Ziara ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Nchini Urusi Julai 2023
Na Ofisi ya Waziri Mkiuu, St. Petersburg, Urusi.
Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka wanadiaspora wa Tanzania wazingatie sheria za nchi wanazoishi ili waendelee kutunza heshima ya nchi yao. Ametoa wito huo wakati akizungumza na Watanzania waishio St. Petersburg, Urusi ambako alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Pili wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi. “Baadhi yenu mko hapa mnatafuta fursa, na wengine wengi wako hapa kwa masomo. Zingatieni sheria za nchi hii, tunzeni heshima ya Tanzania. Teteeni Taifa la Tanzania, zungumzieni fursa zilizopo nyumbani,” alisema Waziri Mkuu. Akisisitiza umuhimu wa kukitangaza Kiswahili, Waziri Mkuu alisema: “Kiswahili kiendelee kutangazwa kwa bidii kwani Kiswahili ni fursa na Kiswahili ni ajira. Tukitangaze Kiswahili na tushike nafasi za kutangaza lugha yetu kwa kasi kwa sababu tuna historia ya muda mrefu na Urusi ambao wamekuwa wakitumia lugha hii,” alisema. Alisema katika baadhi ya vikao vyake na wawekezaji wa Kirusi, hakupata shida ya mkalimani kwa sababu walikuwa na mtu wao ambaye anatafsiri moja kwa moja kutoka Kirusi kwenda Kiswahili na Kiswahili kwenda Kirusi. “Lakini na sisi ubalozini kwetu tuna Afisa Uchumi ambaye alitusaidia kutafsiri Kiswahili kwenda Kirusi kwenye baadhi ya vikao. Tena aliongea kwa ufasaha zaidi. Tusiache fursa hii itupite,” aliwasisitiza. Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwapa picha halisi ya maendeleo na kiuchumi yanayofanyika nchini chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zikiwemo sekta za elimu, afya, miundombinu, utalii, kilimo, maji na akawahakikishia kwamba Tanzania iko salama, wao waweke bidii kwenye masomo yao.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa kikao hicho, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Mbarouk alisema mbali na kazi ya kudumisha mahusiano ya kirafiki na kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi nyingine, Serikali imeendelea kuratibu masuala ya Diaspora. “Hivi sasa, wizara imekamilisha Mapitio ya Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001, ambayo inajumuisha masuala ya Diaspora. Ili kuondokana na tatizo la ukosefu wa takwimu sahihi za idadi ya Diaspora wetu kote ulimwenguni, tarehe 22 Mei, 2023 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax alizindua rasmi Mfumo wa Kuwasajili Diaspora Kidigitali. Mfumo huo, uliotengenezwa na Wataalam Wazawa utasaidia kurahisisha usajili wa Diaspora wenye asili ya Tanzania pamoja na wanafunzi.” “Ni dhahiri kuwa Diaspora waliopo katika eneo zima la uwakilishi wa ubalozi wetu hapa Urusi, sasa hawatalazimika tena kusafiri kwenda ubalozini Moscow ili kujisajili. Napenda kutumia fursa hii kuwahamasisha Diaspora wote wajisajili kwa wingi.” Alisema ana imani kuwa takwimu zitakazopatikana kupitia mfumo huo, zitaiwezesha Serikali kupanga na kuandaa kwa usahihi mahitaji yanayohitajika ili kuwapatia Diaspora huduma wanazozihitaji, ikiwemo huduma za kibenki, Hati za Kusafiria, Vitambulisho vya Taifa na vitambulisho rasmi vya utambuzi wa diaspora wakati wa utekelezaji wa Hadhi Maalum. “Hadi sasa, mfumo huu umetuwezesha kufahamu kuwa tunao diaspora wenye asili ya Tanzania katika nchi za Vanuatu, Albania, Antigua na Barbuda, Kazakhstan, Azerbaijan pamoja na America Samoa ambazo nchi yetu haina uwakilishi wa Kibalozi,” alisema.
