Wahamiaji na wakimbizi ni hali ngumu. Wahamiaji na wakimbizi ni hali ngumu. 

UNHCR:Watu milioni 100 wametawanywa kwa 2022,rekodi isiyosahaulika

Watu milioni 100 wamelazimishwa kuondoka makwao kwa mwaka wa 2022 na Umoja wa Mataifa uliendelea kusaidia wale wanaohitaji msaada kwa njia nyingi na kuhamasisha njia zaidi za kisheria na salama za watu kuhama.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Idadi hiyo ya watu milioni 100, ikiwa ni pamoja na wale wanaokimbia migogoro, ghasia, ukiukaji wa haki za binadamu na mateso, ilikuwa imetangazwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, mnamo  mwezi Mei na kuelezwa  tena na Bwana Filippo Grandi, Mkuu wa shirika hilo, kwamba ni kama  rekodi ambayo haipaswi kamwe kusahulika. Na idadi hiyo imeongezeka kutoka watu milioni 90 mwaka wa 2021. Kuzuka kwa machafuko, au migogoro ya muda mrefu, imekuwa sababu kuu ya uhamaji katika sehemu nyingi za dunia, ikiwemo Ukraine, Ethiopia, Burkina Faso, Siria, na Myanmar. Tathimini hiyo ya Shirika la Umoja wa mataifa la wahamaji UNHCR linasema maelfu ya wahamiaji waliokata tamaa walitazama Ulaya kama eneo linalopendelewa, wakiweka maisha yao mikononi mwa wasafirishaji haramu wa kibinadamu, na kuanza safari za hatari kuvuka bahari ya Mediterania na mara nyingi sana safari hizi ziliishia kwenye mikasa ya kuzama.

Kwa mujibu wa UNHCR sasa imepita zaidi ya miaka saba tangu mzozo wa muda mrefu uanze nchini Yemen, kati ya muungano unaoongozwa na Saudia unaounga mkono Serikali na waasi wa Houthi, pamoja na washirika wao.   Mzozo huo umesababisha janga la kibinadamu, na limewalazimu zaidi ya watu milioni 4.3 kufungasha virago na kukimbia makwao.  Mwezi Mei, shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM na tawi la Muungano wa Ulaya la misaada ya kibinadamu (ECHO), walitangaza kwamba wanaongeza juhudi za kukabiliana na mahitaji ya zaidi ya watu 325,000 waliokimbia makazi yao kutokana na mzozo huo, wakiwemo wahamiaji na jumii zinazowahifadhi.  Naye mkuu wa operesheni za IOM nchini humo Christa Rottensteiner, alibainisha kuwa "Hali pia inazidi kuwa mbaya kwa wahamiaji nchini Yemen, hasa wanawake, ambao wanaishi katika hali mbaya Yemen na udhibiti mdogo wa maisha yao.

Licha ya hali mbaya ya Yemen, nchi hiyo imesalia kuwa kimbilio na kivuko cha wahamiaji wanaoondoka katika nchi za Pembe ya Afrika limesema shirika la UNHCR. Pia limeongeza kuwa watu hao waanapowasili, wanaeleza wasafiri hukabiliana na safari hatari, huku wengi wakielekea kaskazini, na wengine wakielekea katika nchi za Ghuba kutafuta kazi. Watu hawa mara nyingi wanalazimika kuvuka mstari wa mbele, wakiwa katika hatari ya kukumbwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, kama vile kuwekwa kizuizini, hali zisizo za kibinadamu, unyanyasaji, na kuhamishwa kwa kulazimishwa. Nchini Siria, UNHCR inasema vita sasa vimekuwa vikisumbua maisha ya watu kwa miaka 11, karibu watoto milioni tano waliozaliwa nchini Syria hawajawahi kujua au kushuhudia nchi hiyo ikiwa na amani. Zaidi ya Wasiria 80,000 wanaita kambi kubwa ya wakimbizi ya Za'atari, huko Jordan nyumbani na inavyoonekana wengi wao wanaweza kubaki nje ya nchi yao kwa siku zijazo. Dominik Bartsch, mwakilishi wa UNHCR katika mji mkuu wa Jordan Amman, mwezi Julai mwaka huu alisema. "Matarajio ya kurudi kwa sasa hayaonekani kuwa ya matumaini. Hatuoni mazingira nchini Siria ambayo yangefaa kwa watu kurejea nyumbani.  Kwa ujumla, Jordan inawahifadhi wakimbizi 675,000 waliosajiliwa kutoka Siria, na wengi wao wanaishi katika miji na vijiji vyake miongoni mwa jamii za wenyeji,  ni asilimia 17 pekee wanaishi katika kambi mbili kuu za wakimbizi, Za'atari na Azraq.

Warohingya wanaendelea kuikimbia Myanmar

Zaidi ya miaka mitano iliyopita, mamia ya maelfu ya Warohingya walikimbia makazi yao nchini Myanmar, baada ya kampeni ya kijeshi ya mateso.   Takriban Warohingya milioni moja wanaishi katika kambi kubwa ya wakimbizi ya Cox's Bazar iliyoko katika nchi jirani ya Bangladesh.  Mwezi Machi, Umoja wa Mataifa ulizindua mpango wake wa hivi karibuni wa kuchukua hatua kusaidia, ukitoa ombo la zaidi ya dola milioni 881 kwa ajili ya wakimbizi, na jumii za jirani zinazowahifadhi ambao ni watu zaidi ya nusu milioni raia wa Bangladeshi, ambao pia wanategemea sana misaada. Mwaka huu, Warohingya waliendelea kuondoka Myanmar, wengi wakijaribu kuvuka bahari ya Andaman, moja ya vivuko hatari zaidi vya maji duniani.  Wakati zaidi ya wahamiaji zaidi ya 12 wakiwemo watoto, waliripotiwa kufa baharini katika pwani ya Myanmar mwezi Mei, Indrika Ratwatte, mkurugenzi wa UNHCR kwa kanda ya Asia na Pasifiki, alisema “mkasa huo unaonyesha hali ya kukata tamaa inayohisiwa na Warohingya ambao bado wako nchini Myanmar.”

Miezi 10 baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, ambao ulianza tarehe 24 Februari, na inaonekana uwezekano wa kuendelea hadi 2023, takwimu za shirika la UNHCR zinaonyesha kuwa, kufikia Desemba, zaidi ya wakimbizi milioni 7.8 wa Ukraine walikuwa wamerekodiwa kote barani Ulaya.  Mara tu baada ya mzozo kuanza, mashirika ya Umoja wa Mataifa yalihamasishwa kutoa msaada.  UNHCR iliratibu mhatua za msaada kwa wakimbizi pamoja na mashirika dada ya Umoja wa Mataifa na washirika wengine, katika kuunga mkono mamlaka za kitaifa za Ukraine. Kwa mfano, katika nchi jirani ya Poland, wafanyakazi waliunga mkono mamlaka kusajili wakimbizi na kuwapa makao na usaidizi.

Bwana Filippo Grandi alizipongeza nchi za Ulaya kwa nia yao ya kuchukua raia wa Ukraine, ambao wengi wao walitafuta makazi katika nchi jirani, lakini alionyesha huzuni yake kwa nchi hiyo na raia wake.  Kwa hiyo “Familia zimesambaratika bila sababu. Cha kusikitisha ni kwamba vita isiposimamishwa, ndivyo itakavyokuwa kwa wengi zaidi,” alisema Grandi. Na kwa kuongezea alisema “lakini, ukarimu huu wa roho nzuri haukuonekana kila wakati, ilipokuja kwa baadhi ya watu wa jamii za walio wachache. “ Mwezi Machi, Bwana. Grandi alizungumzia ubaguzi, ubaguzi wa rangi na unyanyasaji wanaokabiliana nao.

Akizungumza katika siku ya Kimataifa ya kutokomeza Ubaguzi wa rangi Grandi alisema kuwa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa lina ushahidi "kwa ukweli mbaya, kwamba baadhi ya watu weusi na wa kahawia wanaokimbia Ukraine na vita vingine na migogoro mingine duniani kote hawajapata ukarimu au kutendewa  sawa na wakimbizi wa Ukraine”.  Wasiwasi wa Bwana Grandi ulisisitizwa, mwezi Julai, na González Morales, mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu za wahamiaji. Ambaye alidai kuwa “kulikuwa na hali mbili za jinsi wakimbizi wanavyotendewa nchini Poland na Belarus, hasa inapokuja kwa watu wenye asili ya Kiafrika, na watu wengine wa rangi na makabila madogo.”

Hali mbaya kwenye makambi Ethiopia

Nchini Ethiopia, mamilioni ya watu wamesalia bila makazi kutokana na mzozo wa kivita katika eneo la Tigray, ulioanza tarehe 3 Novemba 2020 kati ya vikosi vya taifa vya Ethiopia, wanajeshi wa Eritrea, wanajeshi wa Amhara na wanamgambo wengine wa upande mmoja, na vikosi vinavyotii ukombozi wa watu wa Tigray kwa upande mwingine.  Mwishoni mwa mwaka huu, makubaliano dhaifu ya kimataifa yalionekana kushikilia kwa msaada kurejea katika maeneo ya kaskazini yenye matatizo ambayo hayakuweza kufikiwa kwa miezi kadhaa, pamoja na watu wengi kurejea nyumbani kujenga upya maisha yao yaliyosambaratika.  Mwezi Januari, shirika la UNHCR lilitoa onyo kali kwamba, kutokana na hali mbaya, wakimbizi katika eneo hilo walikuwa wakihangaika kupata chakula cha kutosha, dawa, na maji safi, na kuhatarisha kifo endapo hali haitaimarika.

"Hali ya kukata tamaa katika kambi hizi ni mfano tosha wa athari za ukosefu wa ufikiaji na vifaa vinavyoathiri mamilioni ya watu waliokimbia makazi na raia wengine katika eneo lote," alisema msemaji wa UNHCR Boris Cheshirkov.  Wakimbizi pia walijikuta wakishambuliwa moja kwa moja mwezi Februari kwa mfano, maelfu ya Waeritrea walilazimika kukimbia kambi katika eneo la Afar, baada ya watu wenye silaha kuvamia, kuiba mali na kuua wakazi.  Kufikia mwezi Agosti, mashirika ya Umoja wa Mataifa yalitoa ombi la dharura la ufadhili kusaidia zaidi ya watu 750,000 wanaotafuta hifadhi nchini Ethiopia. Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP, lilionya kwamba, endfapo halitopokea ufadhili unaohitajika, wakimbizi wengi hawatakuwa na chakula.

Maelfu ya watu wanakufa wakijaribu kuingia Ulaya kwa boti

Idadi ya watu waliokufa au kupotea wakijaribu kufika Ulaya kwa boti iliongezeka maradufu kati ya 2021 na 2022, hadi zaidi ya watu 3,000.   Takwimu hii ya kutisha ilitolewa na UNHCR mwezi Aprili.  Msemaji wa UNHCR Shabia Mantoo aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano wa kawaida na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis kwamba "Nyingi ya safari za vivuko vya baharini zilifanyika katika boti zilizojaa pomoni, zisizo na uwezo wa kubaki na hewa na ambazo nyingi zilipinduka au kuharibiwa na kusababisha watu kupoteza maisha,". Ameongeza kuwa hata hivyo hii haikuwazuia wengi kujiweka katika hatari kubwa, kwa kujaribu kuvuka bahari.  Katika jaribio moja tu, mwezi Machi, wahamiaji wasiopungua 70 waliripotiwa kufariki  dunia au kupotea katika pwani ya Libya, sehemu ya kuanzia kwa vivuko vingi.  Mwezi Agosti, mashua ilipozama kwenye kisiwa cha Ugiriki cha Karpathos Agosti, kulikuwa na vifo vingi vilivyoripotiwa, na mwezi Septemba, zaidi ya miili 70 ilipatikana kufuatia ajali ya meli kwenye pwani ya Siria.

Matumaini ya mustakabali bora

Huku kukiwa na mkasa na matatizo yanayowakabili wengi, kumekuwa na nuru, iliyoripotiwa mwezi Desemba.  UNHCR ilitangazwa kwamba serikali duniani kote zimeahidi takriban dola bilioni 1.13, kiasi ambacho kimevunja rekodi, ili kuwaokoa watu waliokimbia makazi yao kutokana na vita, ghasia na ukiukaji wa haki za binadamu. "Kutokana na mizozo, hali ya dharura ya mabadiliko ya tabianchi, na majanga mengine, watu waliokimbia makazi yao duniani kote wanakabiliwa na mahitaji ambayo hayajawahi kushuhudiwa. Kwa bahati nzuri, wafadhili wakarimu wa UNHCR wanaendelea kuwaunga mkono katika siku hizi ngumu, na kujenga matumaini ya mustakabali bora" alisema Bwana Grandi.

30 December 2022, 13:29