Tafuta

Salama na matashi mema kutoka kwa Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora: Kipindi cha Noeli, Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofiu. Jubilei kuu na ujenzi wa Kanisa Mahalia: Ushuhuda wa imani Salama na matashi mema kutoka kwa Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora: Kipindi cha Noeli, Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofiu. Jubilei kuu na ujenzi wa Kanisa Mahalia: Ushuhuda wa imani  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kardinali Protase Rugambwa: Salam za Noeli na Mwaka Mpya 2025: Ushuhuda wa Imani

Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora katika Salam zake za Noeli na Mwaka Mpya wa 2025 anagusia kuhusu umuhimu wa kipindi cha Noeli, Maadhimisho ya Sinodi ya kumi na sita ya Maaskofu, Kongamano la tano la Ekaristi Takatifu Kitaifa, Ufunguzi wa Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo sanjari na ujenzi wa Kanisa mahalia pamoja na kuendelea kushikiri kikamilifu katika kuombea amani nchini Tanzania na Ulimwengu katika ujumla wake.

Na Protase Kardinali Rugambwa, Jimbo kuu la Tabora, Tanzania

Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora, Tanzania katika Salam zake za Noeli na Mwaka Mpya wa 2025 anasema Kipindi cha Majilio kimekuwa ni fursa ya kukesha, kuitengeneza njia ya Bwana kwa kujisafisha, kutubu na kuongoka tayari kumpokea Kristo Yesu anayekuja mara ya pili katika utukufu wake na anayezaliwa nyoyoni mwa waamini. Umekuwa ni wakati wa kutafakari yaliyopita na kuyaangalia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini ambayo hayataharishi. Kuna matukio ambayo yamefanyika Jimbo kuu la Tabora na kwa hakika yamekuwa ni chachu ya kujenga na kuimarisha umoja, mafungamano ya shughuli za kichungaji na kwamba, Kardinali Rugambwa anapenda kuendeleza hija za kichungaji Parokiani, ili kujenga na kuimarisha roho ya kitume kwa watu wote wa Mungu Jimbo kuu la Tabora. Waamini wameshikiri kikamilifu katika maadhimisho ya Kongamano la 5 la Ekaristi Takatifu Kitaifa kuanzia tarehe 11 hadi tarehe 16 Septemba 2024 kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Udugu wa kuponya Ulimwengu: “Nanyi nyote ni ndugu.” Mt 23: 8 sanjari na kuhitimisha Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Jumuiya Ndogondogo za Kikristo.

Kardinali Polycarp Pengo na Kardinali Protase Rugambwa
Kardinali Polycarp Pengo na Kardinali Protase Rugambwa

Haya ni matukio ambayo yalipania kuwajenga waamini kiimani na kuwaimarisha katika ushuhuda, tayari kuyaishi mafumbo haya ya imani. Watu wa Mungu Jimbo kuu la Tabora waliunganika na Kanisa la Kiulimwengu kuadhimisha Sinodi ya XVI ya Maaskofu iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu: “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pamoja na mambo mengine: kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Tarehe 29 Desemba 2024 ni ufunguzi wa Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo, tayari kukutana na Kristo Yesu, Lango la Matumaini na Wokovu. Huu ni mwaka wa neema na rehema. Watu wa Mungu Jimbo kuu la Tabora wanaitwa na kutumwa kuwa ni watu wa shukrani katika upendo, imani na matumaini, tayari kumwiga Bikira Maria aliyeshiriki kwa namna ya pekee katika mpango wa Mungu wa kumkomboa mwanadamu.

