Tafuta

Waziri mkuu wa Tanzania ametoa hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kza za serikali, makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya Waziri mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2022-2023. Waziri mkuu wa Tanzania ametoa hotuba kuhusu mapitio na mwelekeo wa kza za serikali, makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya Waziri mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2022-2023. 

Hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu wa Tanzania: 2022-2023

Ifuatayo ni hotuba ya Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi yake na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2022-2023: Ujenzi wa Reli ya Kisasa, SGR, Mradi wa kufua umeme wa Maji, Bomba na mafuta ghafi, Ujenzi wa barabara na madaraja makubwa; Usafiri, Elimu, Afya na Mji wa Serikali.

Na Ofisi ya Waziri, - Dodoma, Tanzania

 

UTANGULIZI

1.   Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba kutokana na taarifa zilizowasilishwa leo ndani ya Bunge lako tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti zilizochambua Bajeti ya Mfuko wa Bunge na Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2021/2022 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2022/2023. Aidha, naliomba Bunge lako tukufu likubali kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2022/2023.

2.   Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana hapa leo kwa ajili ya kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa Mwaka 2021/2022 na mwelekeo wake kwa mwaka 2022/2023. Aidha, naomba kuwatakia heri ya Mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani kwa Waislamu na Kwaresima njema kwa Wakristo. Pia, nitumie fursa hii kuwatakia waumini wote sherehe njema za Sikukuu za Pasaka na Eid. InshaAllah, Mwenyezi Mungu atujaalie kwetu sote tukamilishe funga zetu.

Salamu za Pole

3.   Mheshimiwa Spika, tangu tulipohitimisha Mkutano wa Bajeti wa Bunge hili mwaka jana, Nchi yetu imekumbwa na majanga na matukio mbalimbali yaliyosababisha vifo na uharibifu wa mali. Nitumie fursa hii kutoa pole kwa wote waliofiwa na ndugu, jamaa na marafiki. Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amina! Kwa ndugu zetu walioumia na bado wanajiuguza, tumwombe Mwenyezi Mungu awasaidie kupona haraka na kurejea katika shughuli za ujenzi wa Taifa.

Salamu za Pongezi

4.         Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee naomba nimpongeze Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kutimiza mwaka mmoja tangu ashike nafasi ya kuongoza nchi yetu akiwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika kipindi hicho, tumeshuhudia mafanikio makubwa katika kuimarisha miundombinu hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii kama vile ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji, utawala bora, mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, pamoja na kuhamasisha uwekezaji na utalii. Nami niungane na Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wenzangu kuendelea kumuombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumpa nguvu, ulinzi, afya na kila lililo la heri katika kuwatumikia Watanzania.

5.         Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kutokana na fikra na uongozi wao makini katika ujenzi wa Taifa letu. Ni dhahiri kuwa juhudi zao katika kuongoza na kusimamia utekelezaji wa mipango ya Serikali zinaendelea kuleta manufaa makubwa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

6.         Mheshimiwa Spika, kipekee, nikupongeze wewe binafsi Mheshimiwa Spika kwanza kwa kuchaguliwa kwako na Bunge kwa asilimia 100. Ni imani kubwa kwako na ni matokeo ya kuliongoza Bunge hili kwa umahiri na weledi mkubwa. Aidha, niwapongeze Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu (Mb.), Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Bunge Mheshimiwa Najma Murtaza Giga (Mb.), na Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile (Mb.) kwa kuendelea kukusaidia kikamilifu katika kutekeleza majukumu ya kuliongoza Bunge letu tukufu. Nawapongeza pia Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

7.         Mheshimiwa Spika, hivi karibuni Bunge lako tukufu limepata Wabunge wapya. Hivyo, nitumie fursa hii kuwapongeza sana Mheshimiwa Emmanuel Lekishon Shangai kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro na Mheshimiwa Shamsi Vuai Nahodha kwa kuteuliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni matumaini yangu kuwa Bunge lako Tukufu litaendelea kuwapatia ushirikiano wa kutosha ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

8.         Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwashukuru Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa ushauri walioutoa wakati wa kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali zinazojitegemea na Serikali za Mitaa. Kwa namna ya pekee niwashukuru wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Madaba, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI inayoongozwa na Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti chini ya uenyekiti wa Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Babati Vijijini kwa kutoa mchango mkubwa wakati wa uchambuzi wa makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za mafungu ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Mfuko wa Bunge. Maoni na ushauri wao utazingatiwa wakati wa utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2022/2023.

9.         Mheshimiwa Spika, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa George Boniface Simbachawene, Mbunge wa Kibakwe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu); Mheshimiwa Prof. Joyce Lazaro Ndalichako, Mbunge wa Kasulu Mjini na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu); Mheshimiwa Ummy Hamisi Nderiananga, Mbunge wa Viti Maalum na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu); na Mheshimiwa Patrobas Paschal Katambi, Mbunge wa Shinyanga Mjini na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu).

10.        Mheshimiwa Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawashukuru Mheshimiwa Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana (Mb.), Waziri wa Maliasili na Utalii na Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama (Mb.), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa ushirikiano wao mkubwa walionipatia pamoja na kazi nzuri waliyoifanya wakati wote walipokuwa wanatumikia nafasi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu.

11.     Mheshimiwa Spika, vilevile, nawashukuru sana Dkt. John Antony Kiang’u Jingu, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu); Profesa Jamal Adam Katundu, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu); Ndugu Kaspar Kaspar Mmuya, Naibu Katibu Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu); Wakurugenzi na Wakuu wa Vitengo, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi Binafsi ya Waziri Mkuu na wafanyakazi wote kwa ushirikiano mkubwa wanaonipatia wakati nikitekeleza majukumu yangu.

12.     Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuwashukuru washirika wa maendeleo zikiwemo nchi rafiki, taasisi na mashirika ya kimataifa, madhehebu ya dini na mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kujenga uchumi shindani na viwanda na kuiletea nchi yetu maendeleo. Mchango wao umekuwa muhimu katika kuiwezesha nchi yetu kupiga hatua kubwa kimaendeleo kulingana na mipango tuliyojiwekea.

13.     Mheshimiwa Spika, makadirio ya bajeti ninayowasilisha leo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 pamoja na ahadi zilizotolewa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Vilevile, makadirio hayo ya mapato na matumizi yamezingatia vipaumbele vya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 na Mapendekezo ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2022/2023.

UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2021/2022

14.     Mheshimiwa Spika, mwaka 2021/2022, Serikali ilianza utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) ukiwa na dhima ya Kujenga Uchumi Shindani wa Viwanda kwa Maendeleo ya Watu. Aidha, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/2022 uliandaliwa kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mpango huo.

15.     Mheshimiwa Spika, hadi Februari 2022, mafanikio yaliyopatikana kutokana na utekelezaji wa mpango huo ni pamoja na:

Mosi:   Ujenzi wa Reli ya Kisasa kwa Kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway- SGR) ambapo ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam - Morogoro (Km 300) umefikia asilimia 95.3; kipande cha Morogoro - Makutupora (Km 422) asilimia 81.1; na Mwanza - Isaka (Km 341) umefikia asilimia 3.9. Aidha, tarehe 28 Desemba, 2021, Serikali iliingia mkataba na Kampuni ya Yapi Merkezi ya nchini Uturuki kwa ajili ya ujenzi wa njia ya reli kwa kipande cha Makutupora - Tabora (Km 368). Taratibu za kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa kipande cha Tabora - Isaka (Km 165) zinaendelea ili kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa reli hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza yenye urefu wa kilomita 1,219.

Pili:      Utekelezaji wa mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (Megawati 2,115) umefikia asilimia 56.79, ambapo ujenzi wa handaki la kuchepushia maji umekamilika. Kazi zinazoendelea kutekelezwa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha kupokea na kusafirisha umeme kV 400, njia za kupitisha maji ya kufua umeme, nyumba ya mitambo ya kufua umeme, ujenzi wa tuta kuu la bwawa na utengenezaji wa mitambo tisa ya kuzalisha umeme yenye uwezo wa kuzalisha Megawati 235 kila mmoja.

Tatu:    Kukamilika kwa ulipaji wa fidia katika maeneo ya kipaumbele ya Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Chongoleani - Tanga (Tanzania) pamoja na kusaini Mkataba kati ya Nchi Hodhi na Wawekezaji (Host Government Agreement - HGA) na Mkataba wa Ubia (Shareholding Agreement - SHA).

Nne:    Ujenzi wa barabara na madaraja makubwa ambapo ujenzi wa barabara ya mzunguko katika jiji la Dodoma yenye urefu wa kilomita 112.3 umeanza. Aidha, ujenzi wa daraja la Kigongo - Busisi (Mwanza), daraja la Tanzanite (Dar es Salaam) umekamilika na sote tumeshuhudia Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizindua daraja hilo tarehe 24 Machi, 2022. Madaraja mengine yaliyokamilika ujenzi wake ni Kitengule (Kagera), Kiegeya (Morogoro), na Ruhuhu (Ruvuma). Ujenzi na ukarabati wa madaraja makubwa 9 ya Gerezani (Dar es Salaam), Msingi (Singida), Wami (Pwani), Sukuma (Mwanza), Sanza (Singida), Mtera (Dodoma/Iringa), Godegode (Morogoro), Mitomoni (Ruvuma) na Mkenda (Ruvuma) unaendelea.

Tano: Kuboresha Usafiri wa Abiria na Mizigo katika Maziwa Makuu:

Ziwa Victoria: Ujenzi wa gati la Nyamirembe, Magarine, Lushamba, Bukoba, Ntama, Chato, Muleba, pamoja na gati mbili za majahazi katika Bandari ya Mwigobero umekamilika. Aidha, ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu umefikia asilimia 65 na kwa sasa ujenzi unaendelea katika ghorofa ya tatu.

Ziwa Tanganyika: Ujenzi wa gati la Kagunga, Sibwesa na Kabwe (Nkasi) na Bandari ya Lagosa umekamilika. Aidha, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya Bandari za Kigoma, Kibirizi na Ujiji pamoja na upanuzi wa Bandari ya Kasanga unaendelea.

Ziwa Nyasa: Ujenzi wa sakafu ngumu katika bandari za Kiwira na Itungi umekamilika na ujenzi wa sehemu ya kuegesha meli katika Bandari ya Kiwira unaendelea.

Sita:    Viwanja vya Ndege: Ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Songea umefikia asilimia 96 na kiwanja cha ndege cha Mtwara umefikia asilimia 86. Aidha, mkandarasi wa ujenzi wa kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Msalato kutoka China M/s Sinohydro Corporation Limited na wenzake wamekabidhiwa mradi tayari kwa kuanza ujenzi. Vilevile, maandalizi ya ujenzi wa viwanja vya ndege vya Mikoa ya Shinyanga, Kigoma, Tabora na Rukwa yanaendelea.

Saba: Uendelezaji wa Mji wa Serikali - Mtumba: Awamu ya pili ya ujenzi wa majengo 24 ya Wizara ikiwemo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yatakayotosheleza mahitaji ya watumishi wote ulianza Desemba, 2021 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2023. Aidha, ujenzi wa miundombinu ya maji, umeme na mawasiliano unaendelea zikiwemo barabara zenye urefu wa kilomita 51.2 ambazo ujenzi wake umekamilika kwa zaidi ya asilimia 97.Nane: Elimu: Serikali imeendelea kujenga miundombinu ya elimu kwa lengo la kuhakikisha watoto wanapata elimu katika mazingira bora na yenye staha. Kupitia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19, tumefanikiwa kupunguza msongamano wa wanafunzi kwa kuongeza madarasa 12,000 katika shule za sekondari, madarasa 3,000 katika vituo shikizi na mabweni 50 kwa wanafunzi wenye ulemavu. Ujenzi huo wa vyumba vya madarasa umewezesha wanafunzi wote waliochaguliwa katika mwaka 2022 kujiunga na kidato cha kwanza kwa mkupuo mmoja. Kitendo hiki ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020 inayotaka upatikanaji wa elimu hapa nchini; uimarishwe kwa kujenga miundo mbinu ya kutosha na usawa katika utoaji wa elimu.

Tisa:    Afya: Ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma za afya nchini umefanyika. Miundombinu hiyo, inahusisha hospitali za rufaa za kanda, hospitali za rufaa za mikoa, hospitali za halmashauri, vituo vya afya na zahanati. Hatua hii imesaidia kuboresha huduma za afya ikiwa ni pamoja na kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.

16.        Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yaliyopatikana, utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/2022 ulikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo: athari za UVIKO-19 zilizosababisha kuchelewa kwa utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo; kuvurugika kwa mnyororo wa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma katika soko la dunia na hivyo kusababisha ongezeko la gharama za vifaa vya ujenzi; kupungua kwa mapato yatokanayo na shughuli za kiuchumi, misaada na mikopo nafuu. Aidha, kuwepo kwa vita ya Urusi na Ukraine kumesababisha athari ndogo za kiuchumi hususan kupanda kwa bei za bidhaa.

17.        Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii zilizoathirika na UVIKO - 19. Hatua hizo ni pamoja na utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 ambapo jumla ya shilingi trilioni 1.3 zilitumika katika sekta za elimu, afya, maji, biashara na uwezeshaji wananchi kiuchumi. Aidha, Serikali imeendelea kuhamasisha wananchi kupata chanjo na kufuata miongozo mbalimbali ya wataalam wa afya ili kujikinga na vihatarishi vya UVIKO- 19.

