Tafuta

2019.11.18 Mwalimu Julius Nyerere  Rais wa Kwanza na Mwanzilishi wa Tanzania 2019.11.18 Mwalimu Julius Nyerere Rais wa Kwanza na Mwanzilishi wa Tanzania  

Tanzania inamkumbuka Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere

Kika ifikapo tarehe 14 Oktoba nchini Tanzania inafanya kumbukumbuka ya muhasisi wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.Baba aliyekuwa na maono makuu ya nchi yake na bara zima katika muktadha wa Ulimwengu mzima.Anakumbukwa kwa juhudi zake za kutoa taifa la Tanzania katika ukoloni hadi kufikia uhuru kamili.

Na Sr. Angela rwezaula – Vatican.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyeiongiza nchi ya Tanganyika kwanza na baadaye Tanzania, kuanzia 1960 hadi alipostafu mwaka 1985 alitambuliwa  kama Baba wa Taifa. Alifahamika kwa jina la Mwalimu kutokana na taaluma yake ya zamani kwa sababu kabla ya kujitosa katika masuala ya kisiasa alikuwa ni mwalimu, tasnia ambayo ilimpati jina ambalo ghadi leo hii linatambulika ulimwenguni kote.  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alizaliwa Butiama, a Musoma, mkoa wa Mara, mnamo tarehe 13 Aprili 1922 na kuwa rais wa kwanza wa Tanzania. Baba wa Taifa aliiongoza Tanganyika toka mwaka 1961 hadi 1964 kama waziri mkuu, baadaye kama Rais baada ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar kuanzia mwaka 1964 hadi mwaka 1985 kama rais.

Mwaka 1953 alichaguliwa kuwa rais wa chama cha Tanganyika African Association (TAA), chama ambacho alisaidia kukiunda alipokuwa mwanafunzi katika chuo kikuu cha Makerere lakini pia hata akiwa Uingereza. Mwaka 1954 alibadilisha jina la chama cha TAA kwenda chama cha Tanganyika African National Union (TANU), ambacho pia kilikuwa cha kisiasa zaidi kuliko TAA. Ndani ya mwaka mmoja chama cha TANU kikawa tayari chama cha siasa kinachoongoza nchini Tanganyika. Uwezo wa  Mwalimu Nyerere  ulikuw wa kushangaza hadi kuwashitua viongozi wa kikoloni akalazimika kuchagua kati ya siasa na kazi ya ualimu. Katka moja ya usemi wake alisikika akisema “kuwa mwalimu kwa kuchagua na mwanasiasa kwa bahati mbaya”. Hata hivyo alijiuzulu ualimu na kuzunguka nchi nzima ya Tanganyika ili kuzungumza na watu wa kawaida na machifu katika lengo la kuleta umoja katika kupigania uhuru. Pia alizungumza kwa niaba ya TANU katika Baraza la udhamini na Kamati ya nne ya Umoja wa Mataifa (UN) huko New York, Marekani.

Mwalimu Nyerere alikuwa ni kiungo muhimu katika kuleta muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kupta jina moja la Tanzania mara baada ya mapinduzi ya Zanzibar mnamo mwaka 1964 yaliyomtoa madarakani sultani wa Zanzibar Jamshid bin Abdullah. Tarehe 5 Februari 1977 aliongoza chama cha TANU kuungana na chama tawala cha Zanzibar kilichokuwa kinaitwa Afro Shirazi Party na kuanzisha chama kipya cha CCM (Chama cha Mapinduzi ambacho hadi sasa kinatawala nchi) akiwa mwenyekiti wake wa kwanza. Itakumbukwa jambo muhimu ambalo si kawaida kwa viongozi walioko madarakani kwani Mwalimu Nyerere ni mmoja kati ya viongozi walio wachache wa Afrika ambao wameacha madaraka kwa hiari yao  baada ya kutawala kwa muda mrefu akiwa bado anapendwa na wananchi walio wengi. Mnamo 1985 alipostaafu urais na kumkabidho kijiti rais Ali Hassan Mwinyi aongoza taifa la Tanzania, yeye aliamua kurudi kijijini kwake  huko Butiama ambako aliendesha shughuli zake za kilimo. Hata hivyo aliendelea kuongoza CCM hadi 1990 na kuwemo kwenye chama hicho hadi kifo chake.

