Kard.Krajewski katika utume Ukraine kwa Noeli kupeleka zahanati inayotembea
Vatican News.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kutoka Ofisi ya Vyombo vya habari vya Vatican, inabainisha kuwa “Kwa sikukuu zijazo za Noeli, Baba Mtakatifu atatuma tena Mwakilishi wake, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma Kardinali Konrad Krajewski kurudi nchini Ukraine. Kila siku Papa Francisko anasali kwa ajili ya amani katika nchi hii iliyokumbwa na vita, lakini kwa namna madhubuti anataka kuwepo miongoni mwao katika siku hizi, tunapoadhimisha siku kuu ya kuzaliwa kwa Yesu.”
Kwa njia hiyo “Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo ataondoka kuelekea Ukraine akiwa na zawadi ya Gari kubwa lenye vifaa vya matibabu, (kama hospitali ndogo) ya kuzunguka kila eneno, ambapo shughuli za upasuaji pia zinaweza kufanywa ndani humo, na mashine sita za ultrasound ambazo zitatolewa katika hospitali zilizoharibiwa na zilizopigwa mabomu.” Katika taarifa hiyo aidha inabainisha kuwa “Katika safari yake nchini Ukraine, Kardinali Konrad Krajewski, atatembelea pia jumuiya mbalimbali ili kukutana na watu wanaoteseka, na pamoja nao atajaribu kufungua “mlango wa matumaini” mioyoni mwao na kuombea amani inayotamaniwa sana.”