Mahojiano maalum na Balozi Liberata Mulamula Rutageruka kuhusu mkutano wa tatu wa ushirikiano kati ya Italia na Nchi za Bara la Afrika. Mahojiano maalum na Balozi Liberata Mulamula Rutageruka kuhusu mkutano wa tatu wa ushirikiano kati ya Italia na Nchi za Bara la Afrika. 

Mahojiano Maalum na Balozi Mulamula: Mkutano wa Afrika na Italia

Balozi Liberata Mulamula Rutageruka katika mahojiano maalum na Radio Vatican amesema, Italia kama Rais wa G20 inaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika masuala mtambuka yaani: Afya mkazo ukiwa ni kwenye Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, Elimu; Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Italia ambayo kwa sasa ni Rais wa G20 yaani nchi 20 zinazoongoza kiuchumi duniani, tarehe 8 Oktoba 2021 ilifanya mkutano wa tatu wa Mawaziri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa Kimataifa kutoka katika nchi 54 za Bara la Afrika. Mambo makuu matatu yalipewa kipaumbele cha kwanza yaani “People, Planet and Prosperity” yaani “Watu, Sayari na Ustawi.” Katika hotuba yake elekezi, Rais Sergio Mattarella wa Italia pamoja na mambo mengine alikazia umuhimu wa ugavi sawa wa chanjo dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 sanjari na kulijengea Bara la Afrika uwezo wa kutengeneza chanjo hizi Barani Afrika. Italia inatarajia kuwekeza kiasi cha Euro Bilioni moja, ili kuliwezesha Bara la Afrika kutengeneza chanjo dhidi ya UVIKO-19 Barani Afrika. Serikali za Bara la Afrika hazina budi kujifunga kibwebwe ili kudhibiti wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka Barani Afrika na kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na kushikamana kwa dhati katika mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi. Nchi za G20 zinatambua umuhimu wa Bara la Afrika katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kumbe, kuna haja pia ya kushikamana katika mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi na misimamo ya siasa kali, mambo yanayodhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Umoja wa Afrika utakuwa ni mshiriki mwenza kwenye mikutano ya G20 kuanzia tarehe 31 Oktoba 2021. Balozi Liberata Mulamula Rutageruka (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki aliiwakilisha Tanzania katika mkutano huu. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican anazungumzia mambo msingi yaliyojiri katika mkutano huu kadiri ya mustakabali wa Afrika na Tanzania katika ujumla wake. Balozi Liberata Mulamula Rutageruka amesema, Italia kama Rais wa G20 inaendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika masuala mtambuka yaani: Afya mkazo ukiwa ni kwenye Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, Elimu; Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi. Mkutano umefanikiwa kuwakutanisha Mawaziri kutoka katika nchi 54 za Bara la Afrika pamoja na wenyeji wao Italia. Italia imekuwa na uhusiano wa karibu sana na Tanzania kwa zaidi ya miaka 50 iliyopita. Italia imekuwa ni mdau mkubwa wa maendeleo fungamani ya binadamu hususan katika sekta ya elimu na afya pamoja na kuchangia rasilimali fedha na watu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, Bara la Afrika halikupewa kipaumbele cha pekee katika mchakato wa ugavi wa chanjo dhidi ya UVIKO-19. Mgao kwa Bara la Afrika ulikuwa ni “kiduchu sana”. Lakini, ikumbukwe kwamba, usalama wa Bara la Ulaya dhidi ya UVIKO-19 unategemea na jinsi ambavyo nchi za Ulaya zinavyotoa kipaumbele cha pekee kwa Bara la Afrika, kamwe lisiache nyuma. Lakini jambo kubwa zaidi ni Afrika kujengewa uwezo wa kuzalisha chanjo hizi ili kuondokana na tabia ya “ombaomba” ambayo ni hatari kwa mustakabali wa Bara la Afrika. Makampuni makubwa ya dawa yatowe vibali vya kuzalisha na kusambaza chanjo hizi Barani Afrika. Italia imesema, itaendelea kuragibisha wazo hili. Usalama na uhakika wa chakula ni tema ambayo pia ilipewa uzito wa pekee kutokana na athari zake kwa ustawi, maendeleo na mafao ya Bara la Afrika. Uhaba wa chakula kwa sehemu kubwa ni matokeo ya athari za mabadiliko ya tabianchi. Mafuriko na ukame wa kutisha ni mambo yanayoendelea kudhalilisha ut una heshima ya watu wengi kutokana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha.

Uhakika na usalama wa chakula unavihusisha hata viwanda vya kusindika mazao ya wakulima ili kuongeza thamani ya mazao, ili Afrika iweze walau kujitosheleza kwa mazao ya chakula sanjari na kuwa na uhakika wa soko la mazao ya biashara yanayozalishwa Barani Afrika. Balozi Liberata Mulamula Rutageruka katika mahojiano maalum na Radio Vatican anakaza kusema, Bara la Afrika katika mkutano wa mwaka 2021, likekuja kwa kujiamini kabisa, kwa kutambua kwamba, hata G20 kwa kiasi kikubwa zinalitegemea Bara la Afrika kwa ajili ya kupata malighafi na soko la bidhaa zake. Bara la Afrika lina idadi ya watu zaidi ya bilioni moja, ambalo kimsingi ni soko la uhakika kwa bidhaa zinazozaliwa Barani Ulaya. Yote haya yanaonesha umuhimu wa ushirikiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa. Ni katika muktadha huu, Umoja wa Afrika utaanza kushiriki mikutano ya G20 kama mdau wa kutegemewa na wala si kama mtazamaji kama ilivyokuwa hapo awali.

 

Mahojiano maalum na Balozi Liberata Mulamula Rutageruka kuhusu mkutano wa tatu wa ushirikiano kati ya Italia na Nchi za Bara la Afrika.
Mahojiano maalum na Balozi Liberata Mulamula Rutageruka kuhusu mkutano wa tatu wa ushirikiano kati ya Italia na Nchi za Bara la Afrika.

Ili kufanikisha utekelezaji wa Sera hii kwa ukamilifu, kunahitajika ushiriki wa wadau wote wa elimu na mafunzo katika ngazi zote, ikiwemo sekta binafsi, Asasi za Kiraia (AZAKI) na washirika wengine wa maendeleo. Ni katika muktadha huu wa dira ya maendeleo kitaifa, Italia imechangia sana katika mpango wa elimu ya ufundi na soko la ajira. Lengo ni kuwajengea vijana uwezo wa kitaaluma, ili wapate ajira na hatimaye, kuchangia katika mchakato wa uchumi wa maendeleo ya viwanda nchini Tanzania. Balozi Liberata Mulamula Rutageruka (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amehitimisha mahojiano maalum na Radio Vatican kwa kusema kwamba, Italia kupitia Mpango wa chanjo wa COVAX itaipatia Tanzania mgao inaostahili katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Usikose kujiunga na Radio Vatican itakapokunogeshea mahojiano na Balozi Liberata Mulamula Rutageruka (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania kuhusu Mkutano wa 35 wa Sala Kimataifa kwa ajili ya kuombea amani duniani, kwa ushiriki na uwepo wa viongozi wakuu wa kidini kutoka sehemu mbalimbali za duniani, akiwemo Baba Mtakatifu Francisko.

BALOZI LIBERATA
11 October 2021, 14:28