Tafuta

Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa matumaini." Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa matumaini." 

Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo: Mahujaji Wa Matumaini

Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa matumaini. Matumaini ya waamini yako katika Msalaba, yaani katika Kristo Yesu, chemchemi ya wokovu wa mwanadamu aliyezaliwa katika Familia Takatifu iliyopata baraka ya kuwa na Mungu yaani Emanueli kati yake. Maadhimisho ya Sikukuu ya Familia Takatifu tarehe 29 Desemba 2024 imekuwa ni fursa kwa Majimbo kufungua lango la Maadhimisho ya Jubilei kuu.

Na Protase Kardinali Rugambwa, Jimbo kuu la Tabora, Tanzania.

Baba Mtakatifu Francisko, katika mkesha wa Noeli tarehe 24 Desemba 2024 amefungua Lango Kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, mwanzo wa maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo. Hili ni Lango la matumaini, chemchemi ya watu wote wa Mungu. Maadhimisho ya Jubilei ni kwa ajili ya watu wote, ili kuwaonjesha tena matumaini ya Injili, matumaini ya mapendo na matumaini ya msamaha wa kweli. Pango la Noeli ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu; chemchemi ya matumaini; upendo wa Mungu unaovunjilia mbali ukaidi wa mwanadamu pamoja na hofu yake, tayari kutafakari ukuu wa matumaini yaliyo mbele ya mwanadamu. Mwelekeo huu, uwe ni mwangaza wa mapito ya kila siku ya mwanadamu. Ni katika muktadha wa usiku huu ambapo “Lango Takatifu” la Moyo wa Mungu limefunguliwa. Kristo Yesu, Mungu pamoja nasi, anazaliwa kwa ajili ya binadamu wote. Kumbe, pamoja naye, furaha ya dunia inachanua kama “maua ya kondeni.” Pamoja na Kristo Yesu, maisha yanabadilika na pamoja na Kristo Yesu “Spes non confundit" yaani “Tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5.

Kauli mbiu "Mahujaji Katika Matumaini"
Kauli mbiu "Mahujaji Katika Matumaini"

Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji katika matumaini.” Matumaini ya waamini yako katika Msalaba, yaani katika Kristo Yesu, chemchemi ya wokovu wa mwanadamu aliyezaliwa katika Familia Takatifu iliyopata baraka ya kuwa na Mungu yaani Emanueli kati yake. Maadhimisho ya Sikukuu ya Familia Takatifu tarehe 29 Desemba 2024 imekuwa ni fursa kwa Majimbo mbalimbali duniani kufungua lango la Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo. Tarehe Mosi, Januari mwaka 2025 itakuwa ni fursa kwa Parokia kufungua maadhimisho haya. Huu ni wito wa kutangaza na kushuhudia Imani yao kwa Kristo Yesu, Mlango wa uzima wa milele na hivyo wakristo wote wanaalikwa kuwa ni mahujaji wa matumaini yasiyo danganya; umoja unaopaswa kuimarishwa; kukuza na kujenga haki, amani na furaha ya kweli katika Kristo Yesu. Kristo Yesu ndiye Lango la maisha ya uzima wa milele, anayewashirikisha waja wake Fumbo la upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka; huruma inayowakumbatia binadamu wote pasi na ubaguzi, changamoto na mwaliko wa kuambata toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha.

Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu
Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, katika Ibada ya kufungua Maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei kuu ya Mwaka 2025 ya Ukristo, amewataka watu wa Mungu kuzingatia mambo makuu manne: Kuzama zaidi katika kusoma, kutafakari na kuyaishi Maandiko Matakatifu. Waamini wajitanabaishe kwa maisha yao ya Kikatoliki na hivyo kuachana na tabia ya kuwayawaya, kwani kwenye Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume kuna kila kitu waamini wanachohitaji katika maisha yao ya kiroho sanjari na wokovu. Waamini wajitahidi kuimarisha uadilifu, haki, amani na utulivu. Waamini wawe ni mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili, na kiutu katika familia, mahali pao pa kazi, kwenye Jumuiya ndogondogo za Kikristo, Kigangoni, Parokiani, Jimboni na katika Kanisa zima. Maadhimisho ya Jubilei ni fursa ya kuimarika: kiroho na kiutu!

