Vatican,Askofu Mkuu Caccia:hadhi sawa ya mtu inadai tusifumbie macho ubaguzi wa rangi
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kifungu cha kwanza cha Azimio la Kimataifa la Haki za Kibinadamu kinathibitisha kwamba “binadamu wote huzaliwa wakiwa huru na sawa katika utu na haki.” Ingawa huu ni ukweli wa kimsingi unaotambulika na kwa haki ungechukuliwa kuwa haiwezi kujadiliwa, historia imeonesha kwamba inapingwa mara kwa mara. Ndivyo alianza hotuba yake, Askofu Mkuu Gabriele Caccia Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika Mjadala Mkuu wa Kamati ya Tatu ya Mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwenye Ajenda Kipengele cha 69 kuhusu: kutokomeza ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni na kutovumiliana huko jijini New York, Marekani tarehe 7 Novemba 2024. Katika hotuba yake, Askofu Mkuu alisema kuwa “Hakika, data za hivi karibuni zinaonesha kwamba karibu mtu mmoja kati ya sita ulimwenguni kote anabaguliwa, na ubaguzi wa rangi, kulingana na mambo kama vile kabila, rangi au lugha, haya ni miongoni mwa sababu zinazojulikana zaidi.” Kama vile Papa Francisko alivyosema: "hatuwezi kuvumilia au kufumbia macho ubaguzi wa rangi na kutengwa kwa aina yoyote na bado kudai kutetea utakatifu wa kila maisha ya mwanadamu," Ubaguzi wa rangi ni dharau kwa heshima ya asili aliyopewa na Mungu ya kila mwanadamu, na nadharia yoyote au aina yoyote ya ubaguzi wa rangi na na ubaguzi wowote ule havikubaliki.”
Bado kuna mitindo ya hila za kichini chini
Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican aidha alisema kuwa “Ingawa ubaguzi wa wazi wa rangi ni rahisi kutambua na kulaaniwa kwa haki, chuki zinazohusiana mara nyingi huchukua mtindo wa hila zaidi. Katika hilo Vatican inapenda kuzingatia maeneo matatu muhimu:Kwanza, katika ulimwengu, ambapo watu wengi wanahama kuliko hapo awali, wahamiaji, wakimbizi na familia zao mara nyingi hulengwa na aina ya ubaguzi wa rangi.” Na hii aliongeza “Uhamiaji unaweza kuunda hali ya hofu na wasiwasi ambayo mara nyingi huchochewa na kutumiwa kwa malengo ya kisiasa. Kama Papa Francisko alivyobainisha, "hii inaweza kusababisha mawazo ya chuki dhidi ya wageni, kama watu wa karibu.”
Wasi wasi wa ongezeko la kesi za kutovumiliana
Askofu Mkuu Caccia alindelea kuwa “Pili, Vatican inasalia kuwa na wasiwasi mkubwa juu ya kuendelea kuongezeka kwa kesi za kutovumiliana, ubaguzi na mateso ya kidini. Watu binafsi na jamii hukabiliana na vikwazo na mateso kwa kudai imani yao, faraghani na katika nyanja za umma. Vizuizi hivyo vinadhoofisha kanuni ya msingi ya uhuru wa dini au imani. Kwa kuzingatia maeneo mengi ambapo uhuru wa kidini umewekewa vikwazo vikali, Vatican inasisitiza kwamba serikali zina wajibu wa kimsingi wa kulinda haki hii ya raia wake, kwani ni mojawapo ya mahitaji ya chini kabisa yanayohitajika ili kuishi kwa utu.
Kuongezeka chuki dhidi ya wageni mtandaoni
Tatu, Mwakilishi wa Kudumu alieleza kuwa “ Vatican inajali hasa kuhusu kuongezeka kwa ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wageni mtandaoni na kwenye majukwaa ya kidijitali. Hii imeenea hasa kwenye mitandao ya kijamii ambayo haidhibiti maudhui yao. Katika kupambana na janga hili, elimu ni ya umuhimu sana, kama mkakati wa kukabiliana na kama hatua ya muda mrefu ya kuzuia. Hii inajumuisha sio tu dhamira mpya ya elimu bora, ambayo inamwezesha kila mtu kufikia uwezo wake kamili na kutafuta manufaa ya wote, lakini pia kutambua kwamba elimu huanza kwanza na muhimu zaidi katika familia, wazazi wakiwa waelimishaji wa msingi maadili ya binadamu.”
Hadhi sawa ya kila mtu inadai tusifumbie macho ubaguzi
Askofu Mkuu Caccia kwa kusisitiza zaidi alisema kuwa “hadhi sawa ya kila mwanadamu inadai kwamba tusifumbie macho ubaguzi wa rangi au kutengwa, lakini badala yake tukumbatie “mwingine” kwa uwazi, tukitambua “zawadi nono na upekee wa kila mtu na kila watu.” Hili linahitaji mabadiliko ya kimsingi ya mtazamo, kuanzia na utayari wa kushiriki katika mazungumzo katika roho ya mshikamano na udugu ili kuondokana na kutojali na hofu.