Ripoti mpya ya UNICEF kuhusu UVIKO-19 na Mafunzo kwa watoto
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Ripoti iliyopewa jina “Are children really learning? yaani watoto wanajifunza kweli?,inawakilisha takwimu juu ya nchi 23 za kipato cha kati na cha chini kuhusiana na muktadha wa UVIKO-19 na uhusiano wa kufungwa kwa shule kwa watoto zaidi ya vipimo vilivyosasishwa na hali ya kujifunza kwa watoto kabla ya janga la UVIKO. Ripoti hiyo inasisitiza kuwa milioni 147 ya watoto wamepoteza nusu ya mafunzo yao ya ana kwa ana kwa miaka 2 ya mwisho. Hiyo inaongeza idadi ya tirioni 2 za masaa ya kujifunza darasani uliopotezwa kwa ngazi ya ulimwengu.
Hatuwezi kumudu kurudi hali ya kawaida bila juhudi za wote
Kutokana na hiyo Bi Catherine Russell, Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF akizungumzia kuhusiana na ripoti alisema kuwa:“Wakati watoto hawawezi kwenda shule moja kwa moja na walimu na wenzao, kujifunza kwao kunatatizika. Wakati hawawezi kuwa kabisa na walimu na wenzao, hasara yao ya kujifunza inaweza kuwa ya kudumu na kuongezeka huku kwa kukosekana kwa usawa katika kupata fursa ya kujifunza kunamaanisha kuwa elimu ina hatari ya kuwa mgawanyiko mkubwa zaidi, si msawazishaji mkubwa zaidi” Akiongeza alisema: “Wakati dunia inashindwa kusomesha watoto wake, sote tunateseka. Hata kabla ya janga hili, watoto waliotengwa zaidi waliachwa. Ugonjwa unapoingia katika mwaka wake wa tatu, hatuwezi kumudu kurudi katika hali ya kawaida. Tunahitaji hali mpya ya kawaida: watoto wakiwa madarasani, kutathmini mahali walipo katika masomo yao, na kuwapa usaidizi wa kina wanaohitaji kufidia kile walichopoteza, na kuhakikisha kwamba walimu wana mafunzo na nyenzo wanazohitaji. Vigingi ni vya juu sana kufanya chochote kidogo” alihitimisha Russell.
Nchi ambazo zimekumbwa na tatizo kubwa la Uviko barani Afrika
Mbali na takwimu za upotevu wa kujifunza, ripoti inaonesha takwimu mpya kwamba watoto wengi hawakurudi shuleni wakati madarasa yalipofunguliwa. Nchini Liberia, asilimia 43 ya wanafunzi wa shule za umma hawakurudi shule zilipofunguliwa mwezi Desemba 2020. Idadi ya watoto wasiokwenda shule nchini Afrika Kusini iliongezeka mara tatu kutoka 250,000 hadi 750,000 kati ya Machi 2020 na Julai 2021. Nchini Uganda, takriban mwanafunzi 1 kati ya 10 amekosa shule na hawakurudi shuleni mwezi Januari 2022 baada ya shule kufungwa kwa miaka miwili. Nchini Malawi, kiwango cha wasichana kuacha katika elimu ya sekondari kiliongezeka kwa 48%, kutoka 6.4% hadi 9.5% kati ya 2020 na 2021. Nchini Kenya, uchunguzi wa vijana 4,000 kati ya umri wa miaka 10 na 19 uligundua kuwa asilimia 16% ya wasichana na 8% ya wavulana hawakurudi shule zilipofunguliwa. Watoto ambao hawaendi shule ni miongoni mwa watu walio katika mazingira magumu na waliotengwa katika jamii. Wana uwezekano mdogo wa kujua kusoma, kuandika au kufanya hesabu za msingi, na wametengwa na mtandao wa usalama ambao shule hutoa, na ambapo bila hiyo wanawekwa katika hatari kubwa ya kunyonywa na maisha ya umaskini na kunyimwa.
Hakuna uhakika kwamba watoto wa shule wamejifunza mambo msingi
Ripoti hiyo inaweka wazi kuwa wakati watoto wako nje ya mazingira ya shule wanapata hasara nyingi zaidi, takwimu za kabla ya janga kutoka nchi na wilaya 32 zinaonesha kiwango duni cha kujifunza, hali ambayo ina uwezekano kuwa imechochewa na kiwango cha kujifunza kupotea kutokana na janga. Katika nchi zilizochanganuliwa, kasi ya sasa ya kujifunza ni ndogo sana hivi kwamba ingechukua miaka saba kwa watoto wengi wa shule kujifunza stadi za msingi za kusoma ambazo zilipaswa kupatikana katika miaka miwili, na miaka 11 ya kujifunza stadi za msingi za kuhesabu. Mara nyingi, hakuna uhakika kwamba watoto wa shule wamejifunza mambo ya msingi. Katika nchi na maeneo 32 yaliyofanyiwa utafiti, robo ya watoto wa shule wenye umri wa karibu miaka 14 walikosa ujuzi msingi wa kusoma na zaidi ya nusu walikosa ujuzi wa kuhesabu unaotarajiwa kwa mwanafunzi wa umri wa miaka 7.