COP27: Madhara ya Mabadiliko ya Tabianchi Duniani: Umaskini na Magonjwa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) uliofunguliwa huko Sharm El-Sheikh nchini Misri 6 Novemba 2022, umeonesha kusuasua kwa jitahada za Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi, hasa kutokana na kiwango cha joto duniani, kupanda kwa kasi kubwa na hivyo kutishia ongezeko la kina cha bahari duniani. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kuyeyuka kwa barafu, mawimbi ya joto kali pamoja na viashiria vingine vya athari za mabadiliko ya tabianchi ni mambo yanayopaswa kuvaliwa njuga na hivyo kupatiwa ufumbuzi wa kudumu. Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF limesema kiasi cha dola za kimarekani bilioni 2,400 zinahitajika kila mwaka ili kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kuwasaidia watu zaidi ya bilioni nne wanaoishi katika hatari ya kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi. Kuna watoto zaidi ya milioni 27 wameathirika kutoka na mafuriko makubwa yaliyojitokeza sehemu mbalimbali za dunia. Watu wengi wamepoteza maisha na mali zao; wamekosa maji safi na salama kwa ajili ya mahitaji na matumizi ya kibinadamu; watoto wengi wameshindwa kuhudhuria masomo.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF linaitaka Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe kuhakikisha kwamba, linatunga na kutekeleza sera na sheria zitakazojikita zaidi katika kuzuia; kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote; kuwaandaa watoto na vijana wa kizazi kipya kwa kuwajengea uwezo wa kupambana kikamilifu na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kimsingi, watu wote wanahamasishwa kuwa ni wadau muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Fedha za fidia kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchini kutokana na ongezeko la kiwango kikubwa cha uyeyukaji wa barafu kutoka kwenye Milima mirefu, ukiwamo Mlima Kilimanjaro, ulioko nchini Tanzania zinahitajika sana.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani, WMO, limesema usambazaji wa umeme kutoka vyanzo vya nishati safi lazima uongezeke mara mbili ndani ya miaka minane ijayo ili kupunguza ongezeko la joto duniani na iwapo hilo halitafanyika, kuna hatari kwamba mabadiliko ya tabianchi, kuongezeka kwa hali mbaya zaidi ya hewa pamoja na shida ya maji vitadhoofisha uhakika wa upatikanaji wa nishati na hata kuhatarisha usambazaji wa nishati mbadala. Lengo la kupunguza ongezeko la kiwango cha joto hadi nyuzi 1.5 za Celsius inazidi kuwa ngumu kufikiwa na matokeo yake ni ongezeko kubwa la majanga asilia. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterress, anasema COP27 ni mahali muafaka pa kufanya maamuzi magumu ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kusababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao kama inavyojionesha wakati huu nchini Pakistani, Nigeria na katika Ukanda wa Visiwa vya Carribbean.