Akisoma risala yao, Mwenyekiti wa Diaspora katika Shirikisho la Urusi na Nchi huru za Jumuiya ya Madola (CIS), Pascal Gura alisema jumuiya yao (TADRU- CIS), ina wanachama zaidi ya 200 walioko sehemu tofauti za nchi hiyo. Alisema kwa sasa wanadiaspora hao wanakabiliwa na changamoto ya mifumo ya kifedha kutokana na vikwazo vya kiuchumi. “Changamoto hii inatokana na Shirikisho la Urusi kuondolewa katika mfumo wa uhamishaji fedha (Swift) ambao unatumiwa na mabenki kupitia kadi za ‘‘Visa na Master card.’’ “Kwa sasa kadi pekee zinazokubali katika baadhi ya mabenki katika Shirikisho la Urusi ni kadi zinazotumia mfumo wa Union Pay. Hivyo, tunaomba benki za Kitanzania zipanue wigo kwa kutoa kadi zenye mfumo wa Union Pay kwa kuwa itaimarisha pia fursa za kibiashara kati ya Tanzania na Urusi,” alisema. Wanadiaspora hao pia walimkabidhi Waziri Mkuu tuzo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutambua juhudi zake katika kuwaletea wananchi maendeleo. Mkutano huo ulihudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Tabia Maulid Mwita, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Mbarouk, Naibu wa Waziri wa Fedha na Mipango wa SMZ, Ally Suleiman Ameir, Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Balozi Fredrick Kibuta na watendaji wengine wa Serikali.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Jumapili, Julai 30, 2023 alikuwa miongoni mwa Wakuu wa Nchi na Serikali waliohudhuria Maonesho ya Gwaride Maalum la Jeshi la Wanamaji la Urusi yaliyofanyika Senatskaya Marina, St. Petersburg, Urusi. Viongozi hao ni wale walioshiriki Mkutano wa Pili wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka Mataifa ya Afrika na Urusi jijini St. Petersburg, Urusi ambako yeye alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Maonesho hayo yamefanyika ikiwa ni siku ya Jeshi la Wanamaji la Urusi na maadhimisho ya kukumbuka kuanzishwa kwa jeshi hilo ambayo hufanyika Julai 30, kila mwaka. Katika maonesho hayo Rais wa Urusi, Vladmir Putin alipita kwenye boti maalum akiwasalimia wananchi waliojipanga kwenye kingo za mto Bolshaya Neva na kupokea salamu za kijeshi. Alipomaliza akavushwa na boti ndogo kwenda kwenye jukwaa maluum na kuhutubia Taifa. Baada ya hapo meli na boti za kivita zilipita mbele ya jukwaa kuu na kutoa heshima. Kisha akaenda kuwasalimia mmoja baada ya mwingine viongozi wa Afrika waliohudhuria maonesho hayo na baadaye alipanda nao kwenye boti hiyo maalum.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewapongeza wafanyabiashara 19 kutoka Tanzania ambao walishiriki maonesho ya kibiashara kwenye Jukwaa la Kimataifa la Uchumi na Kibinadamu la Afrika na Urusi lililomalizika Julai 28, mwaka huu. Wafanyabiashara hao wanamiliki makampuni yanayohusika na sekta za elimu, afya, kilimo, madini, mafuta na gesi, utalii, ujenzi, utafiti na ushauri wa kibiashara. Ametoa pongezi hizo Jumamosi, Julai 29, 2023 wakati akizungumza nao jijini St. Petersburg, Urusi ambako alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Pili wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka Mataifa ya Afrika na Urusi. “Ninawapongeza kwa kuamua kusafiri na kuja hadi huku ili kutumia fursa ya mkutano wa Urusi na Afrika kutafuta masoko ya bidhaa zenu na wabia wa kufanya nao biashara kule nyumbani. Sekta binafsi ya pande zote mbili za nchi yetu ni muhimu. Nataka mtambue kuwa mna mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa Taifa letu,” alisema. “Udhahiri wa sekta binafsi umeonekana leo kwa kitendo chenu cha kushiriki Expo Forum na mimi nataka niwathibitishie kuwa mnao uwezo mkubwa wa kutafuta mitaji na rasilmali mbalimbali. Niwasihi muungane mkono ili muweze kuwafikia wazalishaji wakubwa huku mkiwaeleza kuwa Tanzania ni nchi iliyokaa kimkakati kwenye sekta ya kibiashara,” alisema. Aliwaambia wafanyabiashara hao kwamba Serikali inathamini majukumu yao na kwamba itawaunga mkono ili waweze kuendelea kufanya vizuri. “Anzisheni viwanda, boresheni biashara zenu na mkutane na wawekezaji mbalimbali,” alisisitiza.
