Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania tarehe 23 Septemba 2021 amehutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu: UVIKO-19, Usawa wa Kijinsia, Mabadiliko ya Tabianchi na Vijana. Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania tarehe 23 Septemba 2021 amehutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu: UVIKO-19, Usawa wa Kijinsia, Mabadiliko ya Tabianchi na Vijana. 

Hotuba ya Rais Samia Kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Sept. 2021

Tanzania kwa kuzingatia misingi ya haki, amani na kuheshimiana, itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa ili kuijenga dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Rais Samia katika hotuba yake, amegusia kuhusu Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na athari zake katika uchumi wa Tanzania, Usawa wa kijinsia, Mabadiliko ya Tabianchi pamoja na maendeleo ya vijana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican. 

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, Alhamisi tarehe 23 Julai 2021 amelihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, New York nchini Marekani, UNGA76, ikiwa ni mara yake ya kwanza kabisa tangu ashike madaraka mwezi Machi, 2021 kufuatia kifo cha Rais wa awamu ya tano Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, aliyefariki dunia tarehe 17 Machi 2021. Amewashukuru viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa waliotuma salam zao za rambirambi kwa watanzania kufuatia msiba huu mzito. Ameushukuru Umoja wa Mataifa kwa kutenga tarehe 16 Aprili 2021 siku maalum kwa ajili ya kumuenzi Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kutokana na mchango wake mkubwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi. Ushiriki wa Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ni katika mustakabali wa kukabiliana na changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza katika uso wa dunia. Tanzania kwa kuzingatia misingi ya haki, amani na kuheshimiana, itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa ili kuijenga dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Rais Samia katika hotuba yake, amegusia kuhusu Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 na athari zake katika uchumi wa Tanzania, Usawa wa kijinsia, Mabadiliko ya Tabianchi pamoja na maendeleo ya vijana wa kizazi kipya! Rais Samia Suluhu Hassan ameyashukuru: Shirika la Fedha Duniani (IMF) pamoja na Shirika la Afya Duniani, WHO, kwa kusaidia kuinua uchumi wa Tanzania na kuokoa maisha ya watanzania wengi, kwa kujiunga na mpango wa COVAX ili kupata chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Kampeni ya chanzo ilizinduliwa rasmi mwezi Julai, 2021 na chanjo inaendelea kutolewa kwa hiyari. UVIKO-19 ni ugonjwa unaosambaa kwa kasi kubwa, ikilinganishwa na uzalishaji na ugavi wa chanjo dhidi ya UVIKO-19. Lengo la Shirika la Afya Duniani, WHO hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2021 lilikuwa ni kutoa chanjo kwa asilimia 40% ya wananchi wote katika kila nchi na asilimia 70% ifikao kati kati ya mwaka 2022. Lakini ukweli wa mambo ni kwamba, hadi sasa nchi nyingi zinazoendelea duniani, zimefanikiwa kutoa chanjo kwa watu wake kwa asilimia 2%. Kumbe, kuna haja ya kushirikishana chanjo, ili watu wengi waweze kupata chanjo na kwamba, chanjo hizi zizalishwe hata kwenye Nchi Zinazoendelea duniani, jambo muhimu sana katika kuokoa maisha ya watu wengi duniani.

Rais Samia Suluhu Hassan amesema, uchumi wa Tanzania ulikuwa unakuwa kwa asilimia 6.9% kabla ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 lakini kwa sasa uchumi wa Tanzania unakuwa kwa asilimia 5.4.% Serikali kwa sasa inajitahidi kufufua sekta ya utalii ambayo iliathirika sana na janga la UVIKO-19. Serikali ya Tanzania inaendelea kuboresha mazingira ya biashara, kwa kuwavutia wawekezaji zaidi; kwa kuimarisha utawala bora, amani na utulivu pamoja na kuzingatia utawala wa sheria na haki msingi za binadamu! Rais Samia Suluhu Hassan amegusia pia kuhusu: Usawa wa kijinsia, Mabadiliko ya Tabianchi pamoja na maendeleo ya vijana wa kizazi kipya! Rais Samia Suluhu Hassan ni mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Tanzania, kumbe usawa wa kijinsia ni kati ya ajenda nzito anazobeba mabegani mwake na kwamba, Tanzania itaendelea kusimama kidete kupigania haki msingi za binadamu, haki za kiuchumi za wanawake pamoja na kuwawezesha wanawake kiuchumi, ili kupunguza umaskini miongoni mwa wanawake na wasichana.

Kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi, Tanzania inatumia kati ya asilimia 2% - 3% ya Pato Ghafi la Taifa, GDP ili kupambana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Ni katika muktadha huu, Tanzania inaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inashikamana kwa dhati ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutekeleza kwa vitendo makubaliano ya Mkutano wa 21 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, Cop21 uliofanyika mjini Paris, nchini Ufaransa, kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2015. Nchi tajiri zaidi duniani zilikuwa zimeahidi kuchangia walau kiasi cha dola za kimarekani bilioni 100 hadi kufikia mwaka 2025. Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania mwishoni mwa hotuba yake amekaza kusema, Tanzania itaendelea kuunga mkono juhudi za Umoja wa Mataifa. Maambukizi makubwa ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 yamekuwa ni fundisho kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na kushikamana, kama sehemu ya mchakato wa kukabiliana na changamoto mamboleo! Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na ujumbe wake, wanaendelea kushiriki katika mikutano mingine kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Rais Samia Suluhu Hassan amesema hali ya kupanda kwa joto nchini Tanzania imesababisha ukame, ambao umesababisha madhara makubwa kwa sekta zinazotegemea maliasili ambazo ni kilimo, uvuvi na misitu zinazochangia asilimia 30% ya Pato la Taifa na kuathiri asilimia 60% ya wananchi wa Tanzania. Ujumbe wa Tanzania unashiriki pia katika mkutano wa Maendeleo ya Mifumo ya Chakula mintarafu Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kufikia mwaka 2030. Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuzalisha chakula kingi na cha kutosha mahitaji ya watu duniani lakini kwa bahati mbaya bado kuna umati mkubwa wa watu unaopekenywa kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha, ukosefu wa maji safi na salama pamoja na tiba muafaka kwa magonjwa yanayowasumbua binadamu. Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa Mwaka 2021 unawashirikisha wakuu wa nchi zaidi ya 100 na wengine wanashiriki kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii hasa kutokana na hofu ya maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19.

Rais Samia UNGA76
24 September 2021, 12:50