Tarehe 16 Juni 2020 Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika Tarehe 16 Juni 2020 Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika 

Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika 16 Juni 2020

Kunako Mwaka 1991, Wakuu wa OAU walianzisha Siku ya Mtoto wa Afrika kama kumbukumbu ya uasi dhidi ya wanafunzi uliotokea hapo tarehe 16 Juni 1976 huko Soweto, Afrika Kusini. Wakati huo, wanafunzi waliandamana, mosi kupinga mfumo na elimu duni waliokuwa wanapatiwa. Pili, waliitaka Serikali ya kibaguzi ya Afrika ya Kusini kuboresha mfumo wa lugha ya kufundishia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa viongozi wa Serikali na wanadiplomasia wakati wa hija yake ya kitume nchini Thailand alisema kwamba, Jumuiya ya Kimataifa kwa Mwaka 2019 ilikuwa inaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 30 ya Tamko la Haki ya Mtoto Duniani. Hii ni changamoto endelevu kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kuendeleza haki msingi za watoto; utu na heshima yao kama binadamu. Watoto wajengewe mazingira mazuri ya maisha, kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao kiroho, kimwili, kisaikolojia na kiakili. Matumaini ya kesho iliyo bora zaidi yanafumbatwa kwa namna ya pekee, katika huduma kwa watoto. Leo hii jamii inawahitaji wajenzi wa ukarimu, watu wanaoweza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kukoleza mchakato wa maendeleo fungamani katika familia ya binadamu kwa kuzama zaidi katika misingi ya haki, mshikamano, udugu wa kibinadamu na utulivu. Kila mmoja anapaswa kuchangia katika: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Kunako Mwaka 1991, Wakuu wa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika, OAU walianzisha Siku ya Mtoto wa Afrika kama kumbukumbu ya uasi dhidi ya wanafunzi uliotokea hapo tarehe 16 Juni 1976 huko Soweto, Afrika Kusini. Wakati huo, wanafunzi watoto wadogo waliandamana, mosi kupinga mfumo na elimu duni waliokuwa wanapatiwa. Pili, waliitaka Serikali ya kibaguzi ya Afrika ya Kusini kuboresha mfumo wa lugha ya kufundishia. Siku ya Mtoto wa Afrika hutumika kuwakumbusha watoto wetu hatua ya kijasiri waliyoichukua wenzao huko Afrika Kusini katika kulinda utu, heshima na haki zao msingi. Watoto wanakumbushwa kwamba wanaweza kuleta mabadiliko hata wakiwa wadogo. Hii ni Siku ya Kimataifa inayopania kuboresha hali na mazingira ya elimu kwa watoto Barani Afrika.

Kwa hivyo, Hivyo Siku Ya Mtoto wa Afrika inaadhimishwa kwa kuangalia maslahi mapana ya watoto wa Afrika na inawapasa watu wazima kujitolea kwa hali na mali katika nafasi zao ili kushughulikia changamoto nyingi zinazokabili watoto katika Bara zima la Afrika. Watoto wanapaswa kulindwa dhidi ya ukatili na unyama wanaoweza kutendewa ndani na nje ya familia zao. Watoto wanapaswa kuepushwa ndoa na mimba za utotoni kwa kupewa na kurithishwa maadili mema. Kipindi cha janga la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, takwimu zinaonesha kwamba, kuna idadi kubwa ya watoto waliopata mimba kwa sababu ya kukaa muda mrefu majumbani mwao. Wazazi wanapaswa kuwajibika kikamilifu juu ya ulinzi na tunza ya watoto wao. Watoto wanapaswa kuepushwa na vishawishi kwa kuhakikisha kwamba, wanapata mahitaji yao msingi kwa wakati. Wafundwe pia kuwa na kiasi kwani katika maisha hawataweza kupata kila kitu wanachohitaji. Watoto wafundishwe umuhimu wa kuwa na nidhamu katika maisha! Waswahili wanasema, watoto wakilindwa vyema, watawaheshimu na kuwakumbuka wazazi wao!

Tunakumbushana kuwa ili kuyafikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030, ipo haja ya kuhakikisha kwamba 'hakuna mtoto anayeachwa nyuma' kwa kuongeza nguvu ili kuwafikia watoto hasa wale wasiofaidika na kukua na maendeleo ya Tanzania. Hivyo, kanuni kuu ni maendeleo ya pamoja kwa watoto, yaani, wakati wowote wa kuandaa mipango na sera za kutekeleza Agenda 2030, watoto wanapaswa kuwa ndani ya mipango ili 'kuhakikisha kwamba hakuna mtoto anaachwa nyuma' katika kuendesha maendeleo ya uchumi fungamani. Wazazi watambue kuwa familia ndio taasisi ya kwanza kuweka msingi wa maendeleo ya watoto kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa yaliyosainiwa na mataifa yaliyo mengi. Mataifa yanapokaa na kukubaliana malengo kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watoto humaanishi kuwa serikali na wadau wamaendeleo wanao wajibu kuyatekeleza, lakini zaidi sisi wazazi na jamii kuanzia katika ngazi ya familia nasi tunayo sehemu ya kutekeleza. Vinginevyo familia zetu zitaachwa nyuma.    

Takwimu za kituo cha Huduma ya Simu kwa Mtoto nchini Tanzania zinaonyesha watoto wamekuwa wakipitia magumu ikiwemo vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia, utelekezwaji, vipigo, utumikishwaji wa kazi ngumu, mimba na ndoa za utotoni ambapo yote haya yanakatiza ndoto zao za kimakuzi na mendeleo. Vitendo hivi hufanywa na ndugu zetu, jamaa zetu na sisi wenyewe wazazi. Namna hii mchango wetu katika maendeleo ya watoto wetu ni hasi. Hawawezi kushindana na watoto wanaolelewa katika mataifa yaliyocharuka mathalani Uchina na kwingineko. Tunaweza kubadili hili kwa kuongeza umakini katika malezi ya watoto wetu. Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yawakumbushe viongozi, wananchi na vyombo vya habari kuwa maendeleo ya taifa lolote lile hayawezi kupiga hatua mbele bila kutilia maanani mahitaji ya watoto, ikiwa ni pamoja na watoto maskini, wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi.

 

Siku ya Mtoto wa Afrika 2020
16 June 2020, 13:38