Ufunguzi wa mkutano wa 67 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani,CSW
Na Angella Rwezaula; - Vatican.
Unyanyasaji dhidi ya wanawake unaofanyika nchini Afghanistan na hata baadhi ya nchi ambazo wanawake na wasichana wanaenda wanatembea au kwenda shule huku wakiwa na wasiwasi wa kuweza kutekwa au kufanyiwa vitendo vya ukatili;pengo la usawa wa kijinsia linaloendelea kuongezeka,vifo wakati wa ujauzito na changamoto zilizo chochewa na Uviko-19 ni baadhi ya masuala yanayorudisha nyuma juhudi za kuwakomboa wanawake. Amesema hayo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa 67 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW ulioanza tarehe 6 Machi 2023 katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani. Bwana Guterres alisema mfumo wa kidunia haufanyi kazi na mfumo dume unasukuma nyuma maendeleo ya wanawake hivyo ni lazima juhudi ziendelee kuhakikisha maslahi na maendeleo ya wanawake yanafikiwa duniani kote.
Pengo la usawa
Bwana Guterres aliendelea kusisitiza kuwa “Mkutano wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake ni moja ya matukio muhimu ya kila mwaka katika Umoja wa Mataifa. Unachukua juhudi muhimu na kubwa zaidi katika wakati huu ambao hali za wanawake zinanyanyaswa, kutishiwa, na kukiukwa kote ulimwenguni. Kuanzia Ukraine mpaka ukanda wa Sahel hali za wanawake zinaendelea kuwa mbaya” alisema Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kutaja unyanyasaji dhidi ya wanawake unaofanyika nchini Afghanistan na hata baadhi ya nchi ambazo wanawake na wasichana wanaenda wanatembea au kwenda shule huku wakiwa na wasiwasi wa kuweza kutekwa au kufanyiwa vitendo vya ukatili". Vile vile mengine ni pengo la usawa wa kijinsia linaendelea kuongezeka, vifo wakati wa ujauzito au wakati wa kujifungua ambavyo vingeweza kuzuilia pamoja na changamoto zilizo chochewa na Uviko-19 kwa hiyo ni baadhi ya masuala yanayorudisha nyuma juhudi za kuwakomboa wanawake. Bwana Guterres alisema ingawa mfumo dume unapigana na juhudi za kuendeleza maendeleo ya wanawake lakini ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anapigana nao ili kufikia maendeleo kamili ya wanawake.
Ziara za viongozi wakuu huko Afghanstan
Kwa maana hiyo alisema “Niko hapa kusema kwa sauti kubwa na kwa uwaz: Umoja wa Mataifa unasimama na wanawake na wasichana kila mahali.” Amesema Guterres na kutaja baadhi ya juhudi zinazofanywa ikiwa ni pamoja na safari ya hivi karibuni ya Naibu katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed na Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake UN WOMEN Sima Bahous nchini Afghanistan walipoenda kuzungumza na utawala wa Taliban kuhusu haki za wanawake na wasichana nchini humo baada ya kupigwa marufuku kufanya kazi na shule.
Madhumuni ya mkutano wa CSW
Lengo la mwaka huu la mkutano huo ni kuhakikisha pengo la teknolojia linapunguzwa, wasichana na wanawake wanajumuishwa kwenye masuala ya teknolojia. Hesabu ipo wazi kabisa bila kuwashirikisha jamii yote dunia itafaidi nusu tu ya uwezo wake kwakuwa wengine watakuwa wameachwa nyuma kwenye masuala ya sayansi na teknolojia. “Watu bilioni tatu bado hawajaunganishwa kwenye huduma ya intaneti na wengi wao ni wanawake na wasichana katika nchi zinazo endelea. Katika nchi zenye uchumi duni 19% ya wanawake ndio wameunganishwa mtandaoni. Ulimwenguni kote wasichana na wanawake ni theluthi moja tu ya wanawafunzi wa masomo ya sayansi, teknolojia, uhandishi na hisabati.” Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kukuza michango ya wanawake kwenye sayansi, teknolojia na uvumbuzi sio kitendo cha hisani au neema kwa wanawake. Inafaidi kila mtu kwani wanawake wanapopata huduma za matibabu kupitia mtandaoni, familia zao na jamii zinapata afya.
Teknolojia ya akili bandia
Kauli hii ya Guterres imeungwa mkono na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Csaba Kőrösi, ambaye naye alizungumza baada ya Katibu Mkuu na kusema teknolojia mpya iwapo itatumika vizuri itasaidia kuleta usawa na kubadili mambo mengi. “Wajasiriamali wachanga wanatengeneza programu mpya za kulinda wanawake na wasichana kutokana na vitendo vya ukatili. kujifunza mtandaoni katika baadhi ya maeneo kunapunguza pengo la usawa kijinsia, kuwaandaa wanawake kwaajili ya kupata kazi kidijitali na kuwaunganisha wanawake na fursa za kufanya kazi.” Amesema Kőrösi. Ameongeza kuwa matumizi ya akili bandia "AI" ambayo yataimarisha uchumi wetu kesho yanaweza kubuniwa kwa njia ambazo zinafuta ubaguzi wa kijinsia ulioko leo. “Kwa kukabiliana na mitindo ambayo inazuia wasichana kuchagua kusoma na hatimaye kupata kazi kwenye eneo la sayansi, hisabati na teknolojia STEM, tunaweza kufanya kazi kubadilisha mawazo na kuongeza utofauti wa mawazo katika maeneo yetu ya kazi.” Akisema Mkuu huyo wa UNGA77