Siku ya walinda amani duniani tarehe 29 Mei:“Amani huanza na mimi”
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa ndio moyo mkuu wa kujitolea kwetu kwa ulimwengu wenye amani zaidi. Kwa miaka 75, wameunga mkono watu na jamii zilizotikiswa na migogoro na machafuko ulimwenguni kote. Amesema hayo Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa, Bwaqna Antonio Guterres, katika fursa ya Siku ya Kimataifa ya wahudumu wa Amani wa Umoja wa Mataifa ambayo uadhimishwa kila ifikapo tarehe 29 mei ya kila mwaka. Kauli mbiu ya mwaka 2023 ni: “Amani huanza na mimi” kwa hiyo, Bwana Guterres alisema kwamba “kwa miaka 75, walinda amani wa Umoja wa Mataifa wamejitahidi kuokoa na kubadilisha maisha katika hali tete zaidi za kisiasa na usalama duniani. Tangu mwaka wa 1948, zaidi ya wafanyakazi milioni mbili waliovalia sare na raia wamesaidia nchi kuhama kutoka vita hadi kwenye amani. Wakifanya kazi pamoja na jumuiya za wenyeji, walinda amani husaidia kuendeleza suluhu za kisiasa, kuzuia migogoro, kulinda raia, kuimarisha haki za binadamu na utawala wa sheria, na kujenga amani endelevu”.
Kampeni na Amani huanza na mimi
Mkuu wa Umoja wa Mataifa anabainisha kuwa “Changamoto wanazokabiliana nazo walinda amani ni kubwa kuliko wakati mwingine wowote, na kuongezeka kwa mivutano ya kimataifa, migogoro ngumu zaidi, na kuenea kwa taarifa potofu na disinformation, ambayo inazuia kazi yao na kutishia usalama wao. Licha ya vikwazo hivyo, walinda amani wanadumu, pamoja na washirika wengi, katika kutafuta amani kwa pamoja.”Kauli mbiu ya maadhimisho ya miaka 75 ya‘Amani inaanza na mimi’ ambapo kuna kampeni ambayo inatambua huduma na kujitolea kwa walinda amani wa zamani na wa sasa, wakiwemo zaidi ya 4200 ambao wamejitolea maisha yao chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa. Pia Kampeni ya Umoja wa Matifa inatoa pongezi kwa jamii tunazohudumia, ambazo zinaendelea kujitahidi kuleta amani licha ya vikwazo vingi. Kampeni hii pia inatoa wito kwa kila mmoja wetu kujiunga na harakati za kimataifa za kutafuta amani. Peke yetu, hatuwezi kamwe kufanikiwa. Lakini, pamoja, tunaweza kuwa nguvu kubwa ya mabadiliko.
Matukio
Katika kuadhimisha hafla hiyo kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York mnamo tarehe 25 Mei, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliweka shada la maua kwa ajili ya heshima ya walinda amani wote waliopoteza maisha katika kipindi cha miaka 75 iliyopita. Hafla ilifanyika ili kuwatunuku nishani ya Dag Hammarskjold baada ya kifo chake kwa walinda amani waliofariki mnamo mwaka wa 2022. Tuzo ya Wakili Bora wa Kijeshi wa Jinsia pia ilitolewa. Katika maonesho ya Jumba la Wageni kuanzia tarehe 1 Mei hadi 6 Juni ni onesho la picha linalofuatilia mchakato wa safari ya miaka 75 ya ulinzi wa amani.
Ulinzi wa Amani Hufanya Nini?
Ulinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa husaidia nchi kuvuka njia ngumu kutoka katika migogoro hadi amani. Kwa mujibu wao wanasema kwamba wananguvu za kipekee, ikiwa ni pamoja na uhalali, kugawana mizigo, na uwezo wa kupeleka askari na polisi kutoka duniani kote, kuwaunganisha na walinda amani wa kiraia kushughulikia majukumu mbalimbali yaliyowekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Baraza Kuu.
Suala la Kimataifa: Amani na Usalama
“Kuokoa vizazi vijavyo na janga la vita” ni kati ya maneno ya kwanza kabisa ya Hati ya Umoja wa Mataifa (katika Dibaji yake), na maneno hayo yalikuwa ni kichocheo kikuu cha kuunda Umoja wa Mataifa, ambao waanzilishi wake walikuwa wameishi katika uharibifu wa dunia mbili ya vita ifikapo 1945. Tangu kuundwa kwa Umoja wa Mataifa tarehe 24 Oktoba 1945 (tarehe ambayo Mkataba wake ulianza kutumika), Umoja wa Mataifa mara nyingi umeitwa kuzuia migogoro isizidi kuwa vita, au kusaidia kurejesha amani kufuatia kuzuka kwa vita, na kuendeleza amani ya kudumu katika jamii zinazotokana na vita.
Kwa nini kuadhimisha Siku za Kimataifa?
Siku na Juma la kimataifa ni hafla za kuelimisha umma juu ya masala yanayohusika, kuhamasisha utashi wa kisiasa na rasilimali kushughulikia shida za ulimwengu, na kusherehekea na kuimarisha mafanikio ya ubinadamu. Kuwepo kwa siku za kimataifa kumetangulia kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, lakini Umoja wa Mataifa umezikubali kama chombo chenye nguvu cha utetezi. Pia wanaadhimisha maadhimisho mengine ya Umoja wa Mataifa.