Silaha za nyuklia na makombora Silaha za nyuklia na makombora 

26 Septemba ni Siku ya Kimataifa ya kutokomeza matumizi ya silaha za nyuklia

Katika siku ya kimataifa ya kutokomeza kabisa matumizi ya silaha za kinyuklia Papa amebainisha kuwa“umiliki wa silaha za atomiki sio maadili.Katibu Mkuu wa UN alipongeza "huduma ya ujasiri ya wafanyakazi wa IAEA waliopo kwenye vinu vya nyuklia nchini Ukraine.Na IAEA wataendelea kufuatilia mwenendo wa nyuklia Ukraine na kwingineko.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Katika  fursa ya Siku ya Kimataifa  ya kutokomeza matumizi ya silaha za kinyuklia inayofanyika kila ifikapo tarehe 26 Septemba ya kila mwaka, kwenye ujumbe mfupi kwenye Mtandao wa Kijamii, Baba Mtakatifu Francisko ameandika kuwa: “Umiliki wa silaha za atomiki sio wa maadili kwa sababu kama alivyokuwa ameona  Yohane XXIII katika Waraka wa Pacem in terris kuwa : “ non è escluso che un fatto imprevedibile metta in moto l’apparato bellico”.  Chini ya tishio la  la silaha za kinyuklia sisi sote daima tumepoteza.”

IAEA:Ufuatiliaji wa mwenendo wa nyuklia kila mahalia 

Katika fursa ya kuelekea kilele cha Siku hiyo, ya kutokomeza matumizi ya nishati ya atomiki katika ujumbe kutoka kwa mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la nguvu ya nishati ya atomiki IAEA, Bwana Rafael Grossi, alissema kuwa: “Hatuendi popote, tutaendelea kufuatilia mwenendo wa nyuklia kila mahali” kuhusu dhamira ya shirika hilo kuendelea kufuatilia vinu vya nyuklia vya Ukraine wakati huu wa uvamizi unaoendelea wa Urussi lakini pia mwenendo wa nyuklia kwingineko duniani kama vile shughuli za uhakiki wa nyuklia nchini Iran na ufuatiliaji wa mipango ya nyuklia wa DPRK. Akihutubia katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa IAEA mjini Vienna  nchini Uswiss tarehe 25 Septemba 2023,  Bwana Grossi alisema kuwa tume 53 zikiwa na zaidi ya wafanyakazi 100 wa shirika hilo zimetumwa kama sehemu ya kuendeleza kuwepo wao ndani ya vinu vitano vya nyuklia nchini Ukraine. Vinu hivyo ni pamoja na kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhya, au ZNPP, kwenye mto Dnipro kusini mwa Ukraine, ambako Bwana Grossi amesema kwamba hali inasalia kuwa tete sana. ZNPP inadhibitiwa na vikosi vya Urusi lakini inaendeshwa na wafanyakazi wake wa Ukraine. Ni kinu kikubwa zaidi cha nyuklia barani Ulaya na IAEA imekuwa ikifuatilia hali huko tangu siku za mwanzo za mzozo.

Kuna nchi mipya zina mipango ya kuanzisha nishati ya nyuklia

Mkuu huyo wa IAEA amendelea kusema: “Ni wazi kwamba kila nchi au jumuiya lazima iamue yenyewe ikiwa nishati ya nyuklia ni sawa kwao. Lakini pia inazidi kuwa bayana kuwa nchi zaidi na zaidi zinaonesha nia ya kuwa na nishati ya nyuklia, na kwamba wanachukua hatua kwa nia hii. Hili lilidhihirika mwaka 2022 huko Washington katika mkutano wetu wa kimataifa wa mawaziri kuhusu nishati ya nyuklia katika karne ya 21. Nchi mpya zilitangaza mipango ya kuanzisha nishati ya nyuklia, wakati mataifa mashuhuri ya nyuklia yalifichua matamanio ya kuanzisha kizazi kipya cha vinu vya hali ya juu vya nyuklia kushughulikia changamoto kuu.” Na hivyo  akikisisiza alisema  juhudi mpya za shirika hilo pia zilioneshwa ili kuisaidia dunia kufikiria upya nishati ya nyuklia kama chanzo safi, cha kutegemewa na endelevu cha nishati kwa karne ya 21. Kwa mfano alisema shirika hilo litaendelea kushirikiana nan chi wanachama katika kutumia nyuklia kukabiliana na magonjwa kama saratani na zoonotics. Hadi miaka michache iliyopita, hatukuwa na sauti za kutosha kuhusu faida za nishati ya nyuklia. Lakini sasa ukurasa huo umegeuzwa aliongeza Bwana Grossi.