18.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali itajikita katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2022/2023 ambao ni wa pili katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 - 2025/2026). Mpango huo utawezesha kufikia malengo yafuatayo: Kuimarisha ukuaji wa Pato la Taifa; kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei; kuimarisha mazingira ya uwekezaji na biashara hususan ushiriki wa sekta binafsi; kuboresha miundombinu ya huduma za kiuchumi na kijamii kama vile afya, elimu, maji, umeme vijijini pamoja na kuimarisha ustawi wa wananchi.

19.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali itahakikisha sera za mapato na matumizi katika muda wa kati zinajikita katika kutekeleza vipaumbele vilivyoainishwa. Msukumo mkubwa utakuwa kuhakikisha usimamizi madhubuti wa fedha za umma na kuzielekeza kwenye maeneo yatakayoongeza tija, ajira na kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja. Aidha, Serikali itahakikisha miradi ya kipaumbele na kimkakati inayoendelea kutekelezwa inakamilika kwa wakati ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi mipya.

HALI YA UCHUMI

20.        Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa ya Januari 2022, kasi ya ukuaji wa uchumi wa Dunia inatarajiwa kupungua hadi kufikia asilimia 4.4 mwaka 2022 ikilinganishwa na asilimia 5.9 mwaka 2021. Kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa Dunia kutachangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo athari za UVIKO-19. Hali hiyo inatarajiwa kusababisha kuvurugika kwa mnyororo wa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma.

21.        Mheshimiwa Spika, ukuaji wa uchumi katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara unatarajiwa kukua kwa asilimia 3.7 mwaka 2022 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4 mwaka 2021. Kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi kunaweza kuchangiwa na athari za UVIKO - 19 pamoja na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia.

22.        Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Januari hadi Septemba, 2021, uchumi wa Taifa ulikua kwa asilimia 4.9 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2020. Kuongezeka kwa kasi ya ukuaji kumetokana na jitihada mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ikiwemo utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO - 19 na miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mfumuko wa Bei

23.        Mheshimiwa Spika, mwaka 2021, mfumuko wa bei ulikua kwa wastani wa asilimia 3.7 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 3.3 mwaka 2020. Mfumuko huo ulikuwa ndani ya lengo la muda wa kati ya asilimia 3 - 5, wigo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki usiozidi asilimia 8 na ndani ya wigo wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika wa kati ya asilimia 3 - 7. Kuongezeka kwa mfumuko wa bei kulichangiwa na sababu mbalimbali zikiwemo: athari za UVIKO-19; kuongezeka kwa gharama za uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma; na kupungua kwa upatikanaji wa mazao ya chakula katika baadhi ya masoko ya ndani kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

24.        Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na ukuaji wa uchumi shirikishi na endelevu na viashiria vingine vya uchumi vinaendelea kuwa imara ikiwa ni pamoja na kutoa msukumo katika kutekeleza vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2022/2023.

UWEKEZAJI

25.        Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati ya kuvutia na kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini. Mikakati hiyo ni pamoja na kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji,  kufanya mapitio ya sera, sheria na kanuni zinazosimamia uwekezaji pamoja na kutenga hekta milioni 1.6 kwa ajili ya uwekezaji. Aidha, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa chachu ya mafanikio hayo hususan kupitia ziara mbalimbali alizozifanya nje ya nchi. Hadi Februari, 2022, Serikali imefanikiwa kuvutia uwekezaji na kusajili jumla ya miradi ya uwekezaji 294 yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 8.04 ambazo ni sawa na shilingi trilioni 18.58 ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 1 mwaka 2020/2021. Miradi hiyo inatarajiwa kuzalisha ajira takriban 62,301.

26.        Mheshimiwa Spika, katika kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini, hivi karibuni nchi yetu ilishiriki kwenye maonesho ya Dubai Expo 2020. Kupitia maonesho hayo, Wizara za kisekta, Taasisi za Umma na Makampuni Binafsi kutoka Tanzania ziliingia makubaliano na makampuni makubwa yenye nia ya kufanya biashara na kuwekeza nchini. Pia, Hati za Makubaliano 37 zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 8 sawa na shilingi trilioni 18.5 zinazotarajiwa kuzalisha ajira 214,575 zilisainiwa.

27.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Uwekezaji ya mwaka 1996 ili iendane na mazingira ya sasa ya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kujumuisha vipaumbele vilivyoainishwa katika Mipango ya Maendeleo ya Taifa. Aidha, Serikali itakuza ushiriki wa Watanzania katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati na uwekezaji nchini na kuimarisha miundombinu wezeshi ya barabara, umeme, maji na mawasiliano katika maeneo ya uwekezaji.

Ukuzaji wa Sekta Binafsi

28.        Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Kufanya Biashara nchini (Blueprint) ili kukuza biashara na uwekezaji. Katika mwaka 2021/2022, tozo na ada sumbufu 14 zilifutwa au kupunguzwa na kufanya jumla ya tozo sumbufu zilizofutwa au kupunguzwa kufikia 232. Aidha, watoa huduma 900 waliunganishwa kwenye Mfumo wa Kieletroniki wa Malipo ya Serikali, Taasisi za Umma 57 zimeboresha miundo na kufanya mapitio ya sheria mbalimbali sambamba na kuanzisha Idara ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. Utekelezaji wa hatua hizo umechochea kasi ya utatuzi wa changamoto za mazingira ya ufanyaji biashara na kuhudumia sekta binafsi kwa haraka. Vilevile, Serikali imeboresha Kituo cha Uwekezaji Tanzania kwa kuanzisha Kituo cha Huduma za Mahala Pamoja ili kupunguza usumbufu na kurahisisha utoaji huduma kwa wawekezaji.

29.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Kufanya Biashara ikiwa ni pamoja na kuendelea kuondoa muingiliano wa majukumu kwa taasisi za udhibiti, kuondoa tozo sumbufu na kuimarisha ushirikiano wa sekta ya umma na sekta binafsi. Aidha, itaimarisha majadiliano na utatuzi wa changamoto zinazoikabili sekta binafsi.

SIASA

30.        Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ni kuendelea kukuza na kuimarisha demokrasia ya vyama vya siasa nchini, sambamba na kudumisha amani, utulivu na umoja wa kitaifa tulionao Tanzania. Katika kuhakikisha dhamira hiyo inatimia, Serikali iliandaa Mkutano wa Wadau wa Demokrasia ya Vyama vya Siasa ambao ulifanyika tarehe 15 na 16 Desemba, 2021 Jijini Dodoma. Katika Mkutano huo, wadau walijadili hali ya mfumo wa demokrasia ya vyama vya siasa nchini na kutoa maoni na mapendekezo ambayo yaliwasilishwa Serikalini kwa ajili ya kufanyiwa kazi. Baada ya kupokea mapendekezo hayo, Serikali iliridhia kuundwa kwa Kikosi Kazi kilichojumuisha wawakilishi kutoka vyama mbalimbali vya siasa nchini. Jukumu kubwa la kikosi kazi hicho ni kuchambua maoni na mapendekezo ya washiriki wa Mkutano wa Wadau wa Demokrasia ya Vyama vya Siasa na kuandaa mapendekezo ya kuwasilisha kwa Mheshimiwa Rais.

31.        Mheshimiwa Spika, baada ya Mheshimiwa Rais kukutana na kikosi kazi kinachoratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa, alielekeza kuwa uchambuzi wa kina ufanyike katika maeneo mbalimbali ikiwemo: vyama vya siasa kuzingatia usawa wa kijinsia kwa kutoa nafasi kwa wanawake kushiriki katika siasa ndani ya vyama vyao; masuala yote ambayo hayaleti siasa isiyo na tija, kukwaza demokrasia na kufanya siasa kuwa za chuki; na kupitia na kuimarisha Kanuni za Maadili za Vyama vya Siasa Kitaifa zilizopo ili zilete tija na zisiwe kandamizi. Aidha, utekelezaji wa maelekezo hayo unaendelea chini ya kikosi kazi kilichoundwa.

32.        Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa maelekezo aliyotoa baada ya kupokea taarifa ya awali ya Kikosi Kazi kwamba, ziandaliwe Kanuni za kuratibu mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa zilizopo ziboreshwe. Lengo ni kuhakikisha vyama vya siasa vinatumia haki yao ya kufanya mikutano kwa mujibu wa Katiba zao, huku vikiheshimu sheria za nchi na kudumisha uzalendo, amani, utulivu, umoja wa kitaifa na kutozuia shughuli za maendeleo. Ni imani yetu kwamba, hatua hizi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali zitadumisha uhusiano mzuri kati ya wadau na Serikali katika kukuza na kudumisha demokrasia ya vyama vingi nchini.

33.        Mheshimiwa Spika, hivi karibuni zimefanyika chaguzi ndogo tatu katika Majimbo ya Konde, Ushetu na Ngorongoro pamoja na Kata 16. Nichukue fursa hii kuvipongeza Vyama vyote vilivyoshiriki katika chaguzi hizo ambazo zilifanyika kwa amani na utulivu. Kipekee nikipongeze Chama cha Mapinduzi kwa ushindi mkubwa kilioupata katika Majimbo ya Ushetu na Ngorongoro pamoja na kata zote 16. Aidha, nikipongeze chama cha ACT – Wazalendo kwa kushinda kiti cha ubunge katika Jimbo la Konde.

BUNGE

34.        Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu limeendelea kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake ya msingi ya kutunga sheria, kushauri na kuisimamia Serikali. Katika mwaka 2021/2022, Bunge limefanya mikutano yake kwa mujibu wa sheria ikiwemo Bunge kukaa kama Kamati ya Mipango kwa ajili ya kupokea, kujadili na kushauri kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika mwaka 2022/2023. Vilevile, Bunge limeratibu shughuli mbalimbali za Kamati za Kudumu za Bunge zikiwemo semina na ziara za kukagua miradi ya maendeleo na kuishauri Serikali. Aidha, mfumo wa Bunge mtandao umeendelea kuboreshwa ili kuuwezesha kufanya kazi kwa ufanisi.

35.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Ofisi ya Bunge itaratibu na kuwezesha ushiriki wa Wabunge na Kamati za Kudumu za Bunge katika shughuli mbalimbali ndani ya nchi, kikanda na kimataifa pamoja na kushiriki katika michezo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, uendeshaji na usimamizi wa ukumbi wa Bunge utaboreshwa ili kuimarisha usalama katika maeneo na majengo ya Bunge.

MAHAKAMA

36.        Mheshimiwa Spika, ili kulinda haki na maslahi ya Watanzania, Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa mahakama katika ngazi mbalimbali nchini na kuimarisha miundombinu ya utoaji haki na huduma. Miradi iliyokamilishwa ni ujenzi wa vituo jumuishi vitano vya utoaji haki katika Mikoa ya Dar es Salaam (Temeke na Kinondoni), Dodoma, Arusha na Morogoro. Ujenzi wa kituo Jumuishi katika Mkoa wa Mwanza unaendelea na upo katika hatua ya kukamilishwa. Ujenzi wa Mahakama mbili za Hakimu Mkazi za Katavi na Lindi; Mahakama za Wilaya nne za Bunda, Chemba, Rungwe na Bahi; na Mahakama za Mwanzo tatu katika maeneo ya Matiri (Mbinga), Hydom (Mbulu) na Kibaigwa (Kongwa) umekamilishwa. Pia, Serikali imekamilisha ujenzi wa jengo la kuhifadhi kumbukumbu Jijini Tanga.

37.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali imeendelea na utekelezaji wa mradi wa Mahakama maalum zinazotembea katika wilaya za  Kinondoni (Bunju), Ilala (Chanika), Temeke (Buza), Ubungo (Kibamba) na Ilemela. Kupitia mahakama hizo jumla ya mashauri 692 yamesikilizwa na kuhitimishwa.

38.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea kukamilisha ujenzi wa majengo mbalimali yakiwemo, kituo Jumuishi cha Utoaji Haki  cha Mwanza; Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Songwe, Mahakama za Wilaya nane za Kilindi, Sikonge, Same, Tandahimba, Mwanga, Ngara, Namtumbo na Nanyumbu.

39.        Mheshimiwa Spika, vilevile, itaendelea na ujenzi wa Mahakama za Wilaya 18 katika Wilaya za Kakonko, Buhingwe na Uvinza (Kigoma), Butiama na Rorya (Mara), Itilima na Busega (Simiyu), Songwe, Mbogwe na Nyang’wale (Geita), Kyerwa na Misenyi (Kagera), Gairo, Mvomero na Kilombero (Morogoro), Mkinga (Tanga), Tanganyika (Katavi) na Kaliua (Tabora). Pamoja na kukamilisha ujenzi wa Mahakama za Mwanzo sita za Mlimba na Mang’ula (Morogoro), Kabanga (Ngara), Kimbe (Kilindi), Chanika (Ilala) na Nyakibimbili (Bukoba) na mradi wa ukarabati na upanuzi wa Mahakama Kuu Tabora na Mahakama ya Hakimu Mkazi, Moshi.

40.        Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutekeleza Programu ya Kutumia Lugha ya Kiswahili katika utoaji haki nchini; kuimarisha mfumo wa utatuzi wa migogoro nje ya Mahakama kwa kutumia njia ya majadiliano, maridhiano, upatanishi na usuluhishi na kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa kuanzisha madawati ya msaada wa kisheria katika baadhi ya mahakama.

SEKTA ZA UZALISHAJI

KILIMO

41.        Mheshimiwa Spika, Sekta ya Kilimo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu na maendeleo ya wananchi wake. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, sekta ya kilimo inatoa ajira kwa wastani wa asilimia 65 ya Watanzania wote na imeendelea kuchangia malighafi za viwanda.

