Tafuta

2025.01.01 Kardinali Angelo Amato ameaga dunia 2025.01.01 Kardinali Angelo Amato ameaga dunia 

Kardinali Angelo Amato ameaga dunia akiwa na miaka 86

Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Watakatifu ameaga dunia,akiwa na umri wa miaka 86 tarehe 31 Desemba 2024. Ni mzawa wa Molfetta na mwanashirikia wa Kisalesiani.

Vatican News 

Jumanne tarehe 31 Desemba 2024, Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Watakatifu aliaga dunia akiwa na  umri wa miaka 86. Alikuwa Mzaliwa wa Molfetta (Bari), tarehe 8 Juni 1938, katika familia ya wajenzi wa meli, mtoto wa kwanza kati ya watoto wanne, alianza masomo yake katika Taasisi ya Nautical ya Bari, katika sehemu ya manahodha wa muda mrefu. Lakini mwanzoni mwa mwaka wa tatu wa masomo, mnamo Oktoba 1953, aliamua kuachana na kazi hii ili kujiunga na Shirika la Wasalesian wa Torre Annunziata. Mnamo 1956, alianza huduma yake ya kidini. Baada ya kuhamia Roma, alisoma katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Salesian akapata leseni ya falsafa. Mnamo 1962 alifanya taaluma yake ya kudumu ya kidini, akianza kutekeleza miaka miwili ya mafunzo ya vitendo katika chuo cha Salesian huko Cisternino (Brindisi), ambapo alifundisha fasihi katika shule ya Sekondari. Baada ya kupata leseni ya taalimungu  kutoka kitivo cha taalimungu  cha Chuo Kikuu cha Salesian huko Roma, alipewa daraja la Upadre  tarehe 22 Desemba 1967.

Mkutano na ulimwengu wa Kiorthodox wa Uigiriki

Baada ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian, alipata udaktari wa taalimungu mwaka 1974 na mara moja aliitwa kufundisha somo hilo. Mnamo 1977 alitumwa Ugiriki na iliyokuwa Sekretarieti ya Umoja wa Kikristo, alitumia miezi minne katika makao ya Wajesuit ya Athene kwa ajili ya maandalizi ya lugha kwa mtazamo wa kujiunga na chuo kikuu. Baada ya kufaulu mtihani wa kuingia (ulioandikwa na kuzungumzwa Kigiriki cha kisasa), alihamia Thesaloniki kama mfadhili wa masomo ya Upatriaki wa  Constantinople. Yeye alikuwa anaishi huko Monì Vlatadon(Makao ya Watawa ya Vlatadon), nyumbani ya watawa wa Kiorthodox na Idrima ton Paterikon Meleton (Taasisi ya Mafunzo ya Mababa wa Kanisa ), yenye maktaba maalumu kwa taalimungu ya Kiorthodox na mkusanyiko wa thamani wa filamu ndogo ndogo za maandishi ya Mlima Athos. Kisha akajiandikisha katika kitivo cha taalimungu cha Chuo Kikuu cha Thesaloniki, kufuatia masomo juu ya historia ya mafundisho ya kweli ya Jannis Kaloghirou na yale ya mafundisho ya kimfumo ya Jannis Romanidis. Wakati huo huo, alifanya utafiti juu ya sakramenti ya toba katika taalimungu ya Kiorthodox ya Uigiriki kutoka karne ya 16 hadi 20, ambayo ilichapishwa katika safu ya Análekta Vlatádon (1982).

Kurudi Roma

Aliporejea Roma, alifundisha Ukristo katika kitivo cha taalimungu cha Chuo Kikuu cha Kipapa cha Salesian, ambacho alikuwa mkuu wake kuanzia 1981 hadi 1987 na kuanzia 1994 hadi 1999. Katika miaka ya 1997-2000 pia alikuwa makamu wa mkurugenzi wa Chuo Kikuu hicho. Mnamo 1988 alitumwa Washington kusoma taalimungu ya dini na kukamilisha mwongozo wa Ukristo. Kisha akateuliwa kuwa mshauri wa Baraza la Kipapa ma Mafundisho Tanzu ya kanisa, Mabaraza ya Kipapa kwa ajili ya kukuza Umoja wa Wakristo na Majadiliano ya kidini, na pia Kansela wa  Chuo cha Kipapa cha Kimataifa cha Maria. Mnamo 1999 aliteuliwa kuwa katibu mkuu wa Chuo cha Kipapa cha Taalimungu kilichorekebishwa na mkurugenzi wa jarida jipya la taalimungu  la Path. Kuanzia 1996 hadi 2000 alikuwa sehemu ya tume ya kitaalimungu-kihistoria ya Jubilei kuu ya Mwaka wa 2000.

Katibu wa Mafundisho Tanzu ya Kanisa

Aliteuliwa mnamo tarehe 19 Desemba 2002 kuwa katibu wa Baraza la Kipapa la  Mafundisho Tnzu ya Kanisa  na kuchaguliwa kwa Jimbo la Sila lenye cheo cha kibinafsi cha Askofu mkuu, alipewa  wakfu tarehe 6 Januari 2003 kutoka kwa Papa Yohane Paulo II katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Mkuu wa Baraza la Kipapa la kuwatazangaza  Watakatifu

Tarehe 9 Julai 2008, Benedikto XVI alimwita kurithi nafasi ya Kardinali José Saraiva Martins kama Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza  Watakatifu na katika Mkutano wa Makardinali tarehe 20 Novemba 2010 aliundwa kuwa Kardinali wa Ushemasi wa Mtakatifu Maria huko Aquiro. Alishiriki katika mkutano wa Uchaguzi mnamo  Machi 2013 uliomchagua Papa Francisko. Tarehe 19 Desemba 2013, Papa Francisko alimthibitisha "donec aliter provideatur" kama Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza watakatifu nafasi ambayo aliiacha mwaka 2018 kabla tu ya kufikisha miaka 80.

Kardinali Amato na Don Tonino Bello

Mnamo Novemba 2013, Kardinali Amato alifunga awamu ya Jimbo  ya kutangazwa kuwa Mwenyeheri na kumtangaza Don Tonino Bello kuwa mtakatifu katika Kanisa Kuu la Molfetta. "Uhuru wa mawazo na matendo, kustahiwa kwa waamini, elimu kwa vijana, thamani ya amani, upendo kwa wengine, kuzingatia maskini - anasema kardinali - ni mafundisho" ya Don Tonino, askofu wa Molfetta kutoka 1982 hadi. 1986. Ushuhuda wake - Kardinali Amato alikuwa amesisitiza - anatuambia kwamba "utakatifu si fursa ya wachache, lakini wito kwa wote", kwa sababu sisi sote tunaitwa kufuata "Yesu na fadhila za kitheolojia: imani, tumaini na mapendo".

Askofu wa Molfetta: "mtu wa imani na mchungaji asiyechoka"

Askofu wa Molfetta, Monsinyo Domenico Cornacchia, pamoja na Jimbo nzima, anamkumbuka “kwa shukurani nyingi” Kardinali Amato kuwa ni “mtu wa imani na mchungaji asiyechoka, ambaye alitumikia Kanisa la ulimwengu wote na watu wa Mungu kwa kujitolea sana”.

01 January 2025, 12:03