Tafuta

2024.11.07 Kardinali Pietro Parolin Katibu wa Vatican akiwa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregoriana. 2024.11.07 Kardinali Pietro Parolin Katibu wa Vatican akiwa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregoriana. 

Kardinali Parolin anatoa salamu za heri kwa Trump kwa ushindi wa uchaguzi

Akizungumza na waandishi wa habari kando ya hafla katika Chuo Kikuu cha Kipapa Gregoriana,Katibu wa Vatican alielezea matumaini yake kwamba Rais mteule wa Marekani Trump atatawala kwa hekima,"kwa sababu hii ndiyo sifa kuu ya viongozi kulingana na Biblia."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kufuatia uchaguzi wa rais wa Marekani na ushinidi wa Donald Trump, Katibu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin, aliwaambia waandishi wa habari, kwamba "Bila shaka tunamtakia  mema Trump. “Mwanzoni mwa mamlaka yake, tunamtakia hekima nyingi, kwa sababu hiyo ndiyo sifa kuu ya viongozi kulingana na Biblia.” Kardinali aliendelea kusema kwamba rais mteule atalazimika kufanya kazi "zaidi ya yote kuwa rais wa nchi nzima" ili kuondokana na ubaguzi unaozidi kuashiria nyakati zetu. Wakati huo huo, alielezea matumaini yake kwamba Trump atakuwa "kipengele cha kutuliza migogoro ya sasa ambayo inaua ulimwengu wake."

Ahadi za Trump

Alipoulizwa kuhusu ahadi za Trump za kukomesha vita kadhaa vinavyoendelea, Kardinali Parolin alijibu, "Tutumaini," huku akisema kwa matani, "Sidhani kama ana fimbo ya mazingaombwe." Aidha alisisitiza kwamba kukomesha vita kunahitaji unyenyekevu, lengo, na nia ya kufuata maslahi ya binadamu kwa ujumla, badala ya kuzingatia maslahi fulani. Kuhusu mizozo ya Ukraine na Nchi  Takatifu, Katibu wa Vatican alibainisha kuwa Trump hajaeleza kwa uthabiti jinsi atakavyofanya kazi hiyo ya kumaliza vita. "Wacha tuone atapendekeza nini baada ya kuchukua madaraka," Kardinali Parolin alisema.

Ahadi za Trump kufukuza wahamiaji

Na akijibu maswali kuhusu ahadi ya Trump ya kuwafukuza "mamilioni" ya wahamiaji kutoka Marekani, Kardinali Parolin alisema, "Inaonekana kwangu kwamba msimamo wa Papa na Vatican  uko wazi sana katika suala hili. Sisi ni kwa ajili ya sera ya busara kwa wahamiaji na kwa hivyo na ambayo haipiti mipaka hii." Aliongeza kuwa Papa Francisko ametoa maelekezo "sahihi sana, yaliyo wazi kabisa" kuhusu uhamiaji, na kuongeza: "Ninaamini hii ndiyo njia pekee ya kushughulikia matatizo na kuyatatua kwa njia ya kibinadamu."

Hata hivyo Kardinali Parolin alikubali kwamba kuna baadhi ya masuala ambapo sera za Trump zinalingana kwa karibu zaidi na misimamo ya Vatican, kama vile "ulinzi wa maisha." Hata hivyo, Kardinali huyo alisema, “Naamini hii inapaswa kuwa sera ya kawaida; inapaswa kujaribu kukusanya makubaliano kuhusu suala hili na isiwe sera tena ya ubaguzi na mgawanyiko." Alisisitiza juu ya hitaji la kusikilizana, na akasema anatumaini ahadi za Trump za kutetea maisha "pia zitapanua makubaliano kwa maana hiyo."

Uhusiano wa Vatican na Marekani 

Kardinali Parolin vile vile alisema hafikirii uhusiano kati ya Vatican na Marekani kubadilika na utawala mpya, kama alivyobainisha kwamba:  "Tulidumisha uhusiano na Rais Trump hata katika kipindi chake cha awali cha uongozi, hivyo zaidi au kidogo tutaendelea.” Kardinali Parolini vile vile alibanisha juu ya kuwepo kwa ukaribu katika baadhi ya masuala na tofauti kwa wengine, ambapo  alisema, hili litakuwa ni tukio la kufanya mazungumzo na kujaribu kutafuta vipengele zaidi vya maafikiano kwa pamoja, daima kwa manufaa ya wote na amani duniani.

Uhusiano wa Vatican na China

Hatimaye, akijibu swali kuhusu uhusiano wa Vatican  na China, Kardinali Parolin alisema, "Tumesonga mbele na China ... mazungumzo yanaendelea, kwa hatua ndogo lakini yanaendelea, kwa hiyo tunathibitisha msimamo huu,” huku akitambua mwitikio wa sera hii kutoka Marekani, Kardinali Parolin alisisitiza maslahi ya Vatican  nchini China "kimsingi ni maslahi ya kikanisa," na kwamba utambuzi mkubwa zaidi wa mwelekeo huu unaweza kubadilisha "tathmini" ya uhusiano na mataifa mengine.

Kardinali Parolin kuhusu Marekani
07 November 2024, 16:24