Tafuta

Waziri mkuu Kassim Majalia amewaomba viongozi wa dini nchini Tanzania kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali katika huduma za kijamii hususna katika sekta ya afya. Waziri mkuu Kassim Majalia amewaomba viongozi wa dini nchini Tanzania kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali katika huduma za kijamii hususna katika sekta ya afya. 

Waziri Mkuu Majaliwa: Viongozi wa Dini Endeleeni Kuiunga Mkono Serikali!

Waziri mkuu hivi karibuni amezindua Mradi wa Mpango wa Kanisa Katoliki wa Mapambano dhidi ya UVIKO-19. Mradi huo unatekelezwa kupitia vituo 12 vya kutolea huduma za afya vya Kanisa Katoliki nchini Tanzania ili kusaidia kujaziliza kazi kubwa inayofanywa na Serikali katika kudhibiti maambukizi ya UVIKO-19. Licha ya Tanzania kuudhibiti mlipuko huo, lakini UVIKO-19 bado upo!

Na Ofisi ya Waziri Mkuu, - Dar es Salaam.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa dini nchini Tanzania waendelee kuiunga mkono Serikali katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO- 19 sambamba na kuelimisha umma umuhimu wa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo. Amesema hadi kufikia tarehe 22 Oktoba 2021, jumla ya wananchi 981,297 walikuwa wamechanjwa na jumla ya wagonjwa 26,154 na vifo 725 vilitolewa taarifa tangu ugonjwa huo uliporipotiwa kuingia nchini kwa mara ya kwanza tarehe 19 Machi 2020. Waziri Mkuu ameyasema hayo Oktoba 27, 2021wakati akizindua Mradi wa Mpango wa Kanisa Katoliki wa Mapambano dhidi ya UVIKO-19 katika Hospitali ya Kardinal Rugambwa iliyopo Ukonga, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Mradi huo unatekelezwa kupitia vituo 12 vya kutolea huduma za afya vya Kanisa Katoliki vilivyopo kwenye maeneo mbalimbali nchini Tanzania ili kusaidia kujaziliza kazi kubwa inayofanywa na Serikali katika kudhibiti maambukizi ya UVIKO – 19. Amesema licha ya Tanzania kuudhibiti mlipuko huo, bado ugonjwa upo na wagonjwa pamoja na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo vinaendelea kufuatiliwa na kutolewa taarifa huku Serikali ikitekeleza afua mbalimbali za kupambana na janga hilo pamoja na kuimarisha uchumi na huduma za jamii.

"Hivyo basi, tuendelee kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huu kwa kujijengea utamaduni wa kuvaa barakoa safi na salama, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono pamoja na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima."  Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ya UVIKO-19 ambayo imethibitishwa na wataalamu wetu hapa nchini kuwa ni bora na salama. "Juhudi hizo za Serikali zinakwenda sambamba na utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19 uliozinduliwa na Rais Mheshimiwa Samia." Kadhalika, Waziri Mkuu amesema hadi kufikia tarehe 25 Oktoba, 2021 kuna jumla ya wagonjwa 243,260,214 na vifo 4,941,039 vimetolewa taarifa duniani na katika Bara la Afrika, jumla ya wagonjwa 6,057,855 na vifo 149,375 vimeripotiwa. Mheshimiwa Majaliwa amesema miongoni mwa hatua iliyochangia kwa kiasi kikubwa kupunguza maambukizi na visa vipya vya UVIKO - 19 ni matumizi ya kinga (maarufu kama chanjo ya UVIKO - 19). “Nasi Tanzania hatukubaki nyuma katika hilo kwani tarehe 29 Julai 2021, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua rasmi kampeni ya chanjo dhidi ya UVIKO -19.”

Mheshimiwa Majaliwa amesema juhudi za jumuiya ya kimataifa zikiongozwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) sambamba na nchi husika zimesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza maambukizi hususan ya visa vipya vya UVIKO-19. “Utoaji wa elimu kuhusu UVIKO - 19, kuhamasisha wananchi kuchanja na kupata huduma muhimu hasa kwa wale wenye magonjwa sugu ni miongoni mwa masuala ambayo sote hatunabudi kuunga mkono utekelezaji wake.” Amesema maeneo yote hayo ni ya kimkakati na muhimu katika mapambano dhidi ya UVIKO19 na wataalamu wanaeleza kwamba tunahitaji kufikia asilimia 60 ya uchanjaji ili tufanikiwe kuwa na kinga ya ujumla (yaani heard immunity) na hivyo, kulitokomeza kabisa janga hili la UVIKO19. “Kwa hiyo, tunalazimika kuongeza uhamasishaji na kuwafikia wananchi wengi zaidi ili tufanikiwe katika afua hii ya kuchanja ukizingatia kuna wimbi la nne limeibuka na tayari baadhi ya nchi za Afrika zinaanza kukumbwa na wimbi hilo.”

Waziri Mkuu amelishukuru Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la Misaada la USAID kwa kukubali kushirikiana na TEC kutekeleza Mradi wa Pambana na UVIKO -19 ambao utagharimu Dola za Marekani 574,259.74. Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kulihakikishia baraza hilo kwamba Serikali itashirikiana nalo katika utekelezaji wa mradi huo ili kufikia malengo kama ambavyo imekuwa ikishirikiana nalo katika miradi mingi ya huduma za afya, elimu na maji. Naye Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, amesema mradi huo wa kupambana na UVIKO - 19 unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa ufadhili wa watu wa Marekani na utazingatia taratibu za Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto. Amesema kwa mradi huo Kanisa Katoliki linaupa kipaumbele utu wa mtu na uhai wake, hivyo wamedhamiria kuchangia kwa njia za kisayansi na kiimani kudhibiti mlipuko wa UVIKO -19, ugonjwa ambao unatishia uhai wa binadamu hapa duniani.

Kwa upande wake, Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Balozi Donald Wright amesema Serikali ya Marekani imedhamiria kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha wananchi wote wanaougua Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO -19 wanapatiwa matibabu. Balozi Wright amesema Serikali ya Marekani imetenga Dola za Marekani milioni 25 kwa ajili ya kuiwezesha Serikali ya Tanzania kupambana na magonjwa mbalimbali kama UVIKO -19 pamoja na UKIMWI.

02 November 2021, 11:34