Papa akutana na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko alifanya mkutano wa dakika 30 asubuhi ya tarehe 12 Desemba 2024 na Mahmoud Abbas, Rais wa Serikali ya Palestina. Akizungumza na Roberto Cetera wa Radio Vatican Media, mara baada ya hapo, Rais Abbas alielezea mkutano huo kuwa ulikuwa wenye matunda, na kuongeza kuwa "kila wakati ninapokutana na Papa, ni kama kukutana na rafiki wa zamani". Hata hivyo ulikuwa ni kwa mara ya kwanza viongozi hao wawili kukutana ana kwa ana katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Kwa njia hiyo Rais Abbas alisema kwamba:"Nilimshukuru Baba Mtakatifu kwa maneno yake ya mara kwa mara kuhusu amani katika Mashariki ya Kati na kwa mshikamano anaouonesha daima na raia wa Palestina ambao ni wahanga wa vita huko Gaza." Aidha aliongeza: kusema kuwa: "Nilimwomba aendelee kukuza kutambuliwa kwa Taifa la Palestina katika jumuiya ya kimataifa. Ikiwa amani itapatikana, hakuna mbadala wa suluhisho la serikali mbili."
Taarifa nyingine kuhusu Mkutano mjini Vatican ni “hali mbaya sana ya kibinadamu huko Gaza" ambayo ilijadiliwa katika mikutano hiyo, kama vile matumaini ya kusitishwa kwa mapigano na kuachiliwa kwa mateka wote haraka iwezekanavyo. Jambo jingine muhimu ilikuwa kuhusu "mchango muhimu wa Kanisa Katoliki kwa jamii ya Wapalestina, ikiwa ni pamoja na juhudi zake za sasa za kibinadamu huko Gaza.
Kwa mujibu wa Taarifa kutoka Ofisi ya Habari ya Vyombo vya Habari Vatican pia ilibainisha kuwa mijadala hiyo imefunika umuhimu wa kutekeleza suluhisho la serikali mbili, si kwa vurugu bali kupitia diplomasia na mazungumzo, na umuhimu wa hadhi maalum kwa ajili ya Yerusalemu, ili kwamba iweze kuwa mahali pa urafiki kwa dini kuu tatu za tauhidi. Hatimaye, kuhusu Mwaka Mtakatifu ujao wa Kanisa Katoliki wa 2025 ulijadiliwa, na matumaini yalionyshwa kwamba Mwaka wa Jubilei unaweza kusababisha kurudi kwa mahujaji kwenye Nchi Takatifu.
Kubadilishana kwa zawadi
Mwishoni mwa mkutano wa Papa na Rais Abbas, viongozi hao walipeana zawadi ambapo Papa Francisko alimpatia Rais wa Palestina zawadi kadhaa, ikiwa ni pamoja na ujumbe wake kwa Siku ya Amani Duniani na Kazi ya kisanii iliyoandikwa maneno "Amani ni ua dhaifu."
Rais Abbas naye alimaptia Papa zawadi kadhaa, ikiwa ni pamoja na mchoro ukimuonesha akiwa na Papa na moja inayoonesha Papa wakati wa ziara yake huko Bethlehem mnamo 2014. Pia alimkabidhi Papa sanamu ya Mtakatifu Porphyrius, ambaye ni mtakatifu msimamizi wa Gaza - zawadi kutoka kwa Patriaki Theophilus, Patriaki wa Kiorthodox wa Ugiriki huko Yerusalemu.