Nembo ya AMECEA iwe ishara na njia ya kuishi Laudato Sì
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Nembo iliyobeba Kauli mbiu ya Mkutano Mkuu wa 20 wa Shirikisho la Mabaraza la Maaskofu (AMECEA) ilikuwa ni wito wa kiishara wa kuchukua hatua na kama kielelezo wazi cha mazingira bora ambayo ulimwengu unatazamia. Katika Mkutano Mkuu wa 20 wa AMECEA ulileta pamoja hata wanaharakati na wasimamizi wa mazingira kutoka nchi wanachama wa AMECEA na nchi mbili shirikishi ili kujadili suluhisho la kudumu kwa ajili ya athari mbaya za uharibifu wa mazingira ambao unaendelea kutishia uwepo wa wanadamu duniani.
Dk. Camillus Kassala, Mkuu wa Idara ya Haki, Amani na Uadilifu wa Uumbaji (JPIC) wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), alitoa ufafanuzi wa kina wakati wa siku ya kwanza ya Mkutano huo kuhusu kuelezea Nembo iliyotumika kufafanua kauli mbiu katika mkutano huo. Dk. Kasala alisema tunapaswa kujiuliza hasa watawa, makuhani na waamini ni kitu gani cha kufanya ili kujibu ujumbe wa Baba Yetu Laudato Si. Baadaye alianza kuonesha vipengele katika nembo, kwamba katika kuhukumu, tunatafuta ishara katika jamii na kutambua kama wanatumikia utume wa Ufalme wa Mungu huku akisisitiza haja ya kuheshimu na kulinda kazi ya uumbaji wa Mungu.
Akimnukuu mtakatifu Papa Paulo VI wakati wa ziara yake ya kutembelea Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) katika kumbukumbu ya miaka 25 ya taasisi hiyo (Jumatatu tarehe 16 Novemba 1970), Dk. Kasala alisistiza umuhimu wa kupunguza changamoto za mazingira na kuokoa nyumba yetu ya pamoja. Kuendelea kuzorota kwa mazingira kunahatarisha kusababisha janga la kiikolojia, uchafuzi wa hewa tunayovuta, maji tunayokunywa hadi kutia hofu ya kifo cha kweli cha kibaolojia katika siku zijazo ikiwa hatua za nguvu hazitachukuliwa mara moja na kwa ujasiri na kutekelezwa kwa uthabiti.
Nembo na maana ya alama zake
Ufafanuzi wa Nembo, alama na vipengele vinavyowakilisha umuhimu wa mazingira, jinsi vitendo vya kibinadamu na kutotenda kunavyoendelea kuharibu na kubadilisha usawa wa ikolojia, na matokeo yanayotarajiwa ambayo yanaweza kupatikana tu kupitia taswira ya busara, uamuzi sahihi, na kupia hatua. Katika suala lililoelekezwa kwa viongozi wa kidini wa Afrika Mashariki, Dk. Kassala aliwaomba viongozi hao kuelewa vema waraka wa Papa Francisko kuhusu mazingira, maadili na imani ya Kikristo ili kukabiliana na madhara ya uchafuzi wa mazingira na kuzorota kwa mazingira na kufikia ikolojia muhimu kwa riziki ya pamoja ya viumbe vyote vya Mungu. Dk. Kassala aliuliza swali kwamba kama wachungaji wa Kanisa la Afrika Mashariki, wanawezaje kutafsiri uelewa wao wa ujumbe wa Laudato Si katika jibu zuri la kichungaji kwa athari mbaya za asili katika maendeleo shirikishi ya binadamu katika mazingira ya Afrika Mashariki?
Ikumbukwe:Mkutano Mkuu wa AMECEA kwa kawaida hufanyika kila baada ya miaka minne. Kwa maana hiyo viongozi hao walihitimisha kwa kuchagua mada na nchi mwenyeji kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa 21 ujao utakaofanyika mnamo 2026 jijini Kampala Uganda.