Tafuta

Habari Njema ya Wokovu inatangazwa na kushuhudia ule uzuri wa Injili bila kumezwa na malimwengu na hivyo kuleta maana ya pekee kwa wale wanaosikiliza na kushuhudia. Habari Njema ya Wokovu inatangazwa na kushuhudia ule uzuri wa Injili bila kumezwa na malimwengu na hivyo kuleta maana ya pekee kwa wale wanaosikiliza na kushuhudia.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Utukufu wa Askofu ni Huduma Kwa Kristo, Kanisa na Waja Wake!

Kardinali Víctor Manuel Fernández, Jumamosi tarehe 28 Septemba 2024 amewaweka wakfu Monsinyo John Joseph Kennedy, Katibu wa Idara ya Nidhamu pamoja na Monsinyo Philippe Curbelié, Katibu mkuu Msaidizi kuwa Maaskofu na watafanya utume wao katika Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na sasa ni waandamizi wa Mtakatifu Petro, wanaopaswa kutekeleza dhamana na utume wao kwa ari kuu na moyo wa unyenyekevu, ili waweze kuwa mashuhuda

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu anayo dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, lakini pia ni mpanzi wa amani, matumaini na imani. Ni kiongozi anayesimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za ndugu zake. Ni kiungo cha ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Askofu anapaswa kuwa mwaminifu kwa tunu msingi za Kiinjili sanjari na kujenga uhusiano mwema na wakleri wake ambao ni wenza wa mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi za binadamu. Askofu apalilie na kutunza miito ya kipadre na kitawa; ashirikiane na waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na kudumisha urika wa Maaskofu kwa njia ya majadiliano na ushirikiano wa Makanisa mahalia! Uhuru wa kuabudu na kidini uwasaidie waamini kupata ukamilifu wa furaha katika maisha yao, daima wakijitahidi kutafuta na kudumisha mafao ya wengi. Viongozi wa Kanisa wakizingatia mchango unaotolewa na sayansi kwenye medani mbalimbali za maisha wanayo haki ya kutoa maoni kuhusu mambo yote yanayoathiri maisha ya watu kwani hii ni sehemu muhimu ya uinjilishaji wa kina. Dini inapaswa kushuhudiwa katika maisha ya hadhara na kamwe haiwezi kufungiwa na kubakia kuwa ni sehemu ya faragha ya mtu binafsi. Maaskofu wanao wajibu na dhamana ya kulinda utu, heshima na haki msingi za ndugu zao wanaochakarika usiku na mchana kujenga taifa linalosimikwa katika mshikamano wa udugu wa kibinadamu pamoja na kuwa na taasisi imara.

Dhamana ya Askofu ni kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu
Dhamana ya Askofu ni kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu

Viongozi wa Kanisa wanayo haki ya kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni kiungo imara cha ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa, ingawa ushirikiano huu unaendelea kubaki kuwa ni sehemu ya changamoto za Kanisa, lakini Kanisa halina budi daima kusoma alama za nyakati, kwa ajili ya kutafuta: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa liwasaidie watu kupata: ustawi na maendeleo; elimu na huduma bora za afya; fursa za ajira na demokrasia ili kukuza utu wa binadamu. Ni kwa njia ya kazi inayotekelezwa kwa uhuru, kwa ubunifu, kwa kushirikiana na kusaidiana na wengine hudhihirisha mchakato wa maendeleo fungamani kwa ajili ya wengi. Maaskofu kama sehemu ya wajibu wao msingi waendelee kusimama kidete kulinda watu wao na hasa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa na kwamba, wao ni walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu na wadau makini wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Maskini wanapaswa kulindwa na kutetewa na Mama Kanisa, kwani kwa kawaida ni watu wanaonyonywa, kudhalilishwa pamoja na kudharauliwa sana. Maaskofu wanao wajibu wa kujenga na kudumisha umoja, udugu na upendo wa dhati na wakleri wao. Kati yao wawe ni mababa na ndugu wa imani na kamwe wasiwaache mapadre wao kujisikia wapweke na yatima. Wawasaidie wakati wa raha na karaha katika maisha na utume wao; wawasikilize na kujiaminisha kwao.

