Kard.Koch:Papa Benedikto XVI,wakati umefika wa kumfikiria Mungu!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Misa maalum ya kumbukizi iliadhimishwa mapema Jumanne tarehe 31 Desemba 2024 katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican kwa ajili ya kukumbuka mwaka wa pili wa kifo cha Joseph Ratzinger yaani Papa Benedikto XVI kilichotokea mnamo tarehe 31 Desemba 2022. Kardinali Kurt Koch, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Kikristo aliongoza ibada hiyo. Katika mahubiri yake alitoa tafakari ya kina ya maisha na urithi wa Papa Benedikto wa kumi na sita, hasa ufahamu wake wa kitaalimungu na kujitolea katika maisha yote kwa Neno la Mungu. Alianza kwa kuzingatia umuhimu wa tarehe za kuzaliwa kwa Joseph Ratzinger, Jumamosi Takatifu ya mnamo 1927, na kifo chake wakati wa kipindi cha Sherehe za Noeli mnamo mwaka 2022 akiweka maisha yake katika fumbo la Pasaka.
Kardinali Koch alisema: "Mungu alihakikisha kwamba mfumo wa maisha ya Joseph Ratzinger umeandikwa katika historia ya Wokovu." Juhudi za Papa Benedikto XVI za kumfanya Mungu awepo katika ulimwengu wa sasa. Uhusiano huu wa kina ulikuwa nguvu inayoongoza katika maisha na kazi ya Papa Benedikto. Kwa hiyo Kardinali Koch alisema: “Aliishi fumbo hili, alilitangaza kwa imani yenye nguvu, na akalifanya lipatikane kwetu leo kwa uwazi wake wa kitaalimungu.” Akibainisha “matukio mazuri” ya Injili iliyosomwa kutoka katika Dibaji ya Mtakatifu Yohane, Kardinali Koch alisema kwamba Neno la Mungu (“Logos”), lilikuwa kiini cha taalimungu ya Benedict: “Kupitia uangalifu na mwelekeo wake wa kudumu kiukweli wa Neno la Mungu, alituonesha kwa kusadikisha maana ya maisha ya kibinadamu,” ambayo yamo ndani ya Mungu na upendo Wake wa milele kupitia Yesu.
Kwa hakika, alikumbuka, kuwa kwa Papa Benedikto kufafanua kuwa Logos yaani Neno la Mungu, alihusishwa sana na upendo: Mungu Mwenyewe ni upendo kama alivyokazia katika Waraka wake wa Kitume wa ‘Deus Caritas Est’, maisha na mafundisho yake yalionesha ufahamu huu wa kimungu, ambapo upendo upo katika moyo wa kuwepo kwa mwanadamu na umilele wake. Kujitolea kwa maisha yote ya Papa Benedikto XVI katika kufanya uwepo wa Mungu kuwa jambo kuu katika ulimwengu wa leo hii. “Kumweka Mungu katikati ya tahadhari lilikuwa lengo kuu la Papa Benedikto XVI. Katika enzi ambayo mara nyingi Mungu huonwa kuwa mgeni na asiyefaa kupita kiasi, nasi tunapatwa na udhaifu fulani wa kusikia au hata kutosikia kwa Mungu, Papa Benedikto wa XVI alitukumbusha kwamba wakati umefika wa kumfikiria Mungu.” Akihitimisha mahubiri yake, Kardinali Koch aliwaalika waamini kuungana katika kushukuru maisha ya Papa Benedikto XV, wakiendelea kutafuta ukweli wa milele ambao aliutangaza kwa uaminifu: kwamba Mungu, kwa njia ya Kristo, ni halisi, na uzima wa milele ni thawabu kwa wale wanaompenda.