Mashirika ya Umoja wa Mataifa tarehe 13 Julai 2020 yamezindua taarifa ya hali ya chakula na lishe kwa mwaka 2019: Kuna hatari ya watu zaidi milioni 132 kukumbwa na baa la njaa duniani kwa mwaka 2020. Mashirika ya Umoja wa Mataifa tarehe 13 Julai 2020 yamezindua taarifa ya hali ya chakula na lishe kwa mwaka 2019: Kuna hatari ya watu zaidi milioni 132 kukumbwa na baa la njaa duniani kwa mwaka 2020. 

Taarifa ya Hali ya Usalama wa Chakula na Lishe kwa Mwaka 2019

Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2020 kutokana na janga kubwa laCOVID-19, inakadiriwa kwamba watu zaidi ya milioni 130 wanaweza kushambuliwa na baa la njaa. Katika kipindi cha mwaka 2019, watoto zaidi ya milioni 191 waliokuwa na umri chini ya miaka 5 wamekumbwa na ugonjwa wa utapiamlo, hali ambayo imepelekea watoto hawa kudumaa katika makuzi yao. Njaa inakuja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaani: Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuendeleza Kilimo na Chakula IFAD pamoja na Shirika la Afya Duniani, WHO, tarehe 13 Julai 2020, yametoa taarifa ya pamoja kuhusu usalama wa chakula na lishe duniani kwa mwaka 2019-2020. Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030 ni mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inajizatiti katika kutokomeza umaskini, baa la njaa na magonjwa duniani. Watu wanapaswa kupatiwa elimu bora, kwa kuhakikisha usawa wa kijinsia pamoja na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wote. Jumuiya ya Kimataifa inataka kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na upatikanaji wa maji safi na salama; nishati mbadala kwa gharama nafuu pamoja na uwepo wa mipango bora ya miji na makazi ya watu, ili kudumisha usalama na upatikanaji wa maendeleo fungamani ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe kulinda mazingira pamoja na kudumisha amani duniani!

Taarifa inaonesha kwamba, zaidi ya watu milioni 690 wameshambuliwa na baa la njaa duniani katika kipindi cha mwaka 2019, hili likiwa ni ongezeko la watu milioni 10 zaidi, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kwa Mwaka 2018. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2020 kutokana na janga kubwa la ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, inakadiriwa kwamba watu zaidi ya milioni 130 wanaweza kushambuliwa na baa la njaa. Takwimu zinabainisha kwamba,  katika kipindi cha mwaka 2019, watoto zaidi ya milioni 191 waliokuwa na umri chini ya miaka 5 wamekumbwa na ugonjwa wa utapiamlo, hali ambayo imepelekea watoto hawa kudumaa katika makuzi yao. Wakati huo huo watoto milioni 38 chini ya umri wa miaka 5 walikuwa na upungufu mkubwa wa uzito. Takwimu za Mashirika ya Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, waathirika wakubwa wa baa la njaa duniani ni watu kutoka: Barani Asia, Afrika, Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean.

Hii ina maana kwamba, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita yaani kuanzia mwaka 2014, kumekuwepo na ongezeko la idadi ya watu sanjari na baa la njaa duniani. Angalisho limetolewa kwa watu wa Mungu Barani Afrika, kuwa macho zaidi kwani takwimu zinaonesha kwamba, hadi kufikia mwaka 2030, nusu ya waathirika wa baa la njaa duniani watakuwa ni kutoka Barani Afrika. Janga la Virusi vya Corona, COVID-19 limesababisha madhara makubwa katika sekta ya kilim ona matokeo yake usalama wa chakula na lishe, uko mashakani kutokana na kuporomoka kwa uchumi kitaifa na kimataifa. Hali imesababisha uzalishaji, ugavi na ulaji kuathirika kwa kiasi kikubwa. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2020, watu zaidi ya milioni 132 wanaweza kukumbwa na baa la njaa na utapiamlo duniani. Kutokana na hali hii, Jumuiya ya Kimataifa inajikuta njia panda katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030 hasa katika mchakato wa kupambana na baa la njaa na utapiamlo duniani. Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanawataka wananchi kubadili tabia mbaya ya ulaji ili kuweza kuwa na uhakika wa usalama wa chakula na lishe duniani.

Bei ya mazao ya chakula inaendelea kupanda, hali inayowafanya baadhi ya watu kushindwa kumudu gharama hizi. Ili kuweza kuwa na uhakika wa usalama wa chakula na lishe duniani, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, kila mwaka walau kiasi cha dola za kimarekani bilioni 1, 300 zinapatikana pamoja na kuendelea kudhibiti uzalishaji wa hewa ya ukaa inayogharimu kiasi cha dola za Kimarekani 1, 7000. Watu wajenge na kudumisha utamaduni wa kujipatia lishe bora kwa ajili ya afya na kuondokana na tabia ya kutaka “kujaza matumbo”. Serikali hazina budi kuwa makini ili kuratibu mambo yanayopelekea ongezeko la bei ya mazao ya chakula tangu wakati wa uzalishaji, hifadhi ya mazao yenyewe, usafirishaji, ugawi na ulaji wake. Watu wajenge utamaduni wa kutunza chakula, huku wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa chakula na lishe ya watoto wadogo. Watu wakitahidi kubadili mtindo wa ulaji wao kwa kujibidiisha kuwana habari muhimu kuhusu chakula na lishe bora. Changamoto na tatizo la usalama wa chakula na lishe linapaswa kuwa ni sehemu sera na mikakati ya kitaifa na kimataifa, ili hatimaye, kuibua mbinu mkakati wa uwekezaji katika uzalishaji wa mazao ya chakula, ili kuwa na uhakika wa usalama wa chakula na lishe duniani!

Usalama wa Chakula 2019

 

 

 

14 July 2020, 13:55