Tafuta

Siku ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere 1922-2022. Miaka 100 tangu alipozaliwa. Miaka 23 tangu alipofariki dunia akiwa na umri wa miaka 77. Siku ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere 1922-2022. Miaka 100 tangu alipozaliwa. Miaka 23 tangu alipofariki dunia akiwa na umri wa miaka 77. 

Kilele cha Siku ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Tanzania 2022

Samia Suluhu Hassan amewataka watanzania kuendelea kuchukua tahadhari juu ya tishio la ugonjwa wa Ebola. Rais Samia amesema hayo Oktoba,14,2022 mjini Bukoba mkoani Kagera katika maadhimisho ya kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa yaliyokwenda sanjari na kumbukizi ya miaka 23 tangu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipofariki dunia London.

Na Faustine Gimu, Bukoba, Kagera, Tanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka watanzania kuendelea kuchukua tahadhari juu ya tishio la ugonjwa wa Ebola. Rais Samia amesema hayo Oktoba,14,2022 mjini Bukoba mkoani Kagera katika maadhimisho ya kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa yaliyokwenda sanjari na kumbukizi ya miaka 23 ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. “Tumekumbana na changamoto za maradhi mbalimbali ikiwemo Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 tumepita, sasa kuna Ebola japo haijatufikia hivyo watanzania tuendelee kuchukua tahadhari dhidi ya Ebola” amesema Rais Samia. Pia, Rais Samia amesema suala la afya ya binadamu linakwenda na lishe bora hivyo ametumia fursa hiyo kuipongeza Wizara ya Afya kwa kuendelea kutoa elimu ya lishe kwa jamii huku akisema kuna haja ya kuongeza jitihada za mapambano dhidi ya malaria na kupunguza vifo vya mama na mtoto. “Kiwango cha maambukizi ya Malaria kimepungua kwa 14.8% mwaka 2015 hadi kufikia 7.3% mwaka 2017, hata hivyo ugonjwa huu bado ni changamoto kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano na akina mama wajawazito maambukizi bado ni makubwa kwa baadhi ya mikoa na yanaanzia 12% hadi 24%” amesema.

Kumbukizi la Miaka 23 tangu Mwl. JK. Nyerere alipofariki dunia
Kumbukizi la Miaka 23 tangu Mwl. JK. Nyerere alipofariki dunia

Rais Samia ameendelea kufafanua kwamba kwa mujibu wa chapicho la “Tanzania Nutritional Survey” la mwaka 2019, udumavu kwa watoto wenye chini ya umri wa miaka 5 ulikuwa 31.8%, uzito pungufu 15% ya watoto wote walio chini ya umri wa miaka 5 na ukondefu ni 3.5% na hali ya lishe kwa wanawake wajawazito walio kwenye wakati wa kujifungua bado inaonesha upungufu wa damu kwa 28% na hali ya utapiamlo uliokithiri unaendelea kuongezeka kufikia 31.8%. “Nafurahi kueleza kwamba juhudi zinazofanywa na serikali kwenye suala la lishe ikiwemo kutoa elimu kuhusu masuala ya lishe, kutenga mafungu maalum kwa halmashauri, kuongeza virutubishi kwenye chakula na kuwapa dhamana wakuu wa mikoa kusimamia masula ya lishe kwenye maeneo yao kumeboresha hali ya lishe ingawa jitihada zaidi zinahitajika” amesema. Kuhusu maambukizi ya virusi vya UKIMWI[VVU]na UKIMWI Rais Samia amesema bado ni makubwa ambapo hupoteza nguvu kazi ya taifa hasa vijana. “Takwimu za Afya zinasema hadi kufikia mwaka 2021 asilimia 88% ya Waviu walikuwa wanajitambua hali zao, huku 89% wakiwa kwenye tiba na 98% wakiwa wamefikia baadhi” amefafanua Rais Samia. Katika suala la mapambano dhidi ya dawa za kulevya Rais Samia amesema vijana ni nguvu kazi hivyo ni muhimu kuweka nguvu za pamoja kuendelea kutoa elimu kwani serikali hugharimu fedha nyingi kutibu waathirika wa dawa za kulevya.

Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru tarehe 14 Oktoba 2022
Kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru tarehe 14 Oktoba 2022

Wakati huo huo, Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema kuna haja ya kuweka mkakati wa kukagua miradi ya mazingira kila wilaya ili kuweza kukabiliana na mabadiliko ya nchi hali ambayo husababisha uhaba wa mvua. Waziri Mkuu wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema sherehe hizo zimehusisha sehemu mbili za muungano ambapo kuna vijana halaiki 200 kutoka Zanzibar huku akibainisha kuwa changamoto ya miradi kutekelezwa kwa kiwango cha chini baadhi ya maeneo zitafanyiwa kazi chini ya Ofisi ya Rais –TAMISEMI. Kwa upande wake waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu [Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu] Prof. Joyce Ndalichako amesema Mwenge wa Uhuru ulikimbizwa kwa siku 190 katika mikoa mbalimbali huku ukiwa na program mbalimbali za kuelimisha jamii ikiwemo umuhimu wa kujikinga na malaria, uhamasishaji wa chanjo, uchangiaji wa damu salama katika mchakato wa kuokoa maisha ya watu wengine.

Miaka 100 tangu alipozaliwa Baba wa Taifa Mwalimu JK. Nyerere: 1922-2022
Miaka 100 tangu alipozaliwa Baba wa Taifa Mwalimu JK. Nyerere: 1922-2022

Akisoma ripoti ya majumuisho Mbio za Mwenge wa Uhuru 2022, kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2022 Sahil Geraruma amesema Mbio za Mwenge wa Uhuru zimeweza kufungua miradi mbalimbali ikiwemo majengo ya wagonjwa wa nje [OPD]vituo vya afya na zahanati ambapo imerahisisha kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania. Aidha, kiongozi huyo wa mbio za mwenge wa uhuru ameendelea kufafanua kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru 2022 kwa kushirikiana na Wizara ya Afya zimekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza, kuzuia vifo vya mama na mtoto kwa kupambana na Malaria, kupambana na UKIMWI. Hata hivyo amesema mbio za mwenge wa uhuru 2022 zimebaini kuwa katika sekta ya afya, baadhi ya wataalam wa afya wamepewa majukumu mazito na yasiyokuwa ya kwao kama vile kusimamia kazi za uhandisi na ukandarasi, uhasibu katika utekelezaji wa miradi ya afya. Pia, Geraruma amesema Mbio za Mwenge 2022 zilibaini changamoto ya kutotekelezwa kwa kiwango baadhi ya miradi ya maendeleo pamoja na matumizi ya fedha kutokwenda na uhalisia na miradi hiyo. Ikumbukwe kuwa mbio za Mwenge wa Uhuru 2022 zimezindua miradi ya maendeleo 1293 yenye zaidi ya Tsh. bililioni 900 ambapo kwa mwaka 2023 Mwenge wa Uhuru utazinduliwa Mtwara na kuzimwa mkoani Manyara.

 

 

15 October 2022, 15:38