Siku ya Kimataifa ya Mzee Nelson Mandela 18 Julai 2022: Haki, Amani na Utu Duniani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela yalianzishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2009 na kuadhimishwa kwa mara ya kwanza tarehe 18 Julai 2010 kama njia ya kumuenzi Mzee Nelson Mandela aliyejisadaka kwa ajili ya kupigania uhuru, utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili kukoleza na kudumisha demokrasia ya kweli inayowaambata wananchi wote wa Afrika ya Kusini. Ni kiongozi aliyesimama kidete, kupambana na utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini, vitendo ambavyo vilidhalilisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa mfano na sura ya Mwenyezi Mungu kwa muda wa miaka 67. Ndiyo maana kama sehemu ya kumbukumbu ya mchango wake, watu wanahimizwa kutekeleza walau mambo mbali mbali kwa muda wa dakika 67 ili kusaidia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Mzee Nelson Mandela anasema, mashujaa ni wale wanaojisadaka kwa ajili ya mchakato wa ujenzi wa udumifu wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela kwa mwaka 2022 yanakwenda sanjari na kumbukumbu ya miaka 104 tangu Mzee Madiba alipozaliwa. Ni kiongozi anayeheshimika sana duniani kutokana na moyo wake wa kusamehe na kusahau, ili kuandika ukurasa wa udugu wa kibinadamu na mshikamano wa kitaifa; kwa kuthamini, haki msingi msingi, utu na heshima ya binadamu wote pasi na ubaguzi wa aina yoyote ile.
Umoja, mshikamano na mafungamano ya kitaifa ni kati ya vipaumbele vya Mzee Madiba. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana António Guterres katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela kwa Mwaka 2022, anasema kwamba, huyu ni kiongozi aliyeheshimika sana; alionesha ujasiri usiokuwa na kifani, akawa ni chemchemi ya mafanikio makubwa; mtu aliye onesha hadhi ya utulivu, utu na ubinadamu wa kina. Mzee Nelson Mandela alikuwa ni chombo cha uponyaji wa kijamii na mshauri wa vizazi, dira ya maadili na utu wema kwa Jumuiya ya Kimataifa. Mzee Madiba ni kiongozi aliyethubutu kutembea katika njia ya uhuru na utu, akiwa na maamuzi thabiti, akatangaza na kushuhudia huruma na upendo na kwamba, kila mtu anayo nafasi ya kuweza kujenga maisha bora kwa leo na kwa siku za usoni. Mzee Nelson Mandela ni mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa kukabiliana na changamoto mamboleo kama vile vita ambayo imeugubika ulimwengu; mifumo mbalimbali ya ubaguzi, baa la umaskini, ukosefu wa haki na usawa pamoja na athari za mabadiliko makubwa ya tabianchi. Mzee Nelson Mandela awe ni chemchemi ya matumaini na msukumo mpya unaobubujika kutoka katika maono yake.
Jumuiya ya Kimataifa, isimame kidete kuchukua hatua za kuondokana na chuki na hivyo kusimama imara kulinda na kutetea haki msingi za binadamu. Watu wawe ni mashuhuda na vyombo vya huruma kwa jirani zao, ili dunia iweze kusimikwa katika katika misingi ya haki, huruma, mafanikio na maendeleo fungamani ya binadamu kwa watu wote. Itakumbukwa kwamba, Mzee Nelson Mandela alizaliwa tarehe 18 Julai 1918. Aliwahi kufungwa kizuizini kwa muda wa miaka 27 na Utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini. Baba Mtakatifu Frsancisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii kunako mwaka 2017 alisema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuvuka mifumo yote ya ubaguzi, hali zote za kutovumiliana pamoja na udhalilishaji wa utu na heshima ya binadamu! Mfano wa Mzee Nelson Mandela usaidie kuleta ari na mwamko mpya kwa vijana wa kizazi kipya nchini Afrika ya Kusini, ili waweze kujikita zaidi katika kukuza na kudumisha, misingi ya haki, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kama sera na mikakati yao ya kisiasa.