Mahujaji wa Matumaini
Mahujaji wa Matumaini

Ni katika muktadha huu, Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania, katika mahubiri yake katika Ibada ya Misa Takatifu, Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Josefu sanjari na ufunguzi wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo, alikazia kuhusu Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, iliyoongozwa na mkono wa Mungu tangu mwanzo hadi pale ilipokamilisha hija yake katika muungano mkamilifu na Mwenyezi Mungu, kiasi hata cha nguvu za mwanga zikakabiliana na nguvu za giza, mwanga wa matumaini ukashinda. Upendo huo wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ulisheheni na moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, kuchukuliana, kusameheana pamoja na fadhila nyingi zilizowasindikiza katika hija ya maisha yao hapa duniani. Upendo uwe ni nguzo na dira ya familia mbalimbali za Kikristo katika safari yao hapa ulimwenguni. Waamini wawe na moyo wa shukrani kwa mambo yote yanayong’ara katika maisha ya familia mintarafu mpango wa Mungu, yaani muungano kamili kati ya Bwana na Bibi. Kwa waamini waliokengeuka na kuanza kufuata mafundisho mengine, washauriwe na kuombewa ili Kanisa liweze kuyaongoza na kuratibu maisha yao. Familia zipambwe na kusimama katika maadili mema, utu, heshima na haki msingi za binadamu; imani, tumaini na upendo. Waamini wamwombe Mungu neema na baraka za kuweza kukabiliana kikamilifu na changamoto mamboleo zinazoendelea kuibuka kila kukicha. Kanisa linawaalika watoto wake wote wawe ni mahujaji wa matumaini. Jubilei hii iwe ni fursa ya kukutana kikweli kweli na Kristo Yesu katika: Neno, Sakramenti na Matukio mbalimbali ya maisha.

Maandamano ya kufungua Mwaka wa Jubilei kuu, Jimbo kuu la Dar es Salaam
Maandamano ya kufungua Mwaka wa Jubilei kuu, Jimbo kuu la Dar es Salaam

Yafuatayo ni mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora kama sehemu ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Kristo kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Theresa. Ndugu zangu katika Kristo, Tunaadhimisha leo Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu tukiwa katika ufunguzi wa Mwaka wa Jubilei Kijimbo ambao, kiulimwengu ulifunguliwa rasmi huko Roma na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 24 Desemba 2024, katika maadhimisho ya Noeli, kwa kufungua Mlango Mtakatifu wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro lililoko mjini Vatican. Kama Waamini, familia ya Mungu inayosonga mbele kuelekea Yerusalemu ya mbinguni, tumealikwa sote katika Jubilei hii kuwa Mahujaji katika matumaini yasiyo tahayarisha.  Matumaini yetu yako katika Msalaba yaani Yesu Kristu, tunayemfuata tukiwa nyuma yake, naye anabaki daima kuwa ni sababu ya wokovu wetu. Ni Yesu Kristo huyo aliyekuwa katika Familia hii Takatifu tunayoikumbuka leo, Familia iliyopata baraka ya pekee na heshima ya kuwa na Mungu - Emanueli kati yake.

Matumaini ya Kikristo Yametundikwa Msalabani: Kristo Yesu
Matumaini ya Kikristo Yametundikwa Msalabani: Kristo Yesu

Ndugu zangu, huyo Mungu-Emanueli aliyekuwa katika hiyo Familia Takatifu ya Nazareti, ni Mungu nafsi ya pili -Yesu Kristo anayekuja na kutaka kuwa katika Familia zetu. Kumbe Sikukuu ya Familia Takatifu inatualika tusiitazame tu hiyo Familia ya Nazareti bali tunapaswa pia tuzitazame familia zetu tukimshukuru kwanza Mwenyezi Mungu anayependa kukaa katika Familia hizi akizisindikiza mpaka mwisho wa Hija inayozipeleka Yerusalemu ya mbinguni na tukiomba tubaki nasi tumeunganika naye mpaka mwisho wa safari yetu. Na hayo yote yawezekana tukifuata mfano wa hiyo Familia Takatifu, iliyoongozwa na mkono wa Mungu tangu mwanzo mpaka ilipokamilisha Hija yake katika muungano mkamilifu na Mungu Baba. Tunapoianza Hija hii ya Matumaini, nawaalika tuifanye safari hii tukiitizama Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu na tuyaone yale waliyopaswa kukabiliana nayo, ya giza na Mwanga ambayo lakini mwisho wake ilikuwa ni nguvu ya mwanga kuishinda nguvu ya giza. Kukinzana kwa nguvu ya giza na nguvu ya mwanga katika kuitayarisha na baadaye katika uwepo kwa Familia hii takatifu kumeifuata Familia hii tangu mwanzo mpaka mwisho wa safari yake hapa ulimwenguni.