42.        Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu huo, katika kipindi cha mwaka 2021/2022 imeendelea kutoa kipaumbele kwenye sekta ya kilimo ili kuinua Pato la Taifa na la mtu mmoja mmoja, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza ajira. Licha ya hayo, imeendelea kuchukua hatua kadhaa katika kuhakikisha pembejeo za kilimo hususan mbolea zinapatikana kwa bei nafuu, kwa wakati na kiwango cha kutosha pamoja na kuimarisha upatikanaji wa masoko ya uhakika ya mazao ya wakulima. Ni dhahiri kuwa matumizi ya mbolea, mbegu bora na viuatilifu ni muhimu katika kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya kilimo.

Hali ya Upatikanaji wa Chakula

43.        Mheshimiwa Spika, hali ya uzalishaji, usalama na upatikanaji wa chakula nchini imeendelea kuimarika. Katika msimu wa kilimo wa mwaka 2020/2021, uzalishaji wa mazao ya chakula kitaifa ulikuwa tani milioni 18.6 ikilinganishwa na mahitaji halisi ya tani milioni 14.8. Kutokana na uzalishaji huo, nchi yetu ina ziada ya tani milioni 3.8 za chakula. Uzalishaji huo umeihakikishia nchi utoshelevu wa chakula kwa asilimia 125 kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022. Ongezeko hilo linatokana na mtawanyiko mzuri wa mvua katika msimu wa mwaka 2020/2021, matumizi ya mbegu bora, mbolea, huduma za ugani zinazoendelea kutolewa na Wataalam pamoja na mipango madhubuti inayotekelezwa na Serikali. Pamoja na uwepo wa ziada hiyo, Serikali imeendelea kuimarisha usalama wa chakula nchini kwa kununua na kuhifadhi nafaka kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ambapo hadi mwishoni mwa Februari, 2022 akiba ghalani ilikuwa tani 199,793.

44.        Mheshimiwa Spika, sambamba na hatua za kuimarisha uzalishaji na usalama wa chakula, Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya kuhifadhi chakula kwa kujenga maghala na vihenge vya kisasa. Ujenzi wa vihenge vya kisasa katika maeneo ya Babati, Mpanda na Sumbawanga umekamilika. Aidha, ujenzi katika maeneo ya Dodoma, Mbozi, Makambako na Songea umefikia asilimia 80. Vilevile, Serikali imekamilisha ujenzi wa maghala katika miji ya Babati, Mpanda na Sumbawanga. Ujenzi katika maeneo ya Songea, Makambako na Shinyanga unaendelea. Kukamilika kwa miundombinu hiyo kutaongeza uwezo wa kuhifadhi chakula kutoka tani 341,000 za sasa hadi tani 501,000.

Hali ya Upatikanaji wa Pembejeo za Kilimo

45.        Mheshimiwa Spika, kwa takriban miaka mitatu sasa, dunia imekumbwa na janga la UVIKO - 19 na nchi nyingi zikiwemo wazalishaji wakubwa wa mbolea duniani ziliweka amri ya watu kusalia majumbani. Hali hiyo, imesababisha kusimama kwa uzalishaji, baadhi ya nchi kusitisha uuzaji wa mbolea nje, kuongezeka kwa gharama za usafirishaji na upungufu wa malighafi za kutengeneza mbolea kutokana na baadhi ya nchi kufunga mipaka yake na hivyo kusababisha mbolea kupanda bei katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania.

46.        Mheshimiwa Spika, mahitaji ya mbolea hapa nchini kwa msimu wa 2021/2022 ni tani 698,260. Hadi kufikia Februari, 2022 upatikanaji wa mbolea ulifikia tani 436,452 sawa na asilimia 63 ya mahitaji. Mikakati iliyopo ya kuhakikisha asilimia 37 iliyobaki inapatikana ni pamoja na kuimarisha uzalishaji wa mbolea, kuhamasisha matumizi ya mbolea zinazozalishwa nchini na kuratibu uagizaji wa pamoja kutoka kwa wazalishaji wa nje.

47.        Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka 2022/2023, itaendelea kuhamasisha uwekezaji wa ujenzi wa viwanda vya ndani vya kuzalisha mbolea, kuhimiza viwanda vilivyopo kuongeza uzalishaji, kuongeza matumizi ya mbolea zinazozalishwa nchini na matumizi ya mbolea mbadala. Pia, Serikali itaendelea kushirikiana na Sekta Binafsi katika kuzalisha, kuagiza na kusambaza pembejeo kwa wakulima hapa nchini.

Kuimarisha Huduma za Ugani

48.        Mheshimiwa Spika, kilimo bora na chenye tija kwa sehemu kubwa hutegemea huduma za ugani. Huduma za ugani zinahusisha utoaji wa elimu na teknolojia bora za uzalishaji wa mazao kwa wakulima, matumizi sahihi ya pembejeo, zana bora za kilimo na upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo na mitaji. Serikali kwa kutambua hilo imeendelea kuimarisha huduma za ugani nchini kwa kuhakikisha kuwa Maafisa Ugani wanawafikia wakulima na kutoa huduma stahiki kwa wakati. Ili kutimiza azma hiyo imepanga kununua pikipiki 6,704 kwa maafisa ugani wote nchini. Sote tumeshuhudia mama yetu mpendwa, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 4 Aprili 2022 akigawa pikipiki 2,716 kwa ajili ya Maafisa Ugani kilimo, vifaa vya kupima afya ya udongo kwa Halmashauri 143, simu janja 327 na visanduku vya ugani 3,483. Kitendo hicho kinathibitisha kuwa Serikali ya awamu ya sita inaiangalia sekta ya kilimo kwa jicho la kipekee ili iendelee kuleta tija kwa Watanzania.

49.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea kuimarisha huduma za ugani kwa kutoa vitendea kazi kwa Maafisa Ugani Kilimo, kununua na kusambaza visanduku vya ugani, kutoa mafunzo rejea kuhusu uzalishaji bora wa mazao, matumizi ya mfumo wa M-Kilimo, na kukarabati na kuanzisha Kituo cha Mawasiliano ya Kilimo kwa ajili ya mawasiliano kwa maafisa ugani na wakulima.

Uzalishaji wa Mazao ya Kimkakati

50.        Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kufuatilia na kuimarisha uzalishaji wa mazao ya kimkakati kwa lengo la kuleta tija zaidi na manufaa kwa mkulima mmoja mmoja na kuinua Pato la Taifa kwa ujumla. Katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea kusimamia mkakati wa kuongeza uzalishaji na masoko ya mazao ya mkonge, pamba, kahawa, korosho, tumbaku, chikichi, chai, alizeti, zabibu, pamoja na ufuta, choroko na mbaazi.

51.        Mheshimiwa Spika, kwa upande wa zao la mkonge, Serikali itaongeza uzalishaji, itasambaza miche bora kwa wakulima, itapima mashamba mapya na kuyagawa kwa wananchi na kutoa elimu kuhusu kilimo bora cha mkonge na ubora wa singa. Jitihada hizo zitafanyika sambamba na kuhamasisha uanzishaji wa viwanda na matumizi ya kamba na magunia ya mkonge.

52.        Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mazao mengine, Serikali itaongeza uzalishaji wa chikichi ili kuongeza mafuta ya kula, chai kavu kutoka tani 27,510 mwaka 2021/2022 hadi tani 30,000 mwaka 2022/2023. Itahamasisha uanzishaji wa mashamba mapya ya korosho na pamba, itakamilisha ujenzi wa ghala za kuhifadhi na kuanzisha kituo cha mafunzo ya usindikaji korosho. Ili kutoa huduma bora kwa wakulima, Serikali itaimarisha kanzidata ya wakulima wa pamba kwa kuwasajili wakulima kupitia mfumo wa kielektroniki katika mikoa 17 pamoja kununua ndege 5 zisizotumia rubani (drone) kwa ajili ya kupulizia viuatilifu.

Kuimarisha Ushirika

53.        Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuimarisha vyama vya ushirika nchini. Hatua hizo ni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa vitendea kazi, kuhamasisha ushirika na kufanya kaguzi za mara kwa mara ili kuhakikisha vyama hivyo vinaendeshwa kwa mujibu wa sheria. Hadi Februari, 2022 Serikali imekagua vyama vya ushirika 6,013 ambapo ilibainika kuwa baadhi ya vyama vimekiuka taratibu za uendeshaji wa vyama vya ushirika nchini. Kati ya hivyo, vyama 357 vilipata hati inayoridhisha, vyama 2,674 hati yenye shaka, vyama 1,253 hati isiyoridhisha na vyama 1,729 hati mbaya. Aidha, hatua mbalimbali za kisheria zimechukuliwa dhidi ya wote waliohusika na ukiukwaji wa taratibu za uendeshaji wa vyama vya ushirika ikiwemo na vitendo vya wizi wa mali na fedha za ushirika.

54.        Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha vyama vya ushirika, Serikali pia imewezesha upatikanaji wa vitendea kazi yakiwemo magari 15, pikipiki 137 na kompyuta 82. Vilevile, imeanzisha Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi na Ukaguzi wa Vyama vya Ushirika pamoja na kuanzisha Benki ya Taifa ya Ushirika Tanzania (National Cooperative Bank - NCB). Aidha, kupitia uhamasishaji wa masoko na uwekezaji katika vyama vya ushirika, jumla ya tani 575,295.74 za mazao mbalimbali yenye thamani ya shilingi trilioni 1.52 yaliuzwa.

55.        Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka 2022/2023, itaendelea kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa ushirika na kuimarisha mifumo ya udhibiti na ukaguzi wa vyama vya ushirika. Nitumie fursa hii kuwataka viongozi wote wa vyama vya ushirika walioomba ridhaa ya kuwaongoza wanaushirika wenzao kufuata taratibu zilizowekwa ili wanaushirika waweze kuona tija ya uwepo wa vyama hivyo.

Benki ya Maendeleo ya Kilimo

56.        Mheshimiwa Spika, mnamo mwezi Desemba 2021, Serikali ya Awamu ya Sita chini uongozi mahiri wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliipatia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania mtaji wa shilingi bilioni 208 ikiwa ni nyongeza kwenye mtaji wa awali wa shilingi bilioni 60 uliowekwa na Serikali wakati wa uanzishwaji wa benki mwaka 2012. Mtaji huo wa shilingi bilioni 208 ni mkubwa kuwahi kuongezwa kwa mkupuo kwa taasisi ya fedha katika historia ya nchi yetu. Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) imetoa shilingi bilioni 210 kwa benki yetu ya kilimo ili kutoa huduma za kifedha kupitia kongani na minyororo ya thamani kwa nia ya kuleta mapinduzi ya kimkakati katika kilimo na kwa wakulima wadogo.

57.        Mheshimiwa Spika, kufikia Februari, 2022, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania imefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 354.64 ambayo imewanufaisha wakulima wadogo, wakulima wa kati na wakulima wakubwa wapatao 1,522,751 katika mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar. Aidha, kupitia Mfuko wa Dhamana kwa wakulima wadogo imetoa jumla ya mikopo ya shilingi bilioni 129.39 tangu Mfuko huo ulipoanza rasmi udhamini wa mikopo mwaka 2018.

58.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo itaendelea kuwawezesha wakulima wadogo kupata mikopo na dhamana kwa ajili ya kuboresha uzalishaji, uchakataji, uhifadhi, usafirishaji na upatikanaji wa masoko. Ni imani ya Serikali kuwa jitihada hizi zitasaidia kukuza uchumi, kuongeza usalama wa chakula sambamba na kupunguza umaskini wa kipato.

MIFUGO

59.        Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa elimu kuhusu ufugaji bora wa kibiashara kwa wadau mbalimbali waliopo kwenye mnyororo wa thamani. Hatua hii imeongeza kiwango cha uzalishaji na usindikaji wa mazao ya mifugo kama vile nyama, maziwa na ngozi.

60.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, uzalishaji wa maziwa umeongezeka kwa asilimia 9.67 kutoka lita bilioni 3.1 zilizozalishwa mwaka 2020/2021 hadi kufikia lita bilioni 3.4. Aidha, uzalishaji wa nyama zinazouzwa nje ya nchi umeongezeka kutoka tani 1,774.29 mwaka 2020/2021 hadi kufikia tani 5,362.9 zenye thamani ya dola za Marekani milioni 22.44. Ongezeko hilo limesababishwa na kukua kwa soko la nyama hususan katika nchi za Oman, Kuwait, Bahrain, Saudi Arabia, Qatar, Vietnam, Comoro na Mji wa Hong Kong.

61.        Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka 2022/2023 itaimarisha huduma za ugani katika ngazi za kata na vijiji, kutoa vitendea kazi zikiwemo pikipiki kwa Maafisa Ugani Mifugo na upatikanaji wa dawa na chanjo. Serikali kupitia Wizara inaanzisha mashamba darasa ya malisho maeneo ya Loliondo na Handeni. Aidha, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara, kuvutia uwekezaji mpya pamoja na kufanya majadiliano na wadau kutoka nchi mbalimbali ili kufungua masoko mapya ya mazao ya mifugo.

UVUVI

62.        Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka 2021/2022 imeendelea kuboresha sekta ya uvuvi ili iweze kuchangia kikamilifu katika Pato la Taifa. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuandaa na kutekeleza Mfumo Shirikishi wa Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi katika Mikoa ya kanda ya Ziwa Victoria kwa lengo la kuwa na uvuvi endelevu, kupunguza kero za wananchi, kudhibiti uvuvi na biashara haramu ya mazao ya uvuvi.

