Tafuta

Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limezindua mwongozo mpya kuhusu VVU na UKIMWI. Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) limezindua mwongozo mpya kuhusu VVU na UKIMWI.  (AFP or licensors)

WHO yazindua Mwongozo mpya kuhusu VVU na UKIMWI

Ni mwongozo ambao pamoja na mambo mengine unafafanua ni kwa jinsi gani matumizi sahihi na ya wakati wa dawa za kupunguza makali ya UKIMWI yanaweza kuondoa hatari ya anayeishi na VVU kuambukiza kwa mpenzi wake au kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.Kuna matumaini makubwa.

Habari za Umoja wa Mataifa

Shirika la Afya Duniani (WHO) Julai 23 limezindua mwongozo wa kisayansi na kimaadili kuhusu Virusi Vya Ukimwi, VVU au HIV vinavyosababisha UKIMWI au AIDS. Mwongozo huo ukiambatana na mapitio maalum kutoka jarida la kitatibu la Lancet yanaelezea nafasi ya ufifishaji wa virusi hivyo na kiwango cha kutoonekana kwa virusi hivyo kwa mgonjwa katika kuimarisha afya ya mhusika na kutokomea maambukizi ya virusi hivyo. Taarifa iliyotolewa leo na WHO inasema mwongozo huo umezinduliwa leo kwenye mkutano wa 12 wa kimataifa wa mashirika yanayohusiana na UKIMWI, IAS ulioanza leo huko Brisbane Australia na ukitarajiwa kumalizika tarehe 26.

Wanaomeza dawa ipasavyo wanapunguza hatari ya maambukizi

Mathalani mwongozo unaelezea kiwango cha msingi cha VVU na hatua za kupima viwango hivyo kwa kutumia vipimo mahsusi. Mathalani watu wanaoishi na VVU wanaofikia kiwango fulani cha virusi kutoonekana mwilini baada ya kutumia kikamilifu dawa za kufifisha makali ya virusi, hawawezi kuambukiza virusi vya Ukimwi kwa mpenzi/wapenzi wao na wako katika hatari ndogo ya kuambukizi virusi hivyo kwa Watoto wao. Ushahidi huu pia unadokeza kuwa kuna kiwango kidogo au sifuri kabisa cha hatari ya kuambukiza VVU pindi mtu amefikia kiwango cha chini ya au sawa na  nakala 1000 za VVU kwenye mililita ya damu, jambo linalotambuliwa kuwa ni kiwango cha VVU kilichofifishwa.

Dawa za kupunguza makali ya UKIMWI ni nuru

WHO inasema dawa za kupunguza au kufifisha makali ya virusi zinaendelea kubadili Maisha ya watu wanaoishi na VVU. Watu wanaoishi na VVU ambao wamepimwa mapema na kubainika kuwa na VVU na kuanza mapema kupata matibabu na kutumia dawa hizo kama wanavyoelekezwa wanaweza kutarajia kuwa na kiwango cha umri wa kuishi kama wenzao wasio na VVU. Akizungumzia mwongozo huu, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk. Tedros Ghebreyesus alisema kwa zaidi ya miaka 20, nchi duniani kote zimezingatia miongozo ya WHO ya kuzuia, kuchunguza na kutibu maambukizi ya VVU. Hivyo amesema mwongozo huu mpya unaochapishwa leo utasaidia nchi kutumia mbinu thabiti zaidi zenye uwezo wa kubadili Maisha ya mamilioni ya watu wanaoishi na VVU au walio hatarini kuambukizwa VVU.

Nuru kwa watu wazima, lakini kwa Watoto hatua zahitajika

Kwa mujibu wa WHO, mwishoni mwa mwaka 2022, watu milioni 29.8 kati ya watu milioni 39 duniani kote wanaoishi na VVU, walikuwa wanatumia dawa za kupunguza makali ya virusi hivyo. Hii ina maana asilimia 76 ya watu wote wanaoishi na VVU ambapo takribani asilimia 71 kati yao wana kiwango cha VVU kilichofifishwa afya zao zimelindwa na hawako hatarini kuambukiza virusi hivyo vya watu wengine. WHO inasema ingawa haya ni maendeleo makubwa kwa watu wazima wanaoishi na VVU, bado kiwango cha ufifishaji wa VVU kwa Watoto ni asilimia 46 pekee, suala ambalo inasema linahitaji kupatiwa umakini wa kipekee.

Tanzania na Rwanda ni miongoni mwa nchi zilizoko kwenye mwelekeo

Kwa njia hiyo WHO inasema mwongozo huu umetolewa tarehe 23 Julai 2023  wakati maendeleo ya kuelekea kutokomeza UKIMWI yakiwa na wasi wasi hasa baada ya janga la UVIKO-19. Hata hivyo kuna nchi ambazo ziko kwenye mwelekeo sahihi kutokomeza UKIMWI nazo ni pamoja na Tanzania, Australia, Botswana, Eswatini, Rwanda na Zimbabwe.

24 July 2023, 16:08