Tafuta

2022.07.12 WAWAKILISHI WA AMECEA WAMEKUTANA NA RAIS WA TANZANIA 2022.07.12 WAWAKILISHI WA AMECEA WAMEKUTANA NA RAIS WA TANZANIA 

Tanzania,Rais Samia Suluhu:Leteni maoni yenu juu ya utunzaji wa mazingira

Washiriki wa Mkutano wa 20 wa AMECEA ,wamekutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mama Samia.Baada ya salamu za makaribisho,Rais amewataka Viongozi wa dini na kisiasa pamoja na waamini kuhakikisha wanadumisha amani na kutunza mazingira kila sehemu.Amemshukuru Papa Francisko kwa wito wa utunzaji wa Mazingira.Na jioni mlo na washiriki wote.

Na Angella Rwezaula – Dar Es Salaam

Katika mkutano unaonendelea wa  20 wa shirikisho la mabaraza ya maaskofu wa Afrika Mashariki (AMECEA) na washiriki wengine kutoka sehemu mbali mbali kwenye ukumbi wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Jumanne 12 Julai 2022 wamekutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan. Katika  hotuba hiyo amesema kuwa uwepo wa amani nchini unasaidia kutunza ikolojia na uharibifu wa mazingiza kama ukataji miti huathiri hali ya hewa duniani ikiwemo kina cha bahari hivyo ni wajibu wa kila mtu  kulinda mazingira ili kutohatarisha maendeleo kwa ujumla.  

Rais Samia wa Tanzania akiwa mgeni katika Mkutano wa 20 wa AMECEA
Rais Samia wa Tanzania akiwa mgeni katika Mkutano wa 20 wa AMECEA

Rais Samia pia amesema hatuna budi kutunza vyanzo vya maji na misitu, kupanda miti na kuhakikisha mazingira ya maeneo yanayotuzunguka yanasafishwa katika miji yote kama inavyoelekezwa kwenye Sera ya Taifa ya Mazingira. Kwa upande mwingine, Rais Samia amesema Serikali ya Tanzania inafuata siasa ya maendeleo jumuishi hivyo ipo tayari kuzipokea na kufanya kazi na taasisi zisizo za kiserikali zikiwemo za kidini na kijamii ili kufikia mustakabali mwema wa maisha na maendeleo ya mwanadamu.

Askofu Kasonde, Rais wa AMECEA akimkaribisha Rais Samia kwenye Mkutano wa AMECEA
Askofu Kasonde, Rais wa AMECEA akimkaribisha Rais Samia kwenye Mkutano wa AMECEA

“Mimi niwashukuru sana kwa kufikiria na mkifika hapa mnakwenda kuendeleza kwa vitendo malengo ya dunia lakini malengo yetu Umoja wa Afrika. Kwahiyo hongereni sana Makardinali na Viongozi wote wa Dini”.

Aidha rais ametiwa moyo sana kuona hata Baba Mtakatifu Francisko ameona inafaa suala la utunzaji wa mazingira. Kwa maana hiyo ameomba uwe sehemu ya ujumbe na mpango mkakati wao na uaote msukumo zaidi kama alivyoeleza Baba Mtakatifu Francisko kwamba, “Dunia ndiyo nyumba yetu sote pamoja. Hakika sisi hapa Tanzania tunathamini maisha ya kijamii yanayoendana na mkakati huo wa Kanisa Katoliki, kwamba sasa tuijenge nyumba yetu sote.”

Askofu Kasonde, Rais wa AMECEA akimkaribisha Rais Samia kwenye Mkutano wa AMECEA
Askofu Kasonde, Rais wa AMECEA akimkaribisha Rais Samia kwenye Mkutano wa AMECEA

Kwa maana hiyo rais Samia ametoa wito kwa Viongozi wa kidini kuendeleza kutekeleza kwa vitendo Malengo Endelevu 17 ya Dunia na Malengo ya Umoja wa Afrika (AU) ikiwemo utunzaji wa mazingira. Na hata hivyo amesema “Niwaombe, serikali yenu ni sikivu, ni serikali inayopokea. Leteni maoni yenu kwenye utunzaji wa mazingira, tukae kwenye vikao. Leo mmekaa wenyewe kuhusu suala la mazingira, tungependa kupata maazimio yenu tukaona tunayameza vipi kwenye sera zetu na Mh. Waziri yupo hapa. Halafu sote tukaenda kutekeleza ili kulinda hazina yetu, tunu yetu, nyumba yetu ambayo Mungu ametuumbia”, alisisitiza rais

Chakula cha usiku

Maaskofu wote na washiriki wa Mkutano 20 wa Shirikisho la AMECEA hata hivyo wamekaribishwa mlo wa jioni huko Ikulu. Mlo uliudhuriwa vile vile na viongozi wa kisiasa na wazee wa baraza. Baada ya makaribisho, sala kabla ya chakula iliongozwa na Askofu Flavian Kasala, ambaye ni  Makamu Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC). Hitimisho la mlo lilikuwa ni kubadilishana zawadi ambapo kati ya zawadi kulikuwa na utambuzi wa makardinali wa AMECEA, Maaskofu wakuu, na wengine kwa ujumla. Rais Samia amerudia kusisitizia ujumbe wake wa kupeleka maoni yao kuhusu utunzaji wa mazingira ili kwa pamoja waweze kujadiliana na kupata suluhisho.

12 July 2022, 22:09