63.        Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka 2022/2023 itaendelea kuimarisha miundombinu wezeshi ya uvuvi ikiwemo kununua meli mbili za uvuvi, ujenzi wa Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji Rubambagwe – Geita, ujenzi wa bandari ya uvuvi Kilwa Masoko na kuimarisha usimamizi wa rasilimali katika Ukanda wa Uchumi wa Bahari na Bahari Kuu.

MALIASILI NA UTALII

64.        Mheshimiwa Spika, utalii ni sekta muhimu ya uchumi yenye mchango mkubwa katika Pato la Taifa. Kutokana na umuhimu huo, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kulinda na kuhifadhi rasilimali za maliasili na malikale pamoja na kuendeleza utalii nchini. Aidha, Serikali imeongeza kasi ya utangazaji utalii kitaifa na kimataifa, kuboresha ulinzi na usalama wa rasilimali za maliasili na malikale na kushirikisha jamii katika kutekeleza mipango ya uhifadhi wa ikolojia.

65.        Mheshimiwa Spika, idadi ya watalii walioingia nchini iliongezeka kwa asilimia 48.6 kutoka watalii 620,867 mwaka 2020 hadi watalii 922,692 mwaka 2021. Utalii wa ndani pia umeendelea kuimarika ambapo idadi ya watalii wa ndani waliotembelea maeneo ya hifadhi iliongezeka kutoka 562,549 mwaka 2020 hadi 788,933 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 40.2. Vilevile, mapato yatokanayo na watalii wa kimataifa yaliongezeka kutoka dola za Marekani milioni 714.59 mwaka 2020 hadi dola za Marekani bilioni 1.25 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 76.

66.        Mheshimiwa Spika, kuimarika kwa utalii nchini kumetokana na mwelekeo na jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika kuanzisha na kutekeleza Mpango wa Kitaifa wa kukabiliana na janga la UVIKO-19 hapa nchini. Hii ni pamoja na kutekeleza mkakati wa kuinua sekta ya utalii nchini na kutekeleza mpango wa chanjo ya UVIKO-19 kitaifa. Mpango huo wa kitaifa umeleta taswira mpya kiutalii ambapo Tanzania imekuwa eneo salama zaidi kutembelewa na watalii.

67.        Mheshimiwa Spika, pamoja na utekelezaji wa mipango hiyo, kumekuwa na jitihada mahsusi za Mheshimiwa Rais katika kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia programu maalum ya Royal Tour. Kupitia programu hiyo, mtandao maarufu wa habari nchini Marekani wa theGrio umetambua juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika kuiongoza vema sekta ya utalii nchini na kuifanya Tanzania kuwa kivutio cha kwanza cha utalii Afrika mwaka 2022.

68.        Mheshimiwa Spika, Kwa upande mwingine Serikali na Wananchi wanaendelea na kuimarisha usimamizi wa pori la vyanzo vya maji na eneo la mazalia ya wanyama la Loliondo ili kulinda uhai wa ikolojia hiyo. Serikali inaimarisha huduma za jamii ikiwemo maji yatakayotumika kwa kunyweshea mifugo. Tumeshachimba visima 4 kati ya 13 vinavyotakiwa kuchimbwa maeneo ya wananchi. Aidha, katika Kijiji cha Msomera, Wilayani Handeni Serikali inaendelea na ujenzi wa nyumba 101 kwa ajili ya wananchi wanaohamia kwa hiari.  

69.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea kuongeza juhudi katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za maliasili na malikale, kukuza utalii wa ndani, kuongeza kasi ya utangazaji utalii kitaifa na kimataifa na kuibua masoko mapya ya utalii. Aidha, Serikali itaendelea kukarabati na kuimarisha miundombinu katika maeneo ya hifadhi, kuibua na kuendeleza mazao ya utalii ya kimkakati. Vilevile, Serikali itaendelea kushirikisha jamii katika mbinu za kujikinga dhidi ya wanyamapori hatarishi, kuimarisha shughuli za upandaji miti, ufugaji wa nyuki na mnyororo wake wa thamani.

MADINI

70.        Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia kikamilifu sekta ya madini na kuhakikisha inakuwa na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa. Mchango wa sekta ya madini katika kipindi cha Januari hadi Septemba umeongezeka kutoka asilimia 6.5 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 7.3 mwaka 2021. Aidha, hadi Februari 2022, kiasi cha shilingi bilioni 406.6 za maduhuli kimekusanywa sawa na asilimia 62.6 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 650 kwa mwaka. Mafanikio hayo ni kielelezo tosha cha kuendelea kuimarika kwa sekta hii kufuatia usimamizi thabiti unaowekwa na Serikali.

71.        Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha usimamizi na kuanzisha masoko mapya ya madini na vituo vya ununuzi nchini kwa lengo la kupata takwimu sahihi za mauzo ya madini, kuongeza ukusanyaji wa maduhuli na kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata soko la uhakika na kupata bei stahiki kwa bidhaa za madini. Hadi Februari, 2022, jumla ya masoko ya madini 44 na vituo vidogo vya ununuzi wa madini 70 vimeanzishwa nchini. Kupitia masoko na vituo hivyo, katika kipindi cha Julai 2021 hadi Januari 2022, mauzo ya madini yaliongezeka kwa asilimia 12.4 ikilinganishwa na kipindi kama hicho kwa mwaka 2020/2021.

72.        Mheshimiwa Spika, katika kuhamasisha na kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo kwenye Sekta ya Madini, Serikali iliandaa na kushiriki katika maonesho, makongamano, mikutano ya kikanda na kimataifa na majukwaa mbalimbali. Kupitia hatua hizo, wawekezaji wameendelea kuiamini nchi yetu kama mahali salama na penye mazingira rafiki ya uwekezaji. Katika mwaka 2021/2022, Serikali imetoa leseni tatu za uchimbaji mkubwa wa madini kwa kampuni za Nyanzaga Mining Company Limited, Williamson Diamond Limited na Tembo Nickel Corporation Limited. Aidha, Serikali ilitoa leseni mbili za uchimbaji wa kati kwa kampuni za Mahenge Resources Limited na Jacana Resources Limited. Vilevile, jumla ya leseni 6,382 za wachimbaji wadogo zilitolewa.

73.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa uchimbaji mkubwa na wa kati wa madini ili uweze kuleta tija kwa Taifa; kubuni na kuimarisha utekelezaji wa mipango ya kuwawezesha wachimbaji wadogo ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija; kuimarisha na kuhimiza uanzishwaji wa masoko kwenye maeneo mbalimbali kunakofanyika shughuli za madini; kuimarisha udhibiti wa vitendo vya utoroshaji wa madini; na kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini.

NISHATI

74.        Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa kutosha, wa uhakika na nafuu wa nishati ya umeme, na mafuta na gesi ili kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii. Katika kufanikisha dhamira hiyo, Serikali imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ya umeme ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (MW 2,115), Mradi wa Kufua Umeme kwa Kutumia Gesi wa Kinyerezi I - Extension (MW 185) na Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Maji wa Rusumo (MW 80).

75.        Mheshimiwa Spika, Mradi wa Kufua Umeme kwa kutumia Gesi wa Kinyerezi I - Extension unatarajia kuongeza MW 185 katika mradi wa sasa unaozalisha MW 150 na hivyo kufanya kituo hicho kuzalisha jumla ya MW 335. Utekelezaji wa mradi huu, umefikia asilimia 86 na unatarajiwa kukamilika Novemba, 2022. Vilevile, Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Maji wa Rusumo (MW 80) unaohusisha ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Kagera nao umefikia asilimia 86.7. Kukamilika kwa miradi hii na mingine mingi itakayoanza kutekelezwa kutachochea kasi ya usambazaji wa umeme vijijini na mijini na hivyo kuongeza hali ya upatikanaji wa umeme nchini.

76.        Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na uimarishaji wa njia za kusafirisha umeme ili kuhakikisha kuwa maeneo yote ya nchi yanafikiwa na umeme nafuu na wa uhakika ikiwa ni pamoja na kuiunganisha kwenye Gridi ya Taifa mikoa minne iliyosalia. Katika mwaka 2021/2022, Serikali imeendelea na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 400 Iringa-Singida-Shinyanga; njia ya kusafirisha umeme kV 400 kutoka Singida-Arusha-Namanga; njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 220, Geita-Nyakanazi; njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 220 (Rusumo-Nyakanazi) na njia ya kusafirisha umeme msongo wa kV 400 kutoka Rufiji-Chalinze-Kinyerezi-Dodoma.

77.        Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na utekelezaji wa mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili (REA III Round 2) ambao lengo lake ni kuunganisha vijiji vyote vya Tanzania Bara. Kutokana na kazi kubwa ya usambazaji wa umeme vijijini iliyofanyika, kiwango cha upatikanaji wa umeme maeneo ya vijijini kimefikia asilimia 69.8. Katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea kutunisha Mfuko wa REA ili kuhakikisha vijiji vilivyosalia pamoja na taasisi zinazotoa huduma za kijamii vijijini zinapata umeme.

78.        Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi nchini ambapo hadi Februari, 2022, kiasi cha futi za ujazo trilioni 57.54 za gesi asilia kiligundulika katika vitalu vya Mnazi Bay Kaskazini na Eyasi Wembere. Aidha, matumizi ya gesi asilia nchini yameendelea kuhamasishwa ambapo magari zaidi ya 750 yameunganishwa na mfumo wa matumizi ya gesi asilia na ujenzi wa miundombinu ya kuunganisha nyumba 300 za Mtwara na nyumba 506 za Dar es Salaam unaendelea. Katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea na shughuli za utafutaji, ugunduzi na kuhamasisha matumizi ya gesi asilia ili kuhakikisha sekta hiyo inakuwa na mchango mkubwa katika Pato la Taifa.

79.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya uzalishaji umeme ikiwemo miradi mikubwa ya kimkakati na kielelezo; uimarishaji wa njia za kusafirisha umeme; Awamu ya Tatu ya Mradi wa REA; na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia viwandani, majumbani na kwenye magari.

ARDHI

80.        Mheshimiwa Spika, ardhi ni rasilimali muhimu katika kukuza uchumi na kuondoa umaskini. Ili nchi yetu iweze kunufaika na rasilimali hiyo muhimu ni vema kuwa na mipango endelevu ya matumizi bora ya ardhi sambamba na upimaji wa ardhi hiyo. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imewezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji 217 katika halmashauri 29 nchini na hivyo kuwa na vijiji 2,556 vyenye mpango wa matumizi ya ardhi. Aidha, imeendelea kuboresha makazi katika maeneo yasiyopangwa ambapo hadi Machi, 2022 makazi 555,285 yalirasimishwa na kufanya idadi ya makazi yaliyorasimishwa nchini kuwa 2,094,879. Vilevile, Serikali imeandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika maeneo ya miradi ya kimkakati kwa lengo la kulinda ikolojia na kuwezesha matumizi bora ya ardhi yasiyoleta athari katika mazingira.

81.        Mheshimiwa Spika, pamoja na mipango hiyo, Serikali inaendelea na zoezi la kubadilisha ramani na michoro ya mipango miji kutoka mfumo wa analojia kwenda mfumo wa dijitali. Hadi Machi, 2022, ramani za viwanja 598,000 katika halmashauri 38 tayari zimewekwa katika mfumo wa kidijitali. Matumizi ya mfumo huo yatarahisisha usimamizi, utoaji wa huduma za ardhi na ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

MIUNDOMBINU YA USAFIRI NA USAFIRISHAJI

82.        Mheshimiwa Spika, miundombinu ya usafiri na usafirishaji ni kichocheo muhimu katika ukuaji wa uchumi. Kwa msingi huo, Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu na huduma za usafirishaji ili kupunguza gharama za uzalishaji na kufanikisha maendeleo ya nchi kwa haraka sambamba na kutumia fursa za kijiografia kuinua uchumi wetu. Ili kufanikisha azma hiyo, Serikali imeendelea kujenga na kukarabati barabara, madaraja, reli, bandari, meli, vivuko, viwanja vya ndege na miundombinu ya mawasiliano.

Barabara na Madaraja

83.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali imejenga jumla ya kilomita 251.9 za barabara kwa kiwango cha lami ambazo zimehusisha barabara kuu, barabara za mikoa na wilaya. Lengo ni kuhakikisha kuwa Makao Makuu ya mikoa yote na nchi jirani zinaunganishwa kwa mtandao wa barabara za lami. Aidha, Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya kupunguza msongamano wa magari katika miji mikubwa kwa kujenga barabara za michepuo pamoja na miundombinu ya mabasi yaendayo haraka.

84.        Mheshimiwa Spika, Serikali pia imeanza awamu ya pili ya ujenzi wa barabara na miundombinu ya mabasi yaendayo haraka katika Jiji la Dar es Salaam na ujenzi wa barabara za mchepuo (bypass) katika Jiji la Mbeya, Dodoma na Mji wa Iringa. Aidha, ujenzi wa barabara za mchepuo katika Jiji la Mwanza na Arusha umekamilika. Vilevile, Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya njia nane kutoka Kimara hadi Kibaha yenye urefu wa kilomita 19.2 ambayo imekamilika kwa asilimia 86 (baada ya nyongeza za kazi za mkataba) na barabara za juu katika eneo la Keko na Kurasini.

Viwanja vya Ndege na Usafiri wa Anga

85.        Mheshimiwa Spika, usafiri wa anga ni muhimu katika kuongeza tija na ufanisi katika sekta zinazotegemea usafiri huo ili kuchochea ukuaji wa uchumi. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imeendelea kuimarisha usafiri wa anga kwa kukarabati viwanja vya ndege, ujenzi wa viwanja vipya vya ndege pamoja na ununuzi wa ndege mpya.

