Desemba 17,Papa ametimiza miaka 88 ya kuzaliwa,hongera sana!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 17 Desemba 2024 ametimiza miaka 88 ya kuzaliwa. Tangu kuchaguliwa kwake kuwa Papa na kuliongoza Kanisa, Baba Mtakatifu amekuwa daima mtetezi wa haki na amani kwa wanyonge duniani kote huku akijipambanua kuendelea mchakato mzima wa uinjilishaji na utamadunisho kama sehemu ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ambalo kwa msimamo wake, alianzisha mchakato huo wa maandalizi na ambapo kwa miaka mitatu ya Sinodi kuanzia 2021 na ukahitimishwa mwishoni mwa Oktoba 2024. Hatuwezi kusahau juu ya upendo mkuu wa Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na mapambano dhidi ya umaskini ili kulinda na kudumisha misingi ya utu, heshima, haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Katika Ujumbe wake kwa ajili ya amani wa hivi karibuni kwa mwaka 2025, sauti inayosikika ni ile ya kusimama kidete akiomba mataifa yaliyoendelea kusemehe madeni kwa nchi zilizo kusini mwa Ulimwengu, na hivyo kuwa karibu na wanyonge zaidi.
Kuzaliwa- Wakfu
Kwa njia hiyo ndugu msikilizaji, tukirudi katika historia kwa ufupi ya Papa Francisko alizaliwa tarehe 17 Desemba 1936 huko Flores, Buenos Aires, nchini Argentina. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kitawa na Kikasisi, tarehe 13 Desemba 1969 alipewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kunako mwaka 1992 Mtakatifu Yohane Paulo II alimteuwa kuwa Askofu na hatimaye, kuwekwa wakfu kuwa Askofu hapo tarehe 27 Juni 1992. Mtakatifu Yohane Paulo II alimteuwa kuwa Askofu mkuu tarehe 22 Februari 1998 na hatimaye, kama Kardinali tarehe 21 Februari 2001.
Upapa
Ilikuwa ni tarehe 13 Machi 2013, Kardinali Georgio Mario Bergoglio alichaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kuanza utume wake rasmi tarehe 19 Machi 2013, katika Siku ambayo Mama Kanisa anaadhimisha Siku Kuu ya Mtakatifu Yosefu, Mlezi wa Yesu. Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro,ameongoza Kanisa kwa upendo wa kibaba. Hata hivyo ujumbe mwingi umefika kutoka sehemu mbalimbli za dunia, na zaidi kuanza na matashi mema ambayo akiwa katika Ndege ya kurudi kutoka Ziara ya Kitume huko Ajaccio, Corsica, waandishi wa habari walimtakia heri na baraka tele.
Siku yake kama Baba haitilii maandani kupita kiasi lakini hiyo haiwezekani kuepusha wingi wa matashi mema kutoka Kanisa zima na ulimwengu wote, kama ishara ya upendo na shukrani kwake kwa siku hii muhimu ya kumbukizi. Kiukweli tunapaswa kumshukuru sana kwa karibu miaka hii kumi na mbili ya upapa wake, ambamo aliongoza Mtumbwi wa Mtume Petro kwa mkono thabiti lakini wakati huo huo wenye upendo, hata wakati maji ya bahari yakichafuka kutokana na pepo za dhoruba.
Kwa hiyo tunaweza kumshukuru Baba Mtakatifu kwa mwengi zadi. Asante kuweka kipaumbele cha mtazamo wetu wa sura ya Mungu wa huruma, ambaye “anasamehe kila kitu na kusamehe daima, (todos todos todos,) kama ambavyo anasema kila wakati. Asante kwa “kufungua milango ya Kanisa kwa wote.” Asante kwa kukuza “sauti ya maskini na waliofukuzwa duniani kote, kuomba haki, mkate na kazi kwa ajili yao pia.” Asante kwa “kupinga kila mara mantiki ya vita kama chombo cha kusuluhisha mizozo ya kimataifa, na biashara ya silaha inayoichochea, ikitajirisha walio wachache tu na kusababisha vifo na huzuni kwa watu wote.” Asante Papa kwa kuwa “jirani na mwenzi wa kusafiri wa kila mwanamume na mwanamke wa wakati wetu, sio tu na safari za kimataifa kama ambavyo amerejea hivi karibuni kutoka Ziara ya 47 ya Kitume, na fupi zaidi ukilinganisha na zilizotangulia, Dominika tarehe 15 Desemba 2024, lakini pia na mikutano, na ishara, ambapo ubinadamu wake uliofurika na ubaba wenye kuzaa huibuka hata akiwa na umri wa miaka 88.
Asante kwa kutetea maisha kila wakati, kukemea utamaduni wa kutupa na kubagua, katikati ya bahari, wanaotoa mimba au katika kuwaacha walio katika awamu ya mwisho wa maisha. Asante kwa kulinda nyumba yetu ya kawaida kutokana na mashambulizi ya kizembe ya ubinafsi wa kibinadamu. Asante, Baba Mtakatifu Francisko kwa kuliongoza Kanisa hadi kwenye kizingiti cha Jubilei mpya, yenye haki ya Matumaini, ile fadhila ambayo ulimwengu wa leo unakosa na ambayo badala yake ni dada mdogo asiyeweza kubadilishwa, anayeweza kuvuta hata aliye mkuu zaidi na imani na mapendo.
Siku chache zijazo Papa Francisko mwenye umri wa miaka 88 atafungua Mlango Mtakatifu wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, na kuanzia kipindi cha Jubilei. Hongera sana Baba Mtakatifu. Kwa matashi bora ya Idhaa ya Kiingereza, Kiswahili na Idhaa zote za Radio Vatican, tunamtakia heri nyingi . Katika mioyo ya kila mmoja wetu, kuuruhusu Moyo wa Yesu uingie, ambaye kama alivyoandika katika waraka wake wa hiti karibuni wa dilexit nos, kwamba alitupenda na anaendelea kutupenda bila mwisho. Na Sisis tunampenda Kiongozi Mkuu wa Kanisa lote.