Maskini ni amana na utajiri wa Kanisa
Maskini ni amana na utajiri wa Kanisa

Maaskofu kama viongozi wa Makanisa mahalia, wanao wajibu na dhamana ya kupandikiza mbegu ya miito ya kipadre na kitawa kwa kuiendeleza na kuitunza. Maaskofu watoe malezi na majiundo makini kwa vijana wanaotaka kujisadaka katika maisha ya kipadre na kitawa, ili waweze kukua na kukomaa, huku wakiendelea kupyaisha na kutakasa nia zao. Wito wa jumla kwa wote ni utakatifu wa maisha ambao ni mvuto wa sura ya Kanisa. Maaskofu washirikiane kikamilifu na waamini walei katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa mwanga na tunu msingi za Kiinjili. Waamini walei wapewe malezi na majiundo ya kutosha, ili mwisho wa siku waweze kuwa kweli ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu. Na kwa njia hii, wataweza kuleta mabadiliko makubwa kwa jamii na katika maisha na utume wa Kanisa.

Simamieni utu, heshima na haki msingi za binadamu
Simamieni utu, heshima na haki msingi za binadamu

Kardinali Víctor Manuel Fernández, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa anasema, Taalimungu haina budi kukua na kukomaa, ikijikita katika majadiliano miongoni mwa wanataalimungu, sayansi na jamii katika ujumla wake. Huu ni mwaliko wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Huu ni wito wa kumwilisha Katiba ya Kitume: “Predicate evangelium” yaani “Hubirini Injili” Juu ya Sekretarieti kuu “Curia Romana” na Huduma Yake Kwa Kanisa na Kwa Ulimwengu.” Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa linabeba uzito wa pekee yaani: Kulinda mafundisho ambayo yanatokana na imani ili kutoa sababu za tumaini la Kanisa. Kulinda imani ya Kanisa inayokua na kukomaa kila kukicha; kulinda imani dhidi ya uzushi na kutoa majibu muafaka badala ya Baraza kujikita katika falsafa ya kulaani tu. Habari Njema ya Wokovu inatangazwa na kushuhudia ule uzuri wa Injili bila kumezwa na malimwengu na hivyo kuleta maana ya pekee kwa wale wanaosikiliza na kushuhudia. Huu ni uinjilishaji unaosimikwa katika majadiliano na tamaduni mbalimbali kwani Mama Kanisa anataka kujikita katika mchakato wa kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ili kuwawezesha watoto wa Kanisa kuishi Injili katika usafi na utilimifu wake, kwa kuendelea kuwa ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha.

Maskini ni walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu
Maskini ni walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu

Ni katika muktadha huu, Kardinali Víctor Manuel Fernández, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Jumamosi tarehe 28 Septemba 2024 amewaweka wakfu Monsinyo John Joseph Kennedy, Katibu wa Idara ya Nidhamu pamoja na Monsinyo Philippe Curbelié, Katibu mkuu Msaidizi kuwa Maaskofu na watafanya utume wao katika Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Maaskofu hawa sasa ni waandamizi wa Mtakatifu Petro, wanaopaswa kutekeleza dhamana na utume wao kwa ari kuu na moyo wa unyenyekevu, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili na matumaini; ukarimu na huduma kwa maskini, huku wakionesha ukaribu kwa watu wote wa Mungu. Kwa kuwekwa wakfu, sasa wamekuwa ni wateule wa Kristo Yesu kwa kuunganika zaidi na Kristo, kwa maana upendo wa Kristo Yesu unawabidiisha! 2 Kor 5:14, daima Kristo Yesu apewe kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wao, kwani Mungu anapenda na Kristo anaokoa kweli kweli na kwamba, wao wanapaswa kufikiri na kutenda kama Kristo Yesu. Kwa kuwekwa wakfu, wamepokea zawadi kubwa kutoka kwa Kristo Yesu, watakayoitumia kwa ajili ya huduma kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican, tayari kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano ya dhati na Makanisa mahalia katika huduma ya upendo; huku tunu msingi za Kiinjili zikipewa kipaumbele cha kwanza. Katika maisha na utume wao, wajiaminishe kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, ili waweze kuwa watu thabiti, huru na wenye furaha kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Francisko wa Assisi. Waendelee kulipenda na kulihudumia Kanisa; Waipende Injili na kuiweka kuwa na dira na mwongozo wa maisha; wawapende na kuwaheshimu watu, kama sehemu ya utimilifu wa Amri ya upendo kwa kutambua kwamba, wao ni zawadi safi na baraka ya Mungu, kwa ajili ya huduma, wao ni kielelezo cha neema ya Mungu katika medani mbalimbali za Kanisa.

Mafundisho Tanzu ya Kanisa
03 October 2024, 13:57