Nia za Baba Mtakatifu kwa Mwezi Desemba 2024:kwa ajili ya hija ya matumaini!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika nia ya maombi iliyochaguliwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa mwezi wa Desemba 2024 anatoa wito maalum, kwa mtazamo wa Jubile ijayo 2025. Papa anatualika kusali ili Jubilei hii ituimarishe katika imani, na itusaidie kutambua Kristo aliyefufuka katikati ya maisha yetu, na kutugeuza kuwa mahujaji wa matumaini ya Mkristo. Mada ya Video ya Papa kwa mwezi Desemba kwa njia hiyo ni Mahujaji na Matumaini, ambayo inaakisi moja ya nguzo msingi za Upapa wake. Kwa sababu hiyo, Papa Francisko anawaalika waamini wote kuwa mashuhuda wa tumaini la Kikristo katika ulimwengu ambamo kukata tamaa na kutoaminiana kunatawala. Tumaini la Kikristo ni zawadi ya Mungu anayejaza maisha yetu kwa furaha. Na leo hii tunahitaji sana. Na dunia inaihitaji sana! Anasema Papa Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video, aliokabidhi Mtandao wa Nia ya Maombi ya Papa na kutayarishwa kwa ushirikiano na Mtandao wa Kimataifa wa mfuko wa Kipapa na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji.
Mtumbwi na nanga
Wakati wa janga la Uviko- 19 , katika fursa ya Njia ya Msalaba (Statio Orbis )katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, Papa Francisko alikuwa ametumia mfano wa kiinjili wa Mtumbwi katikati ya dhoruba, kukumbusha udhaifu na kuchanganyikiwa kwa ubinadamu katika uso wa majaribu makubwa. Kwa namna fulani, katika nia ya maombi ya mwezi huu wa Desemba Baba Mtakatifu anaturudisha tena kwenye mtumbwi huo, lakini ili kusisitiza umuhimu wa nanga akisindikiza maneno yake kwa ishara ya dhati kuwa: Tumaini ni nanga ambayo unatupa kwa kamba na hiyo inazama kwenye mchanga. Lakini ni lazima hubaki umeshikamana na kamba ya matumaini huku ukiwa umeishilia sana.
Katika nyayo za Ibrahimu
Fadhila ya matumaini inatupatia nguvu nyingi za kutembea katika maisha, alisema Papa Francisko katika Katekesi yake, kunako tarehe 28 Desemba 2016 iliyotolewa kwa ajili ya sura ya Ibrahimu, ambaye kwa upande mmoja hakuogopa kuona ukweli kwa jinsi ulivyo na kwa upande mwingine, alikuwa na uwezo wa kupita zaidi ya mawazo ya kibinadamu, hekima na busara ya ulimwengu, kuamini katika kile ambacho hakiwezekani. Kama Ibrahamu, wahusika wakuu wa Video ya Papa katika mwezi huu wa Desemba 2024, pia walianza safari, kuanzia matatizo yao wenyewe: wasiwasi wa mwanamke aliyekabiliwa ghala kuwa tupu, mashaka ya mwanafunzi juu ya maisha yake ya baadaye. Na kwa hiyo, Tujaze maisha yetu ya kila siku na zawadi ambayo Mungu anatupatia ya matumaini na kuiruhusu iwafikie wale wote wanaoitafuta kupitia sisi,” anasema Baba Mtakatifu katika ujumbe unaoambatana na nia yake ya maombi. Na hivi ndivyo inavyotokea kwa wahusika wakuu wawili wa video na: wote hao wanapata, kwenye njia yao, mahujaji wa matumaini ambao wanawakaribisha na kuwafariji, wakiwaalika kuungana na safari yao ya mfano wa kuelekea Mlango Mtakatifu ambao utabaki wazi kwa Jubilei nzima.
Jubilei 2025, ni mwaliko wa kutembea kwa matumaini ambayo ndiyo mada isemayo Mahujaji wa Matumaini, na itakuwa wakati wa sherehe na tafakari ya kina. Kinachoitwa “Mwaka Mtakatifu” si tu jukwaa la safari ya imani, bali pia ni mwaliko wa kumtambua Kristo katika maisha ya kila siku. Katika barua yake kwa Mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji, Askofu Mkuu Rino Fisichella, Papa Francisko alisisitiza kwamba tukio la janga lilidhoofisha matumaini katika jamii na kwamba sasa "lazima tudumishe uhai wa nuru ya matumaini ambayo tumepewa." Katika muktadha huo, Jubilei inajionesha kama fursa ya kuimarisha tumaini hili na kulishiriki katika ulimwengu unaolihitaji kwa haraka.
Baraza la Kipapa la Uinjilishaji likishirikiana na Mtandao wa Maombi ya Nia ya Papa Kimataifa katika uundaji wa video ya mwezi huu, Askofu Mkuu Rino Fisichella alieleza kuwa, inalenga kuleta ujumbe msingi pia kwa vijana: "Tunashukuru kwa nafasi ya kumuunga mkono Baba Mtakatifu na Mpango wa Video ya Papa juu ya Matumaini kwa kuzingatia Jubilei ya 2025. Siku chache kabla ya kufunguliwa kwa Jubilei ya Kawaida ya karne ya 21, tunakumbuka hata aya ya Zaburi ya 27 iliyowekwa na Papa Francisko kwenye hitimisho la Hati ya kutangaza Mwaka Mtakatifu, ya Spes non confundit isemapo: 'Tumaini kwa Bwana, uwe na nguvu, moyo wako na umtumaini Bwana(Zab 27:14)'. Maneno haya ni mwaliko wa kutojiruhusu kamwe kunyimwa tumaini, katika mabishano yoyote au ugumu fulani wa maisha, hata katika hali ambayo ulimwengu wetu huu unajikuta, leo umejeruhiwa na vita, vurugu na mateso. Tunaomba kwamba kupitia video hii, njia ya mawasiliano iliyoundwa kwa ajili ya vijana, ujumbe ambao tumaini haukatishi tamaa kwa sababu umejengwa juu ya upendo wa Mungu unaoweza kumfikia kila mtu.”