Ukraine:Unicef inasema milioni 2 ya watoto wameacha nchi kutafuta usalama
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Watoto milioni mbili wakimbizi wamekimbia Ukraine kutafuta usalama, wengine milioni 2.5 wamekimbia makazi yao nchini humo. Asilimia 60 sasa wanalazimika kuyahama makazi yao huku mashambulizi yakiendelea katika maeneo ya mijini. Haya yamesemwa na Shirika la Kimataifa la kuhudumia watoto UNICEF ambalo, kupitia kwa msemaji wake mkurugenzi mkuu, Bi Catherine Russell, amebainisha kuwa hii inatukumbusha kwamba “Hali ya Ukraine inazidi kuwa mbaya. Kadiri idadi ya watoto wanaokimbia makazi yao inavyozidi kuongezeka, lazima tukumbuke kuwa kila mmoja wao anahitaji ulinzi, elimu, usalama na msaada”. Watoto wanawakilisha nusu ya wakimbizi wote wa vita nchini Ukraine, kulingana na UNICEF na UNHCR.
Zaidi ya watoto 100 ambao wameuawa na 134 kujeruhiwa hadi sasa japokuwa idadi inaweza kuwa ya juu
Zaidi ya watoto milioni 1.1 wamewasili Poland, mamia ya maelfu wamewasili Romania, Moldovia, Hungari, Slovakia na Jamhuri ya Czech. UNICEF inaendelea kukumbusha hatari kubwa za biashara mbaya ya wanadamu na unyonyaji na kwa sababu hiyo pia imeunda “Blue Dots” katika nchi zinazohifadhi wakimbizi, ikiwa ni pamoja na Moldovia, Romania na Slovakia. Haya ni maeneo salama ya kutoa taarifa kwa familia zinazosafiri, kusaidia kutambua watoto ambao hawajasindikizwa na waliotenganishwa na kuhakikisha ulinzi wao dhidi ya unyonyaji na kutumika kama kitovu cha ufikiaji wa huduma muhimu. Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa iliandika kwamba ni zaidi ya watoto 100 waliuawa katika vita hivyo na wengine 134 walijeruhiwa. Idadi kamili labda ni kubwa zaidi ya hiyo.
Watoto milioni 4 wako katika baa la njaa Nchini Afghanistan
Nchini Afghanistan, watoto milioni 14 wanashida ya njaa, magonjwa na unyonyaji huku wafadhili wakikuta ili kuamua hatima yao. Hili lilitangazwa na Save the Children huku likiwaomba viongozi wa dunia wa kushiriki katika mkutano wa mtandaoni kufikia lengo la dola bilioni 4.4 zinazohitajika ili kupunguza janga la kibinadamu. Ni karibu 13% tu ya fedha muhimu zimetengwa hadi sasa. Wafadhili lazima wajitolee kwa ukarimu na kuunga mkono Mpango wa Mwitikio wa Kibinadamu wa 2022 la sivyo watoto wataendelea kufa. Ukweli ni rahisi na wa kusikitisha kwa wakati mmoja kwamba lazima utufanye tufikirie, alisema mkurugenzi wa Save the Children wa Afghanistan, Chris Nyamandi.Kwa kuongeza alisema “Timu zetu hazijawahi kuona chochote kama uharibifu na kukata tamaa tunayoshuhudia kwa sasa. Uchumi ulianguka na kuacha mamilioni ya watoto wakitegemea kabisa misaada ya kibinadamu. Bila ufadhili wa kutosha wa misaada, watoto wataendelea kupoteza maisha kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuilika na utapiamlo”.
Magonjwa kama surua yanaongezeka
Kwa hakika, madaktari wa Save the Children wanaripoti kuwa magonjwa kama vile surua yanaongezeka na kuwapata wahanga, kutokana na watoto kutopata huduma za afya za kutosha na chanjo za kawaida. Mnamo mwaka wa 2022 pekee, kulikuwa na visa zaidi ya 18,000 vya surua na watoto 142 wamekufa kwa ugonjwa huu nchini Afghanistan. Akina mama wengi pia hulazimika kujifungulia nyumbani kwa sababu hawawezi kumudu gharama za usafiri au matibabu, jambo linaloweka maisha yao na ya watoto wao hatarini.