Kongamano la Ekaristi Takatifu: Kiini na hitimisho la maisha na utume wa Kanisa
Kongamano la Ekaristi Takatifu: Kiini na hitimisho la maisha na utume wa Kanisa

Kumbe, waamini wakiongozwa na nguvu ya imani, wakisukumwa na upendo na matumaini wanaweza kushiriki kikamilifu katika mpango wa Mungu na historia ya wokovu, kwa kuitikia “Ndiyo Bwana.” Waamini watekeleze dhamana na wajibu huu wakiwa wanaongozwa na roho ya Kisinodi ili kujenga Kanisa linalo imarika katika: Umoja, Ushirika na Utume. Huu ni mwaliko wa kumpokea Emmanueli, yaani Mungu pamoja nasi, tayari kumtangaza na kumshuhudia. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanayafahamu vyema Maandiko Mtakatifu. Neno la Mungu liwe ni dira na mwongozo wa maisha ya watu wa Mungu. Ikumbukwe kwamba, utume wa waamini unakwenda sanjari na Msalaba kwani ni katika Fumbo la Msalaba mwanadamu amekombolewa. Kristo Yesu ni njia, ukweli na uzima. Waamini wajenge na utamduni wa kushukuru wakati wa shida, magumu na raha katika maisha. Kardinali Protase Rugambwa anawaalika watu wa Mungu kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa kwa nguvu zao na rasilimali walizokirimiwa na Mungu, kwani wanapaswa kuwajibika. Bikira Maria Mama wa Mungu na Mkombozi wa ulimwengu, awasindikize katika maisha na utume wao. Waamini waweke nia kwa mwaka 2025 ili weweze kufanya mapenzi ya Mungu na waendelee kuombea amani kwa Tanzania, amani kwa Mataifa yote duniani. Mwenyezi Mungu alete amani kule kwenye machafuko, kutoelewana, magomvi na vita. Waamini wamwombe Emanueli, Mfalme wa amani aweke mkono wake na amani yake itawale.

Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora
Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora

Zifuatazo ni salamu za noeli kwa mwaka 2024 na mwaka mpya wa 2025: “shukrani katika upendo, imani na matumaini” Kwa Mapadre, Watawa, Waamini Walei na Watu wote wenye Mapenzi Mema. Tunapoadhimisha Sherehe ya kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo, napenda niwaalike wana familia ya Mungu, waamini wote wa Jimbo Kuu la Tabora tuungane na Kanisa la Tanzania na Kanisa zima la kiulimwengu, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mambo mengi aliyotutendea katika Mwaka huu unaoisha. Ni matumaini yangu kuwa, tulipokuwa katika kipindi cha Majilio, tumepata fursa ya kuyatafakari baadhi ya maneno tuliyosikia kutoka katika Maandiko Matakatifu na kutoka katika mafundisho mbali mbali ya wachungaji wetu kama vile kukesha na kuitengeneza njia ya Bwana, ambayo pamoja na kutualika kujisafisha, kuongoka, kubadilika na kuwa tayari kumpokea Bwana anayekuja mara ya pili katika utukufu wake na anayezaliwa mioyoni wetu, yatakuwa yametuelekeza turudi nyuma na kuona tulikotoka na hata kuyafikiria ya huko usoni tunakokwenda, mintarafu, maisha yetu ya kiroho na kukua kwetu kama wana Kanisa tukiwa daima na moyo wa matumaini ambayo hayatahayarishi. Rum. 5:5   Kwa wana Tabora, pamoja na mema mengi aliyotujalia Mwenyezi Mungu, kama ilivyokuwa mwaka jana, tuliweza pia kushiriki na kuyafurahia matukio kadhaa, ndani na nje ya Jimbo letu ambayo naamini yametuimarisha katika umoja wetu na hata kiimani. Binafsi nikiwa ndani ya Jimbo, nikiyaenzi pia mambo mengine mengi tuliyofanya katika utume wa kila siku, nilifarijika na hata kuimarika kiuchungaji, kwa namna ya pekee, kwanza niliposhiriki katika Mkutano Mkuu wa Masista wa Shirika la Mabinti wa Maria - Shirika la kijimbo - tangu kwenye ufunguzi wa Mkutano huo mpaka kwenye uchaguzi wa viongozi wapya na kusimikwa kwao. Tunawashukuru kwa ushirikiano tunaokuwa nao katika utume hapa Jimboni.  Nilifarijika pia na kuimarika kiroho na kichungaji nilipokutana nayi Mapadre, Watawa na Waamini walei nilipowatembelea na kukaa nanyi nikiwa katika Ziara za kichungaji kwenye hizo parokia zilizokuwa zimebainishwa. Asanteni sana kwa yote mnayofanya huko Parokiani na kwa namna ya pekee hilo kundi kubwa la Waamini walei wakishirikiana na viongozi Wachungaji na Wawekwa wakfu wanaokuweko huko.  Kama mtakavyokuwa mmeona kwenye ratiba yetu ya mwaka huu, nitafurahi tena kuendelea na Ziara hizo za kichungaji ambazo naamini kuwa zinatujenga na kutuimarisha kiroho na hata katika utume wetu kwa ujumla.

Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu Oktoba 2024
Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu Oktoba 2024

Tukiwa tumeunganika na Wachungaji pamoja na Waamini waliotawanyika sehemu mbali mbali katika Kanisa lililo Tanzania tumeweza kushiriki kwenye matukio ya kitaifa yaliyotukutanisha pamoja na yakatujenga katika kushuhudia Imani yetu kwa pamoja. Kwa namna ya pekee tutalikumbuka Kongamano la Ekaristi lililofanyika katika Jimbo Kuu la Dar es salaam ikiwa ni pamoja na kuhitimisha maadhimisho ya Jubilei ya miaka hamsini tangu kuundwa kwa Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristu kwenye nchi za AMECEA. Hii nayo ilikuwa ni fursa ya pamoja ya kutujenga kiimani na kutuimarisha katika ushuhuda, tukiyatafakari na ku-nuia kuyaweka kwenye matendo na hasa kuyaishi hayo mafumbo ya imani yetu. Tuliyopata kutoka katika mikusanyiko hiyo naamini kuwa tutayafanyia kazi na yatusaidie kama Kanisa Mahalia la Tabora. Kwenye ngazi ya kiulimwengu tuliunganika pamoja na Waamini wenzetu katika kuhamasishana tukiwa tunafuatilia hitimisho la maadhimisho ya Sinodi ya 16 na ya kawaida ya Maaskofu, iliyokuwa na mada na Kauli Mbiu ya: “Kanisa la Kisinodi – Umoja, Ushiriki na Utume”, iliyoziduliwa mwaka 2021 na kuhitimishwa mwezi Oktoba mwaka huu.  Kama alivyosema Baba Mtakatifu Fransisko, ni kweli mikutano ya Sinodi imehitimishwa lakini roho ya Sinodi hiyo inaendelea na ni lazima ibaki hai katika maisha yetu ya ushuhuda na uenjilishaji wa pamoja. Tukiwa bado tunayaenzi maadhimisho hayo ya Sinodi, Kanisa la kiulimwengu linaalikwa tena na kwa namna ya pekee kushiriki kwenye uzinduzi wa Mwaka wa Jubilei, tendo analofanya Baba Mtakatifu leo tarehe 24 Desemba 2024, kwenye Maadhimisho ya Noeli kwa ufunguzi wa Mlango Mtakatifu wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. 

Kristo Yesu ni Lango la Imani na Matumaini
Kristo Yesu ni Lango la Imani na Matumaini