Pia aliwapa nafasi wafanyabiashara hao watoe maoni yao kuhusiana na ushiriki wao kwenye Jukwaa la Kimataifa la Uchumi na Kibinadamu ili Serikali iweze kuyafanyia kazi. Mapema, akisoma risala kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa wafanyabiashara hao, Bw. Otieno Igogo alisema walikuja na bidhaa mbalimbali ili kuzitangaza na kutafuta fursa za kibiashara kwenye soko la Urusi. Alizitaja bidhaa hizo kuwa ni korosho, mafuta ya alizeti, kahawa, rosella, viungo mbalimbali (spices), mchele, karanga, vanilla, madini mbalimbali, zabibu na mvinyo. “Kati ya hizo, kuna bidhaa ambazo zimependwa zaidi ikiwemo korosho, kahawa, viungo (spices), rosella, karanga, mchele, mafuta ya alizeti na zabibu.” Bw. Igogo alimweleza Waziri Mkuu kwamba makampuni 10 kati ya 19 yaliyoshirki kongamano hilo kutoka Tanzania, yameweza kusaini mikataba ya ushirikiano wa kibishara na makampuni 11 toka Urusi ilhali makampuni mengine matano bado yako kwenye maongezi ya ushirika wa kibiashara. “Baadhi ya makampuni yaliyoshiriki kongamano hili yamefanikiwa kufanya makubaliano ya ushirikiano na mengine yako kwenye maongezi ya uwekezaji katika maeneo mbalimbali ikiwemo ukaushaji wa matunda, uchimbaji na utafiti wa madini, mafuta na gesi, uanzishaji wa viwanda kwa ubia kwenye maeneo ya uchakataji na utengenezaji wa engineered wood product na mitambo kwa ajili ya kilimo cha kisasa. Pia kuna baadhi ya kampuni ambazo zimesaini mikataba ya uwezeshaji katika masuala ya uwekezaji baina ya wafanya biashara wa Urusi na Tanzania.” Alisema. Mkutano huo uilihudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Tabia Maulid Mwita, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Mbarouk, Naibu wa Waziri wa Fedha na Mipango wa SMZ, Ally Suleiman Ameir, Balozi wa Tanzania nchini Urusi, Balozi Fredrick Kibuta na watendaji wengine wa Serikali.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na wawekezaji kutoka kampuni nne za Urusi zenye nia ya kuwekeza nchini katika nyanja ya usindikaji mazao, nishati jadidifu na utengenezaji wa vifungashio vya glasi. Kampuni hizo ni SEIES (usindikaji mazao na mitambo yake), Agrovent (kusindika mazao yanayoharibika haraka), Unigreen Energy (Nishati Jadidifu) na TD Glass NN Expo LLC (utengenezaji wa chupa za vioo vya kutumia mchanga na magadi). Amekutana nao Jumamosi, Julai 29, 2023) kwa nyakati tofauti wakati akizungumza nao jijini St. Petersburg, Urusi ambako alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Pili wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi. Akielezea kuhusu kampuni yao, Mwenyekiti wa Bodi wa kampuni ya SEIES, Bw. Yuri Korobov amesema wanasindika vyakula kwa kukausha mazao bila kuharibu viinilishe (nutrients) na vyakula hivyo vinaweza kuhifadhiwa kwa mwaka mmoja. “Tukianzisha mradi huu tunaweza kuhifadhi matunda na vyakula vingi vilivyoko Tanzania. Tunatumia teknolojia ya kugandisha na kukausha maji yote bila kuharibu viinilishe. Mradi huu unaweza kupanuliwa katika wilaya na mikoa mingine nchini Tanzania kwani tumelenga wakulima walioungana kwenye vyama vya ushirika,” amesema. Bw. Korobov ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Kuratibu Biashara za Taasisi za Umma nchini Urusi (Delovaya Rossiya) alisema wamepanga kuwafundisha wafanyakazi ili wawe na elimu ya uhandisi wa kusindika mazao hayo. Delovaya Rossiya ambayo pia ni maarufu kama “Business Russia” ilianzishwa mwaka 2001, inaunganisha wafanyabiashara zaidi ya 7,000 na ina uwakilishi kwenye majimbo yote 85 ya Shirikisho la Urusi.