86.        Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka 2021/2022 imeendelea kuliimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) ili liweze kutoa huduma bora ya usafiri wa anga ndani na nje ya nchi. Hadi Februari, 2022, Serikali imefanya malipo ya awali ya ununuzi wa ndege tano mpya. Kati ya hizo, ndege moja ni aina ya Boeing 787-8 Dreamliner; ndege mbili aina ya Boeing 737-9; ndege moja aina ya De Havilland Dash 8-Q400; na ndege moja ya mizigo aina ya Boeing 767-300F. Kukamilika kwa ununuzi wa ndege hizo, kutaiwezesha Serikali kuwa na jumla ya ndege mpya 16.

87.        Mheshimiwa Spika, kutokana na kuendelea kuimarika kwa Shirika letu la ndege, hivi karibuni limefanikiwa kuanza safari katika vituo vya Arusha, Geita, na kurejesha safari za Mtwara na Songea. Aidha, limerudisha safari za kikanda katika vituo vya Bujumbura, Entebbe, Harare, Lusaka na Hahaya pamoja na kuanzisha vituo vipya vitatu katika miji ya Lubumbashi, Nairobi na Ndola. Vilevile, Shirika limefanikiwa kurejesha safari ya kimataifa kwenda Mumbai - India pamoja na kuanzisha safari za mizigo kuelekea Guangzhou – China.

Reli

88.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali imeendelea na ukarabati wa njia ya Reli ya Kati kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na Kigoma sambamba na kukamilika kwa ununuzi wa vichwa vya treni vitatu, mabehewa 44 ya mizigo na mtambo wa kupima ubora wa njia ya reli. Katika mwaka  2022/2023, kazi zitakazotekelezwa ni pamoja na kuendelea kutafuta Mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa njia ya reli kwa kipande cha Tabora – Isaka (Km 165) na ujenzi wa njia za reli kwa vipande vya Uvinza – Musongati - Gitega (Burundi) yenye urefu wa Km 282; na Kaliua – Mpanda – Karema (Km 321) kwa kiwango cha SGR.

Bandari

89.        Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mpango wa uboreshaji wa bandari nchini kwa kufanya upanuzi na kuimarisha miundombinu ya Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara. Katika mwaka 2021/2022, Serikali imekamilisha ukarabati wa gati Na. 1 – 7 katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuongeza kina hadi kufikia mita 14.5. Aidha, gati maalum la kuhudumia meli za magari limeanza kutumika na kazi ya kuchimba na kupanua lango la kuingilia meli bandarini na sehemu ya kugeuzia meli inaendelea na ujenzi wake umefikia asilimia 15. Vilevile, Serikali imeendelea kuboresha Bandari za Tanga na Mtwara ambapo kazi ya uongezaji wa kina cha lango la kuingilia Meli kutoka mita nne hadi mita 13 pamoja na kuweka vifaa vya kuongozea Meli katika Bandari ya Tanga umekamilika. Utekelezaji wa awamu ya pili ya uboreshaji wa Bandari ya Tanga umefikia asilimia 25.

90.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali itanunua vivuko vipya vitano vitakavyotoa huduma katika maeneo ya Kisorya - Rugezi, Ijinga - Kahangala, Bwiro - Bukondo, Nyakarilo - Kome, Nyamisati - Mafia na kivuko kipya cha Magogoni - Kigamboni pamoja na kuendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu muhimu ya usafiri na usafirishaji.

MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI

91.        Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya mawasiliano kwa kupanua mtandao wa mkongo wa Taifa wa mawasiliano nchini na katika nchi jirani ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi kwa njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

92.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali imejenga kilomita 409 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kufikia urefu wa kilomita 8,319 sawa na asilimia 55 ya lengo la kufikia kilomita 15,000 ifikapo mwaka 2025. Aidha, kwa upande wa kuunganisha na nchi zinazopakana na Tanzania, Serikali imefanikiwa kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na nchi ya Msumbiji kutokea eneo la Mangaka hadi Mtambaswala. Hatua hii imefanya nchi zilizounganishwa na Mkongo wa Taifa kufikia saba ambazo ni: Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda, Msumbiji, Malawi na Zambia. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inaunganishwa kupitia Ziwa Tanganyika na hivyo kufanya nchi yetu kuwa kitovu cha mawasiliano katika ukanda wa maziwa makuu kuelekea uchumi wa kidijitali.

HUDUMA ZA JAMII

Elimu

93.        Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa elimu kama nyenzo imara kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, Serikali imeendelea kuboresha na kuimarisha elimumsingi, ufundi na elimu ya juu. Katika mwaka 2021/2022, Serikali imeendeela kutekeleza mpango wa Elimumsingi Bila Ada kwa mafanikio makubwa ambapo hadi kufikia Februari 2022, shilingi bilioni 192.4 zimetumika kutekeleza mpango huo katika shule za msingi na sekondari. Pia, kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19, Serikali imetumia shilingi bilioni 304 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 12,000 vya shule za sekondari, vyumba vya madarasa 3,000 ya vituo shikizi na ujenzi wa mabweni 50.

94.        Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi ambapo katika mwaka 2021/2022, imekamilisha ujenzi na ukarabati wa vyuo 14 vya Maendeleo ya Wananchi; na ujenzi wa vyuo vipya 25 vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (VETA) vya Wilaya. Vilevile, Serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo vipya vinne vya ufundi na mafunzo ya Ufundi Stadi vya Mikoa ya Njombe, Simiyu, Geita na Rukwa. Aidha, ukarabati na ujenzi wa vyuo vitatu vya ualimu vya Sumbawanga (Rukwa), Dakawa na Mhonda (Morogoro) unaendelea.

95.        Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa elimu ya juu kwa kuongeza fedha za mikopo kwa ajili ya wanafunzi ambapo katika mwaka 2021/2022, jumla ya Shilingi bilioni 570 zimetumika ikilinganishwa na Shilingi bilioni 464 zilizotumika mwaka 2020/2021. Vilevile, idadi ya wanufaika imeongezeka kutoka 149,398 mwaka 2020/2021 hadi wanafunzi 177,605 mwaka 2021/2022.

 

96.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea kutekeleza Mpango wa Elimumsingi Bila Ada kwa lengo la kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa na kupata elimu bora. Aidha, Serikali itaendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu ili kuimarisha mazingira ya kujifunza na kujifunzia katika ngazi zote za elimu sambamba na kutoa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Maji

97.        Mheshimiwa Spika, kwa upande wa huduma za maji, Serikali imekuwa ikitoa kipaumbele katika kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji ikiwa ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa maji pamoja na usafi wa mazingira vijijini na mijini.

 

98.        Mheshimiwa Spika, Serikali ina dhamira ya dhati kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji mijini na vijijini unafika zaidi ya wastani wa asilimia 95 na 85 mtawalia ifikapo mwaka 2025. Hadi Februari, 2022, hali ya upatikanaji wa maji safi maeneo ya mijini imefikia asilimia 86. Aidha, kati ya miradi 114 inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali, miradi 40 imekamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wapatao 1,978,730 na miradi 74 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Kwa upande wa maeneo ya vijijini, upatikanaji wa maji umefikia asilimia 72.3. Aidha, utekelezaji wa miradi 265 umekamilika na imeanza kutoa huduma ya maji safi kwa wananchi wapatao 1,336,856. Utekelezaji wa miradi mingine 823 unaendelea na upo katika hatua mbalimbali.

 

99.        Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji katika miji 28 pamoja na mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria hadi Dodoma. Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi na utunzaji wa vyanzo vya maji ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji safi.

Afya

100.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini kwa kujenga vituo vya kutoa huduma za afya pamoja na upatikanaji wa dawa na vifaa tiba. Katika mwaka 2021/2022, Serikali imekamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini Mtwara na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato ambazo tayari zimeanza kutoa huduma kwa wananchi. Aidha, upanuzi na ukarabati wa majengo katika Hospitali za Rufaa za Mikoa 13 umefanyika katika Hospitali za Mwananyamala, Iringa, Mawenzi (Kilimanjaro), Ligula (Mtwara), Bombo (Tanga), Manyara, Maweni (Kigoma), Mbeya, Sekou Toure (Mwanza), Songea, Sumbawanga (Rukwa), Kitete (Tabora) na Tumbi (Kibaha Pwani). Ukarabati na upanuzi huo umewezesha kupatikana kwa huduma za kibingwa ambazo awali zilikuwa hazipatikani katika hospitali hizo.

101.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi nchini. Huduma hizo ni pamoja na upandikizaji wa uloto (bone marrow transplant) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye sakafu ya ubongo kupitia tundu la pua katika Taasisi ya Mifupa - MOI na upasuaji mgumu wa moyo kwa kutumia tundu dogo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete. Hatua hizo zimesaidia kuwapunguzia gharama na adha wananchi na Serikali kwa kutafuta huduma hizo nje ya nchi.

102.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali imedhamiria kuendelea kuimarisha miundombinu ya afya ikiwemo ujenzi na ukarabati wa hospitali, vituo vya afya na zahanati. Aidha, itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba, vitendanishi na kuboresha huduma za kibingwa.

Mpango wa Maendeleo na Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19

103.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa UVIKO-19 kwa kuanzisha rasmi utekelezaji wa afua ya chanjo ya UVIKO 19 na kuratibu upatikanaji wa chanjo hizo. Hadi tarehe 28 Februari, 2022, jumla ya dozi 9,845,774 zimepokelewa nchini, dozi 5,426,840 sawa na asilimia 55 zimesambazwa mikoani na watu 2,664,373 walichanjwa dozi kamili. Nitoe wito kwa Watanzania wote kuendelea kupata chanjo hizo ambazo ni za bure na zinapatikana katika maeneo yote nchini.

104.    Mheshimiwa Spika, katika kupunguza athari za UVIKO -19 nchini, Serikali ilipatiwa mkopo wa shilingi trilioni 1.3 na Shirika la Fedha Duniani kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Maendeleo na Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19. Sekta zilizonufaika na Mpango huo ni maji (shilingi bilioni 139.4), elimu (shilingi bilioni 368.9), afya (shilingi bilioni 466.9), utalii (shilingi bilioni 90.2), jamii inayoishi kwenye mazingira magumu (shilingi bilioni 5.5), na kundi la vijana, wanawake na watu wenye ulemavu (shilingi bilioni 5). Aidha, shilingi bilioni 231 zilielekezwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na shilingi bilioni 5 kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo uratibu.

105.    Mheshimiwa Spika, sote ni mashahidi kwamba utekelezaji wa Mpango huo umesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za kijamii katika maeneo yetu ikiwemo afya, elimu, maji, utalii, maeneo ya biashara za wajasiriamali wadogo, uwezeshaji wa makundi ya wanawake, vijana, watu wenye ulemavu pamoja na kaya maskini. Vilevile, Mpango huo umeimarisha upatikanaji sambamba na kusogeza huduma za jamii kwa wananchi.

HUDUMA KWA MAKUNDI MAALUM

106.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha huduma kwa watu wenye ulemavu kwa kutenga kiasi cha shilingi bilioni 3.46 kwa ajili ya ukarabati wa vyuo vya watu wenye ulemavu nchini. Katika mwaka 2021/2022 ukarabati wa Vyuo vya Ufundi Stadi na Marekebisho kwa Watu wenye Ulemavu vya Luanzari (Tabora) na Masiwani (Tanga) umekamilika. Aidha, ukarabati katika vyuo vinne katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Singida na Tabora unaendelea.

107.    Mheshimiwa Spika, Serikali imezindua pia Mwongozo wa Utambuzi wa Mapema na Afua Stahiki kwa Watoto wenye Ulemavu wa mwaka 2021. Mwongozo huu utawezesha utambuzi wa mapema wa watoto wenye ulemavu ili kupunguza makali ya ulemavu ukubwani. Vilevile, Serikali imeendelea kuzisimamia mamlaka za ajira kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata fursa za ajira.

108.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023 Serikali itaifanya maboresho ya Sera ya Taifa ya Huduma na Maendeleo ya watu wenye ulemavu, kuhakikisha upatikanaji wa vifaa saidizi na kuendelea kuhamasisha jamii kuondokana na unyanyapaa dhidi ya watu wenye ulemavu.

109.    Mheshimiwa Spika, nyote mtakubaliana nami kuwa utekelezaji wa masuala ya kijinsia ni mtambuka. Kwa msingi huo, yanahitaji ushiriki wa jamii nzima. Serikali kwa kutambua hilo imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo jumuiya za kimataifa katika kujenga usawa kwa makundi yote kwa kuridhia Itifaki mbalimbali zinazohusu usawa wa kijinsia, haki za mtoto na makundi mengine.

110.    Mheshimiwa Spika, ili kujenga kizazi chenye usawa wa kijinsia, nchi yetu inatekeleza eneo la pili kati ya maeneo sita ya ajenda ya haki za wanawake, usawa wa kijinsia na malengo ya Jukwaa la Kimataifa la Kizazi Chenye Usawa la Umoja wa Mataifa linalohusu haki na usawa wa kiuchumi kwa wanawake. Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo Desemba, 2021 alizindua Kamati ya Ushauri ya Kitaifa ya Utekelezaji wa Ahadi za Nchi kuhusu Kizazi Chenye Usawa ili kuhakikisha eneo hilo linaratibiwa kikamilifu. Aidha, Tanzania imeungana na mataifa mengine katika kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia sambamba na maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.