Sisi kama Jimbo au Kanisa Mahalia (pamoja na Makanisa mbali mbali ulimwenguni) tutaadhimisha ufunguzi wa Mwaka wa Jubilei, Dominika ya tarehe 29 Desemba 2024, ikiwa ni katika maadhimisho ya Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Tayari tumewaalika Waamini wote kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya kwa barua yetu ya tarehe 19 Mwezi huu, ambamo tumetoa maelekezo ya jinsi tutakavyo shiriki kwenye ufunguzi na hata katika maadhimisho mengine yaliyopangwa kwa Mwaka mzima wa Jubilei.  Ndugu zangu, kama anavyosema Baba Mtakatifu kuhusiana na Mwaka huu Mtakatifu: “kwa kila mtu, Jubilei hii iwe ni wasaa wa kukutana kikweli, kibinafsi na Bwana Yesu, “mlango” (rej. Yn. 10:7.9) wa wokovu wetu, ambao Kanisa limeagizwa kumtangaza daima, kila mahali na kwa wote kama ‘tumaini letu’.”  Mwaka wa Jubilei ni Mwaka wa Neema na Mwaka wa Rehema.   Na kwa yote hayo tuliyoyashuhudia Mwaka huu na tutakayoendelea kuyashuhudia tunapoelekea mwisho wa Mwaka, hakika hatuna budi, kama nilivyowaalika kwenye kichwa cha barua hii, kuwa watu wa “Shukrani katika Upendo, Imani na Matumaini.” Tukiongozwa na moyo huo wa Shukrani katika Upendo, Imani na Matumaini tukiwa tumejawa na wingi wa furaha za sherehe ya kuzaliwa kwa Bwana na Mkombozi wetu Yesu Kristo, napenda niwaalike kuwa tayari kufuasa mfano wa mama Bikira Maria aliyeitwa na kuitika akawa tayari daima kuyafanya Mapenzi yake Mungu.  Kwa maneno yake ya “Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyosema” Lk.1:38, Mama Maria alitoa jibu la “Ndiyo Bwana”, likiwa ni jibu chanya na la uhakika akiitikia sauti ya Mungu inayomshirikisha katika mpango wake wa ukombozi. 

Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari
Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari

Mama Maria ameshiriki kwa namna ya pekee katika mpango wa Mungu wa kumkomboa mwanadamu na ulimwengu kwa kumzaa Mkombozi, ndiye huyu Emanueli tunayemshangilia leo na katika kipindi chote cha Noeli.  Nasi tunaalikwa tuwe watu waliotayari daima kusema “Ndiyo Bwana” tukiitikia sauti ya Mungu inayokuja kwetu kupitia katika Kanisa na hata kupitia kwenye matukio mbali mbali ya kila siku.  Tunaweza kufanya hivyo iwapo tutaongozwa na nguvu ya imani, tukisukumwa pia na upendo na matumaini, kama ilivyokuwa kwa Mama Maria na hata kwa wengine wote, waliokuwa tayari kumsikiliza Mungu wakiongozwa na fadhila hizo na hivyo wakaweza kushiriki kikamilifu katika mpango wake wa historia ya wokovu. Ni fadhila hizo zilizomwongoza Baba yetu wa imani, Abramu, akawa tayari kuitikia sauti ya Mungu iliyomuomba aondoke na kwenda asikojua na kweli kuondoka kwake kuliuonesha uwezo wa Mwenyezi Mungu kwa baraka nyingi alizomshushia na kumjalia; “Bwana akamwambia Abramu, toka wewe katika nchi yako na jamaa zako na nyumba ya baba yako uende mpaka nchi nitakayokuonyesha… nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa na kukubariki na kulikuza jina lako”. Mwa. 12:1-2.  “Basi Abramu akaenda kama Bwana alivyomwamuru” Mwa. 12:4. Kama wana Kanisa, tunaitwa wote kushiriki katika kazi ya ukombozi na kila mmoja wetu ataweza kufanya hivyo iwapo hiyo sauti ya “Ndiyo Bwana”, itatoka rohoni mwake na atakuwa tayari kujiweka mikononi mwa huyo anayemwita ili ayafanye mapenzi yake.  Tukifuasa mfano wa Mama Maria nawaalika tuwe watu waliotayari kutoa jibu hilo la “Ndiyo Bwana”.  Kwa namna ya pekee na tukiwa na Roho ya Kanisa la kisinodi, napenda nimwalike kila moja wetu ajisikie na ajione kuwa anawajibika kumsaidia mwenzake kuitikia sauti hiyo ya Mungu anayetuita.  Na hili lituvute tunapoendelea kulijenga Kanisa linaloimarika katika Umoja, Ushirika na Utume.

Neno la Mungu ni taa na dira ya maisha ya waamini.
Neno la Mungu ni taa na dira ya maisha ya waamini.