Kwa upande wake, Mmiliki wa Kampuni ya SEIES, Bw. Mikhail Mikhailov alisema kampuni hiyo pia inabuni ufundi na kutengeneza vifaa vinavyotumika kwenye teknolojia ya kukausha mazao. “Nchi zinazoongoza kwa teknolojia hii ni China na Uturuki, tunaamini Tanzania inaweza kushindana nao na kuwa mbele zaidi kwenye teknolojia hii.” Kuhusu mitambo ya kukaushia mazao, alisema wanaweza kuunda mitambo ambayo ikifika nchini inakuwa rahisi kuunganisha (assembling) na rahisi kuijenga kwa haraka. “Mitambo yetu inaweza kusindika vyakula vya mafuta, vya mimea, matunda, mbogamboga, maziwa, samaki na nyama. Alilitaja eneo jingine wanaloweza kuanzisha ni utenegenezaji wa friji zinazotumia nguvu ya jua badala ya umeme, na teknolojia ya kutengeneza nishati ya umeme kwa kutumia takataka. “Hili ni suluhisho mara mbili kwani tutapata umeme na kuhifadhi mazingira kwa kupunguza takataka,” alisema. Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu na mwanzilishi wa kampuni ya Agrovent, Bw. Sergey Pribysh alimweleza Waziri Mkuu kwamba wana nia ya kuja kuwekeza Tanzania kwenye mazao yanayoharibika haraka kama vile maua na mbogamboga. “Kampuni yetu ni miongoni mwa kampuni kubwa zinazozalisha mitambo ya kusindika maziwa na nyama zinazotokana na ndege kama vile kuku na bata. Tuko tayari kushirikiana na Watanzania na tumejipanga kutoa mafunzo ili kuandaa wataalamu watakaoendesha mitambo hiyo. Itabidi tuwapate maafisa kilimo ili wafundishwe jinsi mitambo inavyofanya kazi,” alisema. Naye Bw. Aleksey Tatarinov wa Kampuni ya Unigreen Energy alisema wana nia kuimarisha sekta ya nishati nchini kwani wana utaalamu wa kutengeneza umeme jua na paneli zake, umeme wa upepo na wa jotoardhi (geothermal).
Naye Mmiliki mwenza wa Kampuni ya TD Glass NN Expo LLC, Bw. Andropov Vasilyevich alisema wana kampuni inayotengeneza chupa za vioo vya kutumia mchanga na magadi kwa hiyo wana nia ya kutengeneza ili wauze kwenye viwanda vingine. Waziri Mkuu amewahakikishia mazingira mazuri ya uwekezaji kwani Serikali ya awamu ya sita imeweka msisitizo kwenye uwekezaji na maamuzi yao ni sahihi kwa sababu Tanzania ni mahali sahihi pa kuwekeza. Amewaeleza wawekezaji hao kuwa Tanzania ina soko la uhakika kwa kuwa inazungukwa na nchi za Kenya, Uganda, DRC, Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi na Msumbiji. “Unaweza kwenda kufanya biashara kokote.” Amesema Serikali ya awamu ya sita imeendelea na mkakati wa ujenzi wa miundombinu ambayo kwa kiasi kikubwa inachangia kuchochea ukuaji wa uchumi kupitia biashara na uwekezaji. “Tuna miundombinu ya reli, tuna barabara nzuri karibu maeneo yote nchini, tuna ndege, tunayo maziwa makuu matatu yanayowezesha usafirishaji wa bidhaa, pia malighafi tunazo za kutosha, kwa hiyo karibuni sana Tanzania.”