Catherine Russell ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la kuhudumia watoto UNICEF
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Tarehe Mosi Februari 2022, Bi Catherine Russell amechukua nafasi mpya ya wajibu wa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) akiwa ni mwanamke wa Nne kuongoza shirika hilo ambalo tayari lina miaka 75 ya historia tangu kuanza kutoa huduma yake ulimwenguni. Bi Russell nafasi hiyo amefikiria kuwa “Ni heshima na bahati kujiunga na UNICEF na kusaidia kuongoza kazi yake ya ajabu kwa ajili ya watoto katika wakati huo muhimu. Wakati ambapo mamilioni ya watoto duniani kote bado wanapata nafuu kutokana na athari za janga la UVIKO na majanga mengine, UNICEF inaongoza wito wa kulinda haki zao na maisha yao ya baadaye”, amesema
Kuanzia 2020 hadi 2022, Russell alikuwa nahudumu kama Msaidizi wa Rais na Mkurugenzi wa Ofisi ya Utumishi wa Rais kwa serikali ya Marekani. Tangu 2013 hadi 2017, alikuwa Balozi Maalum wa Masuala ya Wanawake Ulimwenguni katika Idara ya Marekani. Katika jukumu hilo, amejumuisha masuala ya wanawake katika nyanja zote za sera ya kigeni ya Marekani, akiwakilisha Marekani katika zaidi ya nchi 45, na kufanya kazi na serikali za kigeni, mashirika ya kimataifa na mashirika ya kiraia. Alikuwa mbunifu mkuu wa Mkakati wa Kimataifa wa Marekani wa Uwezeshaji wa Wasichana Vijana.
Hapo awali, Bi Russell alikuwa Naibu Msaidizi wa Rais katika Ikulu, chini ya Rais Barack Obama; Mshauri Mkuu wa Masuala ya Kimataifa ya Wanawake kwenye Kamati ya Mahusiano ya Kigeni ya Seneti, Mwanasheria Mkuu Mshiriki katika Idara ya Haki na Mkurugenzi wa Wafanyakazi wa Tume ya Mahakama ya Seneti. Kabla ya kurejea katika huduma ya serikali mnamo 2020, alifundisha hata katika Shule ya Harvard Kennedy kama Mshirika wa Taasisi ya Siasa. Pia alikuwa mwenyekiti msaidizi wa Kikundi cha Sera za Kigeni za Wanawake, mjumbe wa bodi ya wanawake kimataifa, mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Sesame Street, mjumbe wa shirika lisilo la kiserikali la KIVA na mjumbe wa Mfuko wa Thomson Reuters wa Mpango wa Wanawake. Bi Russell ana BA ya Falsafa kwa heshima kutoka Chuo Kikuu cha Boston na BA katika Sheria kutoka Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha George Washington. Yeye ni Mkurugenzi Mkuu wa nne kuongoza shirika hilo linaloundwa na watu 20,000.
Kwa niaba ya UNICEF, Italia wanayofuraha kumkaribisha Catherine Russell kama Mkurugenzi Mkuu mpya wa UNICEF, mwanamke wa nne kuongoza shirika hilo. Katika historia yake ya miaka 75, UNICEF imesaidia kuokoa, kuponya na kulinda mamilioni ya watoto duniani kote. Wana imani kwamba kwa uzoefu wake mkubwa Catherine Russell ataweza kuongoza shughuli za shirika lao kwa ajili ya haki za watoto duniani kote, hasa wale walio katika hatari zaidi, alisema Carmela Pace, Rais wa UNICEF Italia.