Kutafuta njia zinazofaa za kufikia amani nchini Ukraine
Andrea Tornielli
Siku elfu. Siku elfu moja zimepita tangu tarehe 24 Februari 2022, wakati jeshi la Shirikisho la Urusi liliposhambulia na kuivamia Ukraine kwa amri ya Rais Vladimir Putin. Siku elfu moja na idadi isiyojulikana - lakini kubwa sana - ya vifo, raia na askari, waathiriwa wasio na hatia kama vile watoto waliouawa mitaani, shuleni, majumbani mwao. Siku elfu moja na mamia ya maelfu ya watu waliojeruhiwa na waliopatwa na kiwewe wanaotarajiwa kubaki walemavu maisha yao yote, ya familia zilizoachwa bila makao. Siku elfu na nchi iliyouawa na iliyoharibiwa. Hakuna kinachoweza kuhalalisha janga hili ambalo lingeweza kusitishwa mapema, ikiwa kila mtu angejibidisha juu ya kile ambacho Papa Francisko aliita "mipango ya amani", badala ya kusalimu amri kwa kudhaniwa kuwa ni lazima kwa mzozo. Vita ambayo kama nyingine yoyote huwa inaambatana na masilahi, kwanza kabisa ile ya biashara pekee ambayo haijui shida na hata haikujua wakati wa janga la hivi karibuni, la kitaifa na la kimataifa la wale wanaotengeneza na kuuza silaha zote mbili. Mashariki na Magharibi.
Muda wa kusikitisha wa siku elfu moja ambao umepita tangu kuanza kwa uchokozi wa kijeshi dhidi ya Ukraine unapaswa kuuliza swali moja: jinsi gani ya kukomesha mzozo huu? Jinsi gani ya kufikia usitishaji mapigano na kisha amani ya haki? Tunawezaje kuyapa maisha mazungumzo, yale "mazungumzo ya uaminifu" ambayo Mrithi wa Petro alizungumza hivi karibuni, ambayo huturuhusu kufikia "maafikiano ya heshima" kukomesha mzunguko wa kushangaza ambao unahatarisha kutuvuta kuelekea shimo la vita vya nyuklia?
Huwezi kujificha nyuma ya vidole. Kielelezo cha diplomasia kinaonekana kuwa shwari, mwanga pekee wa matumaini unaonekana kuwa unaohusishwa na matamko ya uchaguzi ya rais mpya wa Marekani. Lakini suluhisho, na kisha amani iliyojadiliwa, ni - au tuseme linapaswa kuwa - lengo linalofuatiliwa na wote na haliwezi kuachwa kwenye ahadi za kiongozi mmoja. Basi nini cha kufanya? Ni kwa jinsi gani Ulaya, hasa, inaweza kupata nafasi inayostahiki maisha yake ya zamani na ya wale viongozi ambao katika kipindi cha baada ya vita walijenga jumuiya ya mataifa yanayohakikisha miongo kadhaa ya amani na ushirikiano kwa Bara la Kale? Nchi zinazoitwa Magharibi, badala ya kukazia fikira tu mbio za kichaa za silaha na mashirikiano ya kijeshi ambayo sasa yalionekana kuwa ya kizamani na urithi wa Vita Baridi, labda yanapaswa kutilia maanani idadi inayoongezeka ya mataifa ambayo hayajitambui katika mpango huu.
Kuna nchi ambazo zimedumisha na hata kuimarisha uhusiano wa hali ya juu na Urusi: kwa nini usichunguze kwa kina uwezekano wa kupata suluhisho la amani ya pamoja?
Kwa nini tusiendeleze hatua za kidiplomasia na mazungumzo ya mara kwa mara kupitia mashauriano yasiyo ya hapa na pale, yasiyo ya urasimu lakini makali na nchi hizi? Na ikiwa Makansela wa Ulaya wanatatizika kuchukua njia hii, je tunaweza kukisia nafasi kubwa zaidi kwa Makanisa na viongozi wa kidini? Tena, zaidi ya mawasiliano rasmi, ambayo hata hivyo ni machache, tungetarajia mpango mkubwa zaidi wa uchambuzi na pendekezo sambamba na nchi zinazounga mkono Ukraine kifedha na kijeshi: kuna hitaji la dharura la "mizinga ya fikra" ya kimataifa inayoweza kuthubutu, ya kuonyesha njia zinazowezekana na madhubuti za suluhisho, kupendekeza mipango ya amani inayokubalika kwa wote. Ili kufanya hivyo, kama vile Kardinali Parolin alivyoviambia vyombo vya habari vya Vatican, kutakuwa na haja kubwa "ya viongozi wenye maono ya mbali, wenye uwezo wa ishara za ujasiri za unyenyekevu, wenye uwezo wa kufikiria mema ya watu wao". Na pia kuna haja, kama kamwe kabla, kwa watu kupaza sauti zao kuomba amani.