulizi wetu mbalimbali, kwa kuzingatia vipaumbele vifuatavyo kati ya vingi:

Umuhimu wa kuyafahamu Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari
Umuhimu wa kuyafahamu Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari

Kuyafahamu vema Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari: Pamoja na jitihada kubwa ambayo imekwishawekwa hadi sasa katika kutoa elimu juu ya Mashirika haya, bado kwa sehemu kubwa hayajafahamika vema. Tunalo deni la kuweka juhudi za pamoja na mahususi kwa ajili ya malezi endelevu juu ya wito wa umisionari, kila mmoja kwa nafasi yake tukikumbuka kuwa: “tumebatizwa na tunatumwa”. Hivyo, tudumu katika ‘bidii kama mwanzo’ na zaidi. Tujitahidi kutumia vema nyenzo mbalimbali zinazotolewa kwetu (ikiwemo semina, machapisho mbalimbali na hata elimu kupitia mitandao ya kijamii) ili kujichotea maarifa stahiki juu ya Mashirika haya. Nafasi ya Sala katika Mashirika ya Kipapa: Kwa kuzingatia kuwa Sala ndio moyo wa umisionari, tukumbuke kuwa Mashirika ya Kipapa ni shule ya sala katika kuliombea Kanisa na ufanisi wa kazi ya Umisionari. Uhai wa Mashirika haya ni matokeo ya Nguvu ya Roho Mtakatifu ambaye analilinda na kuliongoza Kanisa (Rej. Mwongozo na.12). Daima tukumbuke kurejea katika misingi. Tunapowatazama waanzilishi wa Mashirika haya, waliyasimika katika msingi wa SALA. Kwa namna ya pekee kabisa, tukimtazama Mwanzilishi wa Shirika la Kipapa la Uenezaji wa Imani, Mwenyeheri Pauline Marie Jaricot, tunajifunza kwake kuwa pasipo nguvu ya sala, Mashirika haya yasingeweza kufika yalipo sasa kwani alihimiza juu ya Sala ya Rozari Hai, Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, Ekaristi Takatifu, Sala za binafsi na za jumuiya (akianzia na vikundi vya watu kumi kumi), tukitaja kwa uchache. Vivyo hivyo kwa waanzilishi wa Mashirika mengine ya Kipapa. Hivyo, nasi tuwekeze katika SALA.

Ushiriki mkamilifu katika Sikukuu ya Watoto Mashuhuda wa imani.
Ushiriki mkamilifu katika Sikukuu ya Watoto Mashuhuda wa imani.

Kukuza na kustawisha Moyo wa Ukarimu: Moja ya Malengo makuu ya Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari ni Ushirikiano wa Kimisionari (Missionary Cooperation). Ushikiano huu una sura mbili, yaani kiroho na kimahitaji yanayohusiana na kazi ya Umisionari. Ni kwa msingi huu, Mashirika haya huitwa “Mtandao wa Sala na Majitoleo” kwa ajili ya kuwezesha kazi ya Umisionari kupitia Mfuko Maalum wa Kiulimwengu wa Uinjilishaji wa Baba Mtakatifu (Universal Solidarity Fund). Sote tunaalikwa kuuishi wito wa umisionari kwa ushirikiano, kila mmoja akimtegemeza mwenzake. Kwetu hapa Tanzania, japo hadi sasa tayari tumepiga hatua fulani katika eneo hili la kutoa ukarimu kwa ajili ya kuwezesha kazi ya Umisionari kiulimwengu, ila bado kazi kubwa iko mbele yetu. Ninapenda kutoa mwaliko kwa kila mmoja kuendelea kutoa Ukarimu wake wa kila mwaka kwa ajili ya Uinjilishaji. Tuzitumie vizuri fursa zote tunazopewa katika ngazi ya Kanisa kiulimwengu kwa ajili ya lengo hilo; sambamba na kuunga mkono jitihada mbalimbali za Kanisa Mahalia zinazoratibiwa na Ofisi yetu ya Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari Taifa, katika kuhakikisha unapatikana ukarimu wa kutosha kwa ajili ya lengo hili ikiwemo – Bahasha Maalum za Marafiki wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari hapa Tanzania ambazo hutufikia kupitia parokia zetu. Ushiriki hai wa Maadhimisho ya Siku Maalum zihusuzo Utume wa Mashirika ya Kipapa: Kwa ajili ya kuyaenzi Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari na kutoa fursa kwa Waamini kushiriki vema katika kujibu mahitaji ya Umisionari, Mama Kanisa ametenga siku tatu maalum katika Mwaka wa Kanisa kwa lengo hilo. Japo Mashirika hayo yako manne, lakini zimetengwa siku tatu, kila moja ikiwa ni mahususi kwa Utume wa Shirika mojawapo kati ya matatu, hali Shirika la Umoja wa Umisionari likiachwa huru kwani Utume wake unabebwa katika Mashirika mengine. Wito kwa kila muamini ni kuwa na ushiriki hai katika maadhimisho ya siku hizi muhimu hasa kwa njia ya sala na majitoleo:

Waaamini wajenge utamaduni wa upendo, mshikamano na ukarimu
Waaamini wajenge utamaduni wa upendo, mshikamano na ukarimu

Dominika ya Kimisionari: Mnamo tarehe 14 Aprili, 1926, Baba Mtakatifu Pio XI aliidhinisha kuanzishwa rasmi kwa Dominika ya Kimisionari Ulimwenguni, yaani Dominika ya pili kutoka mwisho ya mwezi wa Oktoba. Hii ni siku maalum ya sala, malezi ya kimisionari na majitoleo kwa ajili ya kuwezesha kazi za Umisionari za Baba Mtakatifu. Ukarimu unaotolewa / unaokusanywa siku hii ni kwa ajili ya Mfuko wa Mshikamano wa Baba Mtakatifu unaoratibiwa na Shirika la Kipapa la Uinjilishaji wa watu – ambalo huratibu pia mgawanyo wa ruzuku kwa niaba ya Baba Mtakatifu kwa faida ya wenye mahitaji ya pekee. Aidha, ili kuwasaidia waamini kuiishi/kuiadhaimisha vema Dominika hii, kila mwaka, Baba Mtakatifu hutoa Ujumbe Maalum ambao huwa ndio dira katika kutafakari wito wetu wa Umisionari sio tu katika dominika hii bali kwa mwaka mzima. Kwa mfano, kwa mwaka huu 2024, Ujumbe wa Papa kwa Dominika ya Kimisionari unasema: “Enendeni na Alikeni kila mtu kwenye Karamu” (Rej. Mt. 22:9). Dominika ya Miito: Hii ni Dominika ya Nne ya Pasaka ambayo hujulikana pia kuwa Dominika ya Kristo Mchungaji Mwema. Dominika hii imetengwa mahususi kwa ajili ya kuwapa nafasi waamini wote kiulimwengu kusali kwa ajili ya kuombea Miito hasa ya Upadre na Utawa, kadhalika kutolea ukarimu wao kwa lengo la kutegemeza miito. Ukarimu unaopatikana katika Dominika hii ni kwa ajili ya Mfuko wa Baba Mtakatifu unaoratibiwa na Shirika la Mtakatifu Petro Mtume. Kwa niaba ya Baba Mtakatifu, Shirika hili huratibu mgawanyo wa ruzuku hizi kwa ajili ya kutegemeza malezi ya wale wanaoandaliwa kuwa mapadri na watawa, hasa wazawa kutoka katika nchi za kimisionari.

Nafasi ya Sala katika Mashirika ya Kipapa.
Nafasi ya Sala katika Mashirika ya Kipapa.

Sikukuu ya Watoto Mashahidi: Kwa ajili ya kuenzi na kutegemeza Shirika la Kipapa la Kimisionari la Utoto Mtakatifu, imetengwa siku maalumu kwa lengo hilo. Kulingana na mahitaji mahalia, kwa sehemu nyingi huwa ni katika Sikukuu ya Watoto Mashahidi, tarehe 28 Desemba kila mwaka. Mahali pengine, maadhimisho hayo hufanyika katika Sherehe ya Epifania, Ufunuo wa Bwana. Lengo ni kusali kwa ajili ya watoto hasa walio katika mazingira magumu, kadhalika kutolea ukarimu kwa ajili ya mahitaji ya watoto walio katika nchi za misioni. Ukarimu unaokusanywa katika siku hii huratibiwa na Shirika la Kipapa la Utoto Mtakatifu ambalo huwajibika kugawa ruzuku kutegemeza uinjilishaji miongoni mwa watoto kwa niaba ya Baba Mtakatifu. Kila inapowezekana, huhimizwa kuwa katika siku hii watoto wapewe fursa ya kushiriki maadhimisho husika na kutolea ukarimu wao kwa ajili ya mahitaji ya watoto wenzao walio katika mazingira magumu sana na kwa namna hii kuiishi Kauli Mbiu ya Shirika lao: “Watoto wawainjilishe watoto wenzao”, “watoto wawasaidie watoto wenzao.” Mwaliko wa kudumisha Ushirikiano (Synodality): Kwa kutambua kuwa sisi sote kwa ubatizo wetu ni wamisionari na kwamba umisionari ndio hulka ya Kanisa, kila mmoja wetu yampasa ajione kuwa anao wajibu wa kuyafahamu na kuyaeneza Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari kokote kule anakokuwa. Mashirika haya ni sehemu muhimu na ya lazima katika maisha na utume wa Kanisa, hivi kwamba yanamuhusu kila mwanakanisa, tofauti na hapo atatindikiwa sifa za kuwa mwamini kamili. Ni vema ikaeleweka kuwa ni kupitia Mashirika haya umoja wetu kama Kanisa hudhihirika. Hivyo, tunapokuwa na ushiriki hai ni udhihirisho wazi kuwa Kanisa Mahalia la Tanzania liko hai na linaishi katika muungano wa kweli na wanakanisa wengine kiulimwengu.

Ujumbe Mahususi
18 October 2024, 14:21