Tunaitwa kushiriki katika kuifanya kazi ya ukombozi, tukiongozwa na Neno la Mungu, ambalo inabidi tulielewe na baadae tulipeleke kwa watu. Leo tunalipokea Neno hilo kama Emanueli, Mungu aliye pamoja nasi. “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.” Yoh.1:14. Ni hili Neno lenye nguvu ya uhakika na linaloweza kutuongoza katika ukweli wote, na si vinginevyo. Yeye Mwenyewe anatuambia kuwa: “Mimi ndimi njia, na ukweli, na uzima; mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya mimi.” Yoh. 14:6. Yatufikirishe leo hayo tusomayo kutoka katika maandiko matakatifu: “Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga wa njia yangu” Zab.119:105, tunasoma tena, “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili; tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo” Ebr.4:12. Tunaalikwa leo tumpokee huyu Emanueli (Neno) na tumpeleke kwa wengine. Kama ni kuifanya kazi ya kuhubiri, basi tusijihubiri sisi au kuongozwa na hisia zetu na yale tunayoyapenda au wanayoyapenda wana jamii bali matakwa ya Mungu katika ukamilifu wake na katika lugha inayoeleweka kama yeye Neno alivyoyaleta kwetu.  Hili Neno la Mungu litakalotuongoza katika kazi tuzifanyazo yabidi tulipokee kwa imani, tulifahamu vizuri na tulihubiri kwa bidii na ushujaa zaidi, tukizisoma alama za nyakati.  Wachungaji na yeyote aliye na dhamana ya kulitangaza Neno, tusichoke kusisitiza ukweli huu wa kuyajua vizuri Maandiko Matakatifu ambayo ni muhimu katika utume wetu kwa kuyarudia maneno ya Mtaguso wa pili wa Vatikano aliyoyaandika Mtakatifu Hieronimus akisema kuwa “kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomjua Kristo”.  Tusione aibu na tusiwe na woga kulihubiri Neno. Tuongozwe na maneno ya Mtume Paulo aliyomwambia Timoteo: “Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu waliohai na waliokufa, kwa kufunuliwa kwake na kwa ufalme wake: lihubiri neno, uwe tayari wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho”. 2Tim. 4:1-2.  Ni matumaini na mategemeo yangu kuwa tukikuza utume wa Biblia hapa Jimboni tunaweza kujiwekea mikakati na kuona ni kwa namna gani Neno la Mungu litaweza kuyatawala na kuyaongoza maisha yetu kuanzia kwenye familia mpaka kwenye taasisi zetu zinazotuongoza.

Utume wa waamini unakwenda sanjari na Msalaba
Utume wa waamini unakwenda sanjari na Msalaba

Tuwe tayari kumshuhudia Mungu, Neno aliyefanyika mwili akakaa kwetu, katika Mateso. Na kwa namna hiyo tutakuwa tunafuata nyayo zake zinazotupeleka kule anakotaka na alikotuandalia. Yeye Mwenyewe anatuambia: “Mtu yeyote asiyeuchukua Msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.” Lk. 14:27. Tunaposhiriki kwenye utume wa kuukomboa Ulimwengu na Mwanadamu tukiongozwa na huyo Neno hatuwezi kuepuka vikwazo, matatizo na hata wakati mwingine hali ya kukata tamaa, tukifikiri kuwa labda Mungu ametuacha. Hii ndiyo hali waliyokuwanayo hata hao waliomtegemea Mungu kama tunavyosoma katika Maandiko Matakatifu, “Ee Bwana, hata lini utanisahau, hata milele? Hata lini utanificha uso wako? Hata lini nifanye mashauri nafsini mwangu, nikihuzunika moyoni mchana kutwa? Hata lini adui yangu atukuke juu yangu?”. Zab.13:1-2. Nina hakika kuwa hata sisi tunapoumaliza mwaka huu wa 2024, tumeyashuhudia mengi yaliyojitokeza kama changamoto, vikwazo, shida za kiroho na za kimwili na hata kukata tamaa katika maisha na utume wetu ndani ya Kanisa na hata kwenye Jamii tunamoishi.  Yote hayo yatakuwa yameonekana katika nyanja za kiimani, kiuchumi na hata kisiasa. Hatuwezi kuutenganisha utume wetu na mateso au Msalaba. Ni katika Msalaba sisi tumekombolewa.  Kristu aliyezaliwa ili atukomboe alitukomboa si kwa namna nyingine bali kwa njia ya Msalaba na mateso. “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwemo pia ndani ya Kristo Yesu, ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.” Flp. 2:5-8.  Kama Kristu Mwenyewe tunayemfuata na kupenda kushiriki utume wake huo wa kumkomboa mwanadamu na ulimwengu, ameyafanya hayo kwa njia ya mateso na msalaba, hatuna budi nasi kuwa tayari kuipitia njia hiyo.  Hata vile, yeye mwenyewe aliye njia, ukweli na uzima, anatualika tumwendee tunapokuwa na shida na kukata tamaa: “Njoni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.” Mt. 11:28. 