Jubilei: Toba, wongofu na utakatifu wa maisha
Jubilei: Toba, wongofu na utakatifu wa maisha

Haikuwa rahisi si kwa Mama Maria tu kuyapokea mara moja yale aliyoambiwa na Malaika Gabrieli bali hata kwa Yosefu yalikuwepo maswali mengi ambayo yalimpelekea mpaka atake kumpa talaka mchumba wake Maria. Hata Mtoto Yesu - Emanueli, tunazifahamu changamoto zilizokuwepo katika kuzaliwa kwake: safari ndefu waliyopaswa kufanya Maria na Yosefu kabla ya kuzaliwa kwake, ikifuatiwa na kuzaliwa kwake katika hori ya kulia ng’ombe. Na baadaye akiwa anatafutwa kuuawa na Mfalme Herodi, Familia ilivyokimbilia Misri. Na kama tulivyosikia kwenye Injili ya Yohane iliyosomwa kwenye Misa ya Noeli mchana: ni kwamba huyo Neno ambaye alikuja, ulimwengu haukumtambua. Alikuja kwake, wala waliokuwa wake hawakumpokea. Na tunafahamu yaliyoendelea mpaka alipoikamilisha safari yake hapa duniani kwa kifo cha Msalaba.  Simulizi la Mwinjili Luka tulilosikia muda mfupi uliopita nalo labainisha wazi shida waliyokumbana nayo Maria na Yosefu wakimtafuta Yesu aliyekuwa amepotelea huko Yerusalemu. Hayo yote ndugu zangu twaweza kusema kwa neno moja kuwa ni giza lililojitokeza katika safari ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Pamoja na giza hilo lililoijiri Familia Takatifu bado kulikuwa na Mwanga ulioongoza safari yao, na mwanga huo ulioleta furaha katika Familia hiyo, ulitokana na Upendo wa pekee wa Mungu Baba ambao ulitawala tangu mwanzo mpaka mwisho, Mungu akiwa anaongoza daima historia ya wokovu aliyotaka ikamilike kupitia kwenye Familia hii. Bila shaka huo upendo wa Mungu Baba ulioishinda nguvu ya giza ulijibiwa na upendo wa wote waliokuwa katika Familia hiyo Takatifu ambao twaweza kusema tukitumia maneno ya Mtume Paulo kutoka katika Waraka kwa Wakolosai tuliyosikia leo kuwa walikuwa wamejivika upendo ambao ni kifungo cha ukamilifu.  Na kwa upendo huo Familia Takatifu ya Yesu Maria na Yosefu, ilijawa na moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, kuchukuliana, kusameheana, na fadhila nyingine nyingi zilizowasindikiza wana Familia Takatifu katika safari yao hapa ulimwenguni.

Mahujaji wa Matumaini katika Kristo Yesu
Mahujaji wa Matumaini katika Kristo Yesu

Ndugu zangu katika Kristo, hali hiyo ya giza na mwanga waliyokumbana nayo Yesu, Maria na Yosefu nasi katika familia zetu, ni hali ambayo tunasafiri nayo katika hija yetu hapa duniani.  Ni ukweli usiopingika kuwa yale ya giza na yale ya mwanga yanaonekana na yako nasi katika safari yetu ya kuelekea huko ambako Mungu Baba yetu anataka tufike.  Tukiamini kwamba ni katika Upendo wake, familia zetu za Kikristo zinakuwepo na zinasafiri zikiongozwa na nguvu yake ya mwanga, hata kama giza linatujia tunapaswa tubaki katika moyo wa matumaini ya kulishinda hilo giza.    Tunapozitizama familia zetu za Kikristo, tumshukuru Mungu kwa kila kinachong’ara kama mwanga katika familia na nyumba zetu za ki-Kristo.  Tumshukuru Mungu kwanza kwa kuutambua huo wito wa familia iliyo kweli ya ki-Kristo, kuutambua huo mpango wa Mungu wa muungano wa Mme na Mke na si vinginevyo. Na hapa tuyakumbuke maneno ya kitabu cha Mwanzo yanayosema: “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamme na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, “Zaeni mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha…” Mwa. 1:27-28.  Hizi ndizo familia zinazoongozwa na mafundisho halali ya Kanisa tunayopaswa kuyaenzi na kuyalinda. Kwa wale wanaokengeuka na hasa waamini wenzetu, na kuanza kuyafuata mafundisho tofauti yanayojitokeza katika ulimwengu wa leo hatuna budi kuwashauri na kuwaombea ili warudi katika mafundisho ya Mama Kanisa.  Tunamshukuru Mwenyezi Mungu pia kwa mema mengi tunayoyaona katika familia zetu: maisha ya imani na maadili, watoto tunaowapata, mafanikio mbalimbali katika maisha na hata uwepo wa fadhila kama zile zilizoipamba Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, na tunazoomba ziendelee kuwepo zikiwa zinaongozwa na fadhila hiyo kuu ya Upendo, ambayo Mtume Paulo anaitaja kuwa ni kuu kuliko zote: “Basi sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.” 1Kor. 13:13.