Uwazi unahitajika katika mipango ya nchi kuhusu nyuklia

Kwa mujibu wa IAEA hata kama kura za maoni ya umma ulimwenguni kote zinaonesha mabadiliko katika kupendelea nishati ya nyuklia, nchi bado zinahitaji kushirikisha wenye mamlaka wote kwa uwazi na kwa vitendo katika mipango yao ya nishati ya nyuklia. Juhudi za pamoja na hatua zinahitajika katika kiwango cha kimataifa na kwa hivyo msimu ujao wa kuchipua kutakuwa na mkutano wa kilele wa nishati ya nyuklia. Maamuzi ya kijasiri yanahitajika ili kutufanya tuelekee katika mustakabali wa nishati wagharama nafuu, wa haki na endelevu unaogusa chaguzi zote zinazowezekana za teknolojia inayotoa hewa ukaa ndogo sana ikiwa ni pamoja na nishati ya nyuklia.

Katibu Mkuu wa UN: Ahadi ya kufuatilia mienendo ya matumizi

Katika ujumbe uliosomwa wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Katibu wa Umoja wa Mataifa, Bwana António Guterres alipongeza huduma ya ujasiri ya wafanyakazi wa IAEA waliopo kwenye vinu vya nyuklia nchini Ukraine. Na aliahidi kwamba Umoja wa Mataifa utaendelea kufanya “kila unaloliweza kuhakikisha mzunguko salama wa wataalam wanaofanya kazi katika vituo vitano vya nyuklia vya Ukraine.” Kwa njia hiyo IAEA ilibanisha kuwa leo hii,  duniani kote kuna vinu 410 vya nishati ya nyuklia vinavyofanya kazi katika nchi 31 vikiwa na uwezo wa kuzalisha takriban gigawati 369 za nishati, na kusambaza asilimia 10 ya umeme wa dunia na karibu robo ya umeme wote wa hewa ukaa ya chini. Pia kuna mitambo 58 inayojengwa katika nchi 31, na mitambo hiyo inatarajiwa kuzalisha takriban gigawati 60 za uwezo wa ziada wa nishati.

Zelensky: athari za silaha za nyuklia ni kwa nchi zote duniani

Na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine hivi karibuni tarehe 19Septemba 2023 aliwambia viongozi wa dunia katika mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA 78) kwamba “pamoja na tishio lake la nyuklia linaloendelea, Urussi pia inatumia silaha muhimu kama vile soko la kimataifa la chakula na nishati na inazitumia sio tu dhidi ya nchi yetu, lakini nchi zenu wote pia.” Rais wa Ukraine aliendelea kusema kwamba tangu kuanza kwa vita, bandari za Ukraine katika bahari ya Nyeusi na Azov zilizuiliwa na Urussi na bandari zake kwenye Mto Danube zikilengwa na ndege zisizo na rubani au drones na makombora. “Ni jaribio la wazi la Urussi la kutumia uhaba wa chakula kwenye soko la kimataifa kama silaha, ili kubadilishana na kutambuliwa kwa baadhi ya maeneo yaliyotekwa.” Rais huyo wa Ukraine alisema athari za silaha hizo zinaonekana kuanzia Afrika hadi Kusini-Mashariki mwa Asia. “Nyuklia sio tena jambo la kutisha zaidi kwa sasa. Uharibifu mkubwa unaendelea kushika kasi. Mvamizi huyo anatumia vitu vingi kama silaha, vitu ambavyo vinatumiwa sio tu dhidi ya nchi yetu lakini pia yako, amesema na kuongeza kuwa “Kuna mikataba mingi dhidi ya silaha lakini hakuna hata mmoja dhidi ya silaha ya usambazaji wa chakula na nishati duniani.”

 

26 September 2023, 12:38