Waamini wawe ni vyombo vya haki, amani na maridhiano
Waamini wawe ni vyombo vya haki, amani na maridhiano

Basi ndugu zangu Katika Kristu, nawaalikeni tuwe tayari kuyapokea mapenzi ya Mungu na tumshukuru Yeye mwenye kutupa neema na nguvu: “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu” Flp. 4:15. Tuwashukuru pia wale wote wanaotutia shime, kwa hali na mali, kutuimarisha kwa sala zao tunapokuwa katika wakati mgumu na katika kushindwa kutimiza mapenzi ya Mungu, na tukishirikiana nao tukaweza kwa namna inayofaa kukabiliana na hayo yanayotusibu na hata kuyashinda. Tunaumaliza mwaka wa 2024 na tunaingia katika mwaka mpya wa 2025. Napenda kwa barua hii niwaalike tuzaliwe upya pamoja na Mtoto Yesu,  kupitia kwa Mama Maria na Mtakatifu Yosefu, msimamizi wa familia Takatifu, tukiwa na nia ya kutaka kushiriki kikamilifu katika utume wa kulijenga Kanisa letu la Tabora, Kanisa la Tanzania na Kanisa la kiulimwengu kwa jibu la “ndiyo Bwana” tutakalopenda daima tulitoe, na hasa tunapodhamiria kubuni kila njia na namna zitakazotuwezesha kulijenga Kanisa letu kwa nguvu zetu na kwa rasilimali zetu, kadiri Mwenyezi Mungu anavyotujalia. Na hii iwe ni Mada yetu Kuu kwa Mwaka tunaoanza wa 2025. Hata kama kuna mwenye mapenzi mema au yeyote yule anayependa kuwa mdau wetu isitufanye kusahau kuwa ni sisi kwanza tunaopaswa kuwajibika. Tumwombe Mama Bikira Maria aliyemleta Mkombozi hapa ulimwenguni, kwa jibu lake la “ndiyo Bwana”, awe nasi akitusindikiza na kutuombea ili nia yetu iwe ni kuitikia kama yeye alivyofanya, nasi tuweze kumleta Mkombozi katika maisha yetu na utume wetu wa kumkomboa mwanadamu na ulimwengu.  Neema na baraka za Mwenyezi Mungu tutakazopata katika kipindi hiki cha Noeli zituingize katika Mwaka Mpya wa 2025 tukiwa wenye nia na nguvu ya kuyafanya Mapenzi yake, tukiimba pamoja na Mzaburi kwa kusema, “Ndipo niliposema, ‘tazama nimekuja katika gombo la chuo nimeandikwa, kuyafanya mapenzi yako. Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu: naam, sheria yako imo moyoni mwangu’.” Zab. 40:7-8.  Mkombozi anayezaliwa ni Mfalme wa Amani. Tuiombee Nchi yetu ya Tanzania Amani na tuyaombee Mataifa yote Amani. Kule kwenye machafuko, kutoelewana, magonvi na vita tumuombe Emanueli, Mfalme wa amani aweke Mkono wake na Amani itawale. 

Shukrani katika upendo, imani na matumaini
Shukrani katika upendo, imani na matumaini

Heri ya Noeli na Baraka za Mwenyezi Mungu kwa Mwaka Mpya.

Imetolewa Tabora, 24 Desemba 2024

+Protase Kardinali Rugambwa

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora.

Kardinali Protase Rugambwa
27 December 2024, 14:42