Siku ya kukomesha utumwa kimataifa,Guterres:Nchi zote pyaisheni dhamira ya kutokomeza utumwa
Na Angella Rwezaula; - Vatican.
Kila tarehe 2 Desemba ya kila mwaka ni kumbu kumbu ya Siku ya Kukomesha Biashara ya Utumwa Duniani, ambapo mnamo mwaka 1949, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Mkataba wa Kukomesha aibu hii dhidi ya ubinadamu. Katika fursa ya kukumbuka siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, (UN), Bwana Antonio Guterres ametoa ujumbe wake akisema kwamba: “Tunapoadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Utumwa, ni lazima tutambue kwamba urithi wa biashara ya kupita Atlantiki kwa Waafrika waliokuwa watumwa bado unavuma hadi leo hii na kuacha kovu kwa jamii zetu na kukwamisha maendeleo ya usawa”.
Aina nyingi za utumwa:tangu biashara haramu ya binadamu hadi matumizi ya silaha
Kwa maana hiyo, Bwana Guterres amebainisha kwamba:“Ni lazima pia tutambue na kutokomeza aina za utumwa mambo leo kama vile biashara haramu ya binadamu, unyonyaji wa kingono, ajira ya watoto, ndoa za kulazimishwa na matumizi ya watoto katika migogoro ya silaha. Makadirio ya hivi karibuni kutoka Makadirio ya Ulimwengu wa Utumwa mamboleo juu ya kazi ya kulazimishwa na ndoa za kulazimishwa yanaonesha kwamba, mnamo 2021, watu wapatao milioni 50 walifanywa kuwa watumwa, na idadi hii inaongezeka.
Kuna makundi mengi yanatengwa, wahamiaji, makabila ya wachache
Katika ujumbe wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) aidha unabainisha kwamba: “Makundi yaliyotengwa zaidi kwa namna ya pekee yanasalia katika hatari zaidi, yakijumuisha makabila ya watu wachache, watawa na makabila madogo madogo, wahamiaji, watoto na watu wa mielekeo tofauti ya kijinsia na utambulisho wa kijinsia. Wengi wa watu hawa walio katika mazingira magumu ni wanawake”. Kwa kuongeza amesema kwamba katika Siku hii ya Kimataifa, anatoa wito kwa serikali na jamii kupyaisha dhamira yao ya kutokomeza utumwa. "Hatua kali zaidi zinapaswa kuchukuliwa kwa ushirikishwaji kamili wa wahusika wakuu wote, ikiwa ni pamoja na sekta binafsi, vyama vya wafanyakazi, mashirika ya kiraia na taasisi za haki za binadamu. Pia ametoa wito kwa nchi zote kulinda na kudumisha haki za waathirika na wahanga wa utumwa."