Mwalimu Kambarage Nyerere, alijitahidi kadiri ya uadilifu wa uongozi, hata kama maoni mengine hayakosi kuwa hasi, lakini ni sehemu ya maisha na mchezo wa kisiasa na hasa suala la kulaumiwa juu ya siasa za ujamaa kwamba zilichelewesha maendeleo ya kiuchumi  ya Tanzania, lakini kumbe si hivyo, hayo yalikuwa ni maoni potofu. Kwa upande ukielewa nini maana ya ‘Ubuntu’ ndipo unaweza kueleza maana ya ujamaa wa kweli katika taifa lolote lile. Janga la Uviko- 19  hata hivyo limethihirisha wazi jinsi ambavyo hakuna mtu yeyote anayeweza kujiokoa mwenyewe bila ushirikiano na mshikamano na ndiyo maono ya Mwalimu Nyerere kuhusu Ujamaa. Anayependa  taifa na watu wake kweli, hawezi kupokonya mali au kumkanyaga mwingine kwa ajili ya maslahi binafsi, uchumi, afya, ajira,na utunzaji wa mazingira nyumba yetu ya pamoja, badala yake ni kuweka kwa pamoja, kukusanya kwa pamoja, na kuweka kwa pamoja kwa ajili ya maslahi ya pamoja. Hakika Mwalimu Nyerere atakumbukwa  hasa wakati huu ambao Taifa la Tanzania limepata changamoto.

Ilikuwa ni tarehe tarehe 14 Oktoba 1999 akiwa na umri wa miaka 77, Mwenyezi Mungu alimwita kwake, akiacha watoto wa  taifa lake, Afrika na ulimwengu katika majonzi. Hakika Baba wa Taifa aliyetambua kuunganisha nchi yote kwa lugha moja ya kiswahili zaidi ya lugha mbali mbali za makabila nchini Tanzania alifanya jambo zuri sana. Ni mengi ambayo kama watanzania tunapaswa kuyarithisha kwa kizazi ambacho hakikumjua Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere. Kwa yeyote anayeishi nchi za Nje , anaweza kweli kushuhudia utambuzi wa Baba Nyerere jinis alivyopendwa na kuitangaza nchi yake kwa matendo yake ya kutaka demokrasia na Ujamaa. Basi mdogu msomaji tutafakari sana na kutunza maono ya kinabii yasipotee ya umoja kati yetu, ushirikiano na upendo bila ubaguzi na chuki, bali kusaidiana na kuinuana.

Kati ya mafanikio makubwa ya Mwalimu Nyerere  na ambayo yanahitajika leo hii katika ulimwengu wote ni ile ya  kujenga umoja wa taifa kati ya watu wa makabila na dini tofauti, kwa njia hiyo katika nia ya kuelendelea kudumisha amani ya muda mrefu hadi kuiletea taifa kuitwa “kisiwa cha amani”. Mwalimu Nyerere pia anakumbukwa kwa sababu ya kustawisha utamaduni wa Kiafrika pamoja na lugha ya Kiswahili, lugha ambayo imekuwa muafaka kwa taifa, na kutetea usalama wa taifa katika vita dhidi ya mvamizi Idi Amin wa Uganda. Mwalimu Nyerere atakumbukwa sana katika kutoa mchango kwa vyama vya ukombozi vya nchi za Kusini mwa Afrika kama vile Zimbabwe, Afrika Kusini , Namibia, Angola na Msumbiji. 

14 October 2021, 15:09