111.    Mheshimiwa Spika, nitoe pongezi nyingi sana kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kusimamia vema masuala ya usawa wa kijinsia. Kutokana na jitihada zake katika kuimarisha na kutoa kipaumbele katika masuala ya usawa wa kijinsia nchini, aliombwa na akaridhia kuwa kinara wa Jukwaa la Kimataifa la Kizazi Chenye Usawa la Umoja wa Mataifa linalohusu haki na usawa wa kiuchumi kwa wanawake. Hii imedhihirisha kwamba dunia imetambua kazi njema inayofanywa na jemedari wetu, mama yetu, mpendwa wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

112.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza azma yake ya kujenga mazingira bora kwa kundi maalum la wafanyabiashara wadogo maarufu kama Wamachinga. Katika mwaka 2021/2022, Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO -19 imetoa shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kuboresha miudombinu ya kufanya biashara kwa wafanyabiashara wadogo katika Halmashauri 11 za Dodoma, Mwanza, Arusha, Tanga, Mbeya, Dar es Salaam, Kinondoni, Temeke, Ubungo, Morogoro na Mji wa Tunduma.

113.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea kutekeleza afua mbalimbali za kuimarisha ustawi wa makundi maalum ikiwa ni pamoja na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, watoto na wazee; kuratibu wafanyabiashara wadogo ili kuboresha mazingira ya biashara zao; na kuimarisha uwezeshaji wanawake kiuchumi.

ULINZI NA USALAMA

114.    Mheshimiwa Spika, hali ya ulinzi na usalama katika nchi yetu imeendelea kuwa shwari kutokana na kazi kubwa inayofanywa na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama katika kulinda mipaka yetu pamoja na usalama wa raia na mali zao. Katika kuhakikisha Taifa letu lina usalama wa kutosha na kuchangia usalama wa mataifa mengine, Jeshi letu limeendelea kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vya Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika katika operesheni mbalimbali za ulinzi wa amani. Katika mwaka 2021/2022, nchi yetu imepeleka vikosi, waangalizi wa kijeshi, wanadhimu na makamanda katika nchi za Lebanon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Msumbiji.

115.    Mheshimiwa Spika, Jeshi letu la Kujenga Taifa limeendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi hususan ujenzi, uendeshaji wa viwanda, ufanyaji tafiti, uhawilishaji wa teknolojia pamoja na kushiriki katika kandarasi mbalimbali kupitia Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT). Katika mwaka 2021/2022, SUMAJKT ilishiriki kikamilifu katika ujenzi unaoendelea wa majengo ya Ofisi za Wizara na Taasisi zilizopo Mji wa Serikali - Mtumba Mkoani Dodoma. Aidha, kupitia mradi huo na miradi mingine Shirika limefanikiwa kuzalisha ajira zaidi ya 9,341 kwa vijana ambapo kati ya ajira hizo za kudumu ni 145 na za muda ni 9,196. Kupitia ushiriki wa JKT kwenye miradi hiyo, Serikali imepunguza gharama za uendeshaji wa mafunzo ya vijana wa mujibu wa Sheria na wa kujitolea kwa kushiriki katika shughuli za ujenzi, viwanda, kilimo na mifugo, ulinzi na mradi wa matrekta na zana za kilimo.

116.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea kuimarisha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kuvipatia vifaa na zana bora za kisasa pamoja na kuwezesha mafunzo na mazoezi stahiki ili viweze kutekeleza majukumu yake ya msingi ya ulinzi wa raia na mali zao pamoja na mipaka ya nchi yetu.

MASUALA YA KAZI NA WAFANYAKAZI

117.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na viwango vya kazi kwa kufanya kaguzi ili kuhakikisha waajiri wanazingatia mikataba ya ajira, saa za kazi, ujira kwa lengo la kupunguza migororo na kuongeza tija. Hadi Februari, 2022, jumla ya kaguzi 3,629 za viwango vya kazi zilifanyika sawa na asilimia 76 ya kaguzi 4,800 zilizopangwa kufanyika. Aidha, kaguzi 96,693 za afya na usalama mahala pa kazi zilifanyika ambapo kumekuwa na ongezeko la upimaji afya mahala pa kazi kutoka Wafanyakazi 125,616 hadi Wafanyakazi 169,735. Kufuatia kaguzi hizo, waajiri 2,114 waliobainika kukiuka Sheria za kazi walichukuliwa hatua mbalimbali.

118.    Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi thabiti wa Jemedari wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kutekeleza kwa vitendo azma ya kuimarisha mazingira na kuvutia uwekezaji nchini. Katika mwaka 2021/2022, Serikali imekamilisha Mfumo wa Kielektroniki wa Utoaji wa Vibali vya Kazi kwa Wageni na Wawekezaji. Mfumo huu umepunguza muda wa kushughulikia maombi ya vibali vya kazi kutoka siku za kazi 14 hadi 7 na kupunguza hatua za uchakataji wa kibali kutoka hatua 33 hadi 7. Ni imani ya Serikali kuwa hatua zote hizi muhimu zilizofanyika zitapunguza malalamiko ya muda mrefu ya wadau na hivyo kurahisisha ajira za raia wa kigeni na shughuli za uwekezaji.

119.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa Sheria za kazi na uratibu wa ajira za wageni nchini kwa kufanya ukaguzi katika maeneo ya kazi na kutoa elimu na ushauri.

HIFADHI YA JAMII

120.    Mheshimiwa Spika, sekta ya Hifadhi ya Jamii imekuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi wetu pamoja na ustawi kwa wananchi. Katika mwaka 2021/2022, Serikali iliridhia kulipa deni la shilingi Trilioni 2.17 katika Mfuko wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ambazo ni stahili ya mafao kwa wanachama waliorithiwa kutoka uliokuwa Mfuko wa PSPF mwaka 1999. Kiasi hicho kililipwa kupitia Hati Fungani za Serikali.

121.    Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umelipa mafao kwa wanufaika, wastaafu na wategemezi wapatao 32,467 yenye thamani ya shilingi trilioni 1.05. Aidha, Mfuko umelipa kiasi cha shilingi bilioni 352.51 ikiwa ni pensheni ya kila mwezi kiasi ambacho ni sawa na wastani wa shilingi bilioni 58.75 kila mwezi kwa wastaafu 148,866. Vilevile, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umelipa mafao kwa wanufaika, wastaafu na wategemezi wapatao 98,202 yenye thamani ya shilingi bilioni 363.7. Pia, Mfuko umelipa kiasi cha shilingi bilioni 64.9 ikiwa ni pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu 24,881.

122.    Mheshimiwa Spika, katika kujenga mazingira wezeshi kwa waajiri na kupunguza gharama za uendeshaji, Serikali kupitia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi imepunguza kiwango cha uchangiaji kwa Waajiri wa Sekta Binafsi kutoka asilimia 1 hadi asilimia 0.6. Uamuzi wa kupunguza kiwango hicho cha uchangiaji, umetokana na utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kuhusu taasisi za Serikali kuhakikisha zinaweka mazingira bora ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ili kukuza uchumi wa nchi na kulinda rasilimali watu.

123.    Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka 2022/2023, itaendelea kusimamia Sekta ya Hifadhi ya Jamii ili kuhakikisha inakidhi matarajio ya waajiri na wafanyakazi katika Sekta ya Umma na Sekta Binafsi.

UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI

124.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza azma ya kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kuanzisha vituo maalum vya uwezeshaji wananchi kiuchumi, utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa vikundi mbalimbali na kutekeleza mpango wa kunusuru kaya masikini. Hadi Februari 2022, Serikali kupitia mifuko mbambali ya uwezeshaji wananchi kiuchumi imewezesha utoaji wa mikopo ya masharti nafuu yenye thamani ya shilingi bilioni 631 kwa wanufaika 1,194,155. Aidha, imeanzisha vituo 17 vya uwezeshaji wananchi kiuchumi katika Mikoa ya Shinyanga, Geita, Singida, Rukwa, Kigoma na Dodoma.

125.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na utekelezaji wa kipindi cha pili cha Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika Awamu ya Tatu ya TASAF kwa Tanzania Bara na Zanzibar. Katika mwaka 2021/2022, ruzuku ya shilingi bilioni 117.91 ilihawilishwa kwa kaya 1,279,325 zilizokidhi vigezo vya kuingia katika kipindi cha pili cha mpango kutoka halmashauri 184 kwa Tanzania Bara na Zanzibar. Aidha, Serikali imeendelea kutenga asilimia 10 ya makusanyo ya halmashauri kwa ajili ya uwezeshaji wa wanawake, vijana na wenye ulemavu. Hadi Desemba 2021, halmashauri zilitenga jumla ya shilingi bilioni 35.7 kwa ajili ya uwezeshaji wa wanawake, vijana na wenye ulemavu.

Ukuzaji wa Fursa za Ajira na Ujuzi

126.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali imechukua hatua za makusudi hususan utekelezaji wa miradi ya kielelezo, ujenzi wa viwanda, sambamba na kuimarisha sekta binafsi kwa ajili ya kuongeza fursa za ajira na ujuzi kwa Watanzania. Kutokana na juhudi hizo, idadi ya ajira (kujiajiri na kuajiriwa) zilizozalishwa ni 584,333.

127.    Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu imefanya utafiti wa hali ya nguvukazi nchini ili kupata viashiria muhimu vitakavyotumika katika kuhuisha, kutunga, kufuatilia na kutathmini sera, mikakati na programu za soko la ajira nchini. Utafiti huo umeonesha kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira nchini kimepungua kutoka asilimia 10.3 mwaka 2014 hadi asilimia 9.0 mwaka 2021. Aidha, nguvukazi ya vijana ni watu milioni 14.2 sawa na asilimia 55 ya nguvukazi yote nchini. Vijana milioni 12.5 sawa na asilimia 87.8 ya nguvukazi ya vijana nchini wameajiriwa au kujiajiri. Sekta ya kilimo imeendelea kuongoza kwa kutoa zaidi ya asilimia 63 ya ajira kwa vijana.

128.    Mheshimiwa Spika, kupitia utekelezaji wa Programu ya Kitaifa ya Kukuza Ujuzi Nchini, vijana 22,899 wamepatiwa ujuzi unaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa. Kati ya hao, vijana 14,440 wakiwemo vijana wenye ulemavu 349 wamepatiwa mafunzo ya uanagenzi katika fani za ufundi stadi katika vyuo na taasisi 72 nchini. Vijana 3,600 wamewezeshwa kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba na vijana 2,644 wamepewa mafunzo ya kurasimishiwa ujuzi walioupata kupitia mfumo usio rasmi. Vilevile, Serikali imewezesha wahitimu 2,215 kupata mafunzo ya uzoefu kazini katika taasisi binafsi na umma.

129.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea kuratibu, kusimamia, kufuatilia na kutathmini masuala yanayolenga kuwawezesha wananchi kiuchumi ili wanufaike na fursa zilizopo na kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi. Vilevile, itaendelea kuratibu utekelezaji wa masuala ya ukuzaji ajira na kazi zenye staha kupitia utekelezaji wa Sera, Mikakati na Mipango mbalimbali ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa ili kuhakikisha nguvu kazi ya Taifa inapata ujuzi stahiki pamoja na kuongeza fursa za ajira nchini.

MASUALA MTAMBUKA

SENSA YA WATU NA MAKAZI 2022

130.    Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu Sensa ya Watu na Makazi ni muhimu katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Taifa letu. Hivyo, ifikapo Agosti mwaka huu nchi yetu itaendesha zoezi la sensa ya watu na makazi lenye lengo la kukusanya, kuchakata, kuchambua na kusambaza taarifa za kidemografia, kiuchumi, mazingira na kijamii za watu wote na makazi yao katika nchi kwa kipindi maalum.

131.    Mheshimiwa Spika, sensa ya mwaka huu ni ya kipekee kwa kuwa imeunganishwa na mazoezi mawili makubwa ya kitaifa ambayo ni Sensa ya Anwani za Makazi na Sensa ya Majengo. Aidha, sensa ya majaribio iliyofanyika katika mikoa 13 ya Tanzania Bara na Zanzibar Agosti, 2021 imekamilika kwa ufanisi wa hali ya juu pamoja na mfumo wa kuchakata takwimu husika. Hii ni kwa sababu sensa ya mwaka 2022 ni ya kidijitali katika hatua zote za matayarisho, kuhesabu na kuchapisha takwimu zenyewe.

132.    Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, hadi tarehe 18 Machi, 2022 maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi yamefikia zaidi ya asilimia 76. Sambamba na hilo, kazi ya kutenga maeneo madogo madogo ya kuhesabia watu yapatayo 4,313 katika Shehia 388 upande wa Tanzania Zanzibar imekamilika. Kwa upande wa Tanzania Bara kazi hii imekamilika kwa mikoa 25 katika vitongoji vyote 64,318.

133.    Mheshimiwa Spika, katika kukamilisha azma hiyo, Serikali imetekeleza Mpango wa Uelimishaji Umma kuhusu umuhimu wa sensa pamoja na mpango kazi na uundwaji wa Kamati za Sensa katika ngazi zote za utawala. Hivyo, ninawashukuru wadau wote wa maendeleo kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa zoezi hili muhimu kwa mustakabali wa Taifa letu.

134.    Mheshimiwa Spika, naomba Viongozi wote tusaidiane kuhamasisha na kusimamia utekelezaji wa zoezi la Sensa katika maeneo yetu. Aidha, nitoe wito kwa viongozi wa dini kuwaelimisha waumini wao kuhusu umuhimu wa kuhesabiwa. Vilevile, niwaombe wananchi wote washiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kwa kutoa ushirikiano na taarifa sahihi kwa Makarani wa Sensa na Wasimamizi ambao watatembelea kaya zetu. Niwahakikishie wananchi wote, kuwa taarifa zote zinazokusanywa wakati wa sensa ni siri na zitatumika kwa shughuli za kitakwimu tu. Takwimu hizo hazina uhusiano na dini, kodi, siasa, kabila au mambo mengine kama hayo ambayo hayakukusudiwa.

Vita Dhidi ya Rushwa

135.    Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan inaendelea kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi. Hadi Februari, 2022, kesi 715 zikiwemo kesi mpya 204 zimeendeshwa katika mahakama mbalimbali. Kesi 287 ziliamuliwa mahakamani na watuhumiwa 155 walikutwa na hatia. Aidha, shilingi bilioni 1.39 ziliokolewa kutokana na operesheni za uchunguzi zilizofanyika katika maeneo mbalimbali nchini. Vilevile, katika kuhakikisha kwamba miradi inayotekelezwa nchini inalingana na thamani ya fedha, ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo 370 yenye thamani ya shilingi trilioni 4.6 umefanyika katika sekta za afya, maji, fedha, elimu, kilimo, ujenzi na viwanda.

136.    Mheshimiwa Spika, mikakati iliyotekelezwa na Serikali katika kupambana na rushwa imeleta nidhamu, uadilifu na uwajibikaji na kuiletea sifa nzuri nchi yetu kimataifa. Kwa mujibu wa Taarifa ya Transparency International ya mwaka 2021, Tanzania kwa kupitia kiashiria cha Corruption Perception Index imeendelea kufanya vizuri kwa kushika nafasi ya 87 kati ya nchi 180 ikiwa imepanda kwa nafasi 7 ikilinganishwa na nafasi ya 94 mwaka 2020. Aidha, katika mwaka 2022/2023 Serikali itaendeleza mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi kwa kuweka kipaumbele kwenye utoji wa elimu kwa umma kuhusu madhara ya vitendo hivyo.

Mapambano dhidi ya UKIMWI

137.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali imeweka jitihada za kuendelea kupunguza maambukizi mapya, vifo, unyanyapaa na kuimarisha huduma za msingi kwa WAVIU. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, hadi Desemba 2020, idadi ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI nchini imefika milioni 1.7. Takwimu zinaonesha maambukizi mapya ya VVU kwa wenye umri kuanzia miaka 15 na zaidi yameshuka kutoka watu 110,000 mwaka 2010 hadi 68,000 mwaka 2020. Idadi ya vifo vitokanavyo na UKIMWI vimepungua kwa asilimia 50 kutoka vifo 64,000 mwaka 2010 hadi 32,000 mwaka 2020. Aidha, idadi ya WAVIU wanaopata dawa za kufubaza VVU imeongezeka kutoka asilimia 95 mwaka 2016 hadi asilimia 98.3 mwaka 2020.

138.    Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, takwimu zinaonesha idadi ya wanaume wanaojitokeza kupima na kupata huduma za VVU na UKIMWI ikiwemo kutumia dawa za kufubaza VVU ni ndogo. Hivyo, nitoe wito kwa Watanzania wenzangu hususan wanaume tujitokeze kupima ili tuchukue hatua za mapema kutokana na hali zetu. Katika mwaka 2022/2023, Serikali kwa kushirikiana na wadau itaendelea kutekeleza programu mbalimbali ili kuzuia maambukizi mapya ya VVU kwa makundi yote ili kuwezesha nchi kufikia lengo la Kimataifa la kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.

Mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya

139.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kupambana na dawa za kulevya kwa kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya matumizi ya dawa hizo. Hadi Februari 2022, jumla ya watuhumiwa 11,716 walikamatwa na kilogramu 35,227.25 za dawa za kulevya zikiwemo kilogramu 1,124.52 za heroin, gramu 811.3 za cocaine, tani 22.74 za bangi, tani 10.93 za mirungi na kemikali bashirifu zaidi ya kilogramu 432. Aidha, ekari 185 za bangi na ekari 10 za mirungi ziliteketezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

140.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha huduma za matibabu kwa watumiaji wa dawa za kulevya kwa kuongeza idadi ya kliniki zinazotoa huduma kwa waathirika wa dawa za kulevya kutoka 9 mwaka 2020/2021 hadi kliniki 15 zinazohudumia waathirika zaidi ya 10,600 mwaka 2021/2022. Licha ya hayo, Serikali kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi imewezesha Waraibu wa Dawa za Kulevya waliopata nafuu wapatao 200 kupata mafunzo ya ujuzi kupitia vyuo vya VETA na SIDO. Nitoe wito kwa wadau wote mkiwemo Waheshimiwa Wabunge wenzangu, asasi za kiraia, viongozi wa dini, vyombo vya habari na jamii nzima kushirikiana na Serikali kutoa elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya.

Uratibu wa Masuala ya Lishe

141.    Mheshimiwa Spika, maendeleo ya Taifa yanahitaji uwepo wa nguvu kazi yenye afya njema na inayopata lishe bora ili kuimarisha uwezo wa kufanya kazi. Kutokana na umuhimu huo, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali kuhusu lishe ukiwemo Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa Masuala ya Lishe wa mwaka 2016/2017 - 2020/2021. Mafanikio yaliyopatikana katika kipindi hicho ni pamoja na: kupunguza udumavu kutoka asilimia 34.7 hadi asilimia 31.8; kupunguza kiwango cha ukondefu kutoka asilimia 3.8 hadi asilimia 3.5; kupunguza upungufu wa wekundu wa damu kwa wanawake wenye umri wa miaka 15 - 49 wasio wajawazito kutoka asilimia 44.8 hadi asilimia 28.8; na kuongeza kiwango cha unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa watoto wachanga kutoka asilimia 41.1 hadi asilimia 58.

142.    Mheshimiwa Spika, kufuatia kukamilika kwa mpango huo, Serikali imeandaa Mpango Jumuishi wa Pili wa Kitaifa wa Masuala ya Lishe wa Mwaka 2020/2021 - 2025/2026 sambamba na mkakati wake wa utafutaji fedha. Jumla ya shilingi bilioni  642.3 zitahitajika katika kipindi cha miaka mitano ili kuwezesha utekelezaji wa Mpango huo. Serikali kwa upande wake itaendelea kutenga fedha za kugharimia utekelezaji wa Mpango huo ili kuhakikisha jamii inakuwa na afya bora. Nitoe wito kwa Wadau wa Maendeleo na Sekta Binafsi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha hali ya lishe nchini.

Uratibu wa Maafa

143.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuratibu shughuli za usimamizi wa maafa nchini kwa kuzuia, kupunguza madhara na kujiandaa kukabiliana na maafa pindi yanapotokea. Katika mwaka 2021/2022, Serikali imefanya maboresho ya mfumo wa utendaji wa shughuli za maafa ambapo Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa ya mwaka 2022 umeandaliwa. Kutungwa kwa Sheria hii kutaimarisha mfumo wa kitaasisi wa usimamizi na uratibu wa shughuli za maafa nchini kwa kuzingatia wajibu wa kisekta na taasisi kwa mujibu wa Sheria zilizopo.

144.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza mpango wa kutoa elimu kwa umma na kuimarisha uwezo wa utendaji kazi wa Kamati za Usimamizi wa Maafa, Waratibu wa Maafa na Timu za Wataalam za Kukabiliana na Maafa za Wilaya na Mikoa. Lengo ni kuhamasisha wadau na jamii kuchukua hatua stahiki za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga na kujiandaa kukabiliana na maafa.

145.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea kuzijengea uwezo Kamati za Usimamizi wa Maafa za Mikoa na Wilaya, kuimarisha mifumo ya kielektroniki ya usimamizi wa maafa, kuhakikisha uwepo wa vifaa vya kukabiliana na maafa na misaada ya huduma za kibinadamu.

Mazingira

146.    Mheshimiwa Spika, uhifadhi wa mazingira ni muhimu kwa ustawi wa mifumo-ikolojia na maliasili zilizopo nchini. Serikali kwa kutambua hilo, imeendelea kushughulikia changamoto za uharibifu wa mazingira kwa kusimamia na kutekeleza sera, sheria, kanuni, mikakati, mipango na miongozo ya hifadhi na usimamizi wa mazingira. Aidha, Serikali imeendelea kuratibu utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa ya Mazingira na miradi mbalimbali ya hifadhi ya mazingira.

147.    Mheshimiwa Spika, miongoni mwa kazi zilizotekelezwa katika mwaka 2021/2022 ni kutunga Sera mpya ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 na mkakati wake wa utekelezaji pamoja na kuboresha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira na kanuni zake. Aidha, Serikali imeandaa Mpango Kabambe wa Kutatua Changamoto za Mazingira.

148.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea kutekeleza mikakati ya uhifadhi wa mazingira kwa kushirikiana na wadau mbalimbali; Mpango wa Kitaifa wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi; kutoa elimu ya hifadhi ya mazingira kwa umma na kuhamasisha kampeni ya upandaji miti. Vilevile, itaendelea kusimamia mifumo ya uzalishaji viwandani ili izingatie hifadhi ya mazingira pamoja na kutumia teknolojia rafiki.

Utawala Bora

149.    Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha masuala ya utawala bora, Bunge lako tukufu lilipitisha miswada mbalimbali kuwa Sheria ikiwa ni pamoja na Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa mwaka 2021. Muswada huo ulihusisha Marekebisho ya Sheria ya Tafsiri ya Sheria iliyofanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya Sheria na kutumika katika shughuli za Kimahakama. Hatua hii itawezesha mchakato wa utoaji haki kuwa na uwazi, usawa na wenye gharama nafuu. Aidha, Serikali imepanua wigo wa mfumo wa utoaji haki kwa kuwawezesha Mawakili kuanza kutoa huduma za uwakili katika Mahakama za Mwanzo.

150.    Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka 2022/2023 itaendelea kuimarisha utawala bora na utawala wa Sheria ikiwa ni pamoja na kuimarisha mfumo wa utatuzi wa migogoro. Aidha, itaimarisha mifumo ya ushirikishaji wananchi katika maamuzi na mipango ya maendeleo.

MUUNGANO

151.    Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kudumisha Muungano wetu ambao ni tunu na mfano wa kuigwa Barani Afrika na dunia nzima. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeendelea kushughulikia changamoto mbalimbali zinazojitokeza kwa lengo la kuulinda, kuuenzi na kuudumisha Muungano wetu. Katika mwaka 2021/2022, kupitia vikao mbalimbali, hoja kumi na moja zilifanyiwa kazi na kukamilika. Kati ya hizo, hoja tisa zimeandaliwa Hati za Makubaliano na kusainiwa na hoja mbili za kiutendaji zinaendelea kutekelezwa na mamlaka husika.

152.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023 Serikali itaendelea kuulinda, kuuenzi na kuudumisha Muungano wetu. Aidha, tutaendeleza ushirikiano baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuhakikisha mipango inayotekelezwa inanufaisha pande zote za Muungano na Taifa kwa ujumla.

UHUSIANO WA KIMATAIFA

153.    Mheshimiwa Spika, uhusiano kati ya Tanzania na mataifa mengine umeendelea kuimarika. Uimara huo umechangiwa na ziara za viongozi wakuu wa kitaifa katika nchi mbalimbali sambamba na viongozi wakuu wa nchi hizo na Mashirika ya Kimataifa kuzuru nchini. Kupitia ziara hizo, nchi yetu imepata manufaa makubwa ikiwemo kuingia makubaliano ya ushirikiano katika maeneo mbalimbali kama vile miundombinu, nishati, elimu, teknolojia ya habari na mawasiliano, afya, michezo, kilimo, uwekezaji na kukuza lugha ya Kiswahili.

154.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali imeshiriki katika mikutano mbalimbali ya kimataifa na kikanda ambapo viongozi wakuu wa nchi pamoja na masuala mengine, walipata fursa ya kuielezea dunia kuhusu sera na vipaumbele vya Serikali sambamba na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kisiasa na kiuchumi.

155.    Mheshimiwa Spika, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, aliongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 26 wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya Tabia ya Nchi (COP26) uliofanyika Glasgow nchini Uingereza. Kupitia mkutano huo, Mheshimiwa Rais alipata fursa ya kuainisha vipaumbele vya nchi na Serikali anayoingoza katika majadiliano ya ajenda za mabadiliko ya tabianchi.

156.    Mheshimiwa Spika, nchi yetu ilishiriki pia katika Mkutano wa 10 wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu uliofanyika Kinshasa – Kongo tarehe 24 Februari, 2022. Pamoja na kupokea taarifa mbalimbali kuhusu utekelezaji wa Mpango, mkutano huo ulikuwa ni fursa ya mazungumzo na viongozi mbalimbali kuhusu masuala ya diplomasia na uchumi. Kupitia mazungumzo na viongozi wakuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, tumekubaliana kufanya kongamano kubwa la kibiashara litakalokutanisha wafanyabiashara wakubwa wa Kongo na Tanzania. Hatua hii itawezesha wafanyabiashara wetu kujadili changamoto, kubaini na kuongeza fursa za uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na Kongo. Aidha, wigo wa uwekezaji, ufanyaji biashara na ajira umeendelea kupanuka baada ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kujiunga katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

157.    Mheshimiwa Spika, ninapenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali na Jumuiya ya Ulaya zimekubaliana kurejea kwenye majadiliano ya Kitaalam kuhusu Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi (Economic Partnership Agreement). Ninapenda kukuhakikishia kuwa majadiliano hayo yatazingatia maslahi mapana ya Taifa kwa lengo la kuinua uchumi wetu.

158.    Mheshimiwa Spika; katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje; kuimarisha na kudumisha uhusiano wa kidiplomasia, kuongeza fursa za biashara na uwekezaji kupitia utekelezaji wa diplomasia ya uchumi; kuimarisha na kukuza uhusiano wa kiuchumi na mataifa, jumuiya na taasisi nyingine za kimataifa; kushiriki katika juhudi za kuleta amani na usalama kwa kuunga mkono Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na Jumuiya za Kikanda. Aidha, itaendelea kuweka mazingira wezeshi, kuratibu na kuhamasisha ushiriki wa Watanzania waishio nje ya nchi kuchangia maendeleo ya Taifa.

SANAA NA MICHEZO

159.    Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kufanya jitihada mbalimbali kuhakikisha sekta hii nchini inapiga hatua kwenda mbele. Lengo ni kuimarisha michezo, sanaa na utamaduni ili ziweze kuchangia vema katika Pato la Taifa sambamba na kuzalisha ajira kwa vijana, kutangaza utalii, kuimarisha umoja wa kitaifa na afya za Watanzania.

160.    Mheshimiwa Spika, nyote mtakubaliana nami kwamba michezo na sanaa ni zaidi ya burudani kwani tumeshuhudia katika siku za hivi karibuni wanamichezo wetu wakinufaika kupitia sekta hiyo. Nitumie fursa hii kuwapongeza kwa dhati wanamichezo wote ambao wameiletea heshima nchi yetu kwa kupeperusha bendera nje ya nchi. Tuna timu za mpira wa miguu, ngumi na wasanii mbalimbali.

161.    Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mchezo wa ngumi, niwapongeze wanamasumbwi Hassan Mwakinyo, Tonny Rashid, Twaha Kiduku na Ibrahim Class kwa ushindi mnono uliowawezesha kupata mikanda katika mashindano mbalimbali ya kimataifa waliyoshiriki. Nitumie fursa hii pia kuzipongeza timu za mpira wa miguu za wanawake kwa ushindi wao katika mashindano mbalimbali ya kimataifa. Kipekee, niwapongeze Timu ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) kwa kutwa ubingwa katika mashindano ya COSAFA mwaka 2021. Vilevile, niipongeze sana Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Watu wenye Ulemavu (Tembo Warriors) kwa kufuzu kushiriki mashindano ya dunia yatakayofanyika Oktoba, 2022 nchini Uturuki. Hii ni mara ya kwanza Timu ya Taifa kushinda na kushiriki moja kwa moja mashindano ya dunia.

162.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali imekamilisha ujenzi wa Mfumo wa Usajili na Usimamizi wa Wasanii na Wadau wa Sanaa na kuboresha mfumo wa usajili kwa njia ya kielektroniki. Mfumo huo, umewezesha wabunifu 485 na kazi zao 2,921 kusajiliwa. Aidha, Serikali imewezesha Wasanii wa fani ya muziki ambao kazi zao zimetumika kwenye vituo vya redio na televisheni kupata mirabaha. Nitoe wito kwa wasanii wote nchini kujisajili katika mfumo huo ili kupata manufaa tarajiwa.

163.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Serikali itaendelea kujenga mazingira wezeshi kwa wadau wa michezo, sanaa na utamaduni ili kuifanya Tanzania kuweza kung’ara katika medani za Kimataifa. Sambamba na hilo, Serikali itajenga shule maalum 56 za kukuza vipaji vya michezo katika maeneo mbambali hapa nchini.

HITIMISHO

164.    Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu ni mratibu wa shughuli zote za Serikali. Jukumu hili linaifanya Ofisi hii kuwa nguzo muhimu katika uratibu, usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za Serikali. Aidha, mafanikio ya Serikali kwa mwaka 2021/2022 kwa kiasi kikubwa yamechangiwa na uratibu madhubuti katika sekta mbalimbali nchini.

165.    Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2022/2023, Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kuimarisha uratibu wa shughuli za Serikali ili kuongeza tija na ufanisi katika matumizi ya rasilimali fedha. Aidha, maeneo yatakayopewa kipaumbele ni pamoja na kuratibu utekelezaji wa Sera za Taifa ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii, kuratibu shughuli za maafa, kuboresha utendaji wa Baraza la Taifa la Biashara, uratibu wa shughuli za Serikali Bungeni, ufuatiliaji, tathmini na uratibu wa usimamizi wa shughuli za Serikali. Nitumie fursa hii kuwataka wadau wote waendelee kushirikiana na Serikali ili kurahisisha utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa tija na ufanisi.

166.    Mheshimiwa Spika, nimeeleza kwa muhtasari baadhi ya shughuli ambazo Serikali imetekeleza kwa kipindi kilichopita. Aidha, nimetoa mwelekeo wa kazi zitakazofanyika kwa mwaka 2022/2023. Kwa kuhitimisha, ninapenda kusisitiza mambo muhimu yafuatayo:

Mosi:Serikali ya Awamu ya Sita imepanga kufanya Sensa ya Watu na Makazi ifikapo Agosti, 2022. Zoezi hili ambalo limeshaanza katika hatua za awali lina umuhimu wa kipekee katika kuisadia Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025 na mipango mingine ya kitaifa na kitaifa. Taarifa za idadi ya watu husaidia mamlaka za ngazi ya Wilaya kutekeleza mipango ya maendeleo kwa kuweka uwiano wa mgawanyo wa rasilimali. Aidha, sensa hiyo itasaidia Serikali kupata taarifa za msingi za kidemografia, kijamii na kiuchumi. Hivyo, sote tuna wajibu wa kuhamasisha jamii kushiriki katika sensa, na kutoa taarifa na takwimu sahihi wakati makarani wa sensa ambao watakuwa na vitambulisho maalum vya Serikali watakapopita katika kaya zetu.

Pili:   Jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuvutia uwekezaji zimeleta mwamko na matumaini makubwa kwa wawekezaji. Azma ya Serikali ni kuona kwamba wawekezaji wakubwa wakiwemo wafanyabiashara na wakulima wanashirikiana kwa karibu na wawekezaji wa Kitanzania ili kuinua kipato cha Watanzania ikiwa ni pamoja na kuondoka kwenye kilimo cha kujikimu na kuingia katika kilimo cha kisasa chenye tija na cha kibiashara. Niwahakikishie Watanzania wote kwamba upatikanaji wa ardhi iliyopimwa kwa ajili ya uwekezaji utaendelea kuwa moja ya vipaumbele vya Serikali ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Tatu:Amani na usalama uliopo nchini umetujengea heshima kubwa katika Bara la Afrika na Duniani kote. Sote tuna wajibu wa kuenzi na kusimamia visitoweke. Serikali ya Awamu ya Sita itahakikisha kwamba Amani, usalama na umoja wa Kitaifa vinadumishwa ili kuwawezesha Wananchi kuendelea kufanya shughuli zao za maendeleo bila hofu. Serikali haitavumilia kuona mtu au kikundi cha watu wenye dhamira mbaya wakivuruga Amani, usalama, Umoja na Mshikamano uliopo nchini kwa kisingizio chochote. Nitumie nafasi hii kuwaomba viongozi wa Dini kuendelea kuhubiri juu ya wajibu wa kuheshimu utawala wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo ili kudumisha amani, usalama na mshikamano wa kitaifa.

Nne: Ili kujiletea maendeleo endelevu kwa haraka, ni vema wote tuwajibike kwa vitendo na kufanya kazi kwa bidii, ubunifu, ufanisi na umakini ili kufikia malengo tuliyojiwekea. Tunazo fursa nyingi za kukuza uchumi na kupunguza umaskini. Tujitahidi kuongeza tija na thamani katika bidhaa na mazao yetu ili kuwa na uchumi wa kisasa unaohimili ushindani katika masoko ya kikanda na Kimataifa.

Tano:Mpango wa muda wa kati wa Serikali ni kuendelea kutoa msukumo katika kutekeleza vipaumbele vya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026). Vipaumbele hivyo vinajumuisha kuchochea uchumi shindani na shirikishi; kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani na utoaji huduma; kukuza biashara na uwekezaji; kuchochea maendeleo ya watu na kuendeleza rasilimali watu.

Sita: Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeonesha dhamira ya dhati katika kukuza Sekta Binafsi pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi. Napenda kuuhakikishia Umma wa Tanzania kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kutambua, kuthamini na kushirikiana na sekta binafsi katika kukuza uchumi wa Taifa na jamii kwa ujumla.

Saba:Serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na Jumuiya za Kimataifa katika kukabiliana na kutokomeza maambukizi ya virusi vya UVIKO - 19. Vilevile, itaendelea kuhimiza Watanzania kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalam kuhusu kujikinga na kudhibiti ugonjwa wa UVIKO - 19. Aidha, Serikali itahakikisha kuwa chanjo inaendelea kupatikana katika vituo vya kutolea huduma ya afya.

Nane: Upandaji wa Bei za Bidhaa

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni kumekuwepo na taarifa za uhaba na upandaji wa bei usioendana na uhalisia wa soko kwenye bidhaa za ujenzi, vyakula, nishati na pembejeo za kilimo. Kufuatilia tarifa hizo, niliielekeza Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kuunda jopo la wataalamu ili kufuatilia taarifa hizo. Wizara hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Tume ya Ushindani ilifanya ufuatiliaji na tathmini ya mwenendo wa bei za bidhaa muhimu zinazozalishwa nchini na zile zinazotumia malighafi kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua mbalimbali ili kukabiliana na upandaji huo wa bidhaa muhimu. Hatua hizo ni pamoja na usimamiaji wa Sheria ya Ushindani Na. 8 ya mwaka 2003 ambayo inazuia kupanga bei. Hatua nyingine ni Serikali kutafuta vyanzo mbadala vya upatikanaji wa bidhaa na kuweka mifumo ya kusimamia masoko ya awali na minada.

Mheshimiwa Spika, Serikali inawaelekeza wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa muhimu kushusha mara moja bei za bidhaa walizopandisha pasipo kuendana na uhalisia wa soko ikiwa ni pamoja na kutokutumia kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani na Kwaresma kupandisha bei. Nawasihi wazalishaji na wafanyabiashara wa bidhaa muhimu kuuza bidhaa husika kwa kuzingatia gharama halisi za uingizaji, uzalishaji na usambazaji. Na wale watakaobainika kupandisha bei bidhaa muhimu bila utaratibu hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

167.    Mheshimiwa Spika, ninatoa wito kwa viongozi wenzangu wote kuendelea kuunga mkono jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi chini ya uongozi mahiri na thabiti wa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kufanya kazi kwa bidii, weledi, uadilifu, tija na ufanisi, uaminifu na kupiga vita rushwa. Ni dhahiri kwamba, matokeo ya utendaji huu yatapunguza umaskini kwa Watanzania na kuwaletea maendeleo.

168.    Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuendelea kusisitiza umuhimu wa michezo kwa kuvipongeza vilabu vyetu vya mpira wa miguu vinavyoshiriki kwenye mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara (NBC Premier League) na Ligi Kuu Zanzibar (PBZ Premier League). Hakika kwa mpira mzuri wanaocheza wanakonga mioyo ya washabiki wa mchezo wa mpira wa miguu nchini. Kipekee niipongeze timu ya Simba Sports Club kwa kupeperusha bendera ya Taifa letu katika mashindano ya Shirikisho la Klabu Afrika. Mwenye macho haambiwi tazama, sote tumeshuhudia wakiendelea kuupiga mwingi na kutuwakilisha vema katika medani za kimataifa.

169.    Mheshimiwa Spika, niwapongeze pia wachezaji mahiri wa vilabu mbalimbali vya mpira wa miguu vikiwemo Yanga - Timu ya Wananchi; Simba - Wekundu wa Msimbazi; Namungo - Watoto wa Kusini; Azam - Wazee wa Lambalamba; Biashara United - Wanajeshi wa Mpakani; Dodoma Jiji - Walima Zabibu; Tanzania Prison - Wajelajela na bila kuwasahau Mtibwa Sugar - Wakata Miwa na Kagera Sugar - Wanankurukumbi. Vilevile, nivipongeze vilabu vya Zanzibar vikiwemo KMKM, Mlandege, Malindi, Mafunzo na vilabu vinginevyo.

MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2022/2023

170.    Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2022/2023, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizo chini yake inaliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 148,892,553,000.00 (bilioni mia moja arobaini na nane milioni mia nane tisini na mbili laki tano hamsini na tatu elfu). Kati ya fedha hizo shilingi 101,365,398,000.00 (bilioni mia moja na moja milioni mia tatu sitini na tano laki tatu na tisini na nane elfu) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi 47,527,155,000.00 (bilioni arobaini na saba milioni mia tano ishirini na saba laki moja na hamsini na tanto elfu) ni kwa ajili Matumizi ya Maendeleo.

171.    Mheshimiwa Spika, vilevile naliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya shilingi 132,728,638,000.00 (bilioni mia moja thelathini na mbili milioni mia saba ishirini na nane laki sita na thelathini na nane elfu) kwa ajili ya Mfuko wa Bunge. Kati ya fedha hizo shilingi 127,328,638,000.00 (bilioni mia moja ishirini  na saba milioni mia tatu ishirini na nane laki sita na thelathini na nane elfu)  ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi 5,400,000,000.00 (bilioni tano na milioni mia nne) ni kwa ajili Matumizi ya Maendeleo.

172.    Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

08 April 2022, 15:39