Waamini jengeni familia kadiri ya mpango wa Mungu.
Waamini jengeni familia kadiri ya mpango wa Mungu.

Tukiwa na nguvu hiyo ya Upendo wa ki-Mungu katika familia zetu, bilashaka hata hayo mausiano mazuri anayoyataja Mtume Paulo katika barua yake kwa Wakolosai, yataweza kujengeka: Wazazi watapendana na kuwapenda watoto wao na watoto wakifuata mfano wa wazazi wao nao watawapenda wazazi wao na watoto wenyewe kupendana, ikiwa pia ni kukuza katika familia hata fadhila hizo nyingine za wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, kuchukuliana na kusameheana. Na hali hii haitabaki kwenye familia moja, bali itaonekana pia katika mahusiano na familia nyingine.  Hizo fadhila zinapokosa katika familia zetu basi linaingia giza na kuuondoa mwanga ambao sote kama wafuasi wa Kristu tungependa tuuone. Ziko pia changamoto mbalimbali tunazozikuta katika familia zetu, ni giza linaloingia na kuleta woga, mateso na pengine kukata tamaa: Yaweza kuwakuta wazazi au watoto katika familia na baadae hata nje ya familia yaani katika jamii na kwenye mazingira mbali mbali tunamoishi.

Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo: Mahujaji katika Matumaini.
Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo: Mahujaji katika Matumaini.

Ndugu zangu, Tumeufungua Mwaka mtakatifu wa Jubilei Kuu unaotualika tusikate tamaa na tuwe Mahujaji wa Matumaini.  Katika sikukuu hii ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, iliyo pia Sikukuu ya familia zetu, tumejikumbusha mengi tunayopaswa kuyaona yakitawala kama mwanga katika familia hizi. Yaliyo ya giza hayakosi na tunayafahamu. Kama anavyosema Baba Mtakatifu kuhusiana na Mwaka huu Mtakatifu: kwa kila mtu, Jubilei hii iwe ni wasaa wa kukutana kikweli, kibinafsi na Bwana Yesu, “mlango” (rej. Yn. 10:7.9) wa wokovu wetu, ambao Kanisa limeagizwa kumtangaza daima, kila mahali na kwa wote kama “tumaini letu”.  Basi ndugu zangu, tudhamirie kuifanya safari hii ya hija yetu ya kiuchaji tukimpelekea Bwana wetu Yesu Kristo aliye mlango wa uzima, hayo tunayoyaona kama giza kwenye maisha yetu ya familia na hata maisha yetu binafsi tukimwomba atushushie neema na rehema zitakazo tutakasa, kutupa nguvu na kutuimarisha tena ili hata baada ya Mwaka huu wa Jubilei tuendelee na safari yetu tukisaidiwa na mkono wake unaotulinda na kutuongoza kuelekea kwenye Yerusalemu ya mbinguni.   Tuendelee kusali ili kwa maombezi ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu tuweze nasi kumpokea Mungu - Emanueli katika familia zetu, arudi na kuingia pale ambapo kutokuwepo kwake, kunayafanya maisha yetu yagubikwe na giza linalotuzuia kuuona Mwanga wake unaopaswa kutuangazia na kutuonesha njia. 

Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo katika maisha.
Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo katika maisha.

Kristo!   Tumaini letu.

Mahubiri haya yametolewa Tabora, 29 Desemba 2024

+Protase Kardinali Rugambwa

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora.

Ufunguzi Jubilei kuu
30 December 2024, 15:26