Siku ya Mama duniani ni kuwapongeza kwa yale wanayotenda!
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Uzazi na Idadi ya watu (UNFPA)katika fursa ya maadhimisho ya Siku ya Mama duniani iliyofanyika Dominika tarehe 14 Mei, lilisema kuwa “Katika mwezi wa Mei ni wakati wa kila mwaka kwa akina mama wengi duniani kote kupokea shukrani na kutambuliwa kwa yote wanayofanya. Lakini kwa maelfu ya wanawake duniani kote, shukrani hiyo inakwenda mbali zaidi. Shirika hili UNFPA limesema kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni, mwanamke mmoja hufariki dunia kutokana na ujauzito au kujifungua kila baada ya dakika mbili, huku idadi kubwa ya vifo hivi hutokana na sababu zinazoweza kuzuilika kama vile kutokwa na damu na maambukizi. Mbaya zaidi, ufumbuzi wa matatizo haya umekuwepo kwa miongo kadhaa; lakini unahitaji uwekezaji wa haraka katika upangaji uzazi na kwa ulimwengu kushughulikia uhaba mkubwa wa wakunga, ambao Shirika la Uzazi na Idadi ya Watu ( UNFPA) linaripoti wanaweza kuzuia takriban theluthi mbili ya vifo vya uzazi na watoto wachanga.
Natalia Kanem, Mkurugenzi Mtendaji wa UNFPA alisema “Tuna nyenzo, maarifa na rasilimali za kukomesha vifo vya uzazi vinavyoweza kuzuilika; tunachohitaji sasa ni utashi wa kisiasa. Hii ndio sababu akina mama wanahitaji usaidizi sasa zaidi kuliko hapo awali,” kwa njia hiyo Shirika UNFPA inaripoti juu ya takwimu za vifo wakati wa uzazi katika viwango vya janga, kwamba kati ya mwaka 2000 na 2015, vifo vya uzazi duniani vilipungua kwa zaidi ya theluthi moja, lakini kiwango cha kupungua tangu wakati huo kimedorora katika maeneo kadhaa na hata kubadili mwelekeo kwa wengine. Hii imesababisha vifo vya kina mama 287,000 mwaka 2020, idadi ya vifo ambayo ingetawala vichwa vya habari ikiwa ingetokana na janga la asili au shida nyingine.
Kwa njia hiyo Mkuu wa UNFPA anabainisha kuwa “Haikubaliki kwamba wanawake wengi wanaendelea kufa bila sababu katika ujauzito na kujifungua. Zaidi ya vifo 280,000 katika mwaka mmoja ni jambo lisilo la kawaida. Mara nyingi kama sivyo, wanawake na wasichana hawapati kufanya uamuzi wa kupata mimba, UNFPA inaeleza. Wanawake wanne kati ya kumi walioshiriki utafiti katika nchi 68 hawakuweza kupata huduma ya haraka linapokuja suala la afya, ngono au vidhibiti mimba. Wakati huo huo, baadhi ya takwimu zinaonesha mimba zinazohusiana na ubakaji hutokea angalau mara kwa mara kama vile mimba zinazotokana na tendo la kujamiiana kwa kukubaliana”, Shirika hilo limeripoti
Aidha wamebainisha kwamba “Mambo haya na mengine yanasababisha janga la kimataifa lililopuuzwa, ambapo karibu nusu ya mimba zote duniani hazikutarajiwa, na kusababisha matokeo mabaya kwa wengi wa walioathirika”. Kwa hiyo UNFPA inasema matatizo ya ujauzito na kuzaa yanaweza kusababisha kifo, hasa kwa vijana na wasichana, hivyo wastani wa watoto nusu milioni walizaliwa kwa wasichana wenye umri wa miaka 10-14 mwaka 2021, na kufanya mamia ya maelfu ya akina mama wakiwa bado katika utoto. Idadi kubwa ya mimba zisizotarajiwa inawakilisha kushindwa duniani kote kutetea haki za kimsingi za wanawake na wasichana,” Bi. Kanem alisema.