Hija ya Kitume ya Papa Francisko: Kuomba Msamaha Ni Kitendo cha Ujasiri na Faraja
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Julai 2022 amekutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, wawakilishi wa watu asilia wa Canada pamoja na wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi na Mashirika ya Kimataifa nchini Canada. Hotuba ya Baba Mtakatifu ilijikita zaidi katika nembo zinazopatikana kwenye bendera ya Canada. Baba Mtakatifu amekazia utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; athari za ukoloni na umuhimu wa uinjilishaji unaosimikwa katika utamadunisho, unaozingatia na kuheshimu haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu amegusia kuhusu: mifumo mbalimbali ya ukoloni, lakini hasa ukoloni wa kiitikadi na madhara yake katika maisha ya watu. Amewahimiza watu wa Mungu nchini Canada kujenga na kuimarisha tunu msingi za maisha ya kifamilia na jamii katika ujumla wake. Changamoto zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo ni pamoja na: Ukosefu wa amani, athari za mabadiliko ya tabianchi na Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19; Mchango wa watu asilia wa Canada katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi bila kusahau athari za ongezeko la idadi ya maskini na wahitaji zaidi.
Kumbukumbu ya Watakatifu Joakim na Anna wazazi wake Bikira Maria inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 26 Julai ni muhimu sana kwa watu wa Mungu, kwani ni fursa ya kuwashukuru na kuwabariki wazee kutokana na mchango wao katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia. Maadhimisho ya kumbukumbu hii kwa mwaka 2022 yanakwenda sanjari na Hija ya 37 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Canada kuanzia tarehe 24-30 Julai 2022. Hija hii inanogeshwa na kauli mbiu “Walking Together” yaani “Kutembea Pamoja.” Lengo ni kukoleza mchakato wa upatanisho wa Kitaifa unaosimikwa katika msingi wa toba na wongofu wa ndani; ukweli na uwazi kwa ajili ya kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za watu asilia wa Canada. Ni katika muktadha huu, Waziri mkuu wa Canada Bwana Justin Trudeau katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko na amegusia kuhusu umuhimu wa familia, jitihada za wazazi kuwapatia watoto wao malezi, makuzi na elimu bora. Wazazi wanayo dhamana ya kuwapatia furaha, kuwafariji na kutembea nao katika safari ya maisha yao ya kawaida. Watoto hawa wanapong’olewa kwenye msingi wa familia, wanakumbana na mateso makali, kiasi hata cha kupoteza: lugha, tamaduni na utambulisho wao. Matokeo yake ni kutumbukia katika upweke hasi kwa kukosa faraja kutoka katika familia na jumuiya zao.
Waziri mkuu wa Canada Bwana Justin Trudeau anasema, Kanisa Katoliki kama Taasisi imeshiriki katika nyanyaso za maisha ya kiroho, kitamaduni, kihisia, kimwili na hata nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto hawa waliokuwa wamepewa nafasi ya masomo katika shule za makazi ya watu asilia wa Canada, ambao kwa sasa wanalitaka Kanisa kuomba msamaha kwa kuwatenda kinyume cha haki msingi za binadamu na utu wema. Ujasiri ulioneshwa na Baba Mtakatifu Francisko kule Maskwacis (Masikwa cheese) ni matunda ya ujasiri na udumifu uliowawezesha wahanga wa nyanyaso hizi, kushirikisha mateso na mahangaiko yao ya ndani. Baba Mtakatifu Francisko kwa uchungu na huzuni iliyotanda kwenye sakafu ya moyo wake, tangu mwanzo amewasilikiliza na sasa ameomba msamaha kwa makossa yaliyotendwa na watoto wa Kanisa. Msamaha ni mwanzo wa mchakato wa toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa ambao umeacha mwangwi mkubwa katika akili na nyoyo za watu wa Mungu nchini Canada. Ni wakati wa kutembea pamoja, ili kupyaisha matumaini ya watu asilia wa Canada, sehemu muhimu sana ya mchakato wa uponyaji na mshikamano wa Kitaifa. Kwa hakika, Baba Mtakatifu ameonesha ukomavu na ushujaa wa pekee kwa kuomba msamaha. Watu asilia wa Canada bado wanaendeleza mapambano ili kulinda na kudumisha utamaduni na lugha yao. Mchakato wa upatanisho ni wajibu na dhamana ya watu wote wa Mungu nchini Canada. Hii ni safari endelevu inayotekelezwa na kila mtu kadiri ya nafasi na uwezo wake. Serikali ya Canada pamoja na Taasisi zake, zitaendelea kushikamana na watu asilia wa Canada, ili maendeleo na ustawi wa wote uweze kufikiwa.
Kwa upande wake, Mheshimiwa Mary Simon, Gavana Mkuu wa Canada amewashukuru na kuwapongeza watu asilia wa Canada. Amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kufanya hija ya toba, wongofu wa ndani na upatanisho wa Kitaifa kama njia ya mchakato wa upatanisho, uponyaji, matumaini na upyaisho wa maisha ya watu wa Mungu. Watu asilia wa Canada wamejeruhiwa sana kutoka katika undani wa maisha yao. Walijitahidi kusimama kidete kuwalinda na kuwatunza watoto wao, lakini wakazidiwa nguvu, lakini kwa sasa ni wajasiri na wana nguvu ya kuweza kujikita tena katika safari ya uponyaji, mchakato utakaoendelea kuliimarisha Taifa la Canada. Mheshimiwa Mary Simon, Gavana Mkuu wa Canada, anakaza kusema Serikali itaendelea kuboresha huduma msingi kwa watu asilia nchini Canada. Majadiliano katika ukweli na uwazi ni msingi wa upatanisho wa Kitaifa na kwamba, huu ni wajibu wa kiimani na kimaadili. Uponyaji ni mchakato unaochukua muda mrefu, unaotekelezwa taratibu na kusonga mbele, ili kupyaisha akili, nyoyo na maisha ya watu. Uponyaji unafumbatwa katika maisha ya kijumuiya, wema na upendo, kwa kuthamini lugha, tamaduni na utambulisho wa watu mahalia. Historia, tamaduni na lugha ya watu asilia wa Canada ni tunu inayopaswa kurithishwa na kuendelezwa, ili kuganga na kuponya madonda ya kihistoria. Serikali ya Canada, itaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Vatican katika mchakato wa upatanisho, haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi kwa kujizatiti katika mapambano dhidi ya ujinga, umaskini na maradhi, ili hatimaye, kuwajengea watu hali na tabia ya kuaminiana. Watu wa Mungu nchini Canada wamesikiliza na kuitikia wito wa toba, wongofu wa ndani na uponyaji wa Kitaifa.