Bi Harris ameaga Tanzania akielekea Zambia
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Katika ziara ya mataifa matatu barani Afrika, baada ya Ghana na Tanzania, Nchi anayoelekea ni Zambia. Makamu wa Rais wa Marekani Bi Kamala Harris aliwasili Tanzania usiku wa Jumatano tarehe 29 Machi 2023 baada ya kuitembelea nchini Ghana kuanzia tarehe 26 Machi. Bi Harris mara baada ya kufika Tanzania pia aliweka shada la maua katika kumbukumbu ya ukumbusho wa shambulio la bomu la kigaidi mnamo mwezi Agosti 1998 katika ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam, ambacho kwa kawaida ni kitovu cha uchumi wa Tanzania. Ni ukumbusho wa tukio la Mashambulizi yaliyokuwa ya wakati mmoja ya Al-Qaeda nchini Tanzania na katika ubalozi wa Marekani jijini Nairobi Kenya ambayo kwa wakati ule yalisababisha vifo vya zaidi ya watu 200 na zaidi ya 5,000 kujeruhiwa. Bi Harris kwa hiyo alikutana na kusalimiana na wahanga wa tukio hilo.
Katika ziara hiyo pamekuwapo na uthibitisho kwamba Marekani itaendelea kufanya kazi pamoja na serikali za kidemokrasia katika kuunga mkono matakwa ya kidemokrasia na matarajio ya kidemokrasia hasa ya watu wa bara kwa mujibu wa Rais wa Marekani Bi Kamala alipokutana na rais wa nchi ya Tanzania Bi Samia Suluhu Hassan, Alhamisi tarehe 30 Machi 2023, akiwa katika katikati ya ziara yake ya kwanza rasmi barani Afrika. Katika hotuba yake Bi Harris alisema kuwa "Washington itapanua ushirikiano wa kibiashara kati ya Marekani na Tanzania kufanya kazi kuelekea utoaji wa nikeli ya kiwango cha betri kutoka Tanzania hadi Marekani na soko la kimataifa mnamo 2026; vile vile kwa kupanua mtandao wa bei nafuu; na kushirikiana katika maeneo kama vile maendeleo ya kidemokrasia, bayoanuwai, uwezeshaji wa wanawake na miradi ya afya. Na kwa hiyo ili kufanikisha alitangaza kwamba Marekani itatoa msaada wa dola milioni 560 kwa Tanzania mwaka ujao wa fedha.
Bi Harris alimsifu hata Rais Mama Samia Suluhu kwa maendeleo ya utawala wake, na kwamba amekuwa bingwa wa mageuzi ya kidemokrasia katika nchi hiyo na kwa njia hiyo amepanua ushirikiano wao. Bi Harrisaidha alisema kwamba “Kwa hivyo, leo, basi, ni sehemu ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi zetu na chini ya uongozi wako, na nina imani kamili kwamba tutaweza kufanya hivyo”.
Kwa upande wake Rais wa Tanzania, Mama Samia alisema kwamba: “Leo Tanzania imekuwa na hatua nyingine ya kihistoria ambapo viongozi wawili wa kike, Makamu wa Rais na Rais wamekutana hapa leo". Aliongeza, “Ni msukumo na ushuhuda ulioje kwa wasichana wa Kitanzania. Ninakushukuru sana, Mama Makamu wa Rais, kwa kuheshimu mwaliko wangu na kuja kunitembelea.” Rais alitoa maombi kadhaa kwa Bi Harris, ikiwa ni pamoja na kupanuliwa kwa mpango wa visa vya muda mrefu kwa Watanzania nchini Marekani, kuongezwa kwa miaka 10 kwa Sheria ya Ukuaji na Fursa ya Afrika, na ziara ya baadaye ya rais. Bi Samia alisema: “Watanzania sasa wanasubiri kwa hamu ziara ya Rais Joe Biden nchini Tanzania, na tafadhali utufikishie salamu zetu na mwaliko wetu kwamba Tanzania inasubiri kumkaribisha.”
Wageni hao kutoka Marekani tangu walipolakiwa na wakati wa kuondoka wamesindikizwa na umati mkubwa ambao uliwasubiri katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius K. Nyerere. Bi Harris na mme wake wamekaa siku mbili za usiku nchini Tanzania, ambapo atahitimisha safari yake ya Juma moja akiwa nchini Zambia, nchi nyingine ambayo inajitahidi kuimarisha demokrasia yake na anatarajia kurudi Washington Marekani Dominika tarehe 